UMAMUMA KATIKA UONGOZI WA NCHI NI CHANZO CHA UHARIBIFU WA MAZINGIRA
Na Prudence Karugendo
MAZINGIRA
ni uhai: Neno hilo tulifundishwa shuleni tangu madarasa ya awali. Tulikuwa
tunafundishwa kwamba mimea ndiyo hutoa hewa ya Oksijen tunayoivuta pamoja na
kuchangia upatikanaji wa mvua. Vilevile tulikuwa tukifundishwa kuwa mimea
inalinda nchi isigeuke kuwa jangwa sambamba na kutokea upepo mkali (vimbunga)
katika maeneo yasiyo na miti. Mambo hayo yote tulikuwa tukifundishwa tangu
awali ili tukue tukielewa umuhimu wa kutunza mazingira.
Inastaajabisha
kuona watoto wadogo wanafundishwa na kuelewa
umuhimu wa kulinda mazingira wakati watu wazima hawauoni umuhimu huo!
Lakini sidhani kama hawa watu wazima ni kweli hawayahitaji mazingira, kama
hawahitaji hewa ya oksijeni, hawahitaji mvua, kwamba wao wanatamani jangwa na
vimbunga! Ukweli ni kwamba tofauti ya uelewa wa umuhimu wa kuyahifadhi
mazingira kati ya watu wazima na watoto inasababishwa na majukumu
yanayojitokeza katika mfumo wa maisha ya mwanadamu.
Wakati
mtoto anategemea kila kitu kitoke kwa mzazi wake, chakula, mavazi, malazi,
elimu nakadhalika, mzazi inambidi achangamshe akili kuweza kukabiliana na
jukumu hilo. Na ndipo mzazi anapotumia kila kilicho kwenye upeo wake kama
nyenzo ya kukabiliana na jukumu hilo, jukumu la malezi. Ni kwa kufanya hivyo binadamu
anashtukia yumo kwenye uharibifu wa mazingira.
Mathalani,
mzazi hawezi kuwaacha watoto wakakosa kupikiwa chakula eti kwa kuchelea kukata
miti kwa ajili ya kuni, kutokana na kukosa nishati mbadala, wakati ukataji wa
miti ni sehemu ya uharibifu wa mazingira.
Mtu
mzima anachangia uharibifu wa mazingira pengine si kwa kutotambua au
kutothamini umuhimu wake, bali anasukumwa na hali iliyomzunguka na kujikuta
ameangukia katika uharibifu huo pale anapokuwa anapanga mikakati ya kukabiliana
na hali hiyo kwa kutoa vipaumbele, kipi kianze na kipi kifuatie.
Katika
hali ya umasikini, kama hii ya kwetu
Tanzania, ambayo asilimia kubwa ya wananchi wanaishi katika nyumba za miti na
udongo, nani atakuelewa ukimwambia asikate miti ya kujengea kibanda chake cha
kujihifadhi na familia yake eti kwa lengo la kutunza mazingira? Kati ya ustawi
wa mazingira na uhai wa familia yake kipi kinaonekana kuwa na umuhimu zaidi ya
kingine? Katika akili ya kawaida mtu anajali familia yake kwanza, mambo ya mazingira
ni sawa na habari yoyote ya mitaani.
Baada
kuonyesha, japo kwa ufupi, jinsi umasikini niliokuwa nautaja kama (hali),
unavyotulazimisha kuharibu mazingira yetu, nataka nionyeshe pia jinsi maamuzi
mabovu ya Serikali, ambayo kwa vyovyote vile yanapitishwa na uongozi mbovu,
yanavyousaidia umasikini kulikuza tatizo hilo.
Neno
uongozi, kwa maana nyingine, ni uelekezaji. Hii inaleta maana ya kwamba uongozi
bora ni ule ulio na taswira ya jambo unaloongoza kulielekeza. Vinginevyo
utakuwa ni uongozi kipofu ambao haufai kabisa sababu utakuwa unawaburuza
wanaoongozwa kwenda kusikojulikana, kwa vile uongozi hauoni, matokeo yake yanaweza
yakawa ni kuishia kwenye maangamizi!
