WAPENI WATU TAARIFA WAJIANDAE NA KESHO YAO
Juhudi za uwekezaji nchini zimekuwa zikikumbana na upinzani
mkali kutoka kwa wananchi kila mahala
kunapokuwako na mradi mkubwa wa uwekezaji, na ni ajabu kwangu na
ninaamini kwa wengi wenye kutafakari mambo, kwamba hata sasa serikali
imeshindwa kulimaliza tatizo hili
Migogoro mingi iliyojitokeza na ambayo kusema kweli si
kwamba imemalizika kabisa kati ya wawekezaji na wananchi kwenye maeneo ya
migodi ya madini, ilipaswa kuwa somo kwa watu makini kujiuliza ni nini kinaweza
kufanyika kumaliza kabisa migogoro hii lakini hali ni tofauti.
Nadhani ni kwasababu ya tabia iliyojijenga miongoni mwa
watanzania ya kulifanya kila jambo kuwa ni matokeo ya mbinu ovu za kisiasa na
hivyo kila wananchi wanapopinga miradi ya uwekezaji, serikali ama baadhi ya
watendaji wake wanakimbilia tu kudai kwamba ni hujuma za wapinzani wa kisiasa
katika kuwachochea wananchi.
Mchezo huu ni hatari na unapaswa kukoma. Ndiyo, unapaswa
kukoma kama kweli tunakusudia kweli
kuona maendeleo ya kweli. Ninazo sababu kadhaa za kuwataka wenye mtizamo hasi
kwamba kila linapojitokeza tatizo badala ya kutafuta chanzo cha tatizo
wanakimbilia kulaumu wale wanaodhani ni wabaya wao waache mara moja, na badala
yake watumie nguvu hizo za fikra kufikiri, kusikiliza, kuchanganua na kupata
njia mbadala ya kumaliza kutokuelewana kati ya wawekezaji na wananchi.
Ni muhimu watendaji wa serikali wakatambua kwamba ile dunia
ya watu kuwafuata viongozi kama vipofu imepita na sasa wananchi wanahoji na
hata kuwa na njaa ya taarifa za ni nini kinafanyika kwa kutumia rasilimali za
nchi yao. Wananchi si wa Tanzania peke yake, bali wakaazi wa dunia wamepoteza
imani na watawala na sababu zake ziko nyingi ambazo si hoja yangu ya leo,
lakini itoshe tu kusema, wananchi wanataka uwazi katika mambo kadha wa kadha.
Yako mambo ambayo wananchi “wa kawaida” kama wajulikanavyo na wanasiasa
hayawasumbui na hawana haja ya kuyahoji, lakini mambo yanayogusa maisha yao ya
kila siku, watawala ni lazima wakubali kwamba yatahojiwa na mbinu sahihi ya
kukabiliana na hili ni kuwa na majibu yenye kushibisha nafsi na yenye mantiki
badala ya ama ubabe ama maneno mepesi yasiyo mantiki.
Wote tunakumbuka jinsi ambavyo nguvu zimetumika kukabiliana
na wananchi kule kwenye migodi ya Nyamongo na Buhemba na hata Bulyanhulu hali
haikuwa shwari sana. Mwaka jana umeshuhudia vurugu kubwa mkoani Mtwara wananchi
wakipinga kujengwa bomba la kusaifirsha gesi kutoka Mtwara hadi jijini
Daressalaam. Hayo yote na mengine ni matokeo ya watendaji wa serikali ama kwa
makusudi au kwa uzembe ama ujinga (nimetumia neon ujinga si upumbavu) wa
kutambua kwamba huu ni ulimwengu wa taarifa zaidi kuliko ulivyokuwa ulimwengu
uliopita ambapo wananchi waliwafuata viongozi wao bila kuhoji.
Nasema siungi mkono vurugu
na machafuko katika kutafuta taarifa sahihi, lakini nakubali ukweli kwamba
ni hulka ya binadamu kwamba ikiwa atahitaji kitu Fulani na hawezi kukipata kwa
njia ya kawaida, unategemea matumizi ya nguvu katika kufikia lengo hilo, na
hivyo naona kama ni sahihi kwa serikali badala ya kusubiri hadi migogoro
imekuwa mikubwa, iwape wananchi taarifa sahihi kwa wakati ili wananchi nao
waweze kujiandaa kwa mabadiliko yatakayojitokeza kwenye maeneo yao kutokana na
shughuli ama uwekezaji husika na jinsi ya kuziona na kuzitumia fursa
zinazopatikana.
