Bukobawadau

MIRADI INNAYOBOMOANA NI YA MAENDELEO KWELI?

NA PRUDENCE KARUGENDO
INAWEZEKANA  Tanzania ikawa nchi ya kwanza duniani kwa kubuni miradi na kuibomoa ili kuanzisha miradi mipya kabla miradi iliyotangulia haijaonyesha matunda yoyote! Miradi mingi na mikubwa imekuwa ikibuniwa nchini na kugharimu pesa nyingi, mara nyingi ikiwa ni pesa ya kukopa tunayotakiwa kuilipa kwa riba, lakini kabla ya miradi hiyo kukamilika, au kukamilika na kabla ya kuanza kuonyesha manufaa yake, inabuniwa miradi mipya na hivyo kulazimisha kutumia kiasi kingine kikubwa cha pesa kuiharibu miradi iliyotangulia ili kupisha iliyobuniwa kwa upya!
 Wananchi wanaokuwa wametegemea faraja baada ya miradi mipya kukamilika wanalazimika kurudi kwenye karaha pale inapobuniwa miradi mingine na kuibomoa iliyotangulia. Mwenendo huu wa faraja karaha unawezaje kutoa picha ya maendeleo?
Wakati nchi kama Marekani inabuni mradi wa kuwapa faraja watu wake ikiwa imeupangia muda wa miaka kama 100 kabla ya kufikiria kuufanyia mabadiliko, Tanzania inashindwa kubuni mradi inaoweza kuupangia muda wa walau miaka 10 kabla ya kufikiria kuufanyia mabadiliko! Hapa kwetu kila kukicha unabuniwa mradi mpya wa kuupindua mradi uliobuniwa jana yake!
Tatizo hilo la miradi inayobuniwa kila kukicha tunaweza kuliangalia kwa kuanzia katika jiji kuu la nchi yetu, Dar es salaam.
 Mabadiliko ya kila mara yanayotokana na mamlaka husika kuwa na ubunifu usio na kikomo yameilazimisha Dar es salaam kuwa na sura ya kinyonga! Jiji linalokosa utambulisho maalumu kiasi kwamba mtu anayetoka nje ya jiji kwa miezi miwili akirudi anakuta jiji tofauti na aliloliacha! Je, hayo ndiyo maendeleo?
Majiji makubwa duniani yana utambulisho wake ambao ulio mwingi umedumu kwa zaidi ya miaka 100. Hebu nijaribu kutaja utambulisho wa majiji machache ambao umedumu kwa miaka mingi ukiwa umeyafanya majiji hayo kuepukana na ukinyonga.
 Jiji la Nairobi, Kenya, kwa miaka mingi linatambulishwa na jengo la Kenyatta Conference Centre, Paris, Ufaransa, ni mnara wa Eiffel (Eiffel Tower), New York – Sanamu la mwanamke la Liberty (Satatue of Liberty), London, Uingereza – Mnara wa saa (Big Ben), Copenhagen, Denmark – Sanamu la nguva (Little mamaid), Agra, India – kaburi la mke wa mfalme (Taji Mahal), Rio de Janeiro, Brazil – Sanamu la Yesu (Christ the Redeemer), Brussels, Ubeligiji – Sanamu la mtoto (Manneken Pis) nakadhalika.
Dar es salaam tunaweza kusema ni kitu gani kinalitambulisha jiji letu? Mwanzoni, miaka ya nyuma lilikuwa linatambulishwa na Jengo la Kitegauchumi, lakini kutokana na mabadiliko yanayotokea kila kukicha jengo hilo halionekani tena baada ya kufunikwa na minara inayoota kama uyoga na kuibadili kabisa sura ya jiji letu.
  Sisemi kwamba ni vibaya kubuni vitu vipya kwa lengo la maendeleo, isipokuwa ubunifu huo ungeenda mbali zaidi kwa kubuni vilevile sehemu mpya ambazo bado hazijaendelezwa ukiwa umelinda na kuhifadhi historia ya jiji letu na kuepusha adha kwa wakazi wake. Hayo ndiyo tunayoweza kuyaita maendeleo.
Kwangu mimi siwezi kuuchukulia kama maendeleo uamuzi wa kubomoa jengo la zamani na kupachika jipya lililo kubwa zaidi ilhali bado kuna mapori mengi katika jiji letu ambayo hayajaendelezwa wala kukaliwa na kitu chochote. Hayo nayaona kama mabadiliko yaliyokosa mpangilio na kuishia kuibomoa historia ya sehemu husika iliyokwisha endelezwa, kamwe si maendeleo hayo.
Kwa kuonyesha kuwa mabadiliko ya kimaendeleo hayapaswi kuifuta historia ya sehemu husika, tunaweza kuliangalia jiji la Bamako, Mali, kama mfano mzuri. Jiji hilo limeendelea likiwa limeitunza barabara historia ya kale ya nchi hiyo na Afrika kwa ujumla. Kwa maana hiyo jiji hilo limegawanyika katika sehemu tatu zinazojieleza zenyewe, Bamako ya kale, Bamako mpya na Bamako ya kisasa. Ni historia tosha.
Mabadiliko hayo yaliyo katika mpangilio mwanana ni kivutio tosha cha utalii. Kule mtalii hahitaji kuwa na mwongozaji wa kumweleza kwamba sehemu fulani ilikuwa na kitu fulani miaka kadhaa iliyopita,  kilichoondolewa na kuwekwa kingine kabla nacho kuondolewa na kuwekwa hiki kinachoonekana kwa sasa. Kule kila kitu kinajieleza chenyewe.
Sifikirii kama kuna mtalii anayekuja Dar kwa kuvutiwa na minara inayochomoza kama uyoga katika jiji letu ikiwa imechukua maeneo ya kihistoria ambayo ndiyo kivutio kikubwa cha utalii.
