RAIS KIKWETE NA RAIS NKURUNZIZA WAZINDUA UIMARISHWAJI WA MPAKA WA KIMATAIFA KATI YA TANZANIA NA BURUNDI MUGIKOMERO MKOANI KAGERA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Jamhuri ya
Burundi Pierre Nkurunziza kwa pamoja walizindua uimarishwaji wa mpaka wa
kimataifa kati ya nchi mbili za Tanzania na Burundi kijijini Mugikomero Wilayani Ngara tarehe 27/08/2014
Uzinduzi
wa uimarishwaji wa mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi ulifanyika kwa ushirikiano na makubaliano kati ya
Watanzania na Warundi baada ya miaka 90 toka mipaka iliyowekwa na wakoloni
tarehe 12/08/1924 na iliyokuwa “Anglo Beligian Boundary Commission”.
Rais
Kikwete akiwahutubia wananchi toka nchi za Burundi na Tanzania waliofurika
katika mpaka wa Mugikomero alisema mpaka
umeimarishwa siyo kwasababu kuna mgogoro bali ni kutokana na ushirikiano na
mahusiano mazuri kati ya wananchi wa Tanzania na Burundi.
“Ni
vyema kuimarisha mipaka yetu kusudi wananchi waelewe wapo upande gani wa nchi
hizi mbili ili kuweka mahusiano mazuri na kuondoa mkanganyiko ni wapi baadhi ya
wananchi wanatoka, baada ya kuimarisha mipaka wao wenyewe wataona na kujua ni
raia wan chi gani. Alisema Rais Kikwete.
Rais
kikwete alisema kuwa uimarishwaji wa mpaka kati ya Tanzania na Burundi ni agizo
la Umoja wa Nchi za Afrika (AU) ambapo Umoja wa nchi za Afrika uliagiza nchi
wanachama ifikapo mwaka 2017 nchi zote ziwe zimeimarisha mipaka yao kwa
makubaliano ili kuondoa migogoro kati ya nchi moja na nyingine isiyokuwa ya
lazima.
Mara
baada ya mpaka wote wa Tanzania na Burundi kuwa umeimarishwa utasainiwa mkataba
wa makubaliano kati ya Tanzania na Burundi na kuufuta mkataba wa mipaka
uliowekwa na wakoloni na mkataba huo utakuwa wa Watanzania na Warundi na siyo
Waingereza na Wajerumani.
Rais
Kikwete alisistiza kuwa kwa kizazi cha sasa kilichoshuhudia kazi za kurudisha
mawe ya mipaka kitakuwa mlinzi wa mpaka na anaamini kuwa mawe ya mipaka
hayawezi kuhujumiwa wala kung’olewa kwani sasa wananchi wameelewa nini maana ya
mawe hayo na wataendelea kuyalinda na kudumisha udugu kati ya nchi mbili.
“Marafiki
huchora mipaka kwa kalamu kukiwa na amani na utulivu lakini maadui huchora
mipaka kwa nguvu na wino wa damu sisi ni ndugu na mipaka yetu tumeimarisha kwa
makubaliano makubwa na ushirikiano na tutaendelea kudumisha amani na utulivu
daima” Alisistiza Rais Kikwete.
Waziri
wa Ardhi na Mendendeleo ya Makazi wa Tanzania Profesa Anna Tibaijuka
akizungumzia uimarishwaji wa mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani alisema
kuwa tayari kwa upande majini mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani tayari
imeimarishwa na awamu ya kwanza kati ya Tanzania na Burundi imekamilika kwa kilometa 170. (Ngara Kagera)
Awamu
ya pili itakuwa ni mpaka uliopo upande wa mkoa wa Kigoma kilometa 120 na awamu
ya tatu itakuwa kilometa 160 katika mpaka wa Tanzania na Burundi ulipo mkoani
Kigoma. Profesa Tibaijuka alisema kuwa zoezi la kuimarisha mipaka linahitaji
fedha nyingi na ndiyo maana wanafanya uimarshaji wa mipaka kwa awamu.
Profesa Tibaijuka
alisema uimarishaji wa mipaka unafanywa kwa makubaliano kati ya nchi husika na
makubaliano hayo ni pamoja na kila nchi kukubali kuacha eneo la wazi la meta
12.5 (Buffer Zone) kila upande kutoka
kwenye jiwe la mpaka na kuliacha eneo hilo bila kulifanyia shughuli yoyote ile
ya kibinadamu ili mpaka uonekane vizuri.
Profesa Tibaijuka
alisema kwa sasa zinahitajika zadi ya
billion 2.7 ili kukamilsha uimarishwaji wa mpaka kati ya Tanzania na Burundi
kwa awamu mbili zilizobaki. Rais Kikwete alihaidi mbele ya wananchi kutafuta
fedha hizo ili wizara ikamilishe kazi hiyo kabla ya mwaka 2017 na kuagiza
yafuatayo;
Kwanza
wananchi wote wanaoishi katika maeneo ya mipaka wayalinde mawe yaliyojengwa
kuonyesha mipaka bila kuyahujumu, Pili Mikoa na Halmashauri zote zinazopakana
na nchi jirani itenge bujeti ya kilinda mipaka iliyoimarishwa, na mwisho ni
Kamati zinazohusika na uimarishaji wa mipaka kukamilisha kazi kwa wakati kabla
ya mwaka 2017
Rais wa
Burundi Pierre Nkurunziza akihutubia umati uliofurika Mugikomero Wilayani Ngara
aliishukuru Tanzania kwa kushirikana
na nchi yake katika kushirikishwa,
kuunda kamati ya pamoja ya wataalam hatimaye kufanya kazi kwa pamoja ya kuimarisha mipaka kati ya nchi hizo mbili
Rais Nkurunziza
alisema wakati Burundi inatafuta uhuru Rwagasole alishikwa mkono na Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na kumsaidia sana mpaka Burundi ikapata uhuru. Aidha
alisema kuwa Tanzania imekuwa ikisaidia sana Warundi wanapopata matatizo na
kuyatatua matatizo yao.
“Wakati wa machafuko
huko Burundi zaidi ya warundi milioni moja walikimbilia Tanzania na walifanya
uharibifu mkubwa wa mazingira lakini bado ndugu zetu watanzania walendelea
kutusaidia na kutuvumilia bila kutuchoka ambapo inaonyesha kuwa Tanzania ni
zaidi ya undugu.” Alishukuru Rais Nkurunziza.
Rais Nkurunziza
aliihakikishia Tanzania kuwa Burundi watendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania
aidha, nchi ya Burundi itaendelea kuchangia na kutoa ushirikiano katika
kuimarisha mipaka kati yake na Tanzania.
Tanzania
inapakana na nchi nane na zifuatazo ni kilometa za mipaka kati ya Tanzania na
nchi hizo; Rwanda 217 km, Zambia 338 km,
Uganda 396 km, Burundi 451 km, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
473 km, Malawi 475 km, Msumbiji 756 km, na Kenya 769 km.