Ukiitazama Tanzania ya gesi na mafuta, utagundua kwamba
haina tofauti na Tanzania ya dhahabu na Almasi katika utekelezaji wa miradi
yake. Wakati katika Dhahabu na Almasi Tanzania ilipokea na kuajiri wageni wengi
sana katika miradi karibia yote na kisingizio kikiwa ni kutokuwapo kwa
wataalamu wanaofikia viwango vitakiwavyo katika tasnia husika, tatizo ni
lilelile leo kwenye gesi na mafuta.
Ukweli na usemwe, kama taifa tunazo changamoto mbili kubwa
zinazofanya suala la kutokuwapo na nguvu kazi stahiki kwa kazi husika iwe
ukweli usiopingika. Moja ni ukweli kwamba asilimia kubwa ya rasilimali watu wa
Tanzania ni watu wasiopenda kazi bali maslahi yatokanayo na kazi tu ama kwa
lugha nyingine uvivu. Hili aliwahi kulisema Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mheshimiwa Samweli Sitta na wajuvi wakamzodoa, lakini mioyoni
tunajua kwamba alisema ukweli. Utendaji wetu wa kazi ni mbovu, wa kivivu na
unaohitaji kusukumwa mara zote. Watanzania wanaishi kama watu walio na uchumi
mkubwa kabisa Afrika ilhali ni maskini wa kutupwa. Nimewahi kusikia mara kadhaa
vijana wasomi wakikataa kufanya kazi kwenye mabenki si kwa sababu ya malipo ama
mazingira ya kazi, bali kwamba ni kazi zinazochosha na kwamba muda wa kutoka
kazini kwa wafanyakazi wa mabenki hauwapi uhuru wa kujichanganya na watu na
“kusoshalaizi”, huu ni uvivu wa kufikiri. Hasa kwa kijana ambaye ndiyo kwanza
ametoka chuo na hana uzoefu wowote wa kazi. Wakati katika nchi za wenzetu watu
wanajitolea kufanya kazi pasipo malipo, vijana wa kitanzania wanatoka chuo na
wanapopata kazi wanauliza kwanza, “mshahara shilingi ngapi”?.
Nieleweke sina ugomvi na maslahi mazuri mahala pa kazi,
lakini ninajaribu kuonyesha mtizamo wa vijana walio wengi kuhusu kazi. Jambo la
pili ni kwamba vijana wa Tanzania hawajaandaliwa vyema kuchukua majukumu yao
katika sekta zenye uwekezaji. Jambo hili limefanya kwamba mara zote
tunapokwenda kwenye uwekezaji wowote mkubwa, kilio chetu ni kile kile kwamba
hatuna wataalamu wa Nyanja husika na mimi najiuliza, hivi serikali haikujua
kwamba muda na wakati Fulani kutakuwa na uwekezaji Fulani na hivyo tuwaandae
wananchi kwa kuwapa mafunzo na utayari kwa ajiri hiyo?.
Sitaki kuamini kwamba serikali ama inakuwa na haraka ya
kufanya uwekezaji kila utafiti unapokamilika na maliasili kugunduliwa ama haina
taarifa za ni wapi katika nchi yetu kuna maliasili gani na ambazo uwekezaji
wake unaweza kuwanufaisha wananchi kwa ajira na kadhalika.
Ikiwa basi kwamba serikali haijui ni maliasili gani tunayo
na ni lini tunaweza kuanza kuitumia kuinua uchumi wan chi yetu, ni kwanini kila
baada ya utafiti, hatufungi milango na kuwekeza kwanza kwenye kufundisha watu
wetu hadi tumekuwa na wataalamu katika Nyanja kadha wa kadha kabla ya kuanza
uwekezaji wenyewe!?. Ni kwanini leo tuna wafanyakazi wengi wa kigeni kwenye
miradi ya utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta kama tulivyokuwa kwenye
dhahabu!? Je! Ni kweli kwamba hatujajifunza chochote kwenye dhahabu!?.
Huu ni uzembe wetu wa kufikiri na kupanga mikakakati
endelevu ya jinsi ya kuboresha maisha ya wananchi. Hiki kimekuwa chanzo cha
sheria zetu wenyewe kuhusu ajira hasa katika uwekezaji kukanyagwa chini ya
nyayo za wawekezaji huku tukitazama tu na mara nyingine kutumia maguvu kuzima
malalamiko ya watu wetu, huu ni ukorofi.
Ukiingia kisiwani Mafia kwenye mkoa wa Pwani kwa mfano, kitu
cha kwanza utakachogundua ni ujenzi wa uwanja mkubwa na wa kisasa wa ndege
kisiwani humo. Hili ni jambo jema, lakini ujenzi huu unaendana na utafiti
kabambe wa gesi na mafuta kwenye kijiji cha Ndagoni kisiwani humo.
Mambo mawili yananijia akilini ninapolitazama hili katika
muktadha mzima wa uwekezaji na maslahi yake mapana kwa watu wetu. Moja ni
ukweli kwamba kiwanja hiki kinajengwa “kwa msaada wa watu wa Marekani”. Hakuna
asiyefahamu kwamba Marekani haiwekezi pesa zake ati kwa upendo tu wa watu wa
sehemu husika, bali kwa maslahi mapana ya taifa hilo yatokanayo na sehemu hiyo.
Nieleweke tena, sina ugomvi na ujenzi wa uwanja, wala suala la Marekani kama
taifa kuwa na maslahi labda katika gesi, mafuta ama utalii wa kisiwa hiki,
lakini hoja yangu ni kwamba ukiwauliza wananchi wa eneo hili, utagundua kwamba
hakuna mwenye taarifa za utafiti huu uko kwenye hatua gani na matarajio ni
nini. Si ajabu wakati uwekezaji utakapoanza, wananchi watatakiwa “kulipwa
fidia” ya maeneo yao na kupisha uwekezaji kwa kisingizio cha maslahi mapana
bila kuandaliwa kuwa wahsiriki halisi wa rasilimali iliyogunduliwa kwenye eneo
lao, na ole wa wale watakahoji haya ninayojihoji mimi leo kwenye makala haya
wakati huo.
Swali gumu ni, serikali inaona ugumu gani kuwa wazi kwa
wananchi wake na kuanza kuandaa mipango madhubuti ya kufungua vyuo vya ufundi
kwenye kisiwa hiki, kuomba wale wenye uzoefu na utaalamu katika aina za taaluma
za kifundi zitakiwazo kwenye gesi na mafuta hata kutoka kwa wanaokusudiwa kuwa
wawekezaji wakubwa, kuja na kufundisha vijana wetu ili wakati utakapofika tuwe
tayari na wataalamu?. Ni nini kinaifanya serikali haishirikishi wananchi kwenye
taarifa za utafiti, mipango na malengo ya uwekezaji huu ili nao wajiandae
kupeleka vijana wao shule kusomea mambo kadhaa wakijua kwamba soko la ajira
litapatikana hapa?
Kwanini mipango ya makusudi kuboresha kilimo cha vyakula,
matunda na mbogamboga zitakazohitajika kwa wingi wakati huo kwa kujua na
kuwajulisha wananchi viwango vya ubora vitakiwavyo ili wajifunze na kulima
kibiashara kwa ajiri ya wkati huo? Je! Ni kweli
kwamba unataka kurudia makosa yaleyale yaliyofanyika migodini ambapo
hata machungwa yalikuwa yakiagizwa kutoka Afrika Kusini kwa kisingizio cha ya
hapa kwetu kukosa viwango stahiki!? Kwani sisi tuna kasoro gani kwenye ardhi
yetu inayotufanya tusizalishe kwa viwango vitakiwavyo?
Nadhani ni wakati watendaji wa serikali na watunga sera
waamue kwa makusudi kulisaidia taifa hili kufaidika na uwekezaji vinginevyo
tuendelee hivi hivi hadi tutakaposhtuka mali zimekwisha na hawa waitwao
wawekezaji hawatuhitaji tena, huku tukiwa hatuna faida hata moja iliyopatikana
kwa miradi hiyo kwa wananchi wetu. Tunakumbuka wote jinsi Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alivyokataa kuruhusu uwekezaji hadi pale watanzania
watakapokuwa “wameelimika” na kuwa tayari. Najiuliza kila nionapo yanayoendelea
leo, ikiwa wakati watawala wetu walipoamua kufungua milango ya uwekezaji,
walipima na kujiridhisha juu ya kiwango cha utayari wa watanzania sisi kukabili
changamoto za uwekezaji ama wanasubiri kuvuta shuka kunakucha?.
Salaam nawasalimia.
Mwandishi: G. Jonathan Kamenge
Mail: kamengez@hotmail.com