SHULE YA MSINGI TUMAINI MANISPAA YA BUKOBA KUJENGWA UPYA KATIKA ENEO LA MAFUMBO KUPISHA UWANJA WA NDEGE BUKOBA
Na:
Sylvester Raphael
Habari njema kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera hasa wazazi wa wanafunzi wa
Shule ya Msingi Tumaini iliyopo katika Manispaa ya Bukoba ambayo ipo upande wa Magharibi mwa Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Shule hiyo imepata mfadhili wa kuijenga upya katika eneo
jingine kupisha uwanja wa ndege.
Habari njema hiyo ilitolewa na
Mkuu wa mkoa wa Kagera katika Mkutano na waandishi wa Habari baada ya kuulizwa
swali na waandishi hao kuhusu usalama wa wanafunzi na majengo ya shule hiyo kutokana
na ndege kupita hatua chache sana toka angani wakati wa kutua jambo ambalo ni
hatari kwa shule hiyo.
Mkuu wa Mkoa Massawe
alisema mara baada ya uwanja wa Bukoba kujengwa katika kiwango cha lami
Shule ya Msingi Tumaini ilianza kuonekana kuwa katika hatari hasa ndege kutimua
vumbi kubwa kabla ya kuruka na kelele nyingi zinazosababisha watoto kutotulia
wakati wakiendelea na masomo shule yao.
“Shule hiyo ipo karbu sana na
uwanja wa ndege wa Bukoba na wakati wa ndege kutua hupita karibu sana (hatua chache kutoka angani) jambo ambalo
huleta taharuki kila mara ndege inapotaka kuruka au kutua , katika hali hiyo
watoto hawawezi kusoma kwa amani na utulivu pia.” Alifafanua Mhe. Massawe.
Baada ya kuona kuwa ni tatizo
kubwa na shule hiyo haiwezi kuendelea kuwepo eneo hilo Mkuu wa Mkoa alipeleka wazo la kuhamisha shule hiyo kwa viongozi
wa Benki ya Dunia ambao waliitembelea shule hiyo na kukubali kuijenga upya shule
hiyo katika eneo linguine.
Benki ya Dunia watajenga Shule
hiyo upya katika eneo la Mafumbo ambapo eneo lakujenga tayari limebainishwa na
mara ya ujezi kukamilika majengo ya Shule ya Tumaini ilipo sasa yatabomolewa
ili kuweka usalaama wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
Katika Hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera ameendelea kuhimiza viongozi na wananchi kundelea kujenga maabara kila shule ya kata na kuzikamilisha maabara tatu kwa kila hule ifikapo mwezi Novemba 2014. Mpaka sasa mkoani Kagera zimejengwa maabara 62 kati ya 457, aidha majengo ya maabara ambazo hazijakamilika yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi.