Bukobawadau

TASWIRA WAWINDAJI WA ASILI NA SAYANSI YAKUTENGENEZA POMBE ASILIA ZA WAHAYA: LUBISI NA ENKONYAGI.

Muonekano wa wawindaji wakiwa wanafurahi kwa kunywa pombe za asili  (Olubisi)
Hivi ndivyo walivyokutwa na Camera yetu kijijini Buganguzi siku chache zilizopita
 SAYANSI NA UFUNDI WA KUTENGENEZA POMBE  ASILIA  ZA WAHAYA:
LUBISI NA ENKONYAGI.
         Kabila la Wahaya, ni moja ya makabila zaidi ya 120 yanayoishi ndani ya mipaka ya nchi yetu ya Tanzania. Kama yalivyo makabila mengine yote, kabila la Wahaya limekamilika kwa mila, desturi na utamaduni wake. Sayansi na ufundi (obubuya) wa kutengeneza pombe zake za jadi, ni miongoni mwa tunu za utamaduni huo wa Wahaya.
Wahaya wanazo aina mbili maarufu za pombe (amalwa), achilia mbali aina nyingine ambazo kabila hilo limezipokea na kuzitohoa katika mihula mbalimbali ya kihistoria, kutokana na maingiliano yake na makabila mengine.
 Maandalizi ya kutengeneza pombe ya asili ya wahaya aina ya Lubisi 
Lubisi, ndiyo pombe inayokubalika kuwa ya asili zaidi ya Wahaya. Pombe hii inasadikiwa ‘kuingia’ Mkoani Kagera hata kabla ya kuhamia kwa utawala wa Wahinda, wakitokea pande za Bunyoro na Ankole, nchini Uganda, kupitia Karagwe, mnamo karne ya 16. Hata hivyo, koo (enganda) za awali za Wabantu zilizowatangulia Wahinda kukalia maeneo ya Buhaya (Bantu Bairu, Bantu Basiita, n.k.), zilijihusisha zaidi na kilimo cha mazao ya nafaka (hasa ulezi na mtama) na viazi (viazi vitamu na viazi vikuu).
Kilimo cha migomba (engemu), kilishamiri na kuenea zaidi katika nchi ya Wahaya (Buhaya) baada ya ujio wa Wahinda, kwani samadi (obusha) ya ng’ombe walioletwa na wahamiaji hao wapya, ilisaidia sana kurutubisha mashamba (ebibanja) na kuwezesha uzalishaji wa ndizi (ebitoke) kwa wingi, kwa ajili ya chakula cha uhakika na kwa matumizi ya shughuli nyingine za kijamii na kiutamaduni, hususan sherehe za kimila za arusi, matambiko, ujenzi wa mahusiano na mijumuiko ya kijamii.
Isitoshe, lubisi ni pombe iliyopendwa na watu wa tabaka la watawala (Wahinda), jambo ambalo tunaweza kulithibitisha kwa kubainisha kwamba licha ya itkadi za ubaguzi wa kitabaka zilizojengeka enzi zile, hata mfalme (omukama), wakati akiwa katika ziara zake za kutembelea himaya yake, hakuchelea kuingia kwa mtwana (omwilu) yeyote (aliyekuwa amegema pombe siku husika) kupoza kiu yake. 
 Aidha, methali (omugani) moja ya Kihaya isemayo gajungwa enkunami ganyoobwa enyesiige, inatufundisha jinsi pombe ilivyo na uwezo wa kuondoa mipaka ya hisia za kibaguzi na kudharauliana baina ya watu wanaotofautiana kwa hali na mali.  
 Isitoshe, raia watwana walitakiwa kuandaa na kupeleka Ikulu (ekikaale) ya mfalme vibuyu vya pombe, kama zawadi ya heshima kwa mfalme na wasaidizi wake wakuu (the nobility). Kitendo hicho cha watwana kujinyenyekeza kwa watawala kilijulikana kama okukulata. Moja ya methali za Kihaya, kama tutakavyoona baadaye, hudai kwamba Atakulata, ati “Omukama tagaba”, kwa maana kwamba mtu ambaye haendagi Ikulu kuwasilisha zawadi za heshima, husingizia kwamba eti “Mfalme ni bahili”.   
