UKUBWA WA BUNGE SIO UKUBWA WA UFANISI
NA PRUDENCE KARUGENDO
JUMAPILI iliyopita mwandishi Juvenalis Ngowi aliandika kwenye safu yake ya Wazo Jepesi, katika gazeti hili, kwamba Tupunguze ukubwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ingawa yeye alilichukulia hilo kama wazo jepesi kutokana na jina la safu yake lilivyo, mimi nalichukulia kama wazo zito kulingana na maudhui yake yalivyo. Labda nianze kwa kusema kwamba naliunga mkono asilimia mia kwa mia, na ningewaomba wengine walioshiba Elimu ya Uraia wajitokeze ili tuweze kulijadili kwa pamoja.
Sababu upungufu wa Elimu ya Uraia miongoni mwa wananchi limegeuka tatizo kubwa linalowafanya wananchi washindwe kuelewa dhima ya mambo mbalimbali yanayohusiana na uendeshaji wa nchi yao ukiwemo ubunge.
Wapo wananchi wanaodhani wanampigia mtu kura ili akale, wanadhani ubunge ni kwa ajili ya huyo wanayemchagua na familia yake tu! Kwa maana hiyo ni kama wanampa mtu ubunge ikiwa ni zawadi yake baada ya yeye kuwa amewafurahisha kwa namna fulani, hasa kwa kitu kinachoitwa takrima kwa sasa, ambayo ni rushwa isiyo na pingamizi lolote. Baada ya hapo atakachokifanya mtu huyo huko aendako ni juu yake!
Wananchi wa aina hiyo ndio wanaotaka kwanza wapate chochote toka kwa anayeutaka ubunge kabla ya kupiga kura zao kwake. Akishawapatia vitu vidogo vidogo kama pombe, pilau, sukari, kapero, khanga kwa kina mama nakadhalika, lake limekwisha. Kura zote zake! Na baada ya hapo wasijuane tena mpaka miaka mitano ijayo!
Kwa mpangilio huo hakuna mwananchi anayethubutu kumwajibisha mbunge husika, sababu sio mbunge wake tena bali ni mheshimiwa kana kwamba hakutoka miongoni mwao. Hata mbunge mwenyewe hakumbuki hata kidogo kwamba ana deni la uwakilishi kwa wapiga kura wake, kwa vile aliyowafanyia wakati wa kuupata ubunge yanamtuma aamini kwamba nafasi hiyo kainunua!
Kutokana na hali hiyo ndipo wananchi wanapoamua kumuita mbunge wao kuwa ni kiongozi. Sijui mbunge anamuongoza nani, maana kwa jinsi ilivyo mbunge ni mjumbe anayetumwa na wananchi akayaseme, pamoja na mambo mengine, yale wanayofanyiwa na viongozi wao, hasa pale yanapokuwa hayawaridhishi. Kwa ufupi mbunge sio kiongozi, ila ni mjumbe au mwakilishi wa wananchi.
Upungufu wa Elimu ya Uraia walio nao wananchi unatumiwa vizuri na wabunge kujifanyia mambo kadri watakavyo. Mbali na wabunge wengine kufikia kuwatishia wananchi kuwa watawaweka ndani au kuwachukulia hatua, wanaitumia fursa hiyo kujipangia mishahara, kujiongezea posho, marupurupu na mambo mengine yasiyo na mpangilio huku Bunge likionekana liko wazi wakati vikao vikiendelea!
Sitegemei kama wabunge wangediri kuyafanya hayo yote kama wangekuwa wanajua kwamba wananchi wanakielewa walichowatuma wakakifanye kule Bungeni. Isingewezekana wabunge wauache ukumbi wa Bunge mtupu wakati vikao vikiendelea ilhali wakijua kwamba wapiga kura wao wanakitazama kinachoendelea katika ukumbi huo.
