NDUNGAI ANUSURIKA KIPIGO VURUGU ZA VIJANA KONGWA
Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
amenusurika kujeruhiwa na kundi la vijana waliokuwa wakipinga ongezeko
la ushuru wa mazao na kuvamia ukumbi wa mkutano wa Kilimo uliopo
Kibaigwa, wilayani Kongwa.
Katika vurugu hizo, ambazo zililazimisha polisi
kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya waandamanaji, pia mali
mbalimbali ziliharibiwa, likiwemo gari la Mbunge wa Tanga Mjini, Omary
Nundu.
Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, David Misime
alisema vurugu hizo zilitokea juzi saa 7.30 mchana katika Mji mdogo wa
Kibaigwa. Alisema jumla ya watu 34 wanashikiliwa wakihusishwa na vurugu
hizo.
Misime alisema vijana wanaokadiriwa kuwa zaidi ya
300, wakishirikiana na wabeba mizigo wa Soko Kuu la Mazao la Kibaigwa
walifanya maandamano bila kibali na kung’oa bango la Halmashauri ya
Wilaya ya Kongwa.
Alisema bango lililong’olewa ni la tangazo la
kuzuia wafanyabiashara kuingiza mazao sokoni bila kulipa ushuru
uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Kamanda huyo alisema viwango vya ushuru
vinavyotozwa vilipanda tangu Julai Mosi mwaka jana. Kwa mujibu wa
viwango vipya, ushuru wa gunia la kilo 100 za karanga ulipanda kutoka
Sh1,000 hadi Sh3,000, gunia la mahindi kutoka Sh500 hadi Sh1,000, dumu
la mafuta ya alizeti lilianza kutozwa Sh500, gunia la mashudu Sh1,000 na
gunia la alizeti Sh1,000. Viwango hivyo vinapingwa na wabeba mizigo.
“Vijana hao wabeba mizigo walifanya fujo kwa
kufunga Barabara kuu ya Dodoma – Morogoro kwa mawe na kuchoma matairi,
pia walivamia maduka na baa za jirani na kupora vinywaji na kuvunja
majokofu na kusababisha uharibifu mkubwa,” alisema Misime.