TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika kutekeleza kazi
ya mbunge ya kuisimamia Serikali itakumbukwa kwamba tarehe 12 Mei 2014
nilichukua hatua bungeni ya kutaka Serikali kutatua kwa dharura matatizo katika
mtambo wa maji wa Ruvu Juu yenye kukosesha maji kwa wananchi wa Mkoa wa Dar Es
Salaam na Pwani.
Nilitaka kwa mujibu wa
Kanuni ya 49 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la mwaka 2013, Waziri wa Maji
Prof Jumanne Maghembe atoe kauli bungeni juu ya matatizo ya maji katika maeneo
yanayohudumiwa na mabomba kutoka katika mtambo kwa kuweka bayana iwapo kuna
hujuma na kurejesha kwa haraka huduma kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo
hali ya upatikanaji wa maji iliongezeka katika maeneo machache ndani ya siku
chache lakini kwa sasa katika maeneo mengi yanayohudumiwa na mabomba kutoka
katika mtambo wa Ruvu Juu katika kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani,
Kimara, Saranga, Ubungo na Makuburi matatizo ya maji yamejirudia.
Katika kuendelea
kutekeleza wajibu wa kibunge wa kuishauri na kuisimamia Serikali natoa mwito wa
wazi kwa wenyeviti wa bodi za Wakurugenzi na Maafisa Watendaji Wakuu wa Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka Dar Es Salaam
(DAWASA) na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ndani ya siku tatu
kusimamia kazi ya dharura kuhusu matatizo ya mtambo wa maji wa Ruvu Juu
yanayoendelea mpaka hivi sasa.
Aidha, ndani ya siku
hizo tatu wajitokeze mbele ya vyombo vya habari kutoa maelezo kwa umma kueleza
kwanini mpaka sasa huduma ya maji katika maeneo mengi katika Jimbo la Ubungo na
Jiji la Dar Es Salaam kwa ujumla
yanayohudumiwa na mabomba yanayotoka katika mtambo wa Ruvu Juu hayapati huduma
ya maji inavyostahili na lini matatizo yaliyopo yatapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande mwingine,
ndani ya muda huo huo wa siku tatu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ajitokeze
mbele ya vyombo vya habari na kueleza umma matokeo ya uchunguzi uliopaswa
kufanyika ndani ya mwezi mmoja kubaini kama matatizo ya mara kwa mara ya Mtambo
wa maji wa Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa mengine ya kibinadamu.
DAWASA, DAWASCO na
Wizara ya Maji wasipojitokeza ndani ya siku tatu mbele ya vyombo vya habari
kutoa maelezo kwa umma nitachukua hatua za kibunge nitakazoona zinafaa dhidi ya
Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kwa kulidanganya Bunge kupitia kauli ya
Serikali aliyotoa Bungeni mwezi Mei 2014.
Ikumbukwe kwamba tarehe
12 Mei 2014 ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa mbunge wa kuwawakilisha wananchi
nilieleza Bunge kwamba matatizo katika mtambo wa Ruvu Juu yamekuwa
yakijirudiarudia kwa nyakati mbalimbali kwa kipindi cha takribani miezi mitatu
kati ya Januari mpaka Mei 2014 katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakipata
mgawo wa maji.
Nilichukua hatua hiyo
kwa niaba ya wananchi wanaohudumiwa na
mtambo huo katika kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara,
Saranga, Ubungo na Makuburi kwenye Jimbo
la Ubungo; na kata mbalimbali za majimbo ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini,
Segerea nk.
Kufuatia hatua hiyo,
Mwezi Mei 2014 Waziri wa Maji Prof. Maghembe alitoa kauli ya Serikali ya kueleza
matatizo yanayoukabili mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu kwa ajili ya Jiji
la Dar es salaam na maeneo ya DAWASA katika mkoa wa Pwani.
Katika kauli yake
Waziri Maghembe alikiri kwamba kwa takribani siku 67 (kati ya tarehe 01.03.2014
na tarehe 06.05.2014) mtambo ulizalisha maji chini ya kiwango na kufikia kati
ya lita milioni 8.2 na lita milioni 57.4 ikilinganishwa na lita milioni 82 kwa
siku, ambazo ndio uwezo halisi wa mtambo huo.
Katika kauli yake
bungeni, Waziri Maghembe aliorodhesha matatizo ya mtambo wa Ruvu Juu kuwa ni:
Kuharibika kwa pampu mara kwa mara kunakosababishwa na uchakavu unaosababishwa na umri kua mkubwa miaka (60),
kukatika kwa Umeme mara kwa mara, maji kuwa na tope jingi sana (turbidity)
wakati wa mvua na mafuriko hali inayopunguza uwezo wa pampu za kusukuma maji na
husababisha kusagika kwa vifaa vya pampu na ugumu wa upatikanaji wa vipuri
halisi (genuine parts).
Hata hivyo, Waziri
Maghembe hakukiri wala kukanusha juu ya madai ya kuwepo kwa udhaifu, uzembe,
ufisadi na hujuma katika mitambo ya vyanzo vya maji na mitandao ya mabomba ya
maji.
Waziri Maghembe
alieleza Bunge kwamba Wizara imechukua hatua za kutatua matatizo yaiyopo kwa
kuchonga vipuri na vifaa vya pampu katika karakana zilizopo hapa nchini kwa
kuwatumia wataalamu wa jeshi, kuagiza vipuri nje ya nchi na kutoa matangazo kwa
wananchi kuhusu upungufu wa maji pale uzalishaji unapopungua/kusimama.
Waziri Maghembe
alilieleza bunge kwamba baada ya hatua hizo uzalishaji wa Maji wa Mtambo wa
Ruvu Juu unaendelea kurudi katika hali yake ya kawaida na kutoa mfano wa kwamba
tarehe 17 Mei, 2014 uzalishaji wa maji ulikua lita milioni 80.3 kwa siku.
Aidha, Waziri Maghembe
alitoa kauli Bungeni kwamba Wizara ya Maji imeunda Kamati Maalum ambayo imeanza
kufanya tathmini ya kina juu ya chanzo cha matatizo ya mara kwa mara katika
mtambo wa kusafisha maji wa Ruvu Juu.
Waziri Maghembe
alieleza kwamba kamati hiyo itafanya uchunguzi kubaini kama matatizo hayo
yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa ya binadamu na
kuahidi kwamba kamati itatoa taarifa yake katika kipindi cha mwezi mmoja.
Mwezi mmoja umepita tangu
nilipohoji bungeni tarehe 12 Mei 2014, hivyo ni wakati muafaka kwa mamlaka zote
zinazohusika kuweza kutoa mrejesho juu ya uchunguzi huo na hatua nyingine za
haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi kama nilivyozieleza katika hoja
binafsi niliyoiwasilisha bungeni kwa niaba ya wananchi tarehe 4 Februari 2013.
Wenu
katika uwakilishi wa wananchi,
John
Mnyika (Mb)
22
Juni 2014