HAKUNA TATIZO LA AJIRA NCHINI BALI FIKIRA BILA TAFAKURI
NA PRUDENCE KARUGENDO
KWA sasa kilio kilichotanda nchini ni cha ukosefu
wa ajira! Vijana wengi, hasa wanaomaliza elimu ya juu katika vyuo mbalimbali,
wanalia na wanachokiita ukosefu wa ajira!
Wao wanataka
wakimaliza masomo wakute ajira tele zikiwasubiri, hakuna anayejiuliza hizo
ajira zinatoka wapi au nani mwenye jukumu la kuzitengeneza.
Kabla
sijaenda mbali nihitimishe kwanza kwa kusema kwamba ajira ziko tele ila
kinachokosekana ni uwezo ulio kwenye utashi wa kuzitambua hizo ajira, walio
wengi wamezama kwenye mapokeo ya kwamba kila anayemaliza masomo anapaswa akute ajira inamsubiri kana kwamba ajira
zinatengenezwa na Mungu!
Tatizo
ninaloliona mimi ni la mfumo tulionao wa ufundishaji na uelimishaji katika nchi
yetu, mfumo ambao ni wa kimapokeo usioenda na wakati. Mfumo uliotumika kwa
zaidi ya miaka 50 iliyopita ambapo nchi ingeweza kuzalisha vijana kama 100 au
chini yake wenye shahada ya kwanza kwa mwaka, ukiendelezwa hadi leo ambapo nchi
inaweza kuzalisha vijana kama 10,000 kwa mwaka wenye shahada ya kwanza.
Tatizo hilo
la mfumo wa kimapokeo liko hivi; kijana anaandaliwa akashinde mtihani ili
akapate cheti kitakachomwezesha kupata ajira. Kwahiyo anacholazimika kukiwaza ni ajira anayoamini
iko tayari. Matokeo yake anaweka bidii katika kukariri mambo atakayoulizwa
kwenye mtihani, hahangaiki na uelewa wa mambo mengine nje ya hapo. Huo ni mfumo
wa kimapokeo, kujaza fikira bila tafakuri.
Mfumo huo
uliopitwa na wakati haumpi kijana nafasi ya kuwaza kwamba nchi iliyopata uhuru
wake zaidi ya miaka 50 iliyopita haijaongezeka hata sentimeta moja zaidi ya
kuongezeka tu idadi ya watu wake. Hakuna mwenye wazo la kwamba tulipata uhuru
tukiwa watu karibu milioni 8 na sasa tunakaribia watu milioni 50!
Vijana wanataka
yaliyotokea wakati watu wakiwa milioni 8 ndiyo yaendelee kutokea hata leo
wakati tuko milioni 50!
Kinachowazwa
ni mtu kumaliza masomo na kupata ajira iliyo tayari “ready made”! Ndani ya
fikira bila tafakuri za aina hiyo nani asiyeona kuwa humo kuna tatizo? Ni
tatizo sababu vijana wanajifunza kukariri bila kuona ulazima wa kuelewa. Aliyeelewa
hawezi kutaja ukosefu wa ajira kana kwamba ajira inapatikana kama mvua
inayonyesha bila kujali idadi ya watu waliopo ardhini.
Katika
uelewa ingebidi vijana wanaomaliza masomo, hususan wale wa elimu ya juu,
waelewe ni ajira kiasi gani na za aina gani zinazoweza kupatikana kila mwaka
nchini mwetu na idadi ya wahitimu ambao nchi inawazalisha kila mwaka kabla ya
kulilalamikia suala hilo.
Pia ieleweke
kwamba nafasi za ajira zinazoweza kupatikana kila mwaka haziwezi zikajirudia
zilezile kwa mwaka unaofuatia kwa vile wanaozipata kwa mwaka uliotangulia ndio
kwanza wanakuwa wameanza kuzizoea, hivyo
haiwezekani kwamba watakuwa wamehitaji kustaafu kwa maana ya kuziacha wazi ili kuwapisha
wengine.
