SIKU 67 ZA MIPASHO,MATUSI BUNGENI
Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba linaahirishwa
leo baada ya kukutana kwa siku 67 bila kupitisha hata ibara moja kati ya
240 zilizomo katika Rasimu ya Katiba.
Badala yake Bunge hilo likiongozwa na Samuel Sitta
“Mzee wa Kasi na Viwango” linaahirishwa hadi Agosti, mwaka huu
likiendelea kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita zenye jumla ya Ibara 19,
zinazohusu masuala yanayojenga msingi wa aina ya Muungano
unaopendekezwa.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika rasimu
iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Joseph
Warioba ilipendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu, pendekezo
ambalo limeligawa Bunge hilo vipande viwili.
Kutokana na mgawanyiko huo, kauli zenye utata,
kejeli, matusi, dhihaka na ubaguzi ni mambo yaliyoshika hatamu katika
mjadala wa sura hizo mbili, huku viongozi wa Bunge; Sitta na Makamu
wake, Samia Suluhu Hassan wakilaumiwa kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.
Mwanzoni mwa wiki hii, Mjumbe wa Bunge hilo,
Ezekiah Oluoch alimshutumu Sitta kwamba ameshindwa kudhibiti nidhamu
katika Bunge na kwamba ndiye chanzo cha kuondoka kwa wajumbe wapatao 200
ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Mwenendo wa Bunge Maalumu ulikuwa na dalili zote
za kuonyesha kungetokea matatizo ndani yake kutokana na mipasho ambayo
ilikuwa ikitokea kwa wajumbe pamoja na lugha ambazo siyo za staha wakati
wa kutengeneza kanuni,” alisema Oluoch na kuongeza:
“Kwanza matumizi ya lugha zisizo na staha,
mwenyekiti anaruhusu wajumbe kuchangia hoja kwa kupeana mipasho bila
kujali hoja iliyopo mezani kinyume na kanuni,” alisema Olouch.
Hata hivyo, Suluhu alisema amekuwa akiendesha
Bunge hilo kwa umakini mkubwa na kwamba kila anaposikia lugha chafu
amekuwa akiwabana wajumbe kwa kuwaamuru kufuta kauli au kuomba radhi kwa
matamshi. “Sipendezwi na lugha chafu, kwa hiyo mojawapo ya mambo ambayo
huwa najitahidi kusikiliza kwa makini kila michango inapotolewa na
wajumbe bungeni ni kubaini kama wametumia lugha zisizostahili, kisha
kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni zetu,” alisema Suluhu.
Alikiri kwamba wapo baadhi ya wajumbe ambao
wamekuwa wakigoma au kukataa kuomba radhi na kwamba masuala yao
hupelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo ina mamlaka ya kuchukua hatua
zaidi kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo.
Matakwa ya Kanuni
Sehemu ya Tano ya Kanuni za Bunge Maalumu inatoa mwongozo wa mambo yanayokatazwa na yale yanayopaswa kufuatwa wakati wa mjadala.
Kanuni ya 46 imeorodhesha mambo yasiyoruhusiwa
ambayo ni pamoja na kusema uongo, kutoa taarifa zisizokuwa za kweli,
kuzungumza jambo lolote ambalo halipo kwenye mjadala na kutumia majina
ya marais na waasisi wa Taifa kwa dhihaka.
Pia inazuia matumizi ya lugha ya kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au
inayodhalilisha watu wengine, kuzomea, kupiga kelele za aina yoyote
zinazoweza kuvuruga mjadala au mwenendo bora wa shughuli za Bunge hilo.
Licha ya makatazo hayo, wajumbe wamekuwa wakikiuka
kanuni bila kuchukuliwa hatua na hali hiyo imekuwa chanzo cha mivutano,
zomeazomea, kelele na mambo mengine hadi kundi la Ukawa kususia kikao
wakieleza kutokuridhishwa na mwenendo wa Bunge.
Kuufyata na kuufyatua
Baadhi ya kauli tata zilizojitokeza ni pamoja na
ile iliyotolewa na Asha Bakari Makame kwa mjumbe mwenzake, Ismail Jussa
kuwa anafanana na watu wenye mabusha nyuma ambao ndiyo huufyata.
Makame ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake wa CCM (UWT), alikwenda mbali zaidi na kumwambia Jussa kuwa
ana matatizo ya kiafya na si mwanamume kamili, kwani ameshindwa kuoa na
hana watoto wakati ana umri mkubwa.
“Huyu Jussa anasema kwamba tumeufyata, hapa
tuwekane sawa, maana ya kuufyata ni mtu kuwa na mabusha pale yanapokuwa
nyuma ndiyo kuufyata kwa hiyo yeye ndiyo ameufyata, ana busha huyu,”
alisema Bakari.
Naye Profesa Ibrahim Lipumba alichafua hali ya
hewa pale alipowafananisha wajumbe wa Bunge Maalumu na kundi la mauaji
nchini Rwanda, Intarahamwe.
“Tumechoka kusikiliza matusi. “Tumechoka kudharau
mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la
Intarahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania hili hatulikubali.
Tunawaachia, watu wote tunaotaka Katiba ya wananchi tunawaachia
Intarahamwe mwendelee na Bunge lenu.”
Mjumbe mwingine ni Mwanakhamis Kassim Said
aliyesema: “Mimi nilikuwa namwomba baba yangu mdogo Seif (Maalim Seif
Sharif Hamad) awarejeshe watu wake humu (bungeni) kwa sababu mpira
unachezwa huku ndani. Hatutakii mema humu, tena ana choyo na husuda.
Namwomba baba mdogo atuache, alichokitaka amekipata, king’ora anazunguka
saa 24 Dar es Salaam, Unguja. Mheshimiwa Mwenyekiti Baba mdogo kila
mara yuko kwenye pipa (ndege) mara Uingereza, mara Canada mara wapi?
Hicho ndicho anachokitaka amekipata.”
Mjumbe mwingine, Mohamed Seif Khatibu alisema:
“Nimejifunza kuwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani ni vinyonga. Lakini
Maalim Seif ni kinyonga, wakipita kwenye mvua wanakuwa na rangi ya mvua,
kwenye jua wanakuwa na rangi ya jua, baharini wanakuwa na rangi ya
bahari.”
Tuhuma za rushwa
Mjumbe Ezekiah Wenje alisema baadhi ya mawaziri
wamewahonga wajumbe wa kundi la 201 ili waunge mkono msimamo wao, lakini
alipotakiwa kufuta kauli hiyo alikataa na suala lake kufikishwa kwenye
kamati ya kanuni.
“Kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako
walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku, wengine walikwenda kwa
Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na
kupewa bahasha.”
Kuingia msituni
Kapteni John Komba alitangaza kuingia msituni
iwapo Bunge Maalumu la Katiba litapitisha muundo wa serikali tatu, huku
akimshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba na timu yake ni waasi kama Adamu na Eva waliomuasi Mungu
kutokana na kile walichokifanya cha kupendekeza serikali tatu. Mwingine
katika orodha ni Bernard Membe aliyesema, Tume ya Mzee Warioba itakuja
kukumbukwa kwa kuratibu mauaji ya Muungano na Bunge nalo litakuja
kulaaniwa kwa kubariki mauaji hayo.
Watoto wa shetani
Mjumbe Paul Makonda alisema: “Shetani alikuja
duniani kuiharibu dunia, kuiangamiza na kuteketeza kila kilichostahili
kuungana… watoto wake ni Mheshimiwa Jussa, watoto wake ni Mheshimiwa
Mbowe, watoto wake ni Mheshimiwa Lipumba… Hawa ni watoto wa shetani”.
Mwingine: Waride Bakari Jabu alisema: “Chiku Abwao
mimi namshangaa sana anayesema bora Muungano uvunjike lakini Tanganyika
iwepo. Tunafahamu asili yake mwenyewe ni Mkongo mumewe ndiye
Mtanganyika, namwambia Muungano huu utakuwepo na utaendelea kuwapo.”
Mjumbe Tundu Lissu alisema: “Tanganyika haikuuawa
na makubaliano ya Muungano, bali iliuawa kwa amri za Nyerere…. Mwalimu
Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote ya kikatiba ya kutunga amri na kuua
Tanganyika.”
Imeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema, Sharon Sauwa na Beatrice Moses