UHUSIANO WA TZ NA ISRAEL
Uhusiano na Israel, Tanzania iepuke
jazba
Na Prudence Karugendo
ILIWAHI kutokea
Tanzania ikavunja uhusiano wake wa kibalozi na Israel katika mazingira ya
kiutu, mazingira yaliyoonyesha kwamba Israel iliusahau sana utu na kufanya ma bo
yaliyoonyesha unyama zaidi. Lakini nchi hiyo ilipojirudi mambo yakabadilika,
uhusiano baina ya mataifa haya mawili ukarudi kwenye hali yake ya kawaida.
Nimeshawishika
kulijadili hilo kufuatia maandamano yaliyofanywa hivi majuzi na kundi la wau
Jijini Dar es salaam, wakiitaka serikali ya Tanzania ivunje tena uhusiano wake
na Israel, shinikizo linalofuatia hali mbaya inayoendelea kwa sasa kati ya
Israel na Palestina.
Machafuko
hayo yamesababisha roho za mamia ya watu kupotea bila sababu yoyote ya lazima.
Ninaposema
roho za watu simaanishi za upande mmoja tu, kama baadhi ya watu
wanavyolazimisha ionekane, roho za watu zinazopotea ni za pande zote mbili,
Irael na Palestina.
Kwahiyo
siwezi kuyaangalia machafuko hayo kwa kuuhurumia upande mmoja tu hata kana ndio
unaopoteza sana roho za watu. Upande wa pili nao inabidi uangaliwe na
kuhurumiwa pia, hata ukionekana unapoteza roho chache za watu, upotevu wa roho
ni upotevu wa roho hata iwe ya mtu mmoja, hauna mbadala, roho iliyotoka
hairudi.
Ninachokiona
kuwa kinakosewa na watu wengi ni kule kuonyesha huruma kwa upande mmoja ulio
mnyonge, eti kwa vile unapoteza roho nyingi za watu kutokana na unyonge wake
bila kujali kuwa ni upande huo unaoanzisha uchokozi! Imani yangu ni kwamba
mnyonge anapoleta unyongaji atanyongwa.
La
kustaajabisha ni kwamba wanapouawa Wayaudi inaonekana ni sawa tu, watu hawapigi
kelele! Hivi watu wanataka Wayaudi nao wakubali kuwa ni halali wao kuuawa!
Wanataka Wayaudi wakiuawa wasijibu!
Kama ni
hivyo, ni nini maana ya kuwa na nguvu na
akili za kuzitumia nguvu hizo? Tuseme mtu anaaminika alivyo na nguvu sana
katika kundi fulani la watu, lakini anatokea mtoto mdogo anaamua kumkojolea makusudi na mtu huyo asifanye
kitu kwa kuhofia kuonekana ametumia nguvu zake vibaya! Hizo ni nguvu au
utahira?
Nakumbuka
kama miaka mitano iliyopita niliandika katika gazeti hili, Rai, nikiupinga
ubabe wa nchi ya Marekani, makala hiyo niliipa kichwa cha habari “Marekani ni
taifa nyamaume”. Saa chache baada ya gazeti hilo kutoka nikapigiwa simu toka
ubalozi wa Marekani nikiambiwa kwamba balozi wa nchi hiyo hapa nchini anaomba
tuonane.
Yeye balozi
alitaka tukutane popote ambako ningeona panafaa, nikaamua tukutane ofisini
kwake. Tuliongea tukaelewana kabisa. Moja ya mambo tuliyogusia ni kama haya ya
nchi duni kuichokoza nchi yenye maguvu
kwa imani ya kwamba nchi duni ikianza kutandikwa itaanzisha kelele za kwamba
inaonewa.
Balozi
akatoa mfano wa Tanzania kuitandika Uganda, Vita ya Kagera 1978 – 79, mpaka kufikia kumtoa Idd Amin
madarakani. Akauliza, “kwa maana hiyo hata Tanzania tuseme ni taifa nyamaume?”.
Kusema ukweli swali hilo lilinifanya nipate kigugumizi, ila kama yupo ambaye
angeweza kukabiliana na swali hilo tofauti na mimi ningemkaribisha kwenye
mdahalo huu aonyeshe ni namna gani angejieleza.
Machafuko
yanayoendelea kati ya Israel na Palestina yametokana na unyama wa makusudi wa
Wapalestina walipowaua vijana watatu wa Kiyaudi, Naftali Fraenkel, Gilad Shaer
na Eyal Yifrah, bila kosa lolote. Mimi nilikitabiri ambacho kingejiri, ndicho
hiki sasa.
Tatizo ni
kwamba baadhi ya watu hawataki kabisa kukiangalia kiini cha tatizo bali ukuaji
wa tatizo lenyewe. Na ni vigumu kupata tiba ya tatizo usilotaka kujihangaisha
kujua kiini chake au kukikwepa makusudi kiini hicho. Hivyo utaishia kutibu
dalili za tatizo huku tatizo lenyewe likidi kujiimarisha, hiyo ni sawa na kazi
bure.
Kama mataifa
yangekilaani kitendo kiovu na cha kinyama cha Wapalestina kuwaua vijana hao wa
Kiyaudi ambao hawakuwa na kosa lolote, mpaka Israel ikaamini kuwa kimelaaniwa
vya kutosha huku Palestina ikitubu na kuahidi kutoruhusu kitendo cha aina hiyo
kujirudia tena, bilashaka Israel nayo ingechukua maamuzi tofauti na ya sasa.
Lakini kwa
kuona kitendo hicho ni kama kimebarikiwa na jumuiya ya kimataifa, Israel
haikuwa na lingine la kufanya zaidi ya kulipiza kisasi huku ikijihami.
Ikumbukwe anayeingia kwenye ugomvi haangalii pa kupiga ili kuepuka kumuumiza
anayegombana naye, anachotaka aumie basi.
Na katika
sakata hilo ndipo kikaingilia kikundi cha Hamas, chenye kila dalili za ugaidi.
Nasikitishwa
na wanaoilaumu Israel wakiwa wameikwepa historia ama kwa makusudi, kwa
usahaulifu au kwa kutokujua. Wayaudi ni jamii iliyopata misukosuko mikubwa sana
ikiwa inalengwa kuhangamizwa kusudi ipotee kabisa kwenye uso wa dunia.
Kinachoifanya jamii hiyo iendelee kuwepo mpaka sasa nayo ni maajabu mengine ya
dunia!
Wapalestina,
wakiungwa mkono na jamii yote ya Kiarabu, hawautambui uwepo wa taifa la Israel!
Sasa nini kifanyike kama sio Israel kujihami na kushambulia kwa njia ya
kulipiza kisasi pale inapobidi? Na kwa nini inapotokea hivyo walaumiwe wao tu
bila kuwahusisha maasimu wao wanaotaka kuwahangamiza?
Mashambulizi
dhidi ya Israel yanaendeshwa kwa njia za kigaidi; ugaidi naufananisha na
ujambazi. Lakini walau lengo la ujambazi linaeleweka, kupata mali kwa njia
haramu. Sielewi lengo la ugaidi ni nini!
Ugaidi sawa
na ujambazi, unapaswa utokomezwe. Mfano hapa nchini kwