MKUU WA MKOA WA KAGERA AENDELEZA VITA YA KUTOKOMEZA UGONJWA WA UNYANJANO UNAOTISHIA KUANGAMIZA ZAO LA NDIZI
Vita dhidi ya ugonjwa wa migomba
ujulikanao kama unyanjano imeingia katika hatua nyingine mkoani Kagera
baada ya Mkuu wa Mkoa kutangaza kuwa kipindi
cha kutoa elimu, na wananchi kung’oa migomba iliyoathirika kwa hiari kimeisha
Juni 30, 2014.
Katika kipindi cha kuanzia
Januari hadi Juni 2014
Elimu ilitolewa bure kwa wananchi kuhusu kung’oa kwa hiari migomba
iliyoshambuliwa na ugonjwa huo . Katika mkoa mzima maeneo yote yaliyokuwa
yameathirika na ugonjwa wa unyanjano
umetokomezwa kwa asilimia 60 hadi sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali
Mstaafu Fabian Massawe anasema asilimia
40 ya maeneo yaliyobaki na ungonjwa wa unyanjano itamalizwa na operesheni ambayo inaanza rasmi
Julai 1, 2014 kwa kuhusisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali na
wananchi wenyewe.
Akitoa ratiba ya utekelezaji wa operesheni
hiyo Mkuu wa Mkoa alisema kuanzia wiki ya kwanza mpaka wiki ya nne mwezi Julai
2014 watendaji wa vijiji na vitongoji watapita kwenye maeneo yao kila shamba
kung’oa migomba iliyoathirika kwa lazima kwa kila mkulima katika Wilaya husika.
Mwezi Agosti 2014 itakuwa zamu ya Madiwani kutembelea kata
zao kuhakikisha ugonjwa huo umemalizika. Wiki ya kwanza na ya pili mwezi Agosti
2014 ni wiki ya Afisa Tarafa kutembelea eneo lake na wiki ya tatu na nne ni
wataalam wa Halmashauri kukagua maeneo yao kama ugonjwa umekoma .
Aidha katika mwezi Octoba 2014
wiki ya kwanza na ya pili Wakuu wa Wilaya na Wabunge watahusika katika kukagua
mashamba ya wakulima na kuhakikisha hakuna ugonjwa wa unyanjano.
Mkuu wa Mkoa na Kamati yake ya
Ulinzi na Usalaama atazunguka mkoa mzima
katika wiki ya tatu na nne mwezi Octoba kuhakikisha kuwa ugonjwa wa unyanjano
umekoma katika mkoa wa Kagera na unakuwa historia.
Operesheni hiyo itaambatana na utekelezaji wa sheria ndogo za serikali za Mitaa kwa wananchi ambao wamekaidi kung’oa migomba iliyoathirika katika mashamba . Sheria hizo ni pamoja na kifungo cha miezi sita jela au faini ya shilingi 100,000/= (laki moja) au vyote kwa pamoja.
Aidha Mkuu wa mkoa ametoa maagizo kwa Wilaya zote kuunda vikosi kazi vya kutekeleza operesheni hiyo. Pili watendaji wote watakaohusika na operesheni hiyo kutoa taarifa kila mara zoezi hilo litakavyokuwa linaendelea kutekelezwa, na tathmini itafanyika mwanzoni mwa mwezi Novemba 2014.
Kwa wazee na wasiojiweza hawatatozwa faini bali vikosi kazi vitang’oa migomba iliyoathirika bure kwasababu ni makundi maalum. Pia msaada wa chakula kwa kaya ambazo zitakuwa zimeathirika kwa kiasi kikubwa kitatolewa kwani serikali tayari imetenga tani 200,000 za chakula kwa mkoa wa Kagera.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2014