Kwahiyo
katika suala hili, uongozi wa nchi ilibidi uwe unayaona madhara ya uharibifu wa
mazingira unaofanywa na wananchi, si kwa mapenzi yao, bali katika jitihada za
kukabiliana na hali ya umasikini uliowazunguka na kutishia uhai wao, na hivyo
uongozi kuonyesha njia mbadala ambayo wananchi wangeitumia na kuyaacha
mazingira yasitawi kwa manufaa yao.
Badala
yake uongozi ndio unaokuwa wa kwanza kuzitia kufuli njia zote ambazo
zingetumika ili kulinda mazingira na kuwalazimisha wananchi wazidi kujikita
katika njia za asili. Njia mojawapo kuu ya uharibifu wa mazingira ni ya
nishati.
Tangu
mwanadamu agundue moto aliachana kabisa na matumizi ya vyakula vya porini
vilivyokuwa vinaliwa bila kupikwa. Kwahiyo alianza kutumia kuni na baadaye mkaa
kama njia kuu za kuendeshea nishati yake hiyo aliyoigundua. Na baadaye, kadiri
akili zake zilivyozidi kukua, ndipo mwanadamu akagundua njia nyigine za
kuzalisha na kutunza nishati hiyo kwa njia ya umeme. Sayansi ya umeme
iligunduliwa ili iwe nyepesi na rahisi kuimudu na kuitumia badala ya ile
iliyokuwa inapatikana kwa kupekecha vitu kama vijiti na kugonganisha mawe na
hatimaye kutumia kuni au mkaa ili iweze
kufanya kazi.
Nishati
ya umeme ni kati ya mambo yaliyopatikana kutokana na uvumbuzi wa teknolojia
inayoendelea kuboreshwa kila kukicha. Teknolojia ipo kumrahisishia binadamu
shughuli zake. Kwa maana hiyo nishati ya umeme nayo ipo kumrahisishia binadamu
shughuli zake, siyo katika upatikanaji wake tu,
ambao ni tofauti na ule wa kupekecha miti na mawe ili moto upatikane,
bali pia kumudu gharama zake. Ndiyo maana nishati ya umeme inapaswa kuwa rahisi
kuliko karibu aina zote za nishati.
Nchi
nyingi duniani umeme ni kitu cha lazima. Tena hii haitokani na hatua ya
maendeleo ambayo pengine imefikiwa na nchi hizo inayoweza kulifanya jambo hilo
lionekane kama mbwembwe zitokanazo na jeuri ya maendeleo. Ukweli ni kwamba
kinachotiliwa maanani ni tafsiri ya teknolojia katika kurahisisha maisha na
shughuli za mwanadamu sambamba na kuhifadhi mazingira yanayomzunguka.
Teknolojia ya umeme inavifanya vitu kama ukataji wa miti kwa madhumuni ya kuni
na kuchoma mkaa vibaki kwenye historia tu.
Lakini
jambo la kusikitisha ni kwamba hapa nchini kwetu hali ni tofauti. Nishati ya umeme ni kitu
ambacho kimefanywa kionekane ni cha anasa tu na hivyo kuishia kuwanufaisha
wateule wachache! Sidhani kama nishati hii inafikia kiwango cha kukidhi japo
robo ya umuhimu wake hapa nchini mwetu.
Tatizo
linalotukabili ni la uongozi wetu
kuangalia pafupi. Ingekuwa uongozi wetu unaangalia mbele zaidi, sasa
hivi si ajabu kila Mtanzania angekuwa anatumia umeme na hili tatizo la ukataji
wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa pengine lingeishatoweka.
Inaeleweka
kwamba gharama za umeme na usambazaji wake inabidi zifidiwe. Sasa uongozi
ungekuwa unaangalia mbele zaidi na kuliona janga lililo mbele yetu ambalo
tunajaribu kuliepuka, janga ambalo linatishia zaidi vizazi vijavyo, tusingeng’ang’ania
gharama za umeme zifidiwe na kizazi cha sasa tu kwa kupandisha viwango vya
gharama za umeme kiasi cha kuwafanya wananchi waepukane nao na hivyo kubakia
kwenye njia yao ya asili ya kupata nishati ambayo ni ya mkaa na kuni.
