ULEVI NA UVUTAJI NDIYO MIHIMILI YA UCHUMI WETU?
Na Prudence Karugendo
NIMEJIWA na wazo kwamba neno la tahadhari kwenye sigara
na matangazo ya bidhaa hiyo lisemalo “ uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya
yako” ni la kuondoa kabisa. Sababu kwa maana nyingine neno hilo ni sawa na
kusema ukuzaji wa uchumi wa nchi yetu ni
hatari kwa afya zetu.
Lingine ni
kwamba sheria ndogondogo kama ya kutofungua baa wakati wa kazi na kulazimisha
baa kufungwa ifikapo saa sita usiku inabidi nazo ziondolewe. Sheria hizo
zinaonekana kuuhujumu uchumi wetu.
Hiyo ni
pamoja na kuwakamata walevi kwa kisingizio cha kulewa wakati wa kazi au
kutembeza ulevi hadharani.
Kwa kadri
mambo yalivyo hapa kwetu, walevi na wavuta sigara ni watu muhimu sana katika
uchumi wa nchi yetu. Sidhani kama kuna kazi yoyote nyingine inayochangia katika
ukuzaji wa uchumi wa nchi yetu kama walivyo walevi na wavuta sigara. Nitaeleza.
Kwa kipindi
cha zaidi ya miaka 30 iliyopita, kila mwaka Hazina ya nchi wakati wa Bajeti, ni
lazima ikachungulie kwa walevi na wavutaji kuangalia kuna nini cha kukusanya, kana kwamba hizo ndizo sehemu pekee za
ukusanyaji wa mapato yake!
Ni nani sasa
asiyeona kuwa kuwasumbua watu hao,
wateja wa sigara na pombe, kwa sheria na tahadhari nilizozionyesha hapo juu, ni kuuvuruga uchumi wa nchi?
Kama nchi
haiwezi kuviangalia vyanzo vingine vya mapato zaidi ya sigara na pombe, kwa
nini isiwaheshimu na kuwaendekeza watumiaji wa vitu hivyo muhimu kwa uchumi
wake? Maana kwa nchi iliyo makini ni lazima iviheshimu vyanzo vya uhai wake.
Uchumi kwa nchi ndiyo uhai wake.
Mfano, nchi
za Sudan na Misri zinayaheshimu maji ya mito ya Nile, Blue Nile na White Nile.
Kutokana na nchi hizo kunufaika na maji hayo, ipo imani kwamba maji hayo ni
neema yao kutoka kwa Mungu ili kuulinda uhai katika nchi hizo.
Watu wa nchi
hizo wako tayari kufa na yeyote anayejaribu kuyachezea maji ya mito hiyo kiasi
cha kuyafanya yaache kutiririka kuelekea
kwao. Huo ndio umakini katika kukilinda kinachoonekana kinaulinda uhai katika
nchi husika.
Mfano
mwingine ni wa nchi ya Mauritius. Uchumi wa nchi hiyo kwa kiasi kikubwa
unategemea kilimo cha miwa iliyochukua asilimia 90 ya ardhi yote iliyolimwa
katika nchi hiyo.
Kwa vile zao
la miwa ni mhimili wa uchumi wa nchi hiyo, linaheshimiwa sana na watu wa nchi hiyo.
Wao wanasema chezea kingine lakini sio kuchezea miwa. Sababu kuchezea miwa ni
sawa na kuchezea uchumi wa nchi yao. Wananchi wote wa nchi hiyo wanalielewa
vizuri hilo.
Sasa kama
Tanzania inategemea zaidi sigara na pombe katika uchumi wake, kwa nini
watumiaji wa vitu hivyo wasipewe heshima kama ilivyo kwa nchi nilizozitaja
namna zinavyoyajali mambo yanayohusiana na uchumi wake?
Kama kweli
upo umakini katika kuulinda na kuukuza uchumi wetu, kwa nini matangazo ya
tahadhari kwa wavutaji na bughudha kwa walevi tusivichukulie kama uadui dhidi
ya nchi yetu sawa na Sudan na Misri wanavyowachukulia wanaojaribu kuchezea maji
ya Nile ili yasitiririke kuelekea kwao?
Tofauti na
dhana nzima ilivyo, Tanzania ni nchi iliyojaaliwa mambo mengi ya kuiinua
kiuchumi. Ni nchi tajiri sana kwa upande wa maliasili, sema utajiri huo
hauguswi linapokuja suala la mpangilio wa uchumi wake. Badala yake wahusika
wanaviangalia tu vitu vidogovidogo kama pombe na sigara!
Lakini vitu
hivyo sio vya lazima katika maisha ya mwanadamu japo wachumi wetu wamevipa
kipaumbele kama mhimili wa uchumi wa nchi. Je, iwapo Watanzania wataamua kuachana
navyo, wakaacha kulewa na kuvuta sigara, hayo mapato ambayo Waziri wa Fedha
anayaangalia kila mwaka kwa upande huo atayatoa wapi?
Kwa nini
tuache kutazama mapato ya kwenye vyanzo vya uhakika, kama vile kwenye utajiri
wetu wa asili tuliojaaliwa nao, na badala yake tuendelee na hivi viini macho?
Utajiri wetu tunauacha unasombwa na wageni kwa kisingizio cha kuwavutia
wawekezaji! Ni lini tutanufaika na hao tunaowavutia na kuacha kuwategemea
wavutaji na walevi?
Wakati
baadhi ya wawakilishi wa wananchi, wabunge, wakilalamikia Bajeti ya mwaka huu
katika Bunge linaloendelea, mbunge mmoja aliyeondolewa kwenye uwaziri kwa
tuhuma za ufisadi, amewakebehi wabunge wenzake hao akidai kwamba wanawapotosha
wananchi. Yeye anadai wananchi wanaifurahia Bajeti ya mwaka huu.
Lakini
baadhi ya wananchi wa Jiji la Mwanza wanasema kwamba mbunge huyo asitake
kuigeuza furaha yake kuwa ni ya wananchi wote. Wanasema furaha aliyo nayo yeye
inatokana na ukwasi alio nao ambao hawana hukakika kama anaweza akautolea
maelezo namna alivyoupata.
Nikiwa
Jijini humo, nikaonyeshwa hoteli moja
yenye ghorofa 9 iliyoko Mtaa wa Rufiji, nikaambiwa kuwa ni mali ya mbunge huyo
anayeona raha ya maisha akiwachukulia Watanzania wote kuwa wana raha ya maisha
kama aliyo nayo yeye. Lakini wanasema kwamba hoteli hiyo imeandikwa kwa jina la
ndugu wa mbunge huyo ili kujaribu “kuwazuga” watakaotaka kuifuatilia.
Wananchi
wengine wanaamini kwamba yanayosemwa na mbunge huyo ni upotoshaji katika
kuficha dhana ya kwamba kuna wananchi wanaolalamikia ugumu wa maisha, kwa vile
mbunge huyo anaelewa ni kiasi gani alivyouchangia ugumu huo kwa kujilimbikizia
mali ikiwemo hoteli hiyo katika Mtaa wa Rufiji Jijini Mwanza.
Wananchi hao
wanasema kwamba wao watafurahi, kama yeye anavyodai, iwapo ataweza kuutolea
maelezo utajiri aliojilimbikizia kwa muda mfupi. Sababu wanasema wengi
wanamuelewa tangia kijijini kwao mpaka hapo alipo, matawi ya juu!
Godfrey
David Mollel ni mkazi wa mji wa Arusha, anasema “Niko njiani naelekea nyumbani,
nimekutana na mwanamke, anaonekana
katoka kujifungua sababu kabeba kichanga chenye umri wa masaa tu. Inaonekana
mama huyu kakosa nauli na kuamua kutembea kwa mguu na hali hiyo aliyo nayo!”
Mwananchi
huyo wa Arusha anauliza, haya ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania
tuliyoahidiwa? Anaongeza, “Mwanamke huyo aliyetoka kujifungua na kulazimika
kutembea kwa mguu kwenda nyumbani kwake naye anaifurahia Bajeti ya mwaka huu
kama anavyodai mbunge huyo mkwasi?”
Nikirudi
kwenye mjadala wangu ningetaka kuuliza hivi, katika historia ya dunia ni wapi
panapotajwa kuwa nchi zilizoendelea mwanzo wake ulikuwa ni kuwavutia wawekezaji
toka kwingine wakaende kupora utajiri wa
nchi hizo na kuuhamishia kwao? Na kama hilo halimo kwenye historia ujasiri wa kwamba
linaweza kutusaidia sisi tunautoa wapi?
Kinyume
chake historia inatuonyesha kuwa kila kilichopatikana katika nchi zilizoendelea
kilihakikishwa kinazinufaisha nchi husika, na ilipowezekana kingine kiliporwa
kwingine na kuongezewa, ndiyo maendeleo tunayoyaona kule.
Lakini kwetu
sisi ni tofauti, tunawavutia wawekezaji toka nje waje kusomba utajiri wetu
kadiri wanavyoweza, na wakati mwingine tukisaidiana nao kuipora nchi yetu
kwenda kuficha kwao!
Ndipo zinapokuja
fikra za kutaka kuwa na uraia wa nchi zaidi ya moja kusudi “kikinuka” huku
kwetu tugeuke raia wa Ughaibuni na kuwaachia manyoya wenye kutaka kuleta za
kuleta!
Kwa fikra za
aina hiyo, kutaka kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja, upo uwezekano wa
uzalendo hapo unaoweza kumsukuma mtu ayafikirie maendeleo ya nchi yake?
Ni wazi,
bila uzalendo maendeleo ni muhali. Tutabaki kuwavutia wawekezaji wa kuja na
kusomba utajiri wetu kwa thamani ya matrilioni tukiwa tumewahakikishia usalama
kwa lugha yetu maarufu ya “amani na utulivu” tunayotamba nayo duniani kote,
huku sisi tukipanga Bajeti zetu kwa kuziangalia sigara, bia na soda kama vyanzo
vikuu vya mapato yetu!
Nimalizie
kwa kusema kwamba mimi sio mchumi, wala sio taahira. Ningeomba wanaojiita
wachumi wanieleze kwa lugha nyepesi namna tunavyoweza kujihakikishia pato la
nchi kwa kuvikomalia tu vitu vinavyouzwa kwa shilingi 100 – 2000, tukiwa
tumevipa kisogo vyenye thamani ya matrilioni ya shilingi!
0784 989 512