Kutoweka kwao katika ukumbi wa Bunge wakati vikao vinaendelea kunadhihirisha dharau ya kwamba wananchi hawaelewi wabunge wanapaswa wafanye nini, hivyo hawawezi kuwauliza kwa nini hawaonekani ukumbini wakati Bunge likiendelea na shughuli zake. Ni dharau ya wabunge kwa wapiga kura wao inayosababishwa na ukosefu wa Elimu ya Uraia kwa wananchi.
Kwa mwendelezo huo wa wabunge kuwaona wananchi hawakielewi kinachoendelea katika uwakilishi waliowakabidhi, wawakilishi hao kwa kupungukiwa na uzalendo, wanatumia nafasi hiyo kuzipuuza gharama zinazopotea bure kuwaweka Bungeni kwa kipindi chote wanachokuwa kule. Wabunge hawajali kuwa hilo linalopotea ni jasho la wananchi walipa kodi!
Kutokana na kuliona hilo ndipo ninapoungana na Ngowi kusema kwamba ukubwa wa Bunge letu upunguzwe kwa zaidi ya nusu.
Hiyo ni kwa sababu kila nikijaribu kuwahesabu wabunge waliomo ukumbini hawazidi miamoja wakati Bunge letu linao wabunge zaidi ya 300! Kwa nini tuendelee kuwa na idadi kubwa ya wabunge kimahesabu tu wakati hatuwaoni Bungeni? Sanasana hiyo ni kupoteza muda unaomaanisha gharama inayofyonza bure pesa ya mlipa kodi.
Ukubwa wa Bunge sio ufanisi wa Bunge hilo hata kidogo. Kama alivyosema Ngowi wananchi wanaofika hata milioni 10 wanaweza kuwakilishwa na mbunge mmoja na mambo yakaenda sawa, kimaendeleo, tena kwa gharama nafuu zaidi.
Sababu kama uwakilishi mwingi ungekuwa na manufaa makubwa basi Zanzibar ndiyo ingekuwa inaongoza kimaendeleo katika Afrika. Kule karibu kila wananchi 1000 wana wabunge wawili, mbunge na mwakilishi, ambao kimtazamo wanafanya kazi moja!
Lakini kusuasua kwa maendeleo ya Zanzibar kunadhihirisha kuwa uwakilishi mkubwa walio nao watu wa Zanzibar hauwasaidii lolote zaidi ya kuzidisha mzigo kwa walipa kodi na hilo kuwa tatizo lingine linalokwamisha maendeleo yao.
Nitoe mfano wa jimbo moja la Marekani, California. Jimbo hilo linayo idadi ya watu wanaokaribia milioni 38. Linao wawakilishi 53 tu ambao karibu kila mmoja anawakisha wananchi laki 7. Lakini Zanzibar ambayo idadi ya watu wake haijafika milioni 2 inao wawakilishi karibu 100, kwa maana ya wawakilishi na wabunge.
Hiyo maana yake ni kwamba kule Zanzibar kila watu 2000 wana mbunge wao! Kwahiyo kama uwakilishi unamaanisha maendeleo ya nchi tujaribu kulinganisha maendeleo ya jimbo la California na Zanzibar ndipo tuone ninachokisema hapa. Tena ikumbukwe kwamba wanachi wanaotajwa California sio wanaowakilishwa na wawakilishi wao peke yao, si ajabu wawakilishi hao wanawakilisha zaidi ya watu bilioni moja.
Maana wanapowakilisha hata Watanzania wanawakilishwa vilevile katika uwakilishi wao. Tusisahau kwamba bila wao Bajeti ya nchi yetu haifiki kokote.
Namna ya wawakilishi wachache wanavyoweza kuwawakilisha wananchi wengi ni kitu rahisi. Kila mtaa / kijiji, hapa nchini vina uongozi wake. Uongozi huo unaweza kukusanya mahitaji na matakwa ya kila mwanachi kuanzia nyumba 10, baada ya hapo kuna diwani wa kata ambaye anaweza kufikishiwa matakwa ya wananchi wote katika kata yake na yeye kuyawasilisha kwa mbunge wake atakayeyafikisha kunako husika.