Ikizingatiwa
kuwa kinachofanyika leo si kwa ajili ya wanaoishi leo peke yao, suala hili la
mazingira ingebidi litizamwe kwa upeo mrefu, bila ubinafsi wa kujijali sisi
tunaoishi kwa sasa peke yetu. Ieleweke
kwamba uzembe wowote, katika suala hili la mazingira, utakuwa ni mzigo mkubwa
kwa vizazi vijavyo. Kwa maana hiyo, hata gharama za umeme zingerefushwa mpaka
kwa vizazi vijavyo, kwa maana ya watumia
umeme kuchangia kidogokidogo mradi waweze kumudu gharama za matumizi yake. Bora vizazi vijavyo
vikakuta deni la umeme hata kama ni la miaka mia mbili itakayokuwa imepita
kuliko kukuta nchi ikiwa jangwa.
Malengo
ya muda mfupi yanayowekwa na uongozi husika ndiyo yanayo tuelekeza katika
maangamizi. Haya ni malengo ambayo uongozi, kwa kusukumwa na tamaa ya
kujinufaisha haraka haraka, hayazingatii kabisa masuala muhimu kama hilo la
utunzaji wa mazingira.
Mfano,
kinajengwa kiwanda cha saruji. Mtu atadhani lengo ni kuwawezesha wananchi kuwa
na makazi bora sambamba na kulinda mazingira kwa kuwafanya wananchi waache
kukata miti kwa ajili ya kujengea na badala yake watumie saruji. Ukweli
unabainika pale kiwanda kinapoanza uzalishaji. Bei ya saruji inayopangwa bila
kuzingatia kipato cha mwananchi ndiyo inayodhihirisha kuwa lengo la wenye
kiwanda cha saruji ni kurudisha mtaji wao haraka iwezekanavyo na kutengeneza
faida, na wala ujenzi wa kiwanda hicho cha saruji hauna uhusiano na utunzaji wa
mazingira!
Ingekuwa
Serikali (uongozi) inao mkakati wa kutunza na kuyalinda mazingira isingeshindwa
kushauriana na hawa inaowaita wawekezaji, ili kuwapunguzia kodi au Serikali
yenyewe kutoa ruzuku, kusudi saruji iuzwe katika kiwango ambacho mwananchi wa
kawaida anaweza kukimudu.
Kinyume
chake Serikali ndiyo ya kwanza kuwakoromea wenye viwanda kwa vitisho vya kodi
ambayo moja kwa moja inaingizwa kwenye bidhaa inayozalishwa na kuwafanya
wananchi wazione bidhaa hizo kuwa siyo stahiki yao! Ung’ang’anizi huo wa kodi
umo katika malengo ya muda mfupi ya uongozi wetu niliyoyataja hapo juu. Malengo
ambayo yanalenga zaidi kujinufaisha bila kujali hatima ya nchi.
Sasa
hivi tumo katika msukosuko wa ukame. Mito, mabwawa na hata maziwa vinatishia
kukauka. Hii imechangiwa zaidi na utowekaji wa misitu kitu ambacho ni kama sumu
kwa vyanzo vya maji. Mabwawa ya kuzalisha umeme nayo yamekauka, wenye kutumia
umeme tunawaona wanavyohaha. Lote hilo ni tatizo la uongozi kukosa dira. Kama
Serikali ingekuwa na malengo ya muda mrefu, ikawawezesha wananchi kutumia
umeme, bila tamaa ya kutaka kupata
vipato vikubwa kwa muda mfupi, sasa hivi tusingekuwa tunaongelea tatizo hili la
umeme.
Tatizo
hili limekuja sababu watumiaji wa umeme ni wachache wakati wazalishaji wa umeme
wanataka vipato vikubwa na kwa haraka, maana yake ni kupandisha zaidi viwango
vya gharama ya umeme. Wananchi wa kawaida wakabaki kwenye nishati yao ya asili,
kuni na mkaa. Matokeo yake ni misitu kutoweka, vyanzo vya maji kukauka na ukame
kutamalaki.
Tamaa
ya kujinufaisha kwa muda mfupi inayoonyeshwa na uongozi wa nchi bila kujali
majaaliwa ya nchi yatakuwaje ni tatizo kubwa linalozikandamiza nchi za dunia ya
tatu kwa kuyafanya matatizo yanayozikabili yazidi kurundikana badala ya
kupungua kila kunapojitokeza kinachodaiwa kuwa ni jitihada za kupambana na
matatizo hayo. Hiyo ni kwa sababu tamaa hii imetokea kuwa kivutio kikubwa kwa manyang’au popote yalipo duniani, kuacha
sehemu nyingine na kuamua kukimbilia kwetu.
Mifano
hai ni miradi ya IPTL, Richmond, Dowans, Symbion na mingine ya aina hiyo. Miradi
hiyo ilisukumwa zaidi na tamaa ya kujinufaisha haraka kuliko umuhimu wa miradi
husika uliotokana na tatizo lililokuwa linatukabili kwa wakati ule. Wajanja
walipiga mahesabu ikaonekana kwamba megawati za umeme ambazo zingezalishwa zigelazimishwa
zote kuuzwa TANESCO kwa kipindi fulani bila kujali kama zilikuwa zinahitajika
na kutumika zote ama vinginevyo.
Matokeo
yake ni TANESCO kulipa mabilioni ya
shilingi kila mwezi hata katika kipindi ambacho TANESCO ilikuwa haitumii hata
uniti moja ya umeme wa makampuni hayo mumiani! Hiyo maana yake ni kwamba
TANESCO nayo, ili kujinusuru, inabidi iwakamue wateja wake, wananchi, angalau
ijaribu kufidia gharama za bure zinazopokwa na hao manyang’au.
Isingekuwa
tamaa ya kujinufaisha haraka kwa
wachache, miradi ya makampuni hayo ikalenga kuwanufaisha wananchi wa Tanzania
katika ujumla wao, kwanza pasingekuwepo na ulazima wa makampuni hayo kuiuzia
TANESCO hata kile isichokihitaji, TANESCO nayo isingelazimika kupandisha viwango
vya uuzaji wa umeme wake kitu ambacho
kingekuwa kishawishi kwa wananchi kutumia umeme na kuhifadhi mazingira. Kinyume
chake, makampuni hayo mumiani yanazalisha umeme yanaiuzia TANESCO, wananchi
wanashindwa kuutumia umeme huo kutokana na gharama zake kuwa nje ya uwezo wao,
wanabaki kutumia mkaa na kuni, misitu inaisha, maji yanakauka, umeme
unaozalishwa na maji ambao ndiyo tegemeo la gridi ya Taifa karibu unazimika,
ule wa wawekezaji hautoshi, basi kivumbi, tamaa imezaa balaa!
Mfano
mwingine wa wachache kuwa na tamaa ya kujinufaisha ndani ya matatizo
yanayotukabili ni ule mradi wa gesi ya Songosongo. Niliwahi kuambiwa na mtaalamu
mmoja aliyeshiriki katika utafiti wa gesi hiyo ya Songosongo kwamba gesi hiyo
ikishapatikana ndiyo ungekuwa mwisho wa matatizo. Imani yake, mtaalamu
yule, ilikuwa kwamba kwa vile gesi
ilikuwa inapatikana nchini mwetu tulikuwa na haki ya kuitumia jinsi ambavyo
tungetaka tofauti na bidhaa nyingine za mafuta tunazoagiza kutoka nje. Kinyume
cha matumaini yetu, naona sasa kuna kampuni inayojiita SONGAS inayojifanya
kumiliki gesi hiyo na kutuuzia sawa na bidhaa nyingie za mafuta tunazoagiza
kutoka Mashariki ya Kati!
Jambo
lililonistua ni kwamba kuna mpango wa kuzuia uchomaji mkaa! Mbona mpango huu
umekuja wakati usio wake? Kuna njia gani mbadala ambayo itatumiwa na wananchi
karibia asilimia 98 ya Watanzania ambao uhai wao unategemea nishati ya mkaa? Na
itakuwaje kwa zile asilimia mbili zilizokuwa zinategemea umeme na ghafla
zikaugeukia mkaa baada ya umeme kutokuwa wa uhakika?
Kwa
vile mambo yote yanafanywa kwa mtindo wa zima moto wakati yamesababishwa na
uzembe wetu, inabidi tuchague moja kati ya mawili, ama tukubali kufa ili
kulinda mazingira yetu, au tuyaache mazingira yaalibike kulinda uhai wetu.
0784
989 512