TUSIACHE ULAZALENDO WA LEMBELI USAKAMWE NA WANAMAKUNDI
Na Prudence Karugendo
JAMES Lembeli ni mbunge wa Kahama kupitia chama
tawala, CCM. Lakini uanachama wake kwa chama hicho haumvui uzalendo wake kwa
nchi yake wala mapenzi yake kwa wananchi wenzake. Hataki kuutumia uanachama huo kuwaona
wananchi wengine wasiokuwa wanachama wa chama chake kama maadui zake. Vilevile
hataki kuutumia uanachama huo kuitelekeza nchi yake.
Lembeli
kajiweka wazi kuwa anauvua umakundi wote, u CCM na utetezi wa kundi la wana
Kahama, na badala yake kuuvaa uzalendo wa nchi
linapokuja suala la kuitetea na kuihami nchi yake. Huo ni uzalendo
uliotukuka kwa nchi.
Katika hilo
Lembeli hana u CCM wala u Kahama, anabaki na kundi moja tu, nalo ni kundi la
wananchi ambalo anataka liidai nchi yao ya Tanganyika.
Ikumbukwe
kwamba uzalendo katika umakundi ni adui mkubwa wa uzalendo katika nchi.
Wananchi hawawezi wakazama kwenye uzalendo wa kamundi yao wakaukumbuka tena
uzalendo wa nchi yao. Mfano hai ndio huu ambapo baadhi ya wananchi wanakiona
kikundi chao ndicho bora kuliko kila kitu. Kikundi chao kinaikana nchi yao,
hakitaki hata kulisikia jina la nchi yao wao wanashangilia!
Wanausimamia
msimamo wa kikundi chao mpaka kufikia kulionea kinyaa jina la nchi yao na
kubaki wakilitukuza jina la kikundi chao, ambacho ni kikundi kidogo tu cha
wananchi!
Fikiria nchi
iliyo na idadi ya watu wanaokaribia milioni 50, watu wazima kwa watoto,
vikongwe kwa walemavu nakadhalika, eti matakwa yao yatawaliwe na kikundi cha
watu wasiofikia hata milioni 5 kikijiona ndicho pekee chenye maamuzi juu ya mamilioni ya watu hao wote!
Tukiangalia
kwenye historia tutaona kwamba umakundi ulijionyesha tangu zamani kuwa ni adui
wa uzalendo. Ndio maana wakoloni walibuni mbinu ya kuwagawanya wananchi katika
makundi na kuyajengea uhasama kati ya kundi moja na lingine kusudi makundi hayo
yasielewane na ikibidi yaishie kwenye ugomvi.
Mbinu hiyo
ya wakoloni iliyopata umaarufu kama “divide and rule” gawanya utawale, iliwasahaulisha wananchi uzalendo kwa nchi
zao, na badala yake wananchi wakauhamishia uzalendo wao kwenye makundi ambayo
lakini hayakuwasumbua wakoloni zaidi ya wananchi kupigana wenyewe kwa wenyewe
huku wakoloni wakitawala bila misukosuko yoyote!
Kwa
kulitambua hilo, Lembeli akatamka bila woga wala unafiki, kwamba yeye ni
Tanganyika kwanza mengine baadaye. Uzalendo huo wa Lembeli ni tofauti na
msimamo wa chama chake kilichozama kwenye umakundi zaidi kikiwa kimeusahau
uzalendo pembeni.
Hapo ndipo
Lembeli akatoka na kauli ya kwamba CCM siyo mama yake, kauli iliyowahi kutolewa
na muasisi wa chama hicho, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Tafsiri ya
neno hilo iko wazi. Ni kwamba CCM ni kikundi kilichoasisiwa na watu, kwahiyo
kujiunga au kuachana nacho ni ihari ya mtu kwa kutegemea anavyouona mwenendo wa
kikundi hicho.
Kikundi
hicho hakijamuumba wala kumzaa mtu yeyote. Mtu anaweza akajiunga na kikundi
hicho akiwa anaelewa kwamba wazazi wake, au mabibi na mababu zake hawakuwa
kwenye kikundi hicho, na pengine wengine
hawakukijua kwa vile hakikuwepo enzi hizo.
Hiyo ni
tofauti na nchi ambayo mtu kazaliwa na kukuta wazazi wake na mababu zake wana
asili ya nchi ileile. Hivyo kuyaondoa mapenzi kwa kikundi na kuyaweka kwa nchi
ni jambo linaloweza kuwashangaza tu watu
wenye matatizo ya kimtazamo.
Baada ya
kauli ya Lembeli ya kwamba CCM siyo mama yake
wakazuka wapambe wa chama hicho, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga,
Khamis Mgeja, mjumbe wa NEC ya CCM, Boniface Butondo, Katibu wa CCM mkoa wa
Shinyanga, Adam Ngalawa na Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Shinyanga, Emmanuel
Mlimandago, wakidai kwamba Lembeli kakidhalilisha chama chao!
Watu hao hawasemi
Lembeli kakidhalilisha vipi chama chao. Kusema CCM siyo mama yake! Hivi kweli
wapambe hao wanaweza wakatuhakikishia kuwa CCM ndiyo iliyobeba mimba ya Lembeli
kwa miezi tisa? Kama hawawezi kufanya hivyo basi waelewe kuwa wao ndio
wamemdhalilisha yeye na wawe tayari kumuomba radhi.
Katibu wa
CCM mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Mlimandago, anadai kwamba Lembeli
anajifananisha na Baba wa Taifa, sijui anajifananisha naye kwa lipi! Sababu
hakuna mahali ambako Lembeli alitamka kwamba kwa sasa anaongea kama Nyerere.
Isipokuwa
hizo ni hisia tu za Mlimandago za kumsikia Lembeli akitoa kauli ambayo CCM
ilishindwa kuipiku tangu enzi za Nyerere. Leo hii ndipo anasema Lembeli
kajifananisha na Nyerere!
Pengine
ninachoweza kukiona ni kwamba Lembeli kaufuata uzalendo wa Nyerere, kwa hilo
kuna kosa gani? Nyerere kama muasisi wa Tanganyika, sidhani kama kuna kosa
iwapo wananchi wote wakiamua kufuata nyayo zake. Hapo Mlimandago kachemsha.
Na kwa
taarifa yake, Mlimandago, ni kwamba kauli hiyo Nyerere aliitoa kwa waandishi wa
habari, kama alivyofanya Lembeli,
tofauti na anavyofikiria yeye kwamba Nyerere aliitolea kwenye vikao vya CCM.
Pengine ingebidi tumfahamishe ni wapi na wakati gani Nyerere alitamka kwamba
CCM siyo mama yake.
Ila sitaki
tumpe faida ya kutekeleza majukumu yake anayoonekana kuyatekeleza kwa
kuyumbayumba.
Wapambe hao
wa CCM wanasema kwamba Lembeli atambue kwamba umaarufu wake alionao umetokana
na CCM! Kwamba kabla ya mwaka 2005 hapakuwepo Watanzania waliomjua na waliomfahamu kama ilivyo sasa!
Hiyo ni
kauli ya ajabu lakini iliyozoeleka katika chama hicho. Sababu haina maana
kwamba Lembeli kazaliwa mwaka huo wanaoutaja. Lembeli alikuwepo na wenye kumjua
tulimjua. Juhudi zake ndizo zilizowafanya CCM wamtamani na waone kuwa anawafaa
kukinadi chama chao wilayani Kahama mpaka wananchi wakaamini kuwa anawafaa kuwa
mbunge wao. Sidhani kama CCM imemuongezea lolote mpaka hapo.
Kama suala
ni CCM kumpa umaarufu, wapo makada wangapi wa CCM tusiowajua mpaka sasa? Kwa
nini hao CCM haiwafanyi wawe maarufu kama kweli chama hicho kinao utaalamu huo?
Hata huyo
Mlimandago ndio kwanza nimemsikia pamoja na hao wenzake, ukimuondoa Mzee Mgeja,
wakijaribu kuukwea umaarufu wa Lembeli ili nao wajitengenezee umaarufu wa kwao.
Kama kweli chama chao kingekuwa na utaalamu wa kuwatengenezea umaarufu makada
wake kwa nini wao wamtegemee Lembeli ili wajulikane?
Jambo hilo
linadhihirisha pasipo na shaka kuwa Lembeli katumia jitihada na akili zake
binafsi, vikichangiwa na uaminifu na uzalendo wake, kujulikana. Wala sio juhudi
za kikundi chake, CCM.
Ni kama wao
wanavyofanya juhudi zao binafsi kwa kumtumia yeye kupata umaarufu, kwani
wanaweza kusema kuwa hizo ni juhudi za chama?
Lembeli
kaweka mbele uzalendo kwa nchi yake tofauti na wanaotanguliza mapenzi kwa
vikundi vyao wakiwa wameusahau uzalendo kwa nchi yao. Kama hatabadilika, huo
ndio mfano wa kuigwa.
Faida ya
kuujali uzalendo kwa nchi ni pamoja na kuijali nchi yako ukiwa unawachukulia
wananchi wote kama ndugu zako. Kwa namna hiyo ni vigumu kuwabagua baadhi ya
wananchi ukiwaona kama watu wasiokutakia mema kwa vile hawako kwenye kundi
lako.
Utakuwa
huwezi kuushawishi uhasama miongoni mwa wananchi kutokana na kuwachukulia wote
kama kitu kimoja ambacho wewe mwenyewe ni sehemu yake.
Siri ya
Tanzania, tangu ikiwa Tanganyika, kuwa na kinachoitwa amani na utulivu kwa muda
mrefu, ndiyo hiyo. Wananchi kujiona ni kitu kimoja wakiwa wameyatanguliza
mapenzi kwa nchi yao na wao kupendana bila kuathiriwa na umakundi.
Lakini
linapokuja suala la umimi, huyu ni wa chama changu na huyo ni wa chama kingine,
anaweza akasababisha chama changu kikaanguka na kunifanya nikikose nilichozoea
kukifaidi, uzalendo kwa nchi kupatikana ni muhali.
Mawazo ya
watu yanazama kwenye makundi na kuwashawishi walio kwenye makundi tofauti
wabaki wanatazamana kama maadui. Kinachojitokeza katika hali ya aina hiyo ni
kujengeka mbinu za kundi moja kutaka kulitokomeza kundi lingine.
Hayo
tumeyashuhudia katika chaguzi zinazofanyika kwa sasa ambapo mapenzi katika
makundi, vyama vya siasa, yanawafanya watu watekane nyara, wafanyiane matendo
ya kiharamia na kigaidi na hata kufikia kuuana. Katika hali ya aina hiyo hakuna
anayeweza kuonyesha mapenzi kwa nchi yake.
Ikumbukwe yanayoitwa
mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalitokana na mtindo huo wa maisha. Kujigawanya
katika makundi na kuutukuza mgawanyiko huo, thamani ya utu ikapotea na kubaki
inaonekana tu thamani ya mgawanyiko! Matokeo yake ni maangamizi!
Lembeli
kaamua kuuvaa uzalendo pasipo kuyajali makundi. Tumuunge mkono ili walio na virusi vya umakundi
wasimlazimishe kumuambukiza ugonjwa huo hatari kwa mabavu. Tukimtelekeza na
kumuacha aambukizwe kwa kulazimishwa tuelewe kwamba sote hatutakuwa salama.
0784 989 512