KAULI YA KOMBA KWENDA MSITUNI:Mchelea mwana kulia hulia mwenyewe!
Na Prudence Karugendo
NIANZE kwa kutaja maslahi yangu kwamba mimi nilikuwa
mpenzi mkubwa wa Kapteni John komba. Nyimbo zake, hasa zile za mwanzo akiwa
kiongozi wa kikundi cha kwaya cha JWTZ cha Lugalo, zilikuwa zinanikosha roho
kupita kiasi na kunifanya nizione rangi zote za utukufu wa nchi yangu, huku
yeye nikiwa nimemweka katika daraja la kwanza la wazalendo wa nchi hii.
Lakini
Waswahili walisema kwamba “kua uyaone”! Niliyedhani kwamba yuko kwenye kundi
namba moja la wazalendo wa nchi yangu leo hii anatishia kuwa wakati wowote
anaweza akawa adui namba moja wa nchi hii iwapo matakwa yake hayatazingatiwa!
Anaamini kwamba yeye ndiye mzalendo peke yake, wengine wote wahamiaji sijui!
Komba
katamka kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwamba iwapo maoni ya wananchi ya muundo
wa serikali tatu katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yatayazidi nguvu
matakwa ya chama chake kinachopendelea muundo wa ajabu wa serikali mbili, basi
yeye ataongoza njia kwenda msituni!
Sidhani kama
Komba anatamani kwenda msituni ili
akaishi na ngedere baada ya kuwachoka binadamu wenye mawazo tofauti na ya kwake,
hapana, ni lazima huo ni mpango wake wa kuanzisha vurugu zenye lengo la
kuwakomoa na kuwakomesha wananchi wasiokubaliana na mtazamo wake. Hiyo maana
yake ni vita na mauaji ya wananchi.
Mpaka hapo,
kwangu mimi, uzalendo wa Komba umeyoyoma kwa kasi kubwa. Hayo ndiyo yaliyosemwa
kwenye usemi wa wahenga wa kua uyaone.
Mzalendo wa
kweli ni yule aliye tayari kuilinda nchi yake pamoja na wananchi wenzake. Wawe
wamehitilafiana au kukosana undugu unabaki palepale, kulindana na kuwekeana
kinga dhidi ya mabaya toka nje yao.
Lakini
anayetamani kuingia msituni ili akawadhuru wananchi wenzake eti kwa vile wametofautiana na mawazo
yake, siwezi kuamini kwamba anao uzalendo wa aina yoyote. Uzalendo kwa lipi?
Sababu nchi
ni ya wananchi wote. Uzalendo unatakiwa uyaheshimu matakwa ya wananchi walio
wengi. Uko ndiko kuilinda nchi na watu wake, ikiwa ni pamoja na kuyalinda
matakwa yao. Vinginevyo uzalendo hakuna.
Kauli hiyo
ya hatari ya Komba haikukemewa na yeyote kwa upande wa chama chake, CCM,
imechukuliwa tu kama kauli ya kuwakomoa wapinzani na yeye kubaki akionekana ni
kipenzi kwa chama chake hicho!
Kauli hiyo
ya Komba imenikumbusha jinsi Ossama bin Laden alivyokuwa kipenzi mkubwa wa
Marekani pale nchi hiyo ilipokuwa ikimtumia kuyalinda maslahi yake na kuwakomoa
wale ambao haikuwataka.
Lakini baada
ya Bin Laden kuhitilafiana na Marekani akageuka adui namba moja wa nchi hiyo.
Ikabidi nchi hiyo itumie gharama kubwa sana, tena kwa muda mrefu, kumtafuta na kumuangamiza
mtu huyo, huku yenyewe ikiwa imebaki na majeraha makubwa ambayo haitakaa
iyasahau. Mchelea mwana kulia hulia mwenyewe.
Komba
hakuchukuliwa hatua wala kukemewa kwa aina yoyote na walio madarakani, hususan
chama chake cha CCM, kwa tamko lake hilo la hatari. Ni kwa sababu tamko lake
hilo kwa sasa linaonekana halina madhara kwao, ila limelenga kuwatisha na
kuwanyamazisha wapinzani wanaotamani kuiona nchi yao ikipita mwenye mstari
ulionyooka.
Isipokuwa
kauli hiyo ingekuwa mbaya sana kama ingekuwa imetolewa na mtu wa upande wa
upinzani. Lazima kwa sasa hivi mtu huyo angekuwa anaijutia kauli hiyo.
Kwa uzoefu
tulio nao kwa sasa, hasa kwa upande wa Bara letu la Afrika, Watanzania
hatukupaswa kuichukulia kauli hiyo ya Komba kiurahisi na kuipuuza kiasi hicho.
Sababu anacholenga kwenda kukifanya kule msituni hakitambui nani yuko upande
wake, nani yuko upande wa pili na ni nani hahusiki. Ni machafuko kwa kwenda
mbele, sababu ilishasemwa kwamba vita haina macho.
Nchini
Uganda, kwa mfano, alijitokeza mama mmoja, Alice Auma Lakwena, akadai kwamba
anataka kuendesha nchi kwa kufuata Amri Kumi za Mungu. Akapuuzwa. Sikujua
alikoishia. Lakini akaja kurithiwa na Joseph Kony ambaye naye mwanzoni
alionekana kupuuzwa na serikali ya Uganda.
Baada ya
Kony kuanza kutoa cheche ndipo serikali ya Rais Museven ilipoanza kuhangaika
ikitafuta kumdhibiti bila mafanikio. Wakati huo Kony na kikundi chake
wakizidisha madhara kwa nchi na maafa kwa wananchi.
Tuseme
kikundi hicho kilikuwa na ugomvi na serikali, lakini waliodhurika zaidi ni wananchi.
Wananchi ndio wanaovamiwa na hao walio msituni,
kutekwa na kuuawa wakati serikali ya Rais Museven ikiwa bado iko
palepale.
Inavyoonekana
lengo la kikundi hicho cha Kony ni kuwaua wananchi na wala sio kuiondoa
serikali ya Museven madarakani.
Nakumbuka
kuna wakati Museven aliwahi kumuahidi mwanahabari mmoja wa Uganda, aliyeuliza
swali juu ya Kony, shilingi milioni sita za Kiganda endapo Kony angefika wakati
fulani kabla hajauawa na serikali, zaidi ya miaka kumi iliyopita. Museven
alitimiza ahadi yake, maana mpaka sasa Kony bado “anadunda”.
Kosa kubwa
lililofanywa na serikali ya Uganda ni la kushindwa kumdhibiti Kony mapema, kwa
kumchukulia kwamba yeye na kundi lake ni watu wepesi ambao wangemalizwa mapema
bila madhara yoyote.
Ninapoyaangalia
hayo ndipo nashawishika kuilaani tena na tena kauli ya Komba ya kwamba ataenda
msituni iwapo matakwa ya chama chake ya muundo wa serikali mbili
hayatakubaliwa.
Najiuliza
kwa mshangao, kama maoni ya wananchi yanasema muundo wa muungano wa nchi yetu
uwe wa serikali tatu, hizo serikali mbili zinazotaka kumpeleka Komba msituni ni
kwa manufaa ya nani?
Kwa nini
Komba atamani kuingia msituni kwa lengo la kuziteketeza roho za wananchi
wenzake kisa eti anataka serikali mbili dhidi ya matakwa ya wananchi? Serikali
mbili bila wananchi zina maana gani?
Imeishasemwa
mara kadhaa kwamba Katiba ni maridhiano, bila hivyo Katiba itabaki kuwa
kielelezo cha manyanyaso. Kwa nini Komba anaona maridhiano hayafai na hivyo
apange kukifanikisha anachokitamani kupitia msituni?
Nakumbuka
Mwalimu Nyerere aliwahi kukusudia kuwashitaki wakoloni kwa Mungu, iwapo njia
zote za kuwataka watuachie uhuru wetu zingeshindikana. Baadaye alifafanua
kwamba kuwashitaki kwa Mungu alikokusema kulimaanisha kushika silaha na kuudai
uhuru wetu kwa nguvu, uhuru wa wananchi wote.
Sasa
anayetaka kuingia msituni baada ya maoni ya wananchi walio wengi kupingana na
matakwa yake anataka afanye hivyo kwa faida ya nani? Bilashaka kama sio kwa
maslahi ya kikundi kidogo anachokipenda yeye ni kwa maslahi yake binafsi. Ndiyo
maana nasema kwamba tunatakiwa kumlaani Komba kwa nguvu zote kwa mpango wake
huo mchafu.
Kwa nini
Komba asichukuliwe hatua kwa wakati huu na kudhibitiwa kabla hajaamua kukifanya
anachokikusudia kama alivyotamka yeye mwenyewe? Naamini kwamba gharama ya
kumdhibiti kwa sasa ni ndogo na nyepesi kuliko kumsubiri akaingia msituni.
Tukiichezea
kauli yake kwa kujiridhisha kwamba aliyoyasema ni maneno tu, na hivyo kumwachia
ili kwanza ayaweke maneno yake kwenye vitendo, inabidi tuelewe kwamba tutakuwa
tumeviweka rehani, nchi yetu na roho zetu.
Sababu
ikishakuwa hivyo gharama ya kumpata itakuwa kubwa sana kiasi ambacho pengine
hatutakiweza, muda wa mateso utakuwa mkubwa sana wakati thamani ya roho za
wananchi itakuwa imeshuka kukaribia na sifuri. Maana kwenye hali hiyo mtu
kuuawa haina tofauti na mjusi kuuawa.
Waswahili
wanasema kwamba asiyejua kufa muonyeshe kaburi. Nataka niwaonyeshe Watanzania
wenzangu waiangalie Nigeria ilivyo kwa sasa. Mohammed Yusufu, aliyekuwa
kiongozi wa kikundi cha kijambazi cha Boko Haram kule Bauchi, Kaskazini
Mashariki mwa Nigeria, kabla ya kuuawa na kurithiwa na Abubakari Shekahu,
alitamka maneno kama ya Komba.
Wanigeria
kwa mbwembwe zao wakadharau wakimuona si lolote si chochote.Lakini sasa hivi
walikofikia wanaichukulia Boko Haram kama kiama! Wapende wasipende wanaiheshimu.
Tumeona jinsi
Jeshi la Nigeria lilivyoshindwa kukidhibiti kikundi hicho ambacho mwanzoni
kilidhaniwa ni “tisha toto” tu. Sasa imebidi Marekani, Uingereza na Israeli
waingilie kati kujaribu kukisaka kikundi hicho.
Jambo la
kusikitisha zaidi ni kwamba wanaoathirika sana na unyama wa kikundi hicho ni
wananchi wasio na hatia yoyote, wananchi wasiojua wafanye nini ili kutuliza
mzuka wa majambazi hayo ya Boko Haram.
Kwa sasa
dunia nzima, kila mtu anamuomba Mungu kivyake ili watoto wa kike zaidi ya 200
waliotekwa na kikundi hicho toka shuleni kwao wapatikane wakiwa salama.
Tujiulize,
mabinti hao wamekifanyia kosa gani kikundi hicho? Kwani wao ndio serikali ambayo
kikundi hicho kinadai kuna mambo ambayo hakikubaliani nayo. Bilashaka hapana.
Hapo ndipo
tunapaswa tuelewe kwamba wazo la kuingia msituni linasukumwa zaidi na “umimi”,
mtu kujifikiria yeye binafsi bila kuyajari mahangaiko yanayowapata wengine wala
kujali zahama atakazowasababishia. Kwa ufupi huo ndio unaoitwa ujambazi.
Jambazi
anajali yeye kupata, hajali kwamba anachotaka kukipata ni cha mwingine na
anataka akipate kwa mabavu hata kufikia kuitoa roho ya yule anayekimiliki
kihalali!
Laiti
serikali ya Nigeria ingeliona hilo mapema na kumkamata kiongozi wa kikundi
hicho, marehemu, mwanzoni kabisa kabla hajaanza kuyatekeleza aliyokuwa
anayakusudia, maafa yote haya yanayoikumba nchi hiyo yasingekuwepo. Haya sasa
ni matokeo ya kuudharau mwiba ambapo sasa guu lote limevimba tende!
Hakuna mtu
mwenye kuitakia mema nchi yake, akiipenda na kuwapenda watu wake, halafu
akatamani kuifanyia uasi au ugaidi nchi ileile.
Ndiyo maana
wapinzani hapa nchini wanafanyiwa vituko vya kila aina, kunyanyaswa, kuonewa,
kutukanwa, kudhulumiwa nakadhalika, lakini hakuna mpinzani aliyewahi kuwa na
wazo kama la Komba. Ni kwa sababu wanaoitwa wapinzani wanaipenda nchi yao.
Iweje sasa tuseme Komba anaipenda nchi yake kwa wazo lake hilo la kutaka
kuiangamiza?
Nimalizie
kwa kusema kwamba tunapaswa tuilaani kwa pamoja kauli ya John Komba ya kwamba
ataenda msituni, na tuiombe serikali yetu imshughulikie kwa kuwa hiyo ni kauli
ya kijambazi. Sababu mchelea mwana kulia hulia mwenyewe. Tusiwe kama Nigeria
inayolia kwa sasa.
0784 989 512