Bukobawadau

JAMII YAASWA KUINUA ELIMU

JAMII imetakiwa kufanya mabadiliko chanya katika elimu kwa kuwekeza na kupeleka watoto shule ili kuongeza uhamasishaji wa ufaulu mzuri kwa wahitimu ambao utasaidia kuchangia maendeleo ya haraka.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na mmiliki wa Shule ya Awali na Msingi ya New Vision iliyoko Kata ya Mugajwale, Tarafa ya Rubare, Wilaya ya Bukoba, Prosper Nduke, alipozungumza na mwanahabari wetu
Nduke alisema kumekuwa na mwamko hafifu katika jamii kuhusiana na suala la elimu, badala yake wazazi na jamii nyingi zimekuwa zikitumia muda na rasilimali kubwa kwa ajili ya mambo yasiyokuwa na tija.
Alisema wengine wamekuwa wakisifia na kuzitamani shule zinazotoa elimu bora, lakini wakiwa hawajali, wala kulipa ada na michango inayotakiwa.
“Ili taifa letu lipige hatua, hasa katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia, lazima tubadilike kwa kufuatilia maendeleo yao na kuwajibika kwa kila jambo maana elimu ni gharama,” alisema Nduke.
Alieleza kuwa aliamua kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuanzisha shule hiyo mwaka 2003 ili kuinua elimu kwa watu waishio vijijini, hasa kwa wasichana waliokuwa wanafanya kazi za ndani.
Hata hivyo, Nduke ametoa rai kwa baadhi ya wamiliki wa shule kuacha tabia ya kuwakaririsha mitihani watoto ili kuwajengea uelewa zaidi na kuwezesha taifa kupata wasomi na wataalamu wenye uwezo wa kusaidia kuleta maendeleo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau