UGUMU WA MAISHA NA YATIMA
MWISHONI
mwa mwaka 1983, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilihutubia
Taifa wakati anapokea maandamano ya wakazi wa jiji la Dar es salaam yaliyokuwa
mahususi kuunga mkono operesheni maalumu ya kupambana na watu waliojulikana
kama wahujumu uchumi. Katika hotuba yake hiyo Mwalimu alisema kwamba kulikuwa
kumeanza kujitokeza kundi au tabaka la watu ambao walikuwa wameota pembe na
kuanza kujiona kama vile wana serikali yao, kwa hiyo akatumia nafasi hiyo
kuwataarifu watu hao kuwa kuanzia wakati huo watambue kuwa serikali yao
imepinduliwa rasmi na serikali ya Tanzania.
0784
989 512
Kwa
asilimia kubwa watu waliokuwa wamelengwa na mapinduzi hayo yaliyoendeshwa kwa
mtindo wa vita na kupewa jina la vita dhidi ya wahujumu uchumi, ni
wafanyabiashara. Vita ile iliwafunda wafanya biashara, wakajirudi wakitambua
kuwa kuna mamlaka juu yao ambayo kwake iliwabidi wao kuwajibika.
Siri
ya mafanikio ya vita ile ni kwamba kwa wakati ule ulikuwepo mgawanyo unaoheshimika
katika makundi yaliyokuwa yanatengeneza jamii yetu. Jamii yetu ilikuwa
imegawanyika katika makundi makubwa mawili ambayo ni ya wakulima na
wafanyakazi. Katika makundi hayo ndimo tulimotegemea kuwapata wanasiasa ambao
baadaye waliokuwa wanapata nafasi za
kuwa viongozi wetu.
Vile
vile lilikuwepo kundi lingine ambalo ni la wafanyabiashara. Kundi hilo lililokuwa na uzito kutokana na
nguvu za kiuchumi lilizokuwa nazo lakini likikosa kujiamini kufuatia laana
liliyoipata baada ya Azimio la Arusha lililotanabahisha kuwa nchi hii ni ya
makundi mawili ya mwanzo, wakulima na wafanyakazi.
Ikumbukwe
kwamba Azimio la Arusha liliwajengea wananchi moyo wa kujiamini bila kujali
tofauti zao za kiuchumi, moyo
ulioendelezwa hadi kufikia tajiri na masikini kuanza kuitana ndugu. Zaidi ni
kwamba haikutegemewa mtu mwenye nguvu za kiuchumi zinazojionyesha wazi
ajipenyeze kwenye safu ya uongozi wa wananchi. Sababu ingebidi ajieleze ni njia
gani alizozitumia kuupata utajiri kitu ambacho wengi hawakuwa tayari kukifanya.
Wakati ule kuupata uongozi ilikuwa inahitaji usafi wa maadili sawa na mwanadamu
anayeuhitaji Ufalme wa Mbinguni anavyohitajiwa kuwa na usafi wa roho. Kwahiyo
fumbo lile la “tajiri kuingia mbinguni ni sawa na ngamia kupita kwenye tundu la
sindano” ndivyo ilivyokuwa kwa matajiri wa hapa nchini kuweza kupata upenyo wa
kuingia kwenye uongozi wa nchi.
Kwa
maana hiyo wafanyabiashara walibaki kuuangalia uongozi wa nchi na kuuheshimu
wakiamini kuwa hiyo ni karama ya watu wengine kama nao walivyokuwa na ya kwao
ya biashara. Ila walioutamani uongozi iliwabidi kuukana utajiri kama Kristo
alivyowambia matajiri kwamba mwenye kutaka kumfuata, kwa maana ya kuutamani
Ufalme wa Mbinguni, agawe mali zake zote
kwa masikini kisha amfuate yeye.
Mwenendo
huo ulidumisha nidhamu katika jamii yetu, watu wakauthamini utu kuliko vitu,
matajiri na wafanyabiashara wakiendesha shughuli zao kwa uangalifu wakihofia
kuwa pindi wakijisahau mamlaka iliyo juu yao, serikali, inawawajibisha mara moja.
Tunaweza
kusema kwamba wakati ule wananchi walikuwa na kinga, walikuwa na pa kukimbilia,
walikuwa na mtetezi. Baadaye ukaja wakati wa methali ya sikio la kufa. Watu
wenye nguvu za kiuchumi taratibu wakaanza kujisahau, ndipo serikali ikabidi iwavute sikio kwa
kuwakumbusha kuwa hawakupaswa kujenga himaya ndani ya himaya nyingine, himaya
yao ikapinduliwa na serikali. Kwa muda watu hao wakaufyata.
Sasa hivi habari hiyo imebaki kwenye
kumbukumbu za kale. Mambo ya leo ni
kinyume kabisa cha hayo tunayoyasimulia.
Himaya ile iliyopinduliwa katika mapiduzi tuliyoyaita ya wahujumu uchumi
imeishajijenga upya na sasa ndiyo inayoonekana kukalia kiti cha enzi ndani ya
serikali yetu. Nani atabisha kuwa kwa hivi sasa serikali haikushikwa na wale
wenye nguvu za kiuchumi pamoja na wafanyabiashara? Hali ya mambo inaonekana
kugeuka kwa nyuzi 190 kwa maana ya kuyakumbatia tuliyokuwa tunayakataa. Pale tulipotakiwa kuukana utajiri ili kuupata
uongozi, sasa kuupata uongozi bila utajiri ni muhali.
Hebu
tuiangalie serikali iliyo madarakani kwa sasa.
Ni mtu gani katika safu ya uongozi wa serikali hii, kwa mfano,
aliyetokana na makundi niliyoyataja mwanzo ya wakulima na wafanyakazi?
Tukimuondoa Rais, Makamu wake na Waziri Mkuu, ni nani mwingine atakayesimama na
kusema kwamba si mfanyabiashara? Na katika hali hii tunaushangaaje ugumu wa
maisha? Iwapo watu ambao serikali ilikuwepo kuwadhibiti ili wasilete ugumu wa
maisha kwa wananchi ndio sasa wameishika serikali na kuidhibiti barabara, kuuliza tena ugumu wa maisha si ni sawa na
kuufuata usemi wa vijana wa kuuliza au kuyashangaa makofi Polisi?
Inaeleweka
kabisa kwamba wenye nguvu za kiuchumi mtaji wao ni hela, wanapotamani kitu hela
yao ndiyo inayoongea. Wanapotamani kulinda maslahi yao ni lazima hela yao
iongee. Njia mojawapo ya kulinda maslahi yao wameona sasa ni kuingia kwenye
siasa na kupata uongozi ili kuidhibiti serikali ambayo hapo nyuma ilikuwa
inawadhibiti wao.
Kwa
upande wao mambo yametengamaa. Kwa upande wa walalahoi ili mambo yatengamae ni
lazima wahakikishe wanapata uongozi bora utakaojali maslahi yao kwa kuyatilia
maanani matatizo waliyo nayo. Na katika kufanikisha hilo mtaji pekee walio nao
ni kura zao. Ili kumpata kiongozi ambaye angeweza kusimamia maslahi yetu
walalahoi ilibidi tuwe waangalifu na kura zetu. Lakini bahati mbaya tukakubali
kurubuniwa na mtaji wa wenye nguvu za kiuchumi kupitia katika mbinu mbali mbali
zilizobuniwa kama ile ya takrima na nyinginezo, tukakubali kuyasaliti maslahi
yetu na kuwapitisha waliokuwa wanaenda kuyalinda maslahi yao. Kwa hili
tumejipiga wenyewe tusilie na mtu.
Hebu
ona sasa yanayotokea, ugumu wa maisha kwa walalahoi ni neema kwa wenye nguvu za
kiuchumi. Mathalan, tuchukulie ugumu wa maisha ulioanza kujitokeza kila baada
ya kupitishwa kwa bajeti ya nchi. Wakati
walalahoi wanakipata cha moto hali ni
kinyume chake kwa wenye nacho. Kwa wenye nacho ni wakati wa mavuno ya neema.
Nadhani hii inakamilisha ule usemi wa kwamba mwenye kidogo atanyang’anywa na
kuongezewa mwenye kingi.
Sasa
hivi kuna balaa na neema ya upandaji wa bei ya petroli, ni balaa kwa walalahoi
na neema kwa wenye nacho. Wenye vyombo vya usafirishaji wametumia nafasi hiyo
ya kupanda kwa bei ya petroli kupandisha gharama za usafirishaji kwa kiwango
ambacho hakina uwiano hata kidogo na upandaji wa bei ya mafuta hayo. Sio kwamba
jambo hilo halijulikani kwa wale tuliowatuma wakatuwakilishe, wanalijua sana na
pengine kulishangilia badala ya kulilaani. Ni wabunge wangapi hawanufaiki nalo
kwa maana ya kutokuwa na vyombo vya usafirishaji? Sababu naamini walio wengi
kama siyo wakurugenzi wa makampuni ya usafirishaji basi watakuwa wanamiliki
japo daladala kadhaa. Nani amkumbushe mwenzie madhila wanayoyapata walalahoi?
Nitajaribu
kuonyesha jinsi wenye nacho wanavyojineemesha na upandaji wa gharama za maisha
kwa kutumia mfano wa usafiri katika jiji la Dar es salaam. Tuseme asilimia
sabini ya wakazi wa jiji la Dar es salaam wanaishi kwa kipato kisichozidi
shilingi elfu mbili kwa siku, na ili
waweze kukipata kiasi hicho inawalazimu wengine kupanda mabasi (daladala)
yasiyopungua manne kila siku. Jaribu kufikiria machungu anayoyapata mwananchi
wa aina hii inapopandishwa nauli ya daladala hata kwa shilingi kumi tu. Kwa
hiyo uchungu wa kupanda kwa bei ya petroli wanaupata watu hawa ambao wengi wao
hawatarajii kumiliki chombo chochote cha moto maishani mwao.
Upande
wa pili, wenye kumiliki vyombo vya moto
kwa ajili ya usafiri, hasa wale wenye
daladala, wanakuchukulia kupanda kwa bei
ya mafuta kama habari njema wanayokuwa wameisubiri kwa hamu ili kuboresha
vipato vyao katika biashara zao za usafirishaji.
Tuseme
daladala aina ya DCM linalofanya safari fupi kati ya Segerea na Mnazimmoja
linafanya mizunguko 14 kwa siku, saba
kwenda na saba kurudi. Tukilikadiria abiria 50 kwa kila safari moja litakuwa
limebeba abiria 700 kwa siku, hicho ni kiwango cha chini kabisa sababu hakigusi
abiria wanaoteremka njiani na kupanda wengine. Kwa abiria 700 mwenye daladala
anakuwa amepata shilingi 350,000 kwa nauli ya shilingi 500/=. Baada ya kutoa
hela ya dizeli ambayo haizidi lita 40
kwa bei ya 2140/= sawa na shilingi 85,600/= alikuwa
anajihakikishia kipato kisichopungua shilingi 264,400/= kwa siku.
Fikiria
huyo akilinganishwa na mtu anayehangaika kutwa nzima kupata sh. 2000/= uwiano
uko wapi?
Kwa
mtazamo huo nani atabisha kwamba kupanda kwa gharama ya maisha siyo neema kwa
wenye nacho? Nani awasemee walalahoi wakati waliowachagua kuwasemea wanaonekana
kuneemeka na matatizo yao? Watanzania waliowengi wamegeuka yatima kipindi
hiki, hawana wa kumlilia.
Na
Prudence Karugendo