Inasadikika kwamba, mbali na ushujaa vitani, ‘kuwasilisha’ ilikuwa miongoni mwa sifa nyingine alizohitaji kuwa nazo raia mtwana ili aweze kumshawishi Mfalme kumgawia shamba, n’gombe au hata mke.  
Kwa vile, mtama mwekundu (omugusha) ndio hasa mali ghafi kuu itumikayo kuchachulia togwa au juisi (omulamba) itokanayo na kusindikwa kwa ndizi kali (enkundi) na kuigeuza kilevi cha lubisi, hatuwezi kuwa mbali na ukweli kufikiri kwamba ni kuanzia enzi hizo za karne ya 16, pombe ya lubisi ilipoenea na kujiimarisha kama kinywaji cha heshima kuu na burudani miongoni mwa Wahaya.
Ili kutengeneza lubisi, ndizi kali zilizokomaa, hukatwa na kulundikwa ‘darini’ mwa nyumba (‘omushonge’, hasa, ndiyo nyumba ya kiasili ya Wahaya) juu ya eneo la meko. Kwa msaada wa joto na moshi wa mekoni, ndizi hizo, baada ya wiki moja hivi,  huweza kuwa zimeiva sawa sawa, na kuwa tayari kukamuliwa ili kupata omulamba wa  kutengenezea lubisi. Lakini ilikuwapo njia nyingine tofauti ya kufanya hivyo: kuzivundika (kwalika) ndizi hizo shimoni (omulwina) na kwa kipindi kama hicho, kuzipasha joto humo humo shimoni kwa ufundi maalum.
Kwa kawaida, mchakato wa kusindika ndizi mbivu (ebiise) ili kuzalisha togwa (ambalo huchachuliwa kwa siku tatu kuzalisha lubisi),  huanza  kwa kutayarisha mitumbwi miwili -  ‘amato gabili’. ‘Mtumbwi’ mmoja unaotambuliwa kama eijungilo, ndiyo hasa hutumika kusindika  ndizi mbivu ili kupata togwa. Kama tutakavyoona, kazi ya usindikaji au ukanyagaji (okujunga) hufanywa na vijana kwa miguu.
‘Mtumbwi’ wa pili (eibetelezo), hutumika kuchachulia togwa iliyopatikana kwa usindikaji ulioelezwa. ‘Mitumbwi’ yote husika, huchongwa kutokana na magogo makubwa ya aina ya miti laini, ambayo hukombwa ‘nyama’ ya ndani na kubaki wazi kwa upande wa juu. Aina hizo za ‘mitumbwi’, licha ya matumizi yake kutofautiana, hufanana kwa sura. Omujuju na omulinzi, ni miongoni mwa aina maarufu za miti ifaayo kwa uchongaji wa ‘mitumbwi’ na vinu (ebitwangilo)
 Ndizi mbivu (ebiise), zikiwa zimepopolewa (kuogolwa) kutoka kwenye mikungu yake, hujazwa ndani ya eijungilo na kufunikwa kwa aina ya nyasi (eijungyo) zilizokatwa fupifupi,  zikakanyagwa na kuchanganywa kiustadi kwa miguu ili  kutoa togwa ambalo huwa tamu kama sukari. Nyasi maarufu zifaazo kwa eijungyo, ni pamoja na egunga, eshoju, ehunda  na hata eshanje.
Kijadi,  ukataji wa nyasi mbugani,  ni kazi ya wanawake. Lakini ilikuwa ni mwiko usindikaji wa ndizi mbivu kufanywa na wanawake, kwani ni vigumu kujiridhisha kuwa hawako katika siku zao za kijinsia, jambo lililokuwa ni mwiko!
Na pale uivishaji wa ndizi uwapo umepitiliza kiwango na mchanganyiko kuwa lojolojo sana (kukooka), matunda pori ya enzilo mbichi hutwangwa katika kinu na kumiminwa katika mchanganyiko huo, kama ‘dawa’ ya ‘kutibu’ mtafaruku uliojitokeza. Aghalabu, hufanyika pia zindiko dhidi ya mashambulizi na usumbufu wa nyuki wakali, ambao hutokea wakazusha kero hatarishi katika eneo la shughuli, wakiwa katika harakati zao za kusaka chakula chao.  
