Bukobawadau

RULENGE KANAZI NA NYAMIANGA WILAYANI NGARA KUPATA HUDUMA YA UMEME

 Mkuu wa wilaya ya Ngara Costantine Kanyasu
WANANCHI wa Tarafa za Rulenge Kanazi na Nyamiaga wilayani Ngara Mkoani Kagera wanatarajia kusambaziwa huduma ya nishati ya umeme  baada ya Rais Kikwete kutoa ahadi kwa wananchi wa tarafa hizo  katika ziara yake mwaka jana.
Mkuu wa wilaya ya Ngara Costantine Kanyasu  amesema mpango wa kusambaza umeme huo utaanzia kijiji cha Djululigwa hadi Rulenge kupitia wakala wa umeme vijijini REA ambapo mkandarasi kutoka D’Salaam kaishawasili wilayani humo
Kanyasu amesema kuwa mara baada ya usambazaji umeme katika mji wa Rulenge na maeneo jirani atasambaza umeme huo kutoka mjini Ngara hadi Rusumo na kutoka Rusumo hadi K9 kuelekea mji wa Benaco na baadaye kata ya Mugoma.
“Rai yangu ni kwamba usambazaji wa  umeme wananchi wasikwamishe juhudi za serikali kwa kudai fidia kwenye maeneo zitakaposimikwa nguzo na kupitisha nyaya  badala yake watoe ushirikiano kwa wakandarasi”.Alisema Kanyasu
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha hawajengi kwenye hifadhi za barabara kuu zitakapopita nguzo na nyaya hizo na watumie nishati ya umeme kwa manufaa ya kukuza maendeleo na kuanzisha miradi ya ujasiliamali kujiongezea kipato
Aidha alisema Rais Kikwete alitoa ahadi ya kuondoa kero ya maji katika mji wa Ngara na vitongoji vyake na tayari Tsh.150 mil zimefikishwa katika idara ya mamlaka ya maji ili kununua mashine mbili na kufungwa kwenye chanzo cha maji
Alisema taasisi za serikali katika mji huo hasa polisi na magereza zinadaiwa ankra za maji zaidi ya Tsh.20mil hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha fedha hizo zinalipwa ili kuepuka kukwamisha uendeshaji na utoaji huduma kwa wateja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Hadson Bagege amesema miradi hiyo ya umeme na maji haina budi kusimamiwa kwa ukaribu kuepuka ubadhilifu wa fedha za serikali na kutoa huduma itakayoleta maslahi kwa jamii 
Wilaya ya Ngara ina jumla ya vijiji 72 na wananchi wanaopata nishati ya umeme wa mafuta ni walio katika mji wa Ngara kuelekea barabara kuu iendayo mji wa Kabanga kuelekea nchini Burundi
Ilielezwa kuwa  67 % ya wananchi wilayani humo wanapata huduma ya maji safi na salama hasa vijiji vilivyofanikiwa kupata miradi ya maji kupitia ufadhili wa benki ya dunia na 33% wanachota maji kwenye mito na visima
 NGARA: Na Shaaban Ndyamukama
Next Post Previous Post
Bukobawadau