Bukobawadau

KATIBA YA KWELI ITAPATIKANA NJE YA BMK

NA PRUDENCE KARUGENDO
PAMOJA na baadhi ya wananchi,  akiwemo Mwenyekiti  wa Bunge Maalumu la Katiba, Samweli Sitta, kuonekana wanabeza kwamba kujiondoa kwa Ukawa kwenye Bunge Maalumu la Katiba hakulizuii Bunge hilo kuendelea na mchakato wa kuiandika Katiba mpya, ukweli ni kwamba kauli hiyo ni ya kuwafurahisha kwa muda mashabiki wa mtazamo huo potofu.
Uwezekano mkubwa na ulio sahihi ni wa kwamba Katiba ya kweli ya nchi yetu itatokana na Ukawa. Wenye upeo mfupi na potofu ndio wanaweza kutazama na kuona mambo tofauti na hilo nilionalo mimi.
Wenye mawazo ya kukaririshwa bila kuelewa kuwa wanakaririshwa ndio wanaodai kwamba hawawaelewi Ukawa na msimamo wao wa kulisusia Bunge Maalumu. Kinachosisitizwa na watu hao ni kuwataka Ukawa wakarudi Bungeni eti ili kama kuna upungufu wowote wanaouona Ukawa wakausemee kule.
Lisiloonekana kwa wenye shinikizo la aina hiyo ni kwamba hoja hiyo ni ya kutaka kulazimisha kusudi Katiba iwe na mwonekano wanaoutaka baadhi ya watu huku kukiwa kumejengeka uhalali kuwa muundo wa Katiba umeridhiwa na Bunge Maalumu lililowajumuisha wajumbe wote wa bunge hilo,  kwa kanuni ya wengi wape, wakati ukweli ukidhihirisha kuwa wajumbe wenye hoja za kiuzalendo na waliodhamiria kuona nchi inapata Katiba iliyo bora kwa manufaa ya wananchi wote ni wachache na hawasikilizwi.
Katika hali ya kawaida inawezekanaje watu wasiosikilizwa kutokana na uchache wao waendelee kukaa na watu walio wengi, hata kama wingi wao hauwafanyi wakielewe wanachokijadili, na kukijadili kitu hicho kinachoeleweka kwa wachache na kuwapita pembeni walio wengi?
Fikiria watu wanapaswa wajadili kuhusu ngombe, lakini wanaletewa bata eti wakamjadili ili baadaye ageuke kuwa ng’ombe! Kwa wenye akili timamu ni lazima watasusa na kuachana na mjadala.
Kwahiyo mtu anayegoma kumjadili bata akiamini kwamba hawezi kugeuka kuwa ng’ombe, akitaka aletewe ng’ombe mwenyewe ili mjadala uendelee, atalaumiwa kwa lipi?
Suala la kwamba Katiba itajadiliwa Bungeni tu na sio nje ya hapo ni lazima lionyeshe kuwa wanaofikiria hivyo wana upeo ulio na walakini katika uelewa wao. Sababu kama Katiba inapaswa iongelewe tu Bungeni na sio mitaani maana yake ni kwamba Katiba hiyo itafanya kazi tu Bungeni na sio mitaani. Lakini kama ni Katiba ya watu inayopaswa kugusa maisha yao ya kila siku kule waliko mitaani, sioni kwa nini isiongelewe namna inavyopaswa kuwa kulekule mitaani waliko wananchi.
Nikumbushe  yaliyowahi kutokea hapa kwetu miaka sio mingi iliyopita. Lilijitokeza suala la pesa za EPA, Dk. Slaa, wakati huo akiwa bado mbunge, akalifikisha suala hilo Bungeni. Bunge likachachamaa  kutokana na kutovutiwa na suala hilo. Slaa kuona hivyo akalichomoa Bungeni na kulipeleka likajadiliwe mitaani.
Kilichotokea tulikiona. Suala la EPA liligeuka moto wa nyika. Lakini endapo Slaa angeendelea kulibakiza Bungeni ni lazima angeishia kufukuzwa Bungeni kwa madai ya kulazimisha ya kwamba kalidanganya Bunge baada ya kuwa amechezewa mduara na wabunge walio wengi.
Na sakata hilo lingezimika bila kufanyiwa lolote.
Lakini kwa kulipeleka suala hilo mitaani alichokilenga kilitimia. Nje ya Bunge kulifanikisha mambo kuliko ndani ya Bunge.
Nchini Afrika Kusini, Katiba bora ya nchi hiyo ilitokana na msukumo wa waliokuwa nje ya Bunge la nchi hiyo. Kama ilivyo hapa kwetu, waliokuwa ndani ya Bunge hawakuipenda Katiba mpya sababu ilikuwa inawanyag’anya walichokuwa wakikifaidi pasipo na uhalali wowote.
Kwahiyo waliokuwa nje ya Bunge, na sio hivyo tu bali nje kabisa ya nchi yao, wakiwa Zambia, Tanzania na kwingineko, wengine wakiwa Ughaibuni, ndio walioshinikiza Katiba mpya ya nchi hiyo ipatikane kwa kulitumia jina la mtu aliyekuwa kifungoni na tayari kufa kuliko kuiona nchi yake ikiendelea kuendesha mambo kinyume na uhalali, Nelson Mandela.
Kina Mongosuthu Gatsha Buthelezi, waliokuwa wamelambishwa tamutamu na makaburu na kukubali kuwasaliti wananchi wenzao kuhusu muundo wa serikali ya makaburu, wakajifanya hawauoni kabisa ubaya wa Katiba iliyokuwepo. Kwahiyo wakawa wanajaribu kupingana na msukumo uliokuwepo wa kuidai katiba mpya, toka nje ya Bunge na nje ya nchi, ambayo ingewaweka huru wananchi wa Afrika Kusini. Kwa ufupi, Katiba bora ya nchi hiyo ilipatikana kutoka mitaani, hasa mitaa ya nje ya mipaka ya nchi yao.
Kwa kulitazama hilo tuwafikirie vipi wanaosema kwamba Katiba mpya ya Tanzania haiwezi kuongelewa nje ya Bunge? Wanakijua wanachokisema au wanawaona wananchi wote ni matuyuyu wasiokielewa wanachokisema na kukidai?
Katika mchakato huu wa kuipata Katiba Mpya yanasemwa mengi, wapo wanaosema kwamba Katiba Mpya isijadiliwe kwa msukumo wa itikadi za kisiasa, hilo ni sahihi kabisa. Lakini ajabu wanaosema hivyo mara wanasikika wakisema kwamba Katiba mpya lazima ifuate mambo fulafulani kwa vile ndio msimamo na sera ya chama chao! Unashawishika kujiuliza, msimamo wa kwamba Katiba Mpya isijadiliwe kwa msukumo wa itikadi za vyama ya siasa unakuwa umeenda wapi?
Na wengine wanasema kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu wasisikilize kauli za wanasiasa, papo hapo unawasikia haohao wakielekeza mambo fulanifulani, kama yale ya Ukawa wasisikilizwe, au Bunge la Katiba linaweza kuendelea bila Ukawa! Ukiuliza hao wanasema kwa nguvu gani unaambiwa ni Katibu Mkuu wa Chama tawala, au Makamu wa Mwenyekiti! Na wakati mwingine watu hao wanadiriki kutoa hata makaripio kwa Bunge Maalumu! Je, wanasiasa wanaosemwa wasisikilizwe ni wa aina gani kama hao hawamo kwenye kundi hilo?
Kwa upande mwingine nimemsikia Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samweli Sitta, akivishambulia vyombo vya habari vya ITV na Redio One kwamba vimefanya kufuru kurusha moja kwa moja mjadala uliohusu Mchakato wa Katiba Mpya. Swali ninalojiuliza ni kwamba, mtu huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, anadhani Katiba ni mali ya nani kama hataki wananchi waijadili?
Siamini kama Katiba inayotafutwa ni mali ya Sitta na kundi lake tu. Kama na yeye anaamini hivyo kwa nini achukie kusikia wadau wa Katiba wanarusha moja kwa moja hoja zao kupitia redio na luninga kusudi wananchi, ambao Katiba ni mali yao, wasikilize nchi nzima? Kwa nini Sitta anapendelea usiri katika jambo la wananchi wote?
Katika mchakato huu pia kunajionyesha dalili za watu kusalitiana kimakundi. Katika jambo la umma na lililo nyeti kama Katiba ya nchi, kusalitiana ni jambo hatari sana kwa mustakabali wa nchi. Kama wewe ni mtu uliyejaa usaliti unawezaje kuvuta imani ya wananchi wakuamini kwamba huwezi kufikia wakati nao ukawasaliti na pia kuisaliti nchi yao pale ukilengeshwa kwenye utamu unaoweza kuuona ni zaidi ya nchi yako na wananchi wenzako, utamu unaoweza kuwa umetoka nje ya nchi yako au nje ya jamii uliyomo?  
Hayo nayasema nikiwa nimewalenga watu wanaosemekana wamevisaliti kimaamuzi vikundi vyao. Watu hao, hata kama watajaribu kutengeneza hoja za kujitetea bado ni wasaliti tu, hawafai hata kidogo.
Hao ni watu ambao hawapaswi kuaminiwa kokote kutokana na kukosa moyo wa uzalendo. Asiyekuwa na moyo wa uzalendo kwa kikundi chake kamwe hawezi kuwa na moyo wa uzalendo kwa nchi yake. Sababu kilichomsukuma aukose uzalendo kwa kikundi chake, kikiboreshwa ni lazima kimsukume kiurahisi kuukosa uzalendo kwa nchi yake na hata kuikana kabisa!
Kwahiyo hata CCM wakiwakumbatia watu wa aina hiyo ni lazima waelewe kuwa wanaikumbatia hatari, kama kweli chama hicho kina uzalendo kwa mambo yake kinayoyafanya, vinginevyo kitakuwa kinajisaliti chenyewe na pia kuisaliti nchi kinayoitawala kwa sasa kwa kuwakumbatia wasaliti wanaoachana na misimamo yao eti kwa vile wameonyeshwa pesa.
Na tukae tukielewa kwamba haiwezekani hata kidogo tukaipata Katiba ya nchi iliyo bora ndani ya misimamo ya kusalitiana. Katiba bora ni lazima itokane na maridhiano na sio kusalitiana,kutishana wala kulazimishana. Vinginevyo Katiba hiyo inaweza kupatikana nje ya utaratibu uliowekwa, ambao unaanza kuonyesha dalili za ugonjwa nilioutaja hapo juu. Hiyo ni kwa sababu Katiba ni mali ya wananchi wote na wala sio vikundi tu vinavyoanza kusalitiana vyenyewe kwa vyenyewe.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau