Bukobawadau

MSUGUANO KCU

Na Prudence Karugendo
KUMEKUWEPO  na msuguano mkubwa katika chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha Kagera kati ya mwakilishi wa chama cha msingi cha Kamachumu, Muleba Kaskazini, Archard Felician Muhandiki, kwa upande mmoja,  na uongozi wa KCU (1990) Ltd.
 kwa upande mwingine. Msuguano huo umekuwa mkubwa kiasi cha uongozi wa chama hicho kufikia hatua kuonekana unakiuka maadili ya ushirika kwa kumtenga mwakilishi huyo wa chama cha msingi, ukimfukuza na kumzuia asishiriki vikao vya KCU ambavyo yeye ni mwakilishi halali wa wanaushirika!
Kitendo hicho cha mwakilishi wa chama cha msingi kufukuzwa kwenye mikutano ya chama kikuu ni dhahiri kinakiuka maadili ya uongozi wa ushirika, sababu kinakikosesha uwakilishi chama cha msingi ambacho, pamoja na vyama vingine vya msingi, ndivyo vinavyounda chama kikuu. Kwa mantiki hiyo hakuna mwanaushirika anayepaswa kujiona bora kuliko mwingine kiasi cha kumuamuru mwanaushirika mwenzake atoke nje ya mkutano wa ushirika, na ikizingatiwa kwamba anayeamriwa kutoka nje ya mkutano ni mwakilishi wa wanaushirika wengine.
Moja kwa moja kitendo hicho kinakuwa kimewapora mali yao wanaushirika wa chama husika cha msingi, sababu chama kikuu ni mali yao.
Hali hiyo ya uongozi wa ushirika, au wajumbe (wawakilishi) kutoka vyama vingine vya msingi, kumfukuza na kumtenga mwakilishi mwenzao inaonekana kutishia mustakabali wa ushirika. Sababu katika hali ya kawaida ushirika ni kushirikiana na kufanya mambo yote kwa pamoja, wala sio kufukuzana na kutengana. Kinyume chake ni kwamba hakuna ushirika hapo, bali ni mkusanyiko tu wa watu wenye malengo tofauti tofauti.
 Baada ya kuusikiliza mkwaruzano huo kwa muda mrefu, huku kila upande ukitoa tuhuma za hapa na pale dhidi ya upande mwingine, ambapo upande wa uongozi wa KCU, pamoja na mambo mengine, ukidai kwamba mwakilishi Muhandiki  sio mwanaushirika halali, wakati mwakilishi huyo kwa upande wake akisema kwamba kuna mambo ambayo uongozi wa chama hicho kikuu hautaki kuyaweka wazi ili wanaushirika wote wayaelewe, nimeamua kwenda Bukoba na Kamachumu kushuhudia kinachoendelea kati ya mwakilishi huyo na uongozi wa chama hicho kikuu cha ushirika ili nijaribu kupata kiini cha mkwaruzano huo.
Kwanza kabisa nilitaka kujua kwa nini mwanaushirika huyo, aliye pia mwakilishi wa chama chake cha msingi, anatendewa vitendo na chama chake kikuu cha ushirika sawa na mtu aliye mvamizi katika chama hicho.
Tuhuma nilizokutana nazo dhidi yake ni za kwamba,  mbali na yeye kuuchokonoa ushirika kwa kuulizia mambo ambayo uongozi wa ushirika huo hauoni umuhimu wa kuyaweka wazi, yeye si mwanachama halisi kwa vile hana shamba la mibuni mahali popote. Na inasemwa kwamba ili mtu awe mwanachama wa chama kile anatakiwa awe na shamba la mibuni kwa vile ndiyo inayozalisha zao linaloshughulikiwa na chama hicho, kahawa.
Wanaotoa tuhuma hizo wanashangaa inakuwaje mtu asiyeona umuhimu wa kulima mibuni anavyoweza kujiweka mstari wa mbele katika kuulizia jinsi zao la kahawa linavyoendeshwa katika chama hicho cha wakulima wa mibuni.
Baada ya hapo nikaenda kumuona Mzee Muhandiki kijijini kwake Kamachumu. Nilipomweleza tuhuma zinazomkabili akaamua kunitembeza katika baadhi ya mashamba yake ili nijionee mwenyewe kinachosemwa kusudi niweze kuzipima tuhuma hizo zinazotolewa dhidi yake pasipo kumwachia yeye ajitetee kwa maneno tu.
Katika mashamba yake niliyoyatembelea nilikuta mibuni mingi, ndipo akasema sasa naweza kuzipima vizuri tuhuma zinazotolewa kwake kwamba hana shamba la kahawa na kuona kama ni za kweli au za hila.
Mbali na hiyo akasema kwamba anao ndugu na jamaa wengi ambao ni wakulima wa kahawa. Akaongeza kwamba ushirika haupo kushughulikia kahawa zake tu, kwamba yeye anapopiga kelele kuhusu KCU kuwapunja wanaushirika kwa njia mbalimbali, hajilengi yeye binafsi bali anawalenga wanaushirika wote kwa ujumla wakiwemo ndugu na jamaa zake.
Akijibu swali langu la ni kitu gani kinachomkereketa mpaka akajiona anawajibika kuwasemea wakulima wengine wa kahawa,  alisema kama ifuatavyo. “Mimi siutegemei ushirika hata kidogo katika kuendesha maisha yangu. Ila ninao ndugu na jamaa zangu ambao shughuli yao kubwa ni kilimo, wanakitegemea kilimo kuendesha maisha yao. Hivyo anapotokea mtu akawakwaza anakuwa amenikwaza na mimi vilevile.”
“Sababu siko tayari kuwaona ndugu zangu wanaadhirika na ukata ilhali wanalo zao zuri la kibiashara,  halafu niseme watajijua na ushirika wao, ni lazima niingilie kati na kuwasaidia. Hayo ndiyo maumivu ninayoyapata kutokana na uzembe unaojitokeza ndani ya ushirika wetu.”
Mzee Muhandiki anasema kwamba kwa sasa anasomesha watoto 30 nje ya nchi ambao ni watoto wa ndugu na jamaa zake. Hivyo anasema kwamba kama KCU ingekuwa inafanya mambo yake kiuadilifu na kuwafanya ndugu zake hao wapate kipato chao halisi kinanachotokana na kilimo cha zao lao la biashara, eti hadhani kama angelazimika kuubeba mzigo wote huo.
Eti jasho lao katika kilimo lingewatosha kujisimamia, lakini eti kwa sasa jasho lao linaonekana kufyonzwa na watu wengine na kuwaachia ndugu zake ukata!
Kwahiyo anasema kinachomkereketa ni jinsi KCU inavyombebesha mzigo unaotokana na ukosefu wa uadilifu ndani ya chama hicho cha ushirika.
Anasema kwamba tatizo hilo sio kwamba linampata tu yeye peke yake, eti ni wengi wenye tatizo kama la kwake, wanaolazimika kuwasaidia ndugu na jamaa zao wakati watu hao wanaosaidiwa wakiwa ni wakulima wanaozalisha zao hilo la biashara, kahawa. Lakini eti watu hao wanajikuta wanashindwa kujiinua kiuchumi kutokana na mpangilio usioridhisha wa chama kilichoundwa na wakulima hao kwa ajili ya kulishughulikia zao lao la biashara.
Tatizo kubwa analoliona Mzee Muhandiki ni la ile tabia kongwe iliyojengeka katika jamii ya Wahaya ya “kakitandugao” yenye maana ya kwamba hata kama jambo naliona pamoja na ubaya wake siwezi kulisema, isije ikaonekana kwamba limeanzia kwangu, “kakitandugao”.
Kwahiyo eti tabia ya uwazi aliyo nayo yeye, mwakilishi huyo wa chama cha msingi Kamachumu, ambayo ni kinyume na “kakitandugao” ya kutaka kila kitu kinachofanyika katika chama kikuu kiwe wazi na kujulikana kwa wanaushirika wote,  ndiyo inayomchongea na kumfanya aonekane mbaya kwa baadhi ya viongozi wa ushirika na wawakilishi wa vyama vingine vya msingi.
Sababu baadhi ya wajumbe, wawakilishi wa vyama vya msingi, kwa jinsi nilivyoshuhudia mwenyewe, wanaonekana kukifurahia zaidi kile wanachokipata kwenye uwakilishi wao kuliko kushughulikia matatizo yanayowapata wanaushirika kwa ujumla.
Nilipokuwa Kamachumu, Muleba Kaskazini, Kagera, nilitembelea baadhi ya vyama vya msingi, Ibuga, Kamachumu na Bushagara, na kukutana na wadau wa ushirika katika vyama hivyo.
Wengi nilioongea nao waliyataja mambo yanayowasumbua katika kilimo chao cha kahawa, huku wakishangaa ni kwa nini chama chao cha KCU kinashindwa kuyashughulikia. Katika hilo wapo waliozipongeza juhudi za Muhandiki za kuitaka KCU kujiweka wazi mbele ya wanaushirika.
