KWA WEREMA WATANZANIA NI TUMBIRI WA KUKATWA VICHWA!
Na PRUDENCE KARUGENDO
KATIKA makala yangu ya wiki iliyopita, niliyokuwa naunga mkono wazo la Juvenalis Ngowi la kupunguza ukubwa wa Bunge letu, nilisema kwamba upungufu wa Elimu ya Uraia kwa wananchi ni tatizo kubwa ambalo baadhi ya viongozi wetu wanalitumia kuidumaza nchi yetu kifikra na kimuonekano.
Ukweli huo umejidhihirisha katika Bunge la Bajeti lililomalizika juma lililopita. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema, alithubutu kumuita mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kuwa ni tumbiri! Kituko cha karne.
Kilichomsukuma Werema kutamka tusi hilo lisilo la kiungwana si kingine bali uhakika wa kwamba wananchi hawaelewi umuhimu wa mbunge na jinsi gani wanahusiana na nafasi yake waliyomkabidhi.
Mbali na tusi hilo, Werema akaongeza kwamba kichwa cha Kafulila ni halali yake, akiwa na uhakika kabisa kwamba uelewa mdogo au ukosefu wa Elimu ya Uraia walio nao wananchi usingeweza kuwafanya waelewe kuwa mashambulizi yake hayo hayakuwa dhidi ya Kafulila bali yaliwalenga wao.
Na kweli, wananchi walipoyasikia matusi hayo na vitisho dhidi ya Kafulila wapo waliocheka, wapo walionuna tu na wengine hawakujali kabisa wakiamini kwamba yanayofanyika Bungeni hayawahusu! Yote hiyo ikiwa ni matokeo ya ukosefu wa Elimu ya Uraia ambayo Werema ana uhakika kuwa wananchi hawana.
Sasa tuelimishane kidogo. Kafulila ni mwakilishi wa wananchi Bungeni, wamemtuma. Na usemi wa jadi ni kwamba mjumbe hauawi. Kwahiyo kusema Kafulila ni tumbiri moja kwa moja ni kusema kwamba wananchi wote waliomtuma Bungeni ni tumbiri.
Na Elimu ya Uraia ikishakolea inabidi tuelewe kwamba mbunge akishaingia Bungeni ni mwakilishi wa wananchi wote kwa vile mbunge halazimiki kuwasemea watu wa jimbo lake tu; isipokuwa wapiga kura wa jimbo lake wamewasaidia wananchi wa sehemu nyingine kumpata mwakilishi wanayemuamini anaweza kutoka katika eneo lao kulingana na wanavyomfahamu kwa karibu.
Lakini uwepo wa Werema Bungeni hauna ridhaa ya wananchi. Yeye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyeteuliwa na rais. Bilashaka anaiwakilisha na kuitetea serikali katika jengo lile.
Lakini je, hivyo ndivyo sheria inavyomtuma kwamba akawaite wananchi tumbiri? Je, kamtendea haki bosi wake, rais, aliyempa nafasi hiyo anayoitumia vibaya katika jengo hilo? Hiyo ni kwa sababu rais ndiye mlinzi namba moja wa wananchi ambao Werema anatishia kuwakata vichwa.
Maana yangu hapa ni kwamba Kafulila hakuingia Bungeni kwa utashi wa mtu mmoja kama alivyo yeye Werema, kaingia Bungeni kwa utashi wa wananchi. Kwahiyo matusi kwake ni matusi kwa wananchi, na vitisho kwake, kutokana na nafasi hiyo ya kuwawakilisha vizuri wananchi, ni vitisho kwa wananchi.
Ikumbukwe kwamba tangu Rais Kikwete achaguliwe na wananchi kuwa kiongozi wao mkuu hajawahi hata mara moja kuwatolea matusi wala vitisho kama alivyovitoa Werema. Sio kwamba yeye rais haudhiki, anaudhika sana.
Sababu pamoja na kuwa kiongozi mkuu wa nchi yeye ni binadamu vilevile. Kwa nafasi hiyo aliyo nayo ni lazima ayapate maudhi ya kila aina. Kwa maana hiyo angetumia mamlaka na uwezo wa juu kabisa alivyo navyo kutukana na kutisha kila wakati na kila mahali. Lakini hafanyi hivyo, hekima na busara vinamtawala na kumfanya ailinde heshima yake binafsi, heshima ya wananchi na heshima ya nchi yake kwa ujumla.
Ndiyo maana hakutoa tusi lolote kwa Jaji Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pale alipotofautiana na baadhi ya mambo kwenye Rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume hiyo.
Sasa inapotokea Mwanasheria Mkuu akamuita mbunge, ambaye hakumchagua wala kumteua, kuwa ni tumbiri kisa wametofautiana kimtazamo, je, angekuwa amemteua yeye angemwitaje? Kitendo hicho cha kuwaita wananchi tumbiri, ambacho nina imani rais hakukipenda, rais amwiteje Werema ambaye kamteua yeye mwenyewe bila kuwashirikisha wananchi?
Athari za ukosefu wa Elimu ya Uraia zinajionyesha kwa njia kama hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwaita wananchi tumbiri na wao wakakaa kimya kwa vile tusi hilo limeelekezwa kwa mbunge.
Tusi kama hilo lingetolewa katika nchi ambazo watu wake wameshiba Elimu ya Uraia ni lazima kungekuwepo shinikizo kubwa la kumtaka mhusika “aachie ngazi” mara moja au rais kumfukuza kazi bila kujali uhusiano wao ukoje.
Lakini kwa Tanzania wananchi wana amani na utulivu, hata waitwe tumbiri kwao sawa tu, hakuna anayejali! Elimu ya Uraia.
Hata kama wananchi hawajali, je, rais naye hajali? Bilashaka Werema huyo hajali, vinginevyo tusi hilo na vitisho vilivyofuatia visingetoka kinywani mwake. Kwa nini ajali wakati anaelewa upatikanaji wa cheo chake hauna uhusiano wowote na wananchi?
Katika kupunguza ukubwa wa Bunge letu kwa lengo la kuepuka mambo kama hayo, mara nyingi nimejiuliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) anaingia Bungeni kwa sababu gani? Inadaiwa anaingia kufafanua masuala ya kisheria. Lakini si yupo waziri wa sheria? Kwa nini Mwanasheria Mkuu wa Serikali asiwe kama wakuu wengine wanaosimamia mambo mbalimbali ya kitaalamu wakiwasaidia mawaziri wao bila wao kuwa sehemu ya Bunge?
Mfano, katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tunaye Mkuu wa Majeshi (CDF), Mambo ya Ndani tunaye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Wizara ya Fedha tunaye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) nakadhalika. Hao wote nafasi zao kimuundo ni kama ziko sawa na nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)), lakini mbona wao hawafanywi wabunge na wanayoyasimamia yanaenda vizuri na kwa ufanisi bila ulazima wa kuingia Bungeni na kuwatukana wananchi?
Ni kwamba kwa vile wote hao wako upande wa serikali masuala yote yanayohusu nafasi zao hizo inabidi yakafafanuliwe kwa wabunge kupitia kwa mawaziri husika. Hivyo kuingia kwa AG Bungeni wakati kuna waziri wa sheria ni kulazimisha mgongano wa kimajukumu usio na ulazima wowote. Na matokeo yake, pengine kutokana na kuishiwa majukumu, ndiyo hayo ya AG kuwaita wananchi tumbiri!
Inavyoelezwa ni kwamba Bunge lina pande mbili, upande wa wananchi ukiwakilishwa na wabunge na upande wa serikali ukiwakilishwa na mawaziri. Nyongeza ya AG ni utata unaoishia kwenye hali kama hiyo ya Werema kuwaita wananchi tumbiri na kutishia kuwakata vichwa pale anapobanwa ili afafanue mambo yaliyo nyeti kwa nchi na wananchi.
Mawaziri, hata kama wapo upande wa serikali, wanazichunga sana kauli zao dhidi ya wananchi kwa vile wengi wao wanatokana na wabunge waliochaguliwa na wananchi, wanawajali na kuwathamini wananchi.
Lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatokani na wananchi kwa maana ya kupigiwa kura na wao. Yeye anateuliwa na rais kutokana na anavyopendezwa na uwezo wake. Pengine ndiyo maana Werema anakithamini cheo chake zaidi bila kuwathamini wananchi.
Lakini je, Werema anamtendea haki rais aliyemweka kwenye nafasi hiyo? Iweje rais ashindwe kumuita mbunge tumbiri, kwa vile anaelewa kwamba kwa kufanya hivyo wananchi walioamua kumfanya kiongozi wao mkuu, kwa ajili ya kulinda usalama na heshima zao, atakuwa amewageuza tumbiri, lakini Mwanasheria Mkuu wa serikali atamke hilo bila wasiwasi wowote tena akiwa ameikandamiza sheria aliyowekwa kuisimamia, kwamba kichwa cha mbunge, sawa na vichwa vya wananchi waliomchagua rais, ni halali yake?
Nimkumbushe Rais Kikwete kwamba enzi za uadilifu katika nchi yetu wananchi walithaminiwa na kuheshimiwa sana na uongozi wa nchi. Kila kiongozi aliyetaka kujikomba kwa rais kwa kutumia uduni wa nchi kuwakebehi wananchi aliwajibishwa mara moja.
Wakati huo kuna kiongozi aliyemnukuu Mwalimu kwamba “sageni hivyohivyo”, wakati wa tatizo la chakula nchini, mwingine akasema wananchi wanaweza kwenda kuzimu, wakati wa tatizo la usafiri nchini, hao wote walifanya hivyo wakidhani wanamfurahisha Nyerere, kumbe walimshika pabaya, wakawajibishwa bila kusita!
Iweje sasa kwa mtu anayeonekana anayatetea maslahi binafsi awaite wananchi tumbiri na kutishia maisha yao halafu aendelee “kupeta” katika serikali ya JK? Kwa nini JK amwachie mtu anayempaka matope kiasi hicho aendelee kuwemo kwenye serikali yake?
Baada ya kujibizana na Kafulila Bungeni Werema alionekana akitaka kumfuata Kafulila alipokuwa, akazuiwa na wabunge wenzake. Haikueleweka ni nini alichotaka kukifanya. Sijui kuanzisha vita kati yao au kuua tumbiri kama imani yake ilivyomtuma kuamini? Je, mtu wa aina hiyo anafaa kuendelea kukalia nafasi hiyo aliyopo?
0784 989 512