Tukichukulia
kwamba mtu anaweza akaajiriwa kwenye nafasi fulani kwa zaidi ya miaka 20, ni
wangapi wenye fani kama ya kwake watakaolazimika kusubiri katika kipindi hicho?
Kwangu mimi
siwezi kusema wanaolazimika kusubiri wanafanya hivyo kwa kutokana na ukosefu wa
ajira, hapana, ila naulaumu mfumo kwa kuwanyima uwezo wa kutafakari na kubuni,
ubunifu.
Utoaji wa
elimu haupaswi kuishia kwenye karatasi ya mtu kusahihishwa akapata alama na
baadaye kutunukiwa karatasi nyingine inayoitwa cheti, halafu akaanza mchakamchaka akikimbizana
nacho eti anatafuta ajira. Utoaji wa elimu unatakiwa uende sambamba na
uwezeshaji wa mtu kuitafakari halihalisi na kubuni njia mbalimbali za
kukabiriana nayo. Bila hivyo elimu itakuwa inakaririsha tu bila kuelewesha,
kitu kinacholeta tatizo badala ya kuliondoa.
Sababu elimu
ya juu inapaswa izalishe ajira badala ya kuitafuta au kuiomba. Lakini katika
hali ya kuelimisha kwa njia ya kukaririsha bila kuelewesha, uwezekano wa mtu mwenye elimu ya juu kupata
fikira za kumwajiri mtu mwingine utatoka wapi?
Ila wapo
wasomi, japo ni mmoja mmoja, walioelimika katika maana halisi. Bwana Kashenshero
Kamushoina ni mtu wa kutolea mfano. Baada ya yeye kupata shahada ya uchumi toka
Chuo Kikuu, alihangaika kwa muda akitafuta ajira ambayo kipato chake
kisingefikia hata shilingi milioni moja kwa mwezi. Akaamua kuachana nayo na
kubuni njia ya kujiajiri mwenyewe. Wasomi wenzake wakaendelea kusaka vibarua wakimuona yeye kama mtu
aliyepotea njia.
Kwa sasa
anasema mbali na kipato chake, ambacho kwa utaalamu wake wa uchumi, kajipangia
mshahara wa shilingi milioni 10 kwa mwezi, pia ameajiri watu 10 anaowalipa kila
mmoja mshahara usiopungua shilingi laki 5 kwa mwezi. Anasema kama utaalamu wake
huo angeuuza mahali popote nchini, kwa maana ya kuajiriwa, hakuna mahali ambako
angeweza kupata kipato hicho. Yeye kabuni na kutengeneza ajira badala ya
kulialia kwamba hakuna ajira.
Kwa maneno
ya utani anasema, “akatembya amaizi aibanga” kwa maana ya kuyapandisha maji
mlimani, tofauti na ilivyozoeleka ambapo maji hutoka mlimani na kutiririkia
bondeni.
Fikiria
tungekuwa na watu walau 5000 hapa nchini walioelimika na kuwa wabunifu kama
alivyo Kashenshero Kamushoina nani angekuwa anataja neno ukosefu wa ajira?
Lawama zangu
kwa mamlaka husika ni kutobadili mfumo wa uelimishaji, mfumo unaoendelezwa ni
wa kuwafundisha vijana kukariri badala ya kuelewa. Vijana wanakariri kuanzia
mambo ya darasani mpaka maisha ya uraiani. Utaratibu huo hauwezi kumpa mtu
upenyo wa kuitafakari halihalisi.
Ni kwamba
kila kijana anapokuwa chuoni akiwaangalia waliomtangulia kumaliza na kubahatika
kupata ajira, naye anawaza kumaliza chuo
ili baadaye apate ajira nzuri zaidi, ajenge nyumba kubwa na nzuri katika maeneo
kama ya Mbezi Beach, Masaki na mengine kama hayo yaliyopo Jijini Dar es salaam,
pamoja na kumiliki magari ya kifahari.
Hayo yote
yanatokana na mawazo ya kukariri, yasiyo na aina yoyote ya ubunifu ndani yake.
Hayo yasipofanikiwa kelele zinaanza kwamba hakuna ajira!
Kwa sasa
hakuna kijana anayetafakari kwamba nchi inaweza ikawa na nafasi 30,000 za ajira
zinazohitaji wasomi wenye shahada, lakini nchi ileile ikawa inazalisha wasomi
wenye kiwango kilekile wasiopungua elfu 10 kwa mwaka na wakati huohuo nafasi
zote zikiwa tayari zimejaa, ajira zitatoka wapi?
Sababu
waliopaswa kutengeneza ajira zaidi ndio wanaotaka ajira zilizotengenezwa
tayari!
Kwa nini
mfumo unaotumika kuwaelimisha vijana nchini unawaandaa kuwa vibarua, kwa maana
ya kuajiriwa, badala ya kuwaandaa wawe wabunifu wa kutengeneza ajira? Uko ni
kuwaandaa au kuwahadaa?
Hebu fikiria
iwapo vijana wanaomaliza elimu ya juu kila mmoja angekuwa anapewa changamoto ya
kubuni walau ajira 20 kwa kila mwaka tungekuwa na ajira kiasi gani hapa nchini?
Si ajira zingekuwa zinawatafuta watu badala ya wao kuzitafuta? Je, huu wimbo wa
taifa wa hakuna ajira ungekuwepo?
Lakini
badala yake vijana wanaelekezwa kukariri maisha waliyoyakuta. Watu wenye elimu
ya Chuo Kikuu wanapigana vikumbo na watu wenye elimu ya darasa la 7 kutafuta
vibarua eti ni ajira! Sielewi ni nani wanamtegemea awe amewaandalia vibarua
hivyo! Aliyetoka mbinguni?
Matokeo yake
ukosefu wa elimu ya ubunifu unawafanya wahitimu wa shahada waishie kuajiriwa na
watu waliomaliza darasa la 7!
Mtu mmoja
aliyeniambia kaishia darasa la 6, kwa sasa ni mkurugenzi wa kampuni
iliyowaajiri watu wengi wenye elimu ya shahada! Yeye hakupata elimu ila akapata
ubunifu, wao wakakosa ubunifu na kupata elimu. Kwahiyo waliopata elimu
wakaishia kumuita “bosi” mtu aliyekosa elimu. Kwahiyo tuseme kizuri ni kipi,
elimu au ubunifu?
Mfano
mwingine ni wa bilionea mkubwa duniani, Bill Gate. Mtu huyo angeng’ang’ania
vibarua, akiwa anaulilia ukosefu wa ajira, mambo yote anayoyasimamia
yaliyotokana na ubunifu wake na kuinufaisha sana dunia yangekuwepo?
La
kuzingatia ni kwamba nchi zote zilizoendelea duniani zimeyafikia maendeleo hayo
kwa kutegemea zaidi ubunifu. Sidhani kama kuna nchi yoyote iliyoendelea kwa
kutegemea misaada kama tunayotamba nayo sisi Tanzania. Maana yangu hapa ni
kwamba misaada ni kama ajira, kutegemea kunufaika na vilivyo tayari. Kulilia
ajira ni sawa na kulilia misaada.
Tuangalie
hapa nchini, tunawaona watu kama Reginald Abraham Mengi, Mohammed Gulam Dewji,
Rostam Abdulrasul Aziz, Said Salim Awadh Bakhresa na wengineo. Mbali na watu
hao kuwa na maisha yao binafsi yaliyo bora, pia wana mchango mkubwa katika pato
la nchi, pamoja na kuzalisha ajira nyingi sana. Mtaji wao mkubwa katika mafanikio
yao hayo ni ubunifu.
Je, watu hao
wangetegemea elimu ili iwawezeshe kupata ajira hayo yote yanayotokana na
ubunifu wao yangekuwepo? Ni mtu gani aliyefikia mafanikio kama waliyo nayo wao
kwa kutegemea ajira tu? Kama kuna anayemjua anieleze.
Mwisho niseme,
tuache kulilia ajira, tujikite kwenye ubunifu ndipo tutajikomboa sisi wenyewe
pamoja na kuikomboa nchi yetu kiuchumi na kimaendeleo.
0784 989 512