TUACHANE NA UPUUZI WA PICHA ZA MITANDAONI
Na Prudence Karugendo
NIMESHANGAZWA
na kusikitishwa sana na habari iliyotanda
kwa sasa nchini kuhusu picha za kipuuzi zinazotolewa kwenye mitandao ya
kijamii. Picha hizo zimefikia hata kuliteka Bunge letu, wabunge wameharibu muda
wa kujadili mambo nyeti yanayowagusa wananchi na nchi kwa ujumla na badala yake
wakajikita katika kuzijadili picha hizo za kipuuzi!
Picha hizo,
ziwe za kweli au za kutengenezwa kwa njia ya teknolojia ya kisasa, bado ni za
kipuuzi kiasi kwamba kuacha mambo muhimu na kuzijadili au kuhangaika nazo kwa
namna yoyote ile ni utovu wa uadilifu.
Sababu kuna
mfano unaotolewa kwamba ukiwa unaoga mtoni akapita kichaa akakwapua nguo zako
na kukimbia nazo, wewe kwa hasira ukaamua kumkimbiza ukiwa uchi, nani
ataonekana ni kichaa? Bilashaka wewe uliye uchi ndiye utaonekana kichaa!
Mimi naamini
kwamba tunachokihitaji kwa sasa ni maendeleo yenye kuleta maisha bora tukiwa
tumeziangalia nchi zilizotutangulia kimaendeleo na kuyafikia hayo maisha bora.
Tuangalie zinafanya nini na kupuuza nini ili tuige.
Wingereza kwa
mfano, wakati fulani Malkia Elizabeth II, alikuwa anateremka kwenye ndege upepo
ukainua nguo yake na kuonyesha sehemu yake ya ndani, wanahabari waliokuwa pale
wakapiga picha na kuitoa kwenye magazeti kwa kichwa cha habari “A royal thigh”
kwa maana ya paja la kifalme! Picha hiyo haikujadiliwa mahala popote na mamlaka
yoyote ya Kingereza.
Wakati
mwingine, kulekule Wingereza, mtoto wa kifalme, Prince William, akiwa mdogo
akicheza kwenye busitani akaamua kukojoa kulekule kwenye busitani, mapaparazi
wakamuona na kumpiga picha. Baadaye picha hiyo ikawekwa gazetini na kupewa
kichwa cha habari “A royal wee”, tafsiri isiyo rasmi, mkojo wa kifalme!
Wangereza
hawakushughulika na picha hizo sababu hazikuingiliana kwa namna yoyote na mambo yao ya kimaendeleo.
Waliacha upuuzi ubaki upuuzi.
Hata Baba wa
Taifa, Mwalimu Nyerere, aliwahi kusema kwamba kuna wakati “aliwakoromea” Wangereza nyumbani kwao kuhusu Rhodesia, Zimbabwe
kwa sasa, kesho yake magazeti ya kule yakatoa picha yake akiwa na mkia kama
panya. Nyerere hakujali, maana aliona ni
upuuzi ambao haukuweza kuzuia nguvu ya ukweli aliokuwa akiutoa kuhusu unyama wa
nchi hiyo kule Zimbabwe.
Mfano
mwingine ni wa Marekani, zilitoka picha
nyingi za rais wa nchi hiyo, Clinton, akionekana amewambwa kwenye kinena cha
mwanamke aliye uchi, Monica Lewinsky, lakini taifa hilo lililopiga hatua
kimaendeleo, halikuujali upuuzi huo kwa
vile haukuzuia lolote katika maendeleo yake.
Tunachopaswa
kuelewa ni kwamba tunapowachagua wabunge wetu tunaupima tu uwezo wao wa kutuwakilisha
na kutusemea tunayoyahitaji, wala hatuangalii kama mtu kaoa, kaolewa, ana
wapenzi wangapi nakadhalika. Maana hayo ni mambo yake binafsi, kuyafuatilia
hayo ni kukosa mwelekeo. Ni sawa na kumfukuza ukiwa uchi kichaa aliyekwapua
nguo zako wakati ukioga mtoni.
Kwahiyo picha
ya Komba akiwa na “vimwana” inatugusaje iwapo yeye anatimiza yote aliyotumwa na
wananchi wa Mbinga anaowawakilisha? Sababu mbali na kuyasema mahitaji ya wapiga
kura wake Bungeni, hawajamueleza afanye
nini nje ya uwakilishi wake, ale nini, anywe nini, aongee na nani, nakadhalika.
Hayo ni mambo yake binafsi.
Mimi
binafsi, ugomvi wangu kwa Komba ni kauli yake aliyoitoa Bungeni ya kwamba
ataenda msituni ili atuue na kuiharibu nchi yetu kwa kuyatetea na kuyalinda
maslahi yake binafsi. Lakini siyo picha hizi za kipuuzi.
Ajabu kauli
ya Komba kwenda msituni haikupigiwa kelele kama ilivyo kwa picha zinazoonyesha
sura yake kwenye mtandao! Picha hizi za Komba akiwa na wanawake, hata kama ni
za kweli, zina kitu gani cha kutudhuru kama ambavyo anaweza kutudhuru akiwa
msituni anakotamani kwenda iwapo maslahi yake hayatazingatiwa?
Mimi nahisi
kwamba pengine hiyo ni changamoto kwa kiwango chetu cha kutafakari. Maana
tunapoacha kuyashughulikia mambo yanayotishia uhai wetu na badala yake
kuyapigia kelele mambo yasiyo na maana wala athari yoyote, ni lazima ionekane
kuwa kuna upungufu mkubwa katika fikra zetu.
Kuhusu
maadili, vilevile lipo la kutazamwa. Wabunge wetu kuonekana katika picha za
ufusika, na nchi yetu kujigeuza “Matonya”
ombaomba maarufu, kiasi cha kuomba hata pesa ya kuendesha mambo yake ya ndani,
Bajeti, wakati nchi ikiwa imejaa utajiri wa asili usiosemeka, ni kipi kinachokosa
maadili zaidi kati ya hivyo viwili?
Tuseme
Tanzania inazingatia maadili na Marekani haizingatii maadili, lakini mbona
maadili yetu hayatuzuii kuwa ombaomba kwa Marekani isiyozingatia maadili? Kwa
nini hatuoni kuwa suala la maadili tunaloliimba kila wakati ni la kujidanganya
tu?
Inafaa
kwanza tuuone ukosefu wa maadili wa nchi kujigeuza ombaomba wakati imeulalia
mlima wa utajiri kabla ya kuuangalia ukosefu kiduchu wa unadilifu wa wabunge
wetu.
Tukumbuke
kwamba wabunge sio malaika, ni binadamu kama tulivyo sisi wote. Wanayo mahitaji
ya kawaida na matamanio ya kimwili kama walivyo wananchi wote. Mbali na
tunayowatuma Bungeni, vilevile nao wanahitaji kusitarehe na kuburudika.
Labda kama
picha hizo zingewaonyesha wabunge wanafanya uporaji wa mali ya umma, kinyume na
dhima ya uwakilishi wao, hapo ndipo ningekuwa naongea vingine. Lakini picha
hizi zinazoonyesha mambo yao ya faragha yasiyotuhusu naona ni uzumbukuku
kuzipigia kelele.
Historia ya
karibuni ya nchi ya Marekani inawataja marais wawili wa nchi hiyo waliopendwa
sana na Wamarekani kutokana na kufanya mambo kadri ya mapenzi ya wananchi
yalivyokuwa, kuliongoza taifa hilo kwa mafanikio makubwa. Marais hao ni John F.
Kennedy (JFK) na William Jefferson (Bill) Clinton.
Lakini historia
hiyohiyo ikiwatazama watu hao katika mambo yao ya faragha inaonyesha jinsi
walivyokuwa wachafu kupitiliza. Ila kwa vile uchafu huo ulihusu tu mambo yao
binafsi, Wamarekani mpaka leo hawaujali uchafu huo. Wao wanakijali kile
walichowatuma wakifanye, ambacho marais hao walikifanya kwa ukamilifu na
uadilifu mkubwa.
Kwa maana
hiyo, hata sisi Watanzania, kama tunaitakia nchi yetu historia safi yenye
mwelekeo wa maendeleo, hatunabudi kuachana na fikira potofu za kuyaweka mbele
mambo madogo madogo na mepesi kama haya ya picha za kwenye mitandao, tena
yanayolenga kwenye ufaragha, hata kama watu wanaolengwa ni viongozi wetu.
Sababu hayo ni mambo yao binafsi yasiyoingiliana hata kidogo na dhamana tuliyowapa.
Katika
kuonyesha kuchanganywa na picha hizo, kuna mbunge aliyesema uwekwe utaratibu wa
wabunge kupatiwa ulinzi! Sikubaliani kabisa na hoja hiyo kwa sababu mbili
ninatakazozitaja hapa chini. Moja ni kwamba kila mwananchi atahitaji ulinzi
binafsi, sababu thamani ya uhai wa mbunge ni sawa na ya mwananchi yeyote
mwingine.
Pili ni
kwamba kwa mahitaji hayo ya mbunge ni sawa na kukiri kuwa uchafu unaoonyeshwa
kwenye picha hizo za faragha ni wa kweli, kwahiyo walipakodi inabidi
waugharamie ili uendelee bila bughudha!
Kwahiyo
inabidi tuwaulize kina Komba kama wanakubali kuwa picha hizo ni za kweli ili
tusilipie hewa, na kama wanaona inafaa walipakodi waugharamie uchafu huo kwa
kuwawekea ulinzi ili usiendelee kupigwa picha. Lakini kama wanazikataa yanini
kuweka ulinzi?
Mwisho,
niseme kwamba tuachane kabisa kuhangaika na mambo ya kipuuzi kwa kusingizia neno
maadili. Tunapaswa tuyaangalie maadili yetu kwa kuuchukia sana ufisadi ambamo
ndimo kumejaa uvunjifu mkubwa wa maadili unaokaribia kuiangamiza nchi yetu, sio
picha hizi za kutengenezwa kwenye mitandao. Hizo haziwezi kuiathiri nchi yetu
kwa namna yoyote ile.
0784 989 512