Pamoja na pongezi hizo kwa Muhandiki, wapo wachache waliosema kwamba uwakilishi wake hauna uhalali! Nilipotaka kuelewa wanaosema hivyo wanatoka chama gani cha msingi nikakuta wote hawatoki katika chama cha Kamachumu anachokiwakilisha Muhandiki!
Kwahiyo sikuelewa uhalali wa uwakilishi unaosemwa na watu hao ni upi, maana kuna aina mbili za uwakilishi kulingana na nilivyojionea mwenyewe. Wapo wawakilishi wanaoonekana wanawania tu posho za vikao vya chama kikuu lakini bila kusema lolote la kuwanufaisha wanaushirika wenzao waliowatuma kwenye vikao hivyo. Wawakilishi wa aina hiyo wakishasaini posho zao wanaona mambo yote yamenyooka, kwahiyo hata kuingia kwenye vikao husika wanakuchukulia kama usumbufu tu.
Wanachokifanya wawakilishi wa aina hiyo ni kushangilia kila jambo na kuwazomea wanaotaka kujua kitu gani kimeendaje ndani ya ushirika!
Aina ya pili ya uwakilishi ni ya wale walio na maswali ya kutaka kujua mwenendo wa chama chao kikuu cha ushirika ulivyo. Wajumbe wa aina hiyo ndio wanaoitwa wakorofi. Muhandiki yuko upande huo.
 Nimelishuhudia hilo Aprili 29, 2014, wakati mwakilishi Muhandiki alipozuiwa kuingia kwenye mkutano wa mizania wa KCU (1990) Ltd. kwa sababu ambazo sikuzielewa kwa undani.
Lakini nikiwa nje ya ukumbi wa mikutano, baada ya kuzuiwa na walinzi kwamba mimi sitakiwi kabisa ndani ya mkutano huo, ambapo baadaye niliruhusiwa kuingia, niliwasikia baadhi wawakilishi wakikipongeza kitendo hicho cha mwakilishi huyo wa Kamachumu kuzuiwa kuingia kwenye mkutano! Nilipojaribu kuwahoji kwa nini wanakifurahia kitendo hicho kinachokiuka maadili ya ushirika, walinijibu kwamba mtu huyo hatabiriki. Wakasema kwamba anaweza hata akaja na hoja ya kuwa posho ziondolewe katika vikao vya KCU (1990) Ltd.!
Kusema ukweli majibu hayo yalinivunja nguvu na kunifanya nishindwe kuuona mustakabali mwema wa ushirika. Nilijiuliza inawezekanaje kuujenga ushirika imara iwapo wawakilishi wa wanaushirika wanawaza posho tu badala ya kuuwaza ushirika wao? Na je, wakulima wengine ambao ni wanaushirika lakini si wajumbe wa vikao vya chama kikuu wananufaikaje na ushirika wao?
Nilipomtafuta Mzee Muhandiki anipe maoni yake juu ya posho zinazotolewa na KCU kwa wajumbe, alijibu kwamba hiyo ni mojawapo ya mambo yanayouua ushirika. Anahoji ni kwa nini watu wanaokwenda kushughulikia jambo lililo lao wategemee kulipwa posho? Kwa mtazamo wake anaona posho zinapaswa ziondolewe kabisa.
Kilichonishangaza ni kwamba mwanzoni mwa mkutano wa mizania wa KCU (1990) Ltd. wa tarehe 29 Aprili, 2014, nilizuiwa kuingia mkutanoni kwa madai ya kwamba muda wote naandika mambo yanayoisumbua KCU! Madai mengine yalikuwa kwamba mimi nimepelekwa pale na Muhandiki ili nikaandike mambo ambayo pengine uongozi wa KCU hautaki yawe wazi! Lakini baadaye niliruhusiwa kuingia.
Kwa kadiri nilivyoona na kujiridhisha ugomvi kati ya Muhandiki na KCU ni kuhusu uwazi. Mwakilishi huyo anataka uwepo uwazi katika ushirika huo, wakati kwa upande wa KCU uwazi unaonekana ni sumu kwake!
Nimalizie kwa kusema kwamba ushirika ni uwazi, kuvumiliana, kustahiana, kuelewana na kukubaliana kwa manufaa ya pamoja. Kila mwaushirika anapaswa apewe nafasi ya kujieleza na kuhoji chochote kinachohusu ushirika husika. Na hapanabudi jibu lipatikane ili ushirika usonge mbele.
Vinginevyo, kufukuzana, kutengana, kubaguana na kuwekeana vinyongo ni ishara ya kwamba ushirika umevunjika. Sababu ushirika bila uwazi, upendo, kuelewana na kukubaliana ni kujidanganya tu, hakuna ushirika hapo.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau