Bukobawadau

MADIWANI WILAYANI MULEBA WAONYESHA WASIWASI KWA WATENDAJI

MULEBA:Na Mwandishi wetu, May 16, 2014
BAADHI ya maafisa watendaji wa vijiji na wataalamu wa miradi katika halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera wamelalamikiwa kwa kufuja fedha za wananchi na kujenga miradi iliyo chini ya viwango ili  kuleta maendeleo.
Wakichangia hoja ya  kupunguza changamoto za utekelezaji wa miradi ya maendeleo jana  kwenye kikao cha  robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2013/14  januari hadi  madiwani hao wamesema watendaji hao ni bora wakawajibishwa
Diwani wa kata ya Ruhanga wilayani Muleba  Robert Thadeo amesema baadhi ya watendaji wamekaa katika vituo vya kazi kwa muda mrefu tena katika maeneo wanakozaliwa na kuwa miungu watu na kufanya kazi kinyume na taratibu
Thadeo ametolea mfano mtendaji wa kijiji cha Ruhanga Fortunatus Stima ambaye ni mzaliwa na mkazi wa kijiji hicho  na alipata kazi ya kuwa kiongozi na sasa ameshamaliza miaka 25 bila kupelekwa sehemu nyingine.
Amesema mtendaji huyo hajiwezi kwa kuandika mihtasari ya vikao wala mikutano na wala hajihusishi na mikutano ya kijiji kwa mujibu wa taratibu badala yake ni kutumia muda mwingi kwa ulevi saa za kazi pamoja na rushwa.
“Mtendaji wa kijiji hicho kwa sasa anaongoza vijiji vya Ruhanga na Malele na anafanya kazi bila mshahara lakini anadhulumu michango ya ujenzi wa zahanati na shule ya sekondari kwanini asiondolewe ama kustaafishwa?”Alihoji Thadeo
Alisema mwenzake wa kijiji cha Makongora ameshakusanya Sh.400, 000/-  kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha maabara  lakini mtendaji wa kijiji cha Ruhanga anazo Sh.20,000/- pekee jambo ambalo linaonesha uwajibikaji wake ni hafifu.
Pamoja na hayo diwani wa kata ya Muleba Hassan Millanga amesema halmashauri haina budi kufuatilia migogoro ya kiutendaji baina ya madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo ambao wameanza kuingia hatua ya  kushtakiana mahakamani .
Milanga ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maafa katika halmashauri hiyo alisema madiwani wameingia kwenye migogoro wengine wakishtakiana na mkuu wa wilaya hiyo Lambris Kipuyo na wataalamu wa halmashauri
 Alisema  mhadisi wa barabara na afisa ardhi wamesababisha migogoro kwa kupitisha barabara za mitaa kwenye maeneo ya wananchi bila kuzingatia ramani   ambapo walioporwa ardhi wamelalamika na kufungua kesi mahakamani
Hata hivyo kaimu mkurugenzi John Nko  na kaimu mwenyekiti wa halmashauri  Alhaji Swaibu Mfuruki wamesema  watendaji wanaolalamikiwa watafanyiwa uchunguzi na  madiwani wenye kesi wawe na subira kupata suluhu la mahakama.
Next Post Previous Post
Bukobawadau