Kawaida watalii, hasa wazungu, wanapendelea vitu vya zamani ili wakavilinganishe na vya wakati huu kusudi waweze kujua mahali tulikotoka na tulipo kimaendeleo. Ni vigumu kwao kulijua hilo kwa kuitazama minara mipya ambayo kwao ni kitu cha kawaida kabisa.
Tunaweza kujihakikishia kitu hicho kwa kuangalia namna watalii wanavyopenda sana kutembelea Mji Mkongwe, Zanzibar, Bagamoyo, Pwani na hata Mlima Kilimanjaro. Sababu hizo ni sehemu zenye mambo ya kale. Wanafanya hivyo wakati sisi vya zamani tukiviona ni takataka, tukijitahidi kuvisafisha vyote!
Si ajabu tungekuwa na uwezo hata Mlima Kilimanjaro tungeusambaza na kuusawazisha na badala yake kujenga mahoteli katika eneo lile tukidhani tunawavutia watalii! Wazo hilo linanijia kutokana na kasi ya mpangilio wa mabadiliko ninayoyaona nchini mwetu.
Mama mmoja, Laura Sykes, aliyeandika kitabu cha Dar es salaam: A Dozen Drives Around the City kinachoelezea historia ya Dar es salaam, kilichochapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota Publishers ya Dar es salaam, alisikitishwa sana na mabadiliko yasiyo ya lazima aliyoyashuhudia katika jiji la Dar wakati akiandaa kitabu hicho.
Mama huyo wa Kingereza ni mke wa Roberty Sykes aliyekuwa mkurugenzi wa British Council hapa Tanzania. Yeye kabobea katika uandishi wa historia za majiji anayotokea kuwa mkazi wake.
Mabadiliko mengine yanayoendelea kwa sasa na kuacha maswali ni kama ya kujenga barabara na baadaye kuzibomoa baada ya muda mfupi kupisha miradi mingine, pamona na mambo mengine yanayotengenezwa au kuwekwa mahala na kisha kuharibiwa au kuhamishwa kwenda kwingine kwa madai ya kwamba maeneo husika yana miradi mingine ya kimaendeleo.
Jiji la Dar es salaam lilikuwa linajivunia kituo kizuri cha mabasi yaendayo mikoani na nchi za nje. Ni kituo ambacho kilikuwa hakiko kwingine katika Afrika Mashariki na ya Kati. Kituo hicho sasa kimebaki katika historia.
Kituo hicho maarufu kama “Ubungo Terminal” kimebolewa kupisha mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) ambapo imepangwa kuwa katika kituo hicho ndiko kutakakokuwa kituo kikuu cha mabasi hayo.
Haieleweki kwa nini ubunifu huo haukujielekeza kwingine ambako ni wazi kuliko kuingilia kituo ambacho kilikuwa ni fahari ya nchi, kikiwanufaisha wasafiri kwa kuwa katikati ya maeneo yote ya Dar es salaam, kikiwanufaisha wawekezaji ambao tayari walishajenga mahoteli kukizunguka na wenye mabasi pia.
Niliposikia mabasi yaendayo kasi nilidhani ni usuluhishi wa msongamano wa magari barabarani Dar es salaam. Nilidhani pengine mabasi hayo yatatumia njia ambazo zisigekwamisha magari mengine. Kumbe zinapita chini kama kawaida, kila mahali zitakapokuwa zinapita itabidi magari ya kawaida yasimame kuzipisha, msongamano tayari.
Hata kabla mradi huo wa mabasi yaendayo kasi haujaanza rasmi kufanya kazi tayari umebuniwa mradi mpya wa barabara za ghorofa (flyovers)! Kasheshe lingine katika utengenezaji wake. Hatahivyo mradi huo ni bora kuliko wa mabasi yaendayo kasi, sababu hakuna anayehitaji kuchelewa barabarani hata awe mwenye gari binafsi. Swali ni kwa nini mradi huo haukufikiriwa kabla ya ule unaodaiwa ni wa mabasi ya kasi? Kwa nini ubuniwe mradi mmoja na kabla haujakamilika ubuniwe mwingine wa kuubomoa uliotangulia?
Jambo lingine linalodhihirisha mabadiliko yasiyo na mpangilio ni uhamishaji wa kituo cha daladala cha Mwenge kwenda Makumbusho, Kijitonyama. Kwanza kituo hicho kimeondolewa kwenye eneo kubwa tena lililo katikati ya pande zote zilikokuwa zikielekea daladala. Eneo la mwenge lilikuwa likifikika kwa urahisi kutokana na uzuri wa miundombinu katika eneo lenyewe. Barabara zote zinazoingia au kupita Mwenge ni nzuri sana.
Kule Makumbusho kilikopelekwa kituo hicho ni eneo finyu sana ambalo ukubwa wake ni kama robo ya kituo cha Mwenge. Miundombinu hakuna, maana kuna vichochoro ambavyo vilikuwa ni kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo tu na si kwa ajili ya magari mengi ya abiria.
Ila sishangazwi sana na mabadiliko hayo, sababu kwa mazoea yalivyo si ajabu tukasikia kituo hicho kinahamishiwa kwingine ambako pengine ni kubaya zaidi!
Sielewi mabadiliko haya yasiyo na mpangilio yanalenga kumnufaisha nani. Hivi tunaweza kusema haya mabadiliko yamelenga katika maendeleo ya umma, au ni kuyadumaza maendeleo ya umma na kuyainua maendeleo binafsi hasa ya wale walio katika maamuzi? Tunawezaje kuyategemea maendeleo ya umma kwa mtindo huu wa “bomoa tutajenga kesho”?
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau