KIKWETE USO KWA USO NA UKAWA
Dodoma/Dar. Wakati wowote wiki hii, Rais Jakaya Kikwete
anatarajia kukutana na viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) ili kuzungumzia mchakato wa Katiba.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete atakutaka
‘kiaina’ na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao
unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF.
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wa Ukawa na baadhi
kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM
kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa
katika Rasimu.
TCD inaundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi
bungeni ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, huku
vyama visivyo na uwakilishi bungeni vikiwakilishwa na UPDP
kinachoongozwa na Fahmi Dovutwa.
Jana, kwa nyakati tofauti wenyeviti wenza wa
Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James
Mbatia (NCCR Mageuzi), walisema wako tayari kukutana na Rais, ila
msimamo wao wa kutaka ijadiliwe rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa Ukawa kuomba
wakutane na Rais Kikwete kwa ajili ya kujadiliana namna bora ya
kuendesha mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma
jana, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema Rais atafanya kikao hicho
wakati wowote ndani ya wiki hii na kwamba viongozi wa vyama wakiwamo wa
Ukawa, wamethibitisha kushiriki.
Cheyo alisema, katika kikao walichokutana Dar es
Salaam Agosti 23, wanachama wa TCD walikubaliana kwamba upo umuhimu wa
kukutana na Rais Kikwete kwa mazungumzo na maridhiano.
Kukutana kwa viongozi hao, kunakuja huku wajumbe
wa Bunge Maalumu wakiwa wamemaliza kujadili sura zote 15 zilizokuwa
zimesalia na tayari baadhi ya kamati zimemaliza kupiga kura wakisubiri
kuingia bungeni Septemba 2 kwa kazi ya kupigia kura sura kwa sura.
Kuhusu viongozi wa Ukawa, alisema wanazo taarifa
na baadhi yao walikuwapo katika kikao cha kujadili kukutana na kiongozi
huyo wa nchi, hivyo akasema lazima watashiriki wakati wowote wakiitwa.
Lipumba
Akizungumzia mkutano huo na Rais, Profesa Lipumba
alisema: “Tunakutana na Rais Kikwete kwa sababu sisi ni wanachama wa
TCD.” Alipoulizwa juu ya msimamo wa Ukawa, alisema lengo ni kutafuta
mwafaka ili mchakato wa kupata Katiba Mpya uendeshwe kwa kufuata sheria,
kanuni na taratibu.
“Kikubwa tunachokitaka ni maoni ya wananchi yaliyokusanywa na
Tume ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Warioba kuheshimiwa na siyo
kuchukuliwa maoni mengine kama inavyofanyika sasa huko bungeni,” alisema
Profesa Lipumba.
Mbowe alisema Katiba Mpya ni kwa masilahi ya
Watanzania wote na Taifa lao, hivyo inapotokea mikutano kama hiyo na kwa
hali ilivyo sasa, hakuna mtu mwenye nia njema atakayekataa kushiriki.
Kikubwa ni kwamba hatuwezi kubadili msimamo wetu na huo ndiyo ukweli,”
alisema.
Kuhusu Bunge hilo kupokea maoni ya makundi
mbalimbali wakati tayari ukusanyaji wa maoni umeshafanywa na Tume ya
Jaji Warioba, Mbowe alisema, “Ndiyo maana tulisusia vikao vya Bunge la
Katiba, nadhani sasa Watanzania wamejua kwa nini tulitoka nje.”
Mbowe alisema kuwa mchakato wa Katiba unaendeshwa
kwa mujibu wa sheria, lakini hivi sasa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel
Sitta analiendesha Bunge hilo kinyume na sheria hiyo... “Ukusanyaji wa
maoni unaofanyika sasa ni fedheha kwa CCM na Serikali, ni utoto na aibu
wa CCM. Kwa sasa Ukawa tumetulia tunatazama hali inavyokwenda na tuna
mipango yetu ambayo tunapanga. Kama hali ikiendelea kuwa hivi tutachukua
uamuzi mgumu ili dunia nzima ijue.”
Alisema wako tayari kukutana na Rais Kikwete kwa
ushauriano kwa sababu suala la maridhiano ni la msingi na viongozi wote
wa TCD walikubaliana Agosti 23.
“Mwaliko tumeupata na tutashiriki. Bunge linaweza
kuendelea kwa taratibu zake za kisheria, lakini suala la mashauriano,
lazima tukae tuangalie ni jinsi gani Taifa letu linaweza likavuka kwa
maridhiano kwa amani na utulivu,” alisema.
Kauli ya Ikulu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu
alisema Rais Kikwete yuko tayari kukutana na viongozi wa vyama vya
siasa muda wowote... “Wao wafuate utaratibu tu, Rais hawezi kukataa
kukutana nao na hilo amekuwa akilisema mara nyingi tu.”
MWANANCHI.
MWANANCHI.