CCM NA KERO ZA WANANCHI
Miaka 60 CCM ndipo inakumbuka kero za
wananchi!
Na Prudence Karugendo
MTU mmoja nisiyeelewa yuko upande gani kiitikadi,
kama anafuata itikadi za upinzani au za chama tawala, kanipa wazo la
kufikirisha kama mojawapo ya changamoto za kisiasa.
Kanitumia
ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yangu akisema hivi, “Kinana wa CCM
anazunguka nchi nzima akisikiliza kero za wananchi, Slaa wa Chadema anazunguka
nchi nzima anahubiri serikali tatu. Je, ni yupi tumuombee dua ya mafanikio?”
Katika
kutafakari kwangu nagundua jambo la kushangaza. Kinachonishangaza ni namna
baadhi ya watu wanavyovilinganisha hivi vyama viwili, CCM na Chadema. Maana
kuvilinganisha hivi vyama ni sawa ni na kulinganisha mzee wa miaka 80 na kijana
wa miaka 20.
Ni lazima
kutakuwepo na tofauti kubwa inayoletwa na kupishana sana kwa umri wa watu hao
wawili, mzee na kijana. Mzee ni lazima atakuwa ameyaona mengi, amefanya mengi
au kushindwa mengi kuliko kijana anayelinganishwa naye.
Kwahiyo mzee
kukubali kulinganishwa na kijana, hata kama hakutamka, ni lazima atakuwa
amekubali kushindwa.
Tukiviangalia
vyama vya CCM na Chadema tutaziona tofauti za wazi zinazotokana na kupishana
sana kwa umri wa vyama hivyo. Ni sawa na tofauti zilizokuwepo kati ya chama cha
TANU, kilichokuwa kinapigania uhuru na wakoloni waliokuwa wanatutawala.
Wakati TANU
ikionyesha athari za kutawaliwa wakoloni walikuwa wakidai kwamba chama hicho
hakijawafanyia lolote wananchi!
Sasa wakati
CCM inachezea kwenye umri wa miaka 60 Chadema ndio kwanza inachezea kwenye umri
wa miaka 20. Ni tofauti kubwa sana ambayo kwa mtu mwenye aibu ni vigumu
kutamani kulinganishwa na mtu aliyemzidi kwa kiwango hicho.
Kwa mantiki
hiyo, anayekubali kulinganishwa na mtu aliyemtangulia umri kwa kiasi kikubwa
namna hiyo atakuwa anakiri kushindwa kuitumia vizuri tofauti hiyo ya umri
kukifanya kile alichopaswa kuwa amekifanya.
Sababu mbali
na uzoefu unaotokana na umri mkubwa ilio nao CCM, chama hicho kimekuwa
madarakani kwa zaidi ya nusu karne, lakini Chadema ndio kwanza inataka ipewe
ridhaa ya kuonyesha namna ya kuongoza.
Mbali na CCM
kuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, chama hicho kimeendesha udikteta wa
kutawala kimabavu, bila kutaka kuuona upinzani wowote kwa zaidi ya robo karne!
Lakini kwa
wakati huu chama hicho tawala kinajinadi kwa wananchi kikitaka kilinganishwe na
Chadema huku kikihoji Chadema imewafanyia nini wananchi kana kwamba kuna wakati
kiliwahi kuona Chadema inatawala kama chenyewe kilivo!
CCM
kinajinadi kama chama kipya huku wakati mwingine kikilia na kupiga mayowe kuwa
kinaonewa na Chadema, kikitaka kupata
huruma ya wananchi kama vile chenyewe na Chadema viko sawa kiumri na kiuwezo!
Chama tawala
kinasahau kuwa uzembe wake ndio umevizaa vyama vya upinzani kikiwemo Chadema.
Maana bila uzembe huo sidhani kama kungekuwepo na mwananchi yeyote ambaye
angekuwa anaufikiria upinzani kwa vile kila jambo lingekuwa katika mstari wake.
Wakati huu
ambapo chama kichanga, Chadema,
kinajaribu kufanya kazi ya kuwafumbua wananchi macho ili wauone, wauelewe,
wautambue na kuuthamini muundo wa taifa lao, kazi kama iliyofanywa na TANU enzi
za wakoloni, CCM eti ndio kwanza inajaribu kusikiliza na kuzielewa kero za
wananchi! Tuseme muda wote huo wa zaidi ya nusu karne haikujuwa kama wananchi
walikuwa na kero! Hicho ndicho chama tawala!
Ni yaleyale
yaliyokuwa yakifanywa na wakoloni katika kuzikata makali harakati za TANU za
kuwafumbua macho wananchi ili waione, kuitambua na pia kuidai nchi yao toka
kwenye makucha ya wakoloni.
Hivi kama
kweli CCM ingekuwa nao uwezo wa kuzisikiliza kero za wananchi ingekuwa
inazitafuta hivi sasa baada ya miaka 60 ya uwepo wake? Kipindi hicho
kisingetosha kuifanya ikawa inazielewa kero za wananchi kama mtu anavyolielewa
jina lake? Kinana angelazimika kuzunguka nchi nzima akifanya kazi hii
anayoifanya kwa sasa?
Tunachoweza
kusema ni kwamba CCM haikutaka kutatua kero hizo na sasa imejikuta imekwama,
haiwezi tena kuzitatua kero hizo. Kwahiyo inachokifanya ni kujaribu kukwamisha
juhudi za Chadema na vyama vingine vya upinzani za kuwafumbua wananchi macho.
Inachokifanya
Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kwa sasa ni kuwafanya
wananchi wautambue kwanza muundo wa taifa lao, hiyo ndiyo kero namba moja.
Bila
kuitambua kero hiyo, tiba ya kero
zilizobaki haiwezi kupatikana kamwe. Itapatikana tu dawa ya kutuliza maumivu ya
kero wakati kero zenyewe zikibaki palepale kama CCM ilivyodumu nazo kwa miaka
60.
Sababu hiyo
ni kero iliyodumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa pamoja na kwamba kila kitu ambacho
kingewafanya wananchi wayafurahie maisha yao ndani ya uhuru wao kimekuwepo muda
wote kikiwa kimejaa tele.
Kwa ufupi ni
kwamba kero zote zinazotajwa na wananchi zimetokana na kero hiyo kuu
iliyosababishwa na CCM na kuendelea kulindwa na chama hicho kwa muda wote huu.
Nimejaribu
kufuatilia kampeni za pande hizi mbili, CCM na upinzani, dhidi ya masaibu
yanayowapata Watanzania kwa sasa na kugundua kitu fulani. Sijasikia hata mara
moja wapinzani wakiacha hoja na kushambulia nafsi za watu kwa njia ya kuparamia
kama wanavyofanya CCM.
Mfano, maneno kama jitu, zee, nene, refu, fupi
nakadhalika, ni maneno yanayotolewa pale mtu anapokuwa ameishiwa hoja. Sababu
unene wa mtu, urefu au ufupi wake havina uhusiano wowote na matatizo
yanayowapata wananchi.
Lakini mara
zote ninazomsikiliza Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, nasikia anasema zee
hili limezeeka vibaya, zee hili lina kono sijui limekaaje, sijui lile
linaongeaje! Ilmradi tu ni maneno ya kashfa na matusi kwa kwenda mbele.
Sio kwamba
wapinzani hawawezi kutukana, ila kinachoangaliwa ni kazi iliyopo mbele yao. Kwa
nini wapoteze muda kutukana wakati wanacho cha kuwaeleza wananchi? Asiye na cha
kueleza ndiye anayelazimika kujaza pengo kwa mitusi.
Mtu
anayeonekana anaukashfu uzee tunawezaje kusema anaunufaisha upande
anaoupendelea? Maana atakuwa anawakashfu kuanzia wazazi wake, viongozi wake na
wapenzi wa chama chake waliomzidi umri, kwa vile hakuna upande unaokosa watu wa aina
hiyo.
Kwa
tunaofuata hoja mara moja tunaelewa kwamba pale mtu anapopungukiwa hoja anaamua
kupajazia kwa tusi. Lakini je, tusi linaweza likaziondoa kero zinazotajwa?
Kwa mtindo
huo kweli tushawishike na kuamini kuwa CCM inatafuta kero za wananchi? Na kama
kweli inazitafuta tukubali kwamba itazitatua?
Kero
zilizoishinda kwa miaka 60 kweli itazitatua kwa mtindo uleule ambao umezifanya
kero hizo zikarundikana mithiri ya Mlima Kilimanjaro?
Kwa nini
tusiamini kwamba Chadema ndiyo inaweza ikazitatua kero hizo baada ya kupagundua
zilikorundikana na kukielewa chanzo cha kuzifanya zikarundikana? Huyo ni mganga
mpya aliyekuja na dawa mpya baada ya kulielewa tatizo.
Tuchukulie
kwamba mtu anasumbuliwa na maradhi fulani kwa muda mrefu, mganga yule ambaye
kashindwa kumsaidia kwa muda wote anakuja na dawa ileile iliyoshindikana kuleta
nafuu akidai kuwa itasaidia, kusudi mgonjwa asiitamani dawa mpya inayoletwa na
mganga mpya. Kukubaliana na mawazo ya mganga aliyeshindwa ni nini zaidi ya
kujitakia donda ndugu?
Ieleweke
kwamba huu sio wakati wa kuuziana mbuzi kwenye gunia, hii ni karne ya uwazi.
Chama chenye umri wa miaka 60 hakiwezi kusema sasa hivi ndipo kinasikiliza kero
za wananchi. Kwa umri kilo nao na kwa namna kilivyojijenga, ikiwa ni pamoja na
kutumia mabavu kuviondoa vyama vingine ili kibaki peke yake na kuendesha nchi
kiimla, kilipaswa kuwa kinazielewa kero za wananchi hata zile ambazo hazijajitokeza.
Kujifanya
kinaulizia kero za wananchi kwa wakati huu ni kutaka kukwepa aibu na kutokubali
kushindwa.
Vyama vya
upinzani, au tuseme Chadema, kama mleta mada alivyotaka iwe, ndivyo tunavyoweza
kuvifikiria katika utatuzi wa kero za wananchi zilizotamalaki kwa sasa. Sio
chama ambacho kimeshindwa kwa miaka 60.
Kwa wakati
huu CCM isingekuwa inajifanya kusikiliza kero, ingekuwa inatafuta wapi
paboreshwe baada ya kero zote kuwa zimefutika. Imeshindwa. Kwahiyo hayo ya kero
za wananchi iviachie vyama vya upinzani ili navyo vionyeshe ni kitu gani
vinaweza kukifanya kuhusu kero hizi zilizorimbikizwa na CCM kwa zaidi ya miaka
50.
Nimalizie
kwa kusema kwamba anachokifanya Kinana na timu yake ya kina Nape, ni sawa na
muziki wa zilipendwa, kwa maana ya kwamba sio kitu kipya wanachokionyesha na
kukifanya. Kwa watu wenye kutafakari hiki ni kitu kilichopitwa na wakati na
sasa kimekwama, sababu kilianza kufanyika tangu mwaka 1957.
Jibu langu
kwa swali mtoa mada ni kwamba, nadhani ni hekima na haki tukamuombea dua ya
mafanikio Slaa.
0784 989 512