Bukobawadau

AOMBA MSAADA WA MAKAZI BORA

NGARA:Na Shaaban Ndyamukama,Mwanamke wa kijiji cha Murugina kata Mabawe wilayani Ngara mkoani Kagera   anaomba msaada wa kujengewa nyumba baada  ya kuishi katika mazingira magumu akilea wajukuu wake watatu bila msaada wa ndugu jamaa na marafiki
Akizungumza na Bukobawadau jana kijijini humo bibi huyo  aliyetambuliwa kwa jina la Nastazia Mathayo (87) anasema alizaa watoto 10 kati yao wa kike walikuwa wanne na walishafariki na wanaume walibaki watatu lakini  wana maisha duni kiuchumi
Alisema kuwa mume wake alifariki miaka mingi iliyopita na alikuwa na mali hasa mifugo lakini haikuweza kuendelezwa kutokana na sababu mbalimbali na hatimaye familia nzima kubaki maskini
Alisema katika maisha yake nyumba anayolala ni ya kupindisha fito na kuezekwa kwa makuti ya migomba ambayo huwekwa shambani kuzuia kuota kwa magugu na wakati wa mvua huadhilika na kiangazi makuti hayo hushambuliwa na mchwa
“Maisha yangu na  wajukuu  wangu ni kuogopa kulala peke yangu lakini mwanangu mvua jua na baridi vyote hunikuta mimi na sijapata msaada hata kwa uongozi wa kijiji”Alisema Nastazia
Aidha alisema msaada mwingine ni kuhitaji kupata lishe kwani anakula chakula ambacho ni cha kubabaisha kwani hana nguvu za kujishughulisha  na kilimo bali hujitafutia baada ya kutegemea kulima nmagugu kwenye mashamba ya watu
Ngudu wa karibu na bibi huyo ni wafanyakazi wa kituo cha Afya mabawe wanaotoka sehemu mbalimbali na kuajiriwa eneo hilo na wenye moyo wa huruma ndio humpatia mahitaji  kwa uchache kulingana wanavyotumwa na  mioyo yao
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili wamesema kuwa bibi huyo alikuwa na mifugo mingi na akaitumia bila malengo sasa anajutia hali hiyo baada ya kufanya matumizi bila kuendeleza wtoto wake walipokuwa niwadogo
Mmoja wa wananchi hao Jumanne Kazosi alisema pia bibi huyo amekuwa akikumbwa na matukio ya kuunguliwa nyumba bila kupata madhara na kumuingiza katika Imani za ushirikina alisema kutokana na matukio hayo
Alisema wananchi walikuwa wakimsaidia miti kwa ajili ya kujenga nyumba ya kujihifadhi ingawa wanakijiji hawajawahi kuungana pamoja kuona umuhimu wa kusaidia wasiojiweza kiuchumi licha ya kuchangishana fedha za arusi kila kukicha
 Hata mtoto wake wa kiume  Paulo Mathayo Rulenga alisema yeye ni mgonjwa ana ulemavu wa macho ndugu yake mwingine Agustini Mathayo anasumbuliwa na tezi la shingo na mwenzao kalenzo akili yake sio timamu
Katika hatua nyingine Afisa mtendaji wa  kijiji cha Murugina  Joseph Festo alisema baadhi ya wananchi  walimnyanyapaa kwa sababu ambazo sio za msingi (hakuzitaja)  lakini mpango uliopo ni kuelimisha jamii kusaidia wasiojiweza
Alisema katika mipango ya maendeleo kwa sasa wanapanga kuzibana taasisi za dini na madhehebu yake kujenga nyumba za ibada na kuwafikia wananchi maskini kwa kuwapa matumaini ya maisha kwa kuhakikisha wanasaidiwa  changamoto zao
Aliongeza kuwa pamoja na misaada kuhitajika kwa wasiojiweza bado idara ya maendeleo na ustawi wa jamii pamoja na SAWATA hazijafika vijijini kubaini wananchi maskini wasiokuwa na jamaa wa kuwasaidia maisha.
Jitihada za kuwapata maafisa maendeleo na ustawi wa jamii hazikufanikiwa baada ya kufika katika ofisi zao na kuwakosa wasemaji wa idaa hiyo ambapo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ngara Cornel Ngudungi anahudhuria vikao vya serikali za mitaa mkoani Tanga.
Next Post Previous Post
Bukobawadau