Katika hatua mbalimbali za mchakato wa kukamua togwa, eijungilo huinuliwa upande mmoja ili togwa litiririke na kujikusanya upande wa chini, ambapo huchotwa (kutawa) kwa kata (omutao) na kuhifadhiwa, kwa muda, katika vibuyu vikubwa (ebishusi). Ebishusi sasa vimetoweka, vikiwa vimepata mbadala wa madumu ya plastiki kutoka viwandani (keni). Vifaa vingine vilivyotoweka, ni pamoja na ebilele, obugwi na emiitizo (chujio).
Kwa kawaida, ‘omulamba’ huwa katika gredi tatu zinazotofautiana kwa wingi na ubora. Kundi la kwanza hujulikana kama omunene. Hii ni togwa au juisi safi na tamu kama sukari au asali isiyochanganywa na maji yoyote. Gredi hii ya lubisi, hutengwa na kuchachuliwa katika vibuyu maalum, na baadaye huzawadiwa (kutangililwa) kwa wageni mashuhuri wanaotembelea kwa mgema.
Gredi ya pili ya togwa, hujulikana kama omushaju. Hii hasa ndiyo togwa itumikayo kuandaa olubisi halisi. Omushaju huongezewa maji kiasi cha kutosha ili ipatikane pombe kiasi cha kukidhi malengo ya mgemaji, kwa kuzingatia idadi ya wanywaji wa omulamba kwa ajili ya kukata kiu ya kawaida na wengine wanaotarajiwa kufika kushiriki sherehe ya unywaji wa pombe hiyo. 
 Vivyo hivyo, katika sherehe za mipango ya harusi, kwa mfano, wingi wa pombe inayotengenezwa, huzingatia viwango vya  vipengele husika vya mahali inayotozwa, kwa mujibu wa mila, kwa muda unaokuwepo.
Uchachuaji na uivishaji wa omushaju, huwezekana kwa omushaju kuchanganywa na omugusha (uliokaangwa na kusagwa kidogo). Hatua hii ya mchakato, hutendeka katika eibetelezo katika kipindi cha siku tatu. Katika siku hizo,  uchachuaji hukamilishwa kwa kulipasha joto eibetelezo, kwa moto wa mkaa au kuni uliokokwa mekoni, jirani na eibetelezo. (Kwa vile Omushaju hupatikana kwa kuongezewa maji mengi kiasi, utamu wake huwa ni wa wastani tu, tofauti na omunene).
Entabani ni  gredi ya tatu na ya mwisho, kwa ubora na thamani. Togwa hii hupatikana kwa kuongeza maji mengi zaidi katika mchanganyiko. Kitendo hicho, hupunguza sana utamu na ladha yake, kwa kulinganisha na gredi nyingine zilizotangulia: omunene na omushaju.
 Kama tutakavyoona baadaye, entabani (ambayo ndiyo huchemshwa na kuzalisha enkonyagi) ilisaidia sana kuinua pato la Wahaya wengi na kupunguza umasikini vijijini. Kwa pato lililotokana na mauzo ya  enkonyagi, wazazi wengi waliweza kuwalipia karo watoto wao shuleni. Na haipingiki hata kidogo kwamba wapo wasomi wengi wa Kihaya, ambao wasingalisonga mbele katika safari yao ya kusaka elimu, bila msaada wa mapato hayo. Kwa lugha ya Misahafu, basi, entabani inaweza kumithilishwa na jiwe lililopuuzwa na waashi, lakini likatokea baadaye kuwa jiwe kuu la pembeni. Waswahili husema: ‘hawavumi, lakini wapo’.
  Baada ya mchakato wa usindikaji kukamilika, mabaki makavu (ebikamulo) huondolewa na kutupwa shambani ili kutumika kama mbolea, ikihakikishwa kwamba yanawekwa kwenye mashina ya viazi vikuu vya aina ya amakongo na kashuli.
Kama tulivyokwishaona, Eibetelezo ni ‘mtumbwi’ ule wa pili unaotumika kwa ‘kemia’ ya uchachuzi. ‘Mtumbwi’ huo wenye togwa  inayofanyiwa uchachuzi, hauachwi wazi, bali hurembwa na kufunikwa kwa makuti ya migomba (okushembwa).
Na siku ya pili jioni, wazee wenye heshima, hususan kutoka ndani ya ukoo wa mgema au majirani zake, hufika pale nyumbani kwake kwa tukio muhimu la kuonja (kuloza) na, baada ya kila mmoja wao kugawiwa sampuli ya pombe husika na kupiga mafunda machache, hutoa ithibati au ‘hukumu’ yake kama pombe ile ilikuwa tayari imeiva na kukolea sawasawa au la.
Nikiwa bado mtoto mnamo miaka ya 1960, niliweza kushuhudia wazee vikongwe wakiimung’unya (kujubata/kubuuta) pombe ile vinywani mwao na kuitafakari kwa makini kwa muda, kabla ya kuitolea tathmini na maoni, kulingana na vigezo vya ubora vinavyotambulika na wazee wenyewe wa Kihaya.  
Katika hatua hii, ile  iliyoitwa  emize (maradhi au mapungufu ya lubisi ile ) iliwekwa bayana, na ‘matibabu’ yake kutajwa. Kama mapungufu hayo yatahusishwa, kwa mfano, na joto hafifu lisilowezesha uchachuzi kufikia kiwango cha kuridhisha, mgema hushauriwa kukoleza (okuembela) zaidi ule moto unaokokwa jirani na eibetelezo, hata ikibidi usiku kucha.
Aidha, kama tatizo ni uchache wa mtama (omugusha) uliowekwa ndani ya eibetelezo, mgema hushauriwa kuongeza mtama (kama upo) ili kuchochea kasi ya uchachuzi. Lakini wazee wakiridhika kwamba pombe ile ilikuwa imekidhi viwango vya ubora na ukali,  wote (kwa sauti moja)   humpongeza mgema kwa furaha na faraja: “Kihembo, waitu!”. Naye mgema aliyesifiwa na kupongezwa, huitikia kwa majivuno na furaha ya wazi: Kihembo kya malwa, waitu.
Siku inayofuata, huwa ni ya pekee pale nyumbani kwa mgema na maeneo jirani kwa jumla. Tangu asubuhi na mapema, watu mbalimbali, hasa wanaume wa umri wa utu uzima (majirani, wanaukoo, jamaa, marafiki wa karibu na hata kutoka mbali- enkungu), wakiwa wameshikilia mkononi vibuyu ebilele)  vyao vyenye mirija (ebisheke) ndani kwa kufyonzea, huwasili nyumbani kwa mgema kushiriki sherehe ya unywaji wa pombe ile. Nyumba hujaa watu pomoni, wakinywa, wakifurahi na kusherehekea. Wakati wote huonekana wakibadilishana habari na kutaniana.
Kipindi chote cha kukaa kwao, mgema huhakikisha hakuna mtu anayetindikiwa kinywaji. Lilikuwa ni jambo la kawaida kwa mtu mwenye kilele chake kujaziwa (kutekelwa) hata mara mbili au zaidi. Na bado angaliweza kurudi tena kwa mgawo zaidi siku hiyo baadaye au hata kesho yake.
Watu wengine huitumia fursa hiyo adhimu kufunga mikataba ya urafiki, ikiwa ni pamoja na kuliana yamini (kunywana). Inaelezwa kwamba zamani zaidi, wazee waliweza hata kutangaza uamuzi wa kuwaoza mabinti zao kwa maswahiba wao au watoto wao.
Aidha, nilipata kushuhudia katika vikao hivyo vya unywaji, (ebinywi) malumbano makali lakini yenye amani, yakiibuka na kuzua ubishi juu ya mambo ya siasa, sera na utawala wa nchi. Isitoshe, wananchi (abanyansi) wenye umri mkubwa, waliweza kutumia nafasi hiyo kubadilishana mawazo juu ya kero mbalimbali zinazoikabili jamii yao ( kama vile magonjwa hatarishi ya binadamu na mifugo, athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa mazingira, n.k.) Changamoto za kiuchumi na umasikini nazo ziliweza kugusiwa kwa viwango mbalimbali vya uelewa na uchambuzi.
 Katika mikusanyiko ya kijamii niliyowahi kushuhudia katika nyakati mbalimbali, vikao vya sherehe za pombe vilinivutia kama vikao shirikishi zaidi, kwa maana ya kutoa fursa kwa wananchi wanaofahamiana na kuhusiana, kujadili mambo yao ya siku hadi siku, kwa uwazi na ukweli - bila dharau, kebehi wala kejeli za kibabe.
Hata hivyo, hutokea (japo mara chache) watu kusigana na kupimana nguvu. Ilitokea watu waliokwaruzana, wakatiana ngeu na  kusababishiana majeraha hatarishi mwilini (kutemangana embale). Ndio maana ni kawaida ya Wahaya, siku chache baada ya sherehe mbalimbali, kuwajulia hali jamaa zao kwa kauli: Buhole? Au kuwapongeza kwa maneno:Waitu mwaihuka.
Lakini kwa bahati nzuri, mitafaruku mingi kama hiyo, ilisuluhishwa na kudhibitiwa na wazee kabla haijalipuka na kusababisha madhara makubwa zaidi. Ndiyo mantiki ya msemo kwamba ‘penye wengi, hasa wazee, hapaharibiki neno’.
Hata wanawake na watoto (ambao kwa kawaida ushiriki wao katika sherehe za kijamii huwa ni dhaifu) nao hawakukosa kufaidi matunda ya jasho lao katika hatua mbalimbali za maandalizi ya pombe zile.  Wanawake, kwa mfano, ndio hushiriki  kuteka maji ambayo huhitajika kwa wingi katika shughuli nzima. Ni wanawake na wasichana ambao hukata nyasi za eijungyo, kukaanga na kusaga mtama (omugusha) unaotumika kuchachua togwa, n.k. Watoto nao hushiriki kusomba vichwani mikungu ya enkundi kutoka shamba la nyumbani  au hata kwa jamaa, marafiki wa familia na majirani kijijini. Watoto pia huteka maji kutoka mtoni. Watoto hufurahiandizi mbivu za obushukari na ebijoge.
  Vijana, licha ya majukumu mengine, ndio huhusika zaidi  na kazi ngumu ya kukamua togwa (kwa kutumia miguu yao), katika ile mitumbwi ya eijungilo.  Kazi hii nzito ya kujunga huhitaji nguvukazi ambayo ni vijana wanaoweza kuimudu zaidi, kwani hujumuisha pia ubebaji wa vibuyu vya maji na togwa. Usafirishaji wa ‘mitumbwi’ (amaato) mizito nao huwategemea vijana.
 Isitoshe, shughuli nzima ya usindikaji wa ndizi, hufanyika chini ya uangalizi  mkali wa wazee na wazazi husika. Wakati mwingine, hali hiyo humaanisha hata kijana ndani ya ‘mtumbwi’ kutiwa adabu kwa kipigo cha mkongojo wa kutembelea (oluguma) pale mzee aonapo dalili zozote za kuzembea kazi.
Tusisahau pia kwamba miaka ya nyuma, kijana aliweza, ghafla na wakati wowote (hata alfajiri),  kuamriwa na baba yake au mlezi wake kwenda kwa mzee mwingine yeyote swahiba kijijini kutoa nguvukazi ya ukamuaji  (okujunga). Visingizio na ubishi, kwa upande wa vijana, havikuwa na nafasi! Zilikuwa bado ni enzi ambapo vijana na watoto vijijini waliwajibika kwa wazee wote. Kwabahatimbaya, hilo limetoweka sasa!
Wanawake na watoto, kama tulivyoona, walifaidi kwa kutafuna ndizi mbivu za aina ya obushukari na ebijoge, ambazo hupendwa kwa utamu na ladha yake ya sukari. Waliweza pia kufakamia togwa (omulamba) kadiri ya haja zao za kiu, hadi kudhihakiwa kwa misemo kama vile: haka akana akabunda, oti omwabo bajunga. Watoto pia  walitafuna mabaki au ‘machicha’ ya mtama (enkanja). Machicha hayo yanasemekana kufaa kwa matatizo ya matumbo, ingawa yakiliwa kwa wingi, huweza kuwalewesha watoto na vijana wa umri mdogo.
 Mila na desturi nyingi za Wahaya zilizoendana na lubisi, leo hii zinatoweka kwa kasi. Kwa mfano, enzi zile lilikuwa ni jambo muhimu kwa mgema kuonyesha ukarimu usiobagua au kutilia mashaka, ili kuimarisha kiwango cha mhusika na kaya yake kukubalika na kuheshimiwa katika jamii. Kufifia kwa mila hii kumechochewa na kuibuka na kukua kwa uchumi wa fedha na mfumo wa maisha ya kibiashara, ambapo sasa ni nadra kuona bidhaa yoyote ya thamani ikitolewa kwa mtu yeyote bila malipo. Jambo hili linashadidiwa zaidi na msemo kwamba ‘hizi ni enzi za Kyakaela; Byabusha alifariki siku nyingi’.      
Hebu sasa tuhitimishe maelezo haya kwa kugusia kidogo aina nyingine ya pombe maarufu miongoni mwa Wahaya – enkonyagi. Enkonyagi, kama jina lake linavyodhihirisha, ni konyagi asilia ya Wahaya. Ni gongo. Na hivyo, kwa mtazamo wa serikali na sheria zake, ni pombe haramu, isiyotofautiana na bangi au madawa ya kulevya. Lakini kwa ushuhuda wetu halisi, baadhi yetu hatuna budi kukiri kwamba ni pombe iliyowatoa mbali Wahaya, kiuchumi na kijamii. 
 Konyagi hii hupatikana kwa njia na utaratibu mwingine wa kisayansi, ambapo lubisi huchemshwa, na mvuke wake kukusanywa kwa njia ya kimaabara (condensation). Kiasi fulani cha pombe hiyo, hujazwa katika debe lililotengenezwa kiwandani kwa madini ya  aluminium au tin. Jambo hili linashadidia kwamba utengenezaji wa pombe hii hauwezi kuwa na historia inayokwenda kabla ya ukoloni barani Afrika.
Kijadi, debe lililojazwa (kiasi) lubisi ndani, huinjikwa juu ya mafiga matatu mekoni, na moto hukokwa kwa kutumia mkaa au kuni. Katika sehemu ya juu ya debe hilo, huchomoza bomba la mti (omusheke) linaloingia kwenye mtungi (ekimuga) uliokalishwa ndani ya karai lenye maji. Mtungi huo humwagiliwa maji (kusheshela) kila unapoonekana kukauka au kupauka. Na kila mara mtungi unaponyunyiziwa maji, kete fulani (empiki) hutengwa kando. Idadi maalum ya kete inapofikiwa, shughuli ya uchocheaji moto husitishwa na mtungi huipuliwa mekoni (kutelulwa) ili enkonyagi iliyopatikana, iweze kumiminwa katika chupa kwa kuhifadhiwa au kutumiwa.
Muda mrefu unaotumika kwa zoezi hili, humaanisha enkonyagi itakayopatikana ndani ya mtungi, itakuwa nyingi, lakini isiyokuwa kali sana. Kwa mantiki hiyo, enkonyagi kali hupatikana pale zinapotumika kete chache zaidi, kwa maana ya muda mfupi uliotumika kwa uchemshaji.    
Katika miaka ya karibuni, enkonyagi  imekuwa ‘ikitengenezewa’ zaidi karibu na mito, ambapo mtungi huzamishwa ndani ya maji yanayotiririka kila wakati. Maji hayo ya mto, ndiyo hutumika kupoza mvuke (olwohya) unaotokea kwenye debe, baada ya lubisi ndani yake kuanza kuchemka.  Kwa kemia ya condensation tuliyoieleza hapo juu, ubaridi wa maji huufanya mvuke ubadilike kuwa kimiminika. Na hicho kimiminika ndani ya mtungi ndiyo enkonyagi yenyewe.
Sina hakika na jinsi muda unavyopangwa au kukokotolewa  kwa kutumia utaratibu huu mpya wa upatikanaji wa kilevi hiki mtoni.  Nimesikia ikisemwa kwamba katika mazingira ya shughuli hii kufanyika mitoni, muda sasa unahesabiwa kwa kutumia saa. Nimesikia pia kwamba badala ya madebe, siku hizi vyombo vya chuma vyenye ujazo mkubwa zaidi, hususan mapipa ya chuma, ndiyo yanayotumika kuchemshia lubisi, lengo kuu likiwa ni kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya enkonyagi kama zao la kibiashara.  Yote haya ni mabadiliko makubwa kiuchumi na kiteknolojia katika uzalishaji wa pombe asilia za Wahaya.   
Utengenezaji wa enkonyagi, japo unaweza kufanywa na mtu yeyote  wengi huko vijijini, bado unahitaji uangalifu mkubwa. Bila kuziba nyufa na kudhibiti mianya ya hatari, mtambo wa kutengeneza pombe hiyo unaweza kuvuja na kulipuka; na hilo likitokea, huweza kusababisha madhara kwa mtu anayehusika, au wale walio karibu na eneo la shughuli. Mbali na kulipuka, tahadhali za kiufundi zisipochukuliwa kudhibiti viwango vya moto, pombe inayochemka katika debe, inaweza ‘kufoka’ (kuletelana) na kuingia katika bomba la kusafirisha mvuke, na hatimaye nayo ikachanganyika na kimiminika ndani ya mtungi.
Zaidi ya takribani miongo mitatu sasa, enkonyagi  imepata thamani kubwa kutokana na kupendwa na watu wengi zaidi, wazee kwa vijana - pengine zaidi ya lubisi (ambao ndio chimbuko na mali ghafi yake). Hii ni kwa sababu ukali wake, hupelekea wanywaji kulewa (kutamiira) na kufikia malengo yao mapema. Kwa mfano, kijana aliyekusudia kupata ridhaa ya penzi la mwana dada, hataangaika kumnunulia lubisi mama huyo, kwani, kwa kinywaji hicho, itamchukua mwanamke muda mrefu sana kupandisha hisia na kufikia uamuzi wa kukidhi haja za kijana. Kinyume chake, kitu ‘kitaeleweka’ mapema zaidi iwapo kijana atakuwa tayari kugharamika zaidi, kwa kumnunulia mrembo wake kilevi kikali zaidi cha konyagi asilia
Tunadiriki kusema kwa uhakika kwamba enkonyagi leo ndicho kinywaji kilichoshika chati miongoni mwa Wahaya. Hata hivyo, tofauti na lubisi kihistoria, enkonyagi sio kinywaji cha sherehe, wala sio kinywaji cha wote. Kwa miaka mingi sasa, tangu miaka ya 1960, enkonyagi imeendelea kuwa kinywaji cha biashara, ikiwa inaelekea kushika nafasi ya pili katika orodha ya vyanzo vya mapato, nyuma tu ya kahawa.  Ni muhimu kutambua kwamba, wanyonge wengi kiuchumi, hasa wanawake, wameweza kujikomboa kutokana na biashara ya kuuza enkonyagi.
 Lakini kwa bahati mbaya, serikali imeendelea kukinunia kinywaji hiki, licha ya mapendekezo yenye nia njema, ambayo yamekuwa yakitolewa kwamba wakati umefika kukihalalisha na kukiboresha, kwa njia za kisasa, kinywaji cha gongo, kwa manufaa ya watengenezaji na wanywaji wake. Nchi kama Uganda zinasemekana kuanza kufanya hivyo.
Lakini baadhi yetu na watu wa dini, tutaendelea kukiangalia kilevi hiki kwa ‘jicho la kona’, tukichelea mchango wake hasi kama kichocheo cha ‘ngono - zembe’, uzinzi na uasherati, tabia zinazopelekea vifo vya vijana wetu wengi, kutokana na gonjwa hatari la UKIMWI (Obutagambilwa).
Stori Na Festo  Mukerebe Via Bukobawadau
Next Post Previous Post
Bukobawadau