Haina haja ya kuwa na rundo la wabunge wasioonekana ni nini wanachokifanya. Wabunge wasiosikika wanajenga hoja gani, au wakati mwingine wakionekana wamesinzia Bungeni pale inapotokea kwa nadra wakaonekana tofauti na ilivyozoeleka kuonekana viti vitupu.
Nakubaliana na Ngowi kuwa nafasi za Viti Maalumu ziondolewe katika Bunge letu. Kuwepo kwa nafasi hizo kunasisimua uhasama wa kijinsia ambao tunakaribia kuuzika. Sababu hatuwezi kusema kuwa tunahitaji usawa wa kijinsia huku tukitenga nafasi za upendeleo kwa ajili ya jinsia fulani. Kwa namna hiyo usawa utatoka wapi?
Katika hilo namuelewa mbunge mmoja ambaye amekalia nafasi ya Viti Maalumu kwa zaidi ya miaka 30! Sielewi hao wa Viti maalumu wanamwakilisha nani, maana jinsia zote mbili zinashiriki kumchagua mbunge mmoja anayeziwakilisha kwa pamoja. Sasa huyo wa Viti Maalumu anamwakilisha nani wakati ambao angewawakilisha wanaye mbunge wao?
Ikumbukwe, tofauti ya jinsia sio ulemavu. Kwahiyo kuendelea kuipendelea jinsia moja dhidi ya jinsia nyingine ni kuzichonganisha jinsia hizo. Lengo ni kupunguza ukubwa wa Bunge, vinginevyo ningesema kwamba jinsia zote mbili zitengewe Viti Maalumu basi.
Sehemu pekee ninayotaka kutofautiana na Ngowi ni kwa watu wenye ulemavu, hao ndio wanaopaswa kuwa na nafasi maalumu. Sababu kama wabunge wanayasahau au wanayaacha makusudi mambo yanayowagusa hata wao, kama barabara, maji, umeme nakadhalika, kweli wataweza kuyakumbuka mambo yasiyowagusa kama matatizo ya walemavu?
Kwa upande wangu ningependelea walemavu wapewe nafasi zao hata kama nao wanashiriki kuwachagua wabunge wa kawaida. Wabunge walemavu wawepo kuwawakilisha walemavu wenzao kwa vile ndio wanaoelewa matatizo yanayowagusa.
Bunge dogo, kwa maana ya Bunge lenye wabunge wachache, liko kwenye nafasi nzuri ya kuchochea maendeleo ya nchi kuliko lenye utitiri wa wabunge. Wabunge wachache watatumia muda mfupi kujadili kwa ufasaha yanayotakiwa kujadiliwa.
Na kwa vile ni wachache uwezekano wa kuwa na makundi ya kuzomeana badala ya kujenga hoja zenye tija unakuwa mdogo. Na juu ya yote hayo nchi itakuwa imeokoa pesa nyingi sana inayotumika kuwalipa wabunge wengi kwa kazi ambayo manufaa yake hayana uwiano hata kidogo na malipo hayo.
Kama wingi wa uwakilishi na uongozi wa wananchi ungekuwa na tija inayowiana na ukubwa maendeleo yanayopatikana, kiasi cha kuwepo uhalali wa kila wananchi 50,000 kwenda chini mpaka 2000, kuwa na mbunge wao, basi nchi yenye watu wanaokaribia milioni 50 ingetakiwa iwe na marais zaidi ya 10 na wajumbe wa kudumu Umoja wa Mataifa wasiopungua 100 ili kuleta ufanisi kwa haraka zaidi katika nchi husika.
Lakini kama rais mmoja anaweza akaongoza nchi yenye idadi hiyo ya watu kwa ufanisi mkubwa, tunashindwaje kuona kwamba hata mbunge mmoja anaweza akauwakilisha kwa ufanisi mkubwa mkoa wenye idadi ya watu wasiofikia milioni 3?
Kama kweli tunaipenda na kuitakia mema nchi yetu, hayo ndiyo mambo ya kuyatafakari. Lakini kama tunaiona nchi yetu kama shamba la bibi, basi kila familia inaweza ikawa na mbunge wake.
0784 989 512