WA TZ WEPESI WA KUSAMEHE
Kifo cha Gaddafi, Watanzania ni
wepesi wa kusamehe na kusahau
Na Prudence Karugendo
JUMA
lililopita niliandika makala yenye kichwa cha habari “Kifo cha Gaddafi ba
maajabau ya Watanzania” lakini kutokana na hitilafu za kiufundi makala hiyo
ikaonyesha anwani ya Padri Privatus Karugendo. Huyo ni mtu tofauti na Prudence
Karugendo, mtazamo wake na wa kwangu zinapishana katika baadhi ya mambo. Naomba radhi kwa usumbufu wowote uliotokana na
hitilafu hiyo.
Lakini
hatahivyo ujumbe wa makala hiyo uliwafikia walengwa, Watanzania. Waliobahatika
kuupata ujumbe wa makala hiyo waligawanyika katika sehemu tatu, wapo waliotokea
kuuelewa na kukubaliana nao wakati wengine wakiwa wameuelewa lakini hawakutaka
kukubaliana nao kutokana na sababu wanazozielewa wao wenyewe. Pia wapo ambao
hawakuuelewa kabisa ujumbe wa makala yangu hiyo, wakaishia kutoa maoni yenye
vichekesho vya kuduwaza.
Hoja yangu
kuu katika makala yangu hiyo ya juma lililopita ilikuwa kwamba mtawala wa Libya
aliyeangushwa na baadaye kuuawa na wapinzani wake, Muammar Gaddafi, hakuwa mtu
mwema kwetu, sisi Watanzania, na pengine Waafrika weusi kwa ujumla.
Nilijaribu
kukumbusha maovu aliyotufanyia Gaddafi, sisi Watanzania, kwa kusukumwa na
ukwasi wa mafuta ya nchi yake mwishoni miaka ya 1970 na mwanzoni mwa 1980.
Maovu hayo yanaonekana kusahaulika vichwani mwa baadhi ya Watanzania, wengi wao wakiwa wameingizwa kwenye vishawishi
vya Gaddafi vilivyokuwa vinakuja kwa njia ya zawadi za “lambalamba”, tende na
halua. Utamu wa tende na halua ukawa umemsafisha Gaddafi machoni mwa Watanzania
huku kumbukumbu zote chafu za mtu huyo zikiwa zimefutika kabisa!
Pia
nilieleza kwamba Waarabu wa Afrika Kaskazini mpaka Kaskazini Magharibi
wanajiita Waafrika kwa lugha ya kisiasa tu, lakini kilicho ndani ya roho zao
wanakielewa wao. Na hiyo si siri, ni kwamba wao wanajitambua kuwa sio Waafrika
bali Waarabu, kitu ambacho hakina ubishi wowote. Sie weusi ndio tunaodai wale
ni Waafrika wenzetu wakati wao, katika nyakati tofautitofauti, hawakubaliani na
jambo hilo.
Ndiyo maana
kitendo cha Gaddafi kutumia nguvu zake zote kutaka Afrika iungane na kuwa nchi
moja kilikuwa kinanipa mashaka makubwa sana. Ni kwa sababu nilikuwa naelewa
kwamba hakuna muungano unaokubalika kati ya mtu mweusi na Mwarabu.
Mifano hai
ipo mingi. Bara la Afrika ni la watu weusi, lakini kule Kasikazini kulikovamiwa
na kukaliwa na Warabu tunaona kwamba weusi hawapo kabisa kitu ambacho
kinawafanya baadhi ya watu waamini kwamba Warabu ni watu wa asili katika maeneo
hayo. Lakini ukweli ni kwamba Waarabu ni wavamizi tu waliowahamisha wenyeji
weusi kuja kusini wengi wao wakiwa wameangamizwa.
Mfano
mwingine ni wa hivi karibuni wa nchi ya Sudan. Tumeona jinsi Waarabu wa Sudan,
tena Waarabu koko, walivyoshindwa kuishi
kwa amani katika nchi moja na weusi wa Sudan Kusini mpaka ikalazimika nchi hiyo
itengwe ili weusi wa Kusini nao wawe na nchi yao.
Kwa ufupi ni
kwamba mpango wa Gaddafi kutaka kuharakisha muungano wa Afrika binafsi nilikuwa
nautafsiri kama mpango wa kuyaharakisha maangamizi ya weusi. Kama hilo halikuwa
kichwani mwa Gaddafi, tuseme hizo ni fikra zangu potofu, ni kitu gani
kilichomzuia Gaddafi, mtu msomi na mweledi wa historia na asili za watu, kuanza
na kuwatafuta watu wa asili ya Libya ili awarudishe kwao kama walivyowahi
kufanya Wayaudi kwa ndugu zao waliokuwa wamesambaa katika sehemu mbalimbali za
dunia? Katika kufanya hivyo ndipo tungemuamini Gaddafi kwamba alikuwa
amedhamiria kuwaona Waafrika wakiwa kitu kimoja bila kujali tofauti zao za
rangi.
Lakini
kumuamini mtu aliyekuwa akiwabagua hata Waarabu wenzake kwa misingi ya kwamba
wanatoka sehemu alikozaliwa mfalme aliyempindua yeye Gaddafi mwaka 1969, kwamba
angeweza kuiunganisha Afrika ya weusi na ya Waarabu kuwa kitu kimoja, ilikuwa
sawa na watu weusi kuuchezea moto ambao baadaye ungekuja kuwaunguza kijuha! Kwa
hilo siamini kabisa kwamba Gaddafi alikuwa na dhamiri ya haki. Na kilichompata sasa ni ile adhabu
iliyoumbiwa ndani ya kosa kama alivyowahi kuielezea Mwalimu Nyerere. Gaddafi
kapanga kuwaangamiza Waafrika kaangamia mwenyewe. Kapanga kosa na kupata adhabu
ndani ya kosa lilelile.
Tukirudi
kwenye usahaulifu wa Watanzania tutaona kwamba hali hiyo inaweza kutupeleka
kwenye maangamizi endapo hatutaifanyia marekebisho. Watanzania ni wepesi sana
wa kusamehe na kusahau. Tunaweza tukasamehe ndiyo, lakini kusahau ni kosa la
mauti. Kusahau ndiko husababisha kosa kujirudia tena na tena kwa njia ileile na kumfanya anayeathirika na
kosa husika kuonekana zuzu!
Katika
makala iliyopita nilieleza juu ya Vita ya Kagera, vita ambayo tulilazimika
kupigana ili kuikomboa nchi yetu baada ya kuvamiwa na kutekwa na mtawala
mwendawazimu wa Uganda, Idd Amin Dada. Na nilieleza jinsi Muammar Gaddafi wa
Libya alivyojiunga na mwendawazimu huyo wa Uganda ili kumsaidia kuimarisha
uvamizi wake nchini mwetu. Tendo hilo la kishenzi tungeweza kulisamehe, kama
tulivyolisamehe, lakini kulisahau ni ujinga uliopitiliza.
Bahati mbaya
baadhi ya Watanzania wameishausahau uovu huo aliotufanyia Gaddafi, wanakumbuka
tu tende na halua ambazo Gaddafi amekuwa akizileta siku za karibuni kuelekea
kuangamia kwake.
Inawezekana
asilimia kubwa ya Watanzania wa sasa haikuwepo wakati huo wa Vita ya Kagera,
lakini hatahivyo vita hiyo iko kwenye historia ya nchi yetu tunayoienzi kama
ilivyo tarehe ya uhuru wa nchi yetu ambao ulishuhudiwa na asilimia ndogo sana
ya Watanzania waliopo kwa sasa.
Baadhi ya
makamanda wastaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania, walioongoza Vita ya Kagera, wameisoma makala yangu ya juma lililopita na
kutoa mitazamo yao. Mmoja wa makamanda hao wastaafu aliyejitambulisha kuwa
alikuwa akiongoza kikosi cha uhandisi cha utegaji na uteguaji wa mabomu,
amenieleza kama ifuatavyo.
Kamanda huyo
anasema kwamba jukumu la uandishi ni kuelewesha, kukumbusha, ikiwa ni njia ya
kuelimisha. Anasema uandishi wa Tanzania juu ya Vita ya Kagera ulimsamehe
Gaddafi na kujikita zaidi kwa Idd Amin na hivyo kuwafanya Watanzania wamuone Amin
ndiye mbaya wao tu wakiwa wameyaacha pembeni madhara ya Gaddafi ambaye kwa
kiasi kikubwa ndiye aliyemuwezesha Amin kutufanyia jeuri hiyo.
Kamanda huyo
anasema kwamba tathimin iliyokuwa imefanywa na wataalamu wa JWTZ baada ya Amin
kuivamia nchi yetu ilikuwa ni ya kumtandika Amin na kumsambaratisha kabisa
ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na nusu na miezi miwili bila kujali zana za
kivita alizokuwa amejidhatiti nazo
zilizozizidi tulizokuwa nazo sisi. Lakini kujiingiza kwa Gaddafi katika vita
hiyo kulitugarimu miezi minane mpaka kutangaza ushindi kamili na miezi mingine mine
kusafisha kabisa mabaki ya Amin.
Ni kwamba
uchumi wa nchi yetu ulipata majeraha yaliyosababishwa na ubabe wa Gaddafi wa
kuingilia vita hiyo ambayo bila yeye tungeweza kuimaliza kama tulivyopanga bila
kuathiri sana uchumi wetu. Lakini sasa Gaddafi kautia kilema uchumi wetu maana
tokea wakati huo umeshindwa kutengamaa tena.
Jambo la kujiuliza
ni kwamba uzuri wa Gaddafi ambao umetajwa kwa nyakati tofauti na viongozi wetu
wa kitaifa wakiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, unatokana na nini hasa kwetu
Watanzania?
Ina maana
Watanzania waliouawa Kagera na Amin akiwezeshwa na Gaddafi walikuwa wametolewa
kafara? Na je, vijana wa Kitanzania, wapiganaji, waliokuwa wanapigana kuikomboa
nchi yao mara wakalipuliwa kwa kuviziwa na askari mamuluki wa Gaddafi nao
walitolewa kafara?
Kuna
ushuhuda kwamba baadhi ya askari wetu wa kikosi cha kutega na kutegua mabomu,
wakiwa wamepanda gari lililokuwa limesheheni milipuko walitegeshewa bomu na
majeshi mamuluki ya Gaddafi lililolilipua gari hilo la vijana wetu kiasi cha
gari lenyewe na waliokuwemo kuyeyuka kabisa na kutoonekana tena!
Baadhi ya
askari wetu waliopoteza maisha katika shambulio hilo lililofanywa na majeshi ya
Gaddafi, kwa mujibu wa mashuhuda wa JWTZ ni hawa wafuatao. 1. SSGT Brighton
Lububula (alikuwa kaoa), 2. PTE Salum Ngwangwa (kapera), 3. PTE Mathayo
Mamboleo (alikuwa kaoa), 4. PTE Bahati Mashimi (kapera), 5. SGT Weston Chikwera
(alikuwa kaoa), 6. SGT Filbert Ndunguru (alikuwa kaoa), 7. SGT John Banda
(alikuwa kaoa), 8. CPL Aureus Kawonga (alikuwa kaoa), 9. CPL Jacob Mbepera
(alikuwa kaoa) na 10. PTE Salum Seif (alikuwa kaoa).
Familia za
mashujaa hao zinajisikiaje kwa wakati huu zinaposikia mtu aliyesababisha
kutoweka kwa wapendwa wao hao akisifiwa na viongozi wetu kuwa alikuwa mtu mzuri
wakati kalaaniwa hata nchini kwake?
Nadhani ipo haja ya viongozi wetu waliotoa kauli za kumsifia Gaddafi kuwaomba
radhi Watanzania hususan familia za hao waliopoteza wapendwa wao kusudi dhana
ya kuwaenzi hao mashujaa wetu ibaki salama mahali pake.
Hatuwezi
kudai kwamba tunawaenzi mashujaa wetu huku upande wa pili tukikisifia kile
walichopoteza maisha wakipambana nacho hao mashujaa wetu, kwa maana ya kuenzi
huku na huku.
Kuna wenye
maoni ya kwamba ingefaa uwepo mdahalo hai wa kuyapima mazuri na mabaya ya
Gaddafi kwa Watanzania kama njia ya kuipima thamani yetu kifikira na kimtazamo.
Hatuwezi kuishusha thamani yetu kwa kurubuniwa na vitu vidogo kama “lambalamba”.
Ndiyo maana
hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliwarudisha kwao askari wote mamuluki wa
Gaddafi, waliotekwa kwenye vita ya Kagera, bila masharti yoyote wakati Gaddafi
alikuwa tayari kutoa mabilioni ya shilingi kwa kila mmoja wao. Nyerere hakuwa
mtu wa kurubuniwa na lambalamba, ingebidi tumuenzi kwa vitendo katika hilo.
Nimalizie
kwa kusema kwamba, kwa uzuzu wetu tunayalaani mataifa ya Magharibi kwamba ndiyo
yaliyosababisha kuangushwa kwa utawala wa Gaddafi na hatimaye kifo chake tukiwa
tumesahau kwamba hata yeye Gaddafi, kwa jeuri ya pesa ya mafuta, alikuwa
akishindana na hayo mataifa ya Magharibi kiubeberu. Mifano ya ubeberu wa
Gaddafi ni kama hiyo ya kumsaidia Amin kuivamia na kuiteka ardhi ya nchi yetu
ikiwa ni pamoja na kuua maefu ya Watanzania bila kosa lolote, kuvifadhiri
vikundi vya kigaidi bila sababu yoyote ya msingi ila tu kuonyesha umwamba na
jeuri ya pesa nakadhalika. Kwahiyo tunapoyalaani mataifa ya Magharibi kwa
ubeberu tusisahau kwamba hata Gaddafi alikuwa mwenzao.
Swali la
mwisho tujiulize, iwapo ubeberu wa Gaddafi alioufanya kwa Tanzania wa
kumwezesha Amin kuivamia nchi yetu ungefanikiwa kuiangusha serikali ya Nyerere,
je, Gaddafi angekuwa hajafanya kama kile kilichofanywa na NATO kwa utawala
wake? Je, hapo kuna tofauti gani kati ya NATO na Gaddafi? Kinachoonekana ni
kuzidiana uwezo lakini malengo ya Gaddafi naNATO yalikuwa ni yaleyale mamoja.
0784 989 512