Bukobawadau

CHIKU ABWAO; NITAKUWA WA MWISHO KUISALITI CHADEMA

Kwenye mkutano na waandishi wa habari leo, Dodoma Hotel, Mjumbe wa Kamati ya Chama na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao ametoa kauli nzito akisema atakuwa mtu wa mwisho kusaliti CHADEMA na siasa za mabadiliko kwa ujumla.
Abwao ambaye ni mmoja wa akina mama shupavu na imara wa CHADEMA akiwa ametumikia Watanzania kwenye siasa za mabadiliko tangu miaka ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi, amesema hawezi kwenda kinyume na maamuzi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao umeazimia kusimamia maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.

Mbunge huyo amelazimika kuweka kumbukumbu sawa mbele ya mkutano na waandishi wa habari, baada ya kuwepo taarifa za upotoshaji kuwa yuko Mjini Dodoma kushiriki vikao vya Bunge Maalum la Katiba Mpya vinavyoendelea mjini humo.

"Hizi ni mbinu za kitoto za kutaka kuniharibia jina langu na kazi zangu za kisiasa. Mimi Chiku Abwao nitakuwa mmoja wa watu wa mwisho kabisa kukisaliti chama changu...nitakuwa mmoja wa watu wa mwisho kabisa kusaliti mageuzi na mabadiliko ya mfumo na utaawala ambayo nimeyapigania sehemu kubwa ya maisha yangu.

"Natambua msimamo wa kuwataka wabunge na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na chama chetu kutohudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba Mpya ni azimio la Kamati Kuu ya Chama ambayo mimi pia ni mjumbe, siwezi kukiuka maagizo ya chama.

"Chama kupitia Kamati Kuu kiliazimia kwamba wajumbe wanaotokana na CHADEMA tutaungana na wenzetu wengine kwenye UKAWA kutohudhuria vikao vya Bunge Maalum kwa sababu hakuna nia ya dhati ya kutafuta maridhiano ya kitaifa katika mchakato huu kwa kujadili maoni ya wananchi bungeni.

"Mimi siwezi kuja hapa Dodoma kusaliti UKAWA na kushiriki vikao vya Bunge Maalum la Katiba...maamuzi ya UKAWA ni maamuzi ya wananchi, siwezi kuja hapa kuwasaliti wananchi. Ninajua ninachokifanya katika siasa za mageuzi, ni kutumikia wananchi si kutafuta maslahi," amesema Abwao.

Abwao amezidi kufafanua kwamba aliwasili Dodoma kwa ajili ya kuchukua gari yake aliyoiacha katika yard ya bunge wakati alipoondoka nchini kwenda Australia akiwa sehemu ya ujumbe wa Bunge, kuiwakilisha nchi kwenye mkutano wa masuala ya UKIMWI.

Amesema kuwa alipofika mjini Dodoma alikwenda kulichukua gari lake kwenye yard ya bunge (viunga vya bunge) na akaanza kulifanyia matengenezo kwa ajili ya safari ya kwenda Iringa.

"Siku ya jana (Jumatano) nimekuwa na kazi ya kuzunguka hapa mjini kutafuta spares kwa ajili ya kutengeneza gari langu...sasa nimeonekana sana huko kwa sababu nilikuwa natumia usafiri wa taksi...wao wakaamua kufanya propaganda za kwamba mimi niko hapa kuhudhuria Bunge Maalum. Wanapoteza muda wao. Tuko na wananchi," amesema Abwao.
Next Post Previous Post
Bukobawadau