UKAWA NA ELIMU YA URAIA
Ukawa ijikite zaidi kwenye Elimu ya Uraia
NA PRUDENCE KARUGENDO
KUNA usemi wa kwamba kwenye msafara wa mamba na kenge wamo. Usemi huo umejidhihirisha kwa kauli ya mama mmoja aliye kwenye kundi la Wanaukawa. Mama huyo aliyekuwa kwenye maongezi ya kawaida katika mkoa mmojawapo wa Kanda ya Ziwa, alitoa kauli za kuulaani uamuzi wa Ukawa wa kususia Bunge Maalumu la Katiba akisema huo ni uamuzi usiofaa kwa vile ni wa kujikosesha maslahi!
Akiongea bila kujua kwamba kuna watu waliokuwa wakichomwa na maneno yake hayo, mama huyo ambaye ni mjumbe wa Bunge Maalumu lakini akionekana kuwa mtovu wa uzalendo na aliye mbali na Elimu ya Uraia, aliwalaumu sana viongozi wa Ukawa akisema kwamba uamuzi huo unasukumwa zaidi na ukwasi walio nao viongozi hao wakati wajumbe wengine waliomo kwenye Ukawa wakililia maslahi kutokana na madeni makubwa waliyo nayo.
Watu waliokuwa wanamsikiliza mama huyo walimwangalia wakishindwa kummaliza, huku wengine wakinong’ona kwamba kumbe Bunge Maalumu limeundwa kwa ajili ya kuwafanya wajumbe wake (wabunge) wamalize shida zao ikiwa ni pamoja na kuondokana na ukata!
Sababu picha iliyojionyesha ni ya kwamba yeye yumo kwenye Bunge hilo Maalumu kwa ajili ya maslahi yake binafsi, masuala ya Katiba Mpya hayamo kabisa kichwani mwake. Kwahiyo suala la kwamba Rasimu ya Katiba Mpya imechakachuliwa ni kitu ambacho hakimpotezei muda, ila anajikuta kwenye kundi la Ukawa kutokana na mazingira yalivyo. Ni sawa na kenge kwenye msafara wa mamba!
Hiyo inadhihirisha kwamba ukosefu wa Elimu ya Uraia ni tatizo linalowakumba hata wawakilishi wa wananchi. Haiwezekani hata kidogo mtu aliyeshiba Elimu ya Uraia, tena mwenye jukumu la kuwawalisha wananchi kwenye suala nyeti kama hilo, awe na fikira zilizolenga kwenye maslahi binafsi akiwa ameupiga kisogo umma anaouwakilisha.
Ni kwamba mtu huyo hajui Katiba ni nini na ina umhimu gani kwa nchi na wananchi. Lakini bahati mbaya yumo kwenye kundi la kuiandika Katiba ya nchi, na hasa kwenye kundi maalumu linalojitambulisha kuwa linaitetea Katiba hiyo.
Inavyoonekana ni kwamba amejikuta upande huo wa Ukawa kwa bahati mbaya katika harakati zake za kuyasaka maslahi binafsi. Wananchi wakamuona ni mwakilishi wao anayeweza kuyalinda na kuyatetea maslahi yao na maslahi ya nchi, kumbe mwenzao anachokiwaza ni tofauti kabisa, maslahi binafsi!
Kumbe kama tungekuwa na Elimu ya Uraia inayojitosheleza tusingeyawekea chambo masuala nyeti kwa nchi na wananchi kama lilivyo hili la kuandika Katiba ya nchi. Maana yangu ni kwamba kama tungeitaka Katiba bora kusingekuwepo na posho zilizokufuru, ambazo zinamshawishi kila mmoja kuutaka kwa udi na uvumba ujumbe / ubunge wa Bunge Maalumu, kiasi kwamba hata asiyejua anachokifanya kujitokeza na kudai ataweza.
Bila kutangaza posho, wangetafutwa watu walio na uzalendo na wanaokielewa vizuri kinachohitajika kufanyika wakatuandikia Katiba mpya isiyo na mizengwe yoyote. Watu wa aina hiyo wapo tele, sema wanakoseshwa nafasi na watu wenye kuangalia tu maslahi binafsi.
Utaratibu wa aina hiyo ungetoa nafasi kwa wenye utovu wa uzalendo na wasiokijua wanachopaswa kukifanya kujichuja wenyewe, sababu wangeona kwenda kule ni kupoteza muda wao bure. Kilicho bora na cha manufaa kwa nchi na wananchi kingepatikana bila gharama kubwa kama ilivyo kwa sasa.
Lakini inapotokea upatikanaji wa kitu mhimu na nyeti kwa nchi ukawekewa bei namna hii uwezekano wa kukipata kilicho bora na sahihi unakuwa kwenye hatihati. Sababu wenye uwezo wa kukitoa au kukipata kilicho bora wanajikuta hawana uwezo wa kuzipata nafasi za kufanya hivyo, nafasi zote zinaishia kwa wasio na uwezo wa kutoa kilicho na ubora ila uwezo wa kuzipata nafasi hizo tu.
Kwahiyo katika kuipigania Katiba bora ya nchi ingewabidi Ukawa waunganishe madai yao pamoja na kusambaza Elimu ya Uraia kwa umma, na hata kwa hao wanaowapinga ndani ya Bunge Maalumu. Wengi wa wanaowapinga wakiwa ndani ya Bunge Maalumu wanafanya hivyo kwa ukosefu wa elimu hiyo.
Watu walioiva kwa Elimu ya Uraia ni vigumu kufanya mambo ya kukomoana kwa kitu kinachogusa maslahi ya nchi wakidhani wanawakomoa wanaotaka kukitia mchanga kitumbua chao. Mtazamo wa aina hiyo unaletwa na ugonjwa wa ukosefu wa Elimu ya Uraia.
Ndiyo maana wanaowapinga Ukawa wanadiriki kuiweka pembeni Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyotokana na maoni ya wananchi, na kuanza kujadili mawazo yao binasi na kutaka ndiyo yaingizwe kwenye Katiba mpya ya nchi!
Ukosefu wa Elimu ya Uraia unakuja kwa aina mbili, kuna wasiokuwa nayo kabisa na wengine wakiwa nayo lakini kwa kuelewa kwamba umma unaiokosa elimu hiyo, wanataka waitumie nafasi hiyo kujinufaisha wao kwa kufanya mambo yasiyokubalika lakini yenye manufaa kwao lakini yakiwa na hasara kwa wananchi.
Mama ninayemtaja hapa anadai viongozi wa Ukawa wana ukwasi unaowatosha, eti ndiyo maana hawajali kuziacha posho, ambazo kuna tetesi kuwa zimeongezwa kwa zaidi ya asilimia 100 ili kuwarubuni Ukawa warudi Bungeni na kuacha kususa, na kuendelea kusisitiza kwamba ni lazima wao wajadili Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba badala ya mawazo yanayoletwa na kikundi cha watu, chama tawala.
Kwa mawazo ya mama huyo, ninavyomuona, yuko tayari kufanya lolote linalotakiwa na watu wa kikundi badala ya maoni ya wananchi ilmradi posho ipo.
Mimi ninachoweza kukiona kwa viongozi wa Ukawa sio ukwasi wa pesa kama anavyodai mama huyo, bali ukwasi wa Elimu ya Uraia iliyoambatana na uzalendo.
Sababu viongozi wa Ukawa tunawaelewa. Kuna Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mheshimiwa James Mbatia, Prof. Ibrahimu Lipumba na Maalimu Seif Sharif Hamad. Hao wangekuwa ni watu wa kuujali ukwasi binafsi wa pesa kusingekuwepo na kitu Ukawa. Wangeacha tu ili mambo yapelekwe ovyoovyo na wanaotaka kufanya hivyo, na wao wanaodaiwa ni wakwasi, wabaki wanajitafunia pesa yao bila kelele wala mikwaruzo.
Lakini kwa vile roho zao zimejaa uzalendo, wakiitumia vizuri elimu yao ya uraia, ndipo tunayaona haya kwa sasa, Ukawa.
La kuwasisitizia wananchi ni kwamba yanayofanywa na Ukawa hayalengi kwa manufaa ya Ukawa peke yake, bali kwa manufaa ya nchi nzima. Ila yanayofanywa na wapinzani wa Ukawa ndiyo yamelenga kuwanufaisha baadhi ya watu yakiwa yameuweka pembeni umma wote wa Watanzania.
Watanzania wanaweza wakajiuliza, kama Ukawa wanatetea Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyotokana na maoni yao, hao wanaoipinga Ukawa wanatetea kitu gani? Mawazo wanayoyatetea yametoka kwa nani?
Wapo wanaodiriki kusema kwamba yaliyo kwenye Rasimu ni kama mambo ya kughushi! Mawazo ya ajabu kweli. Sababu wakati wa kukusanya maoni ya wananchi zilikuwa zinachukuliwa sauti, picha za mnato na za video, lakini bado kuna madai ya kulazimisha yanayoonyesha kutokuwa na imani na maoni yaliyokusanywa na Tume kabla ya kutayarisha rasimu!
Wanaoonyesha wasiwasi huo ili kutaka kuhalalisha mawazo yao hawatuonyeshi ushahidi wowote ili kuhalalisha wanachokiamini! Ila wanataka wananchi wawaamini wao wakiwa wameegemea kwenye ukweli wa kwamba Watanzania wanakichukulia kila kitu kiurahisirahisi tu!
Ndiyo maana maoni ya wananchi yanachakachuliwa ili yaonekane hayafai na badala yake
yajadiliwe maoni ya watu wachache ambayo hayamo kwenye Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Maoni yangu ni kwamba; kama kweli tunaitaka Katiba mpya iliyotokana na maoni ya wananchi ni bora posho zingeondolewa, kusudi wabunge wa Bunge maalumu wakaifikirie Katiba badala ya kuzifikiria posho.
Hapo ndipo tutakapokuwa tumeonyesha kuwa tunaipenda nchi yetu na kuitakia mema, lakini kuendekeza posho tuelewe kwamba hakuna kitachopatikana, maana katika utafutaji wa pesa wapo watu ambao wako tayari kuingia hata kwenye moto ilmradi tu pesa waipate!
0784 989 512