KINACHOFICHWA NA UKAWA NI HIKI HAPA
Na Mchakachuaji
Kama kuna
chama cha siasa kisichoeleweka malengo yake hapa nchini basi chama hicho ni
CUF. Nashawishika kukifananisha chama hicho na mwanamke ambaye hajatulia,
mwanamke ambaye leo anaolewa na
mwanamume huyu na kesho yake kumtamani mwanamume Yule, na akishaolewa kule
kesho yake anadai talaka! Kwa tabia ya
aina hiyo ni vigumu kujenga imani kwa mwanamke huyo au kukiamini
anachokikusudia katika ndoa zake hizo za pata potea.
Tunakumbuka
kwamba baada ya mikwaruzano ya muda mrefu kati ya chama cha CUF na chama
tawala, CCM, kwa upande wa Zanzibar, baadaye vyama hivyo vilifikia makubaliano
ya kusitisha mikwaruzano kwa kitu kilichojulikana kama muafaka, na hivyo chama
tawala kukubali kupunguza madaraka yake na kuigawa nusu ya madaraka hayo kwa CUF.
Vyote viwili vikawa vyama tawala kwa upande huo wa muungano.
Vyama hivyo
vilikubaliana kuunda kwa pamoja Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa maana hiyo
CUF nayo ikawa chama tawala kwa upande wa Zanzibar. Kitendo cha CUF kukubali
kuungana na CCM, nacho kuhesabika kama
chama tawala kina maana ya kwamba chama hicho kilikuwa kimekubaliana na sera za
chama hicho tawala.
Kwahiyo kwa
vile sera ya CCM ilikuwa ni kuendesha nchi ya Tanzania kwa muundo wa Muungano
wa serikali mbili, Zanzibar na Tanzania, basi CUF kukubali kuungana na CCM na
kuendesha nchi kwa pamoja kwa upande wa Zanzibar, tayari chama hicho cha
wananchi kilikuwa kinaamini katika muundo huo wa muungano. Muungano wa serikali
mbili.
Sasa katika
mchakato wa kuandika katiba mpya ya nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikaja na kitu kipya ilichodai ni maoni
ya wananchi, Muungano wa Serikali tatu. Kwa vile Rasimu hiyo moja kwa moja
inakinzana na msimamo wa utawala wa CCM ilikuwa ni lazima chama hicho tawala kikionyeshe kitu hicho kilicho kinyume na
mfumo wa uendeshaji wake wa serikali bila uficho wowote. Bila hivyo CCM
ingekuwa inakubali kuwa imeiongoza nchi hii muda wote kinyume na matakwa ya
wananchi.
Katika hilo
nilitegemea Chama Cha Wananchi kiwe mshirika namba moja wa CCM katika kuipinga
Rasimu hiyo inayopendekeza kwamba Katiba mpya itamke kwamba Serikali ya Tanzania
ni muungano wa serikali tatu. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba baada ya
makubaliano ya muafaka wa kuendesha nchi kwa pamoja tayari CUF ilikuwa
imekubaliana na muundo huo wa serikali mbili unaotambuliwa na CCM.
Lakini kwa
mshangao wa kila mmoja, ghafla CUF ikaruka mara moja na kujiunga na vyama
vingine vya upinzani vikiongozwa na Chadema, kuunda kitu kinachoitwa UKAWA, Umoja wa Katiba
ya Wananchi. Umoja huo unaunga mkono Rasimu iliyoletwa katika Bunge maalumu kwa
ajili ya kujadiliwa ili baadaye irekebishwe, kama hapanabudi, au kupitishwa jinsi ilivyo na kuwa Katiba
mpya.
Mbali na
kuishangaa CUF kwa ukinyonga wake huo, bado naishangaa UKAWA kwa msimamo wake
kwamba Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapaswa iheshimiwe.
Swali ni kwamba kama Rasimu hiyo inapaswa iheshimiwe kazi ya Bunge Maalumu ni
nini? Si Rasimu hiyo, baada ya kuwasilishwa kwa rais, moja kwa moja ingepelekwa
na kutengenezwa katiba mpya bila usumbufu wa kuitisha Bunge Maalumu.
Bunge
maalumu maana yake ni kwamba Rasimu ikajadiliwe na Bunge hilo ili kama kuna
mapungufu yaondolewe katika kuiboresha kabla haijawa Katiba kamili. Moja ya
mapungufu yaliyojionyesha katika Rasimu hiyo ni hilo la muundo wa serikali
tatu, muundo ambao vyama tawala, CCM na CUF, vilikuwa makini kabisa kuliepuka
kutokana na madhara yanayotishia kutokea kufuatia serikali kuukumbatia muundo
wa muungano aina hiyo.
Kwa mantiki
hiyo tutaona kwamba kinachoongelewa na Ukawa kwamba Rasimu iheshimiwe hakina
mashiko yoyote.
Kitendo cha
CUF kutoulinda msimamo wake, kama ilivyo CCM inayoulinda wa kwake, ndicho
kinachonipa wasiwasi na kunifanya nishindwe kukiamini chama hicho. Chama
ambacho kwa zaidi ya miaka mitano kimeongoza nchi, kupitia kwenye maridhiano na
muafaka, bila matatizo yoyote katika
muundo wa serikali mbili, leo hii
kinasema lazima katiba mpya iandikwe kwa mfumo wa serikali tatu!
Kwa msimamo
huo wa kuyumbayumba wa chama hicho tunaweza kukiamini kile ambacho kimekuwa
kikisemwa muda wote kuwa chama hicho kina ajenda ya siri. Si ajabu, katika
usiri huo, yakajitokeza yale ya kwamba kinataka Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar uvunjike ili kiweze kuirudisha hali iliyokuwepo Zanzibar kabla ya
Mapinduzi Matukufu ya 1964, kwa maana ya kuurudisha utawala wa kisultani.
Muungano wa
serikali tatu ni hoja iliyokuwa inashikiliwa na wapinzani. Maana ya upinzani ni
kuupinga utawala uliopo madarakani hata kama upinzani huo hauna hoja
zinazojitosheleza. Lakini hatutegemei chama kinachoongoza dola kijipinge
chenyewe. Kwa hapa CUF ni chama tawala sio chama cha upinzani. Kitakuwaje chama
cha upinzani wakati Katibu wake Mkuu, Maalimu Seifu, akiwa ni makamu wa rais wa
serikali iliyoko madarakani, hata kama ni kwa upande mmoja wa muungano?
Ina maana
mtu anaweza akawa madarakani halafu akawa mpinzani? Anampinga nani kama
hajipingi yeye mwenyewe?
Kilichomfanya
Maalimu Seif akawa makamu wa kwanza wa rais kwa upande wa Zanzibar, wakati
chama tawala ni CCM, ndicho kinachonifanya niamini kwamba CCM na CUF kwa sasa
ni kitu kimoja.
Sioni ajabu
yoyote kwa vyama vya upinzani, mfano, Chadema, NCCR Mageuzi, DP na vinginevyo, kutaka kuwepo na muundo wa serikali mbili,
maana hayo ndiyo malengo ya upinzani. Lakini inapotokea hata chama kilicho
madarakani kikajiunga na upinzani kwa madai ya kuyakataa yanayoendeshwa na
utawala au kuupinga mfumo wa utawala pamoja na muundo wa serikali iliyoko
madarakani, ni lazima tuhisi kuwa kuna
kinachoendelea chini ya uvungu. Hali hiyo ni lazima ilete mashaka kabla ya
kuiunga mkono.
Kwahiyo
tunaposema Ukawa hatunabudi kuuelewa vizuri umoja huo una lengo gani. Hatuwezi
kujiridhisha tu kwamba huo ni Umoja wa katiba ya Wananchi kama wenyewe
unavyojinadi, sababu katiba inayoandaliwa ni ya wananchi. Sasa kunapojitokeza
kinachojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi tuelewe nini? Kuna siri gani katika
kitu hicho, hasa pale umoja huo unapoonekana kushinikizwa pamoja na kuongozwa
na chama kilicho Ikulu?
Watanzania
tunapaswa kuongozwa na umakini katika mchakato huu unaoendelea wa kuandika
Katiba mpya ya nchi yetu, vingenevyo tukiuachia upofu ndio utuongoze si ajabu
hawa wanaojiita Ukawa tukashtukia wanatufanyia mazingaombwe. Tuwe macho na
kikundi hiki cha UKAWA kama kweli tunaitakia nchi yaliyo mema.