WAKULIMA MULEBA WARUHUSIWA KUSAFIRISHA KAHAWA
WAKULIMA na wanunuzi wa zao la kahawa katika Kata ya Nshamba, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, wameruhusiwa kusafirisha zao hilo kwenda sehemu yoyote ndani ya wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kutotozwa faini kinyume na sheria kwa makosa yanayohusu biashara ya usafirishaji wa zao hilo.
.Profesa Tibaijuka alikataza adhabu ya faini ya sh 100,000 wanazotozwa wakulima na wanunuzi wa zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Mbunge wa Muleba Kusini, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo
“Haiwezekani mkulima asafirishe kahawa kutoka kata moja kwenda nyingine halafu atozwe faini ya sh laki moja kwa kosa la kutokuwa na kibali kwa kufanya biashara ya magendo jambo ambalo ni kukiuka sheria,” alisema Tibaijuka.Alitaka vibali kwa wanunuzi na wauzaji wa zao hilo vitolewe bure huku akiitaka serikali iendelee kutafuta masoko ya nje yenye tija.
Wakizungumza kwenye mkutano huo, wakulima wa kahawa wamesema kuwa wanasafirisha na kuuza zao hilo sehemu nyingine kwa kuwa wanauza kwa bei ya hasara katika chama cha ushirika (KCU) kwa sh 800 kwa kilo moja, ukilinganisha na masoko huria yanayotoa bei ya sh 1,800 hadi 2,200 kwa kilo.
Mmoja wa wakulima hao, Solo Zuberi, alisema kuwa alitozwa faini ya sh 100,000 kwa kusafirisha kahawa yake, badala ya 1,500 inayokubalika kisheria.