Bukobawadau

WATOTO WAWILI WAFA MAJI MJINI BUKOBA

WATOTO wawili wakazi wa jijini Dar es Salaam wamefariki dunia juzi walipokuwa wakiogelea kwenye Ziwa Victoria, eneo la gati la Kishimba mjini Bukoba.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, George Mayunga, aliwataja watoto hao kuwa ni Irene Alloys (14) mkazi wa Migombani na Mariam Juma (11) mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam.
Alisema tukio hilo liligunduliwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kastam, ambaye alifanikiwa kuopoa mwili wa mtoto mmoja akishirikiana na baadhi ya wananchi kisha kutoa taarifa Kituo cha Polisi Bukoba Mjini.

Alisema baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hiyo walifika eneo la tukio na kuendelea kutafuta mwili wa mtoto mwingine aliyekuwa hajapatikana.
Kamanda Mayunga alisema haijajulikana watoto hao walikuwa wanaishi kwa nani mjini hapa, wala mwenyeji wao.
Alisema uchunguzi unafanyika ili kubaini watoto hao waliletwa na nani, kwa malengo gani ama kama walikuwa wenyewe walitumwa na wazazi wao ama vipi.

Taarifa zilizopatikana zinaeleza watoto hao walitoroka kutoka jijini Dar es Salaam wakiwa na mtoto mwingine wa kiume kwa sababu ambazo hazijafahamika na kupelekwa na wasamaria wema katika kituo kikuu cha polisi.
Kutokana na kutokuwa na mahali pa kuishi walikuwa wakiishi katika mazingira ya kituo hicho mjini Bukoba kwa takriban wiki moja hadi walipotoroka kwenda kuogelea na kukutwa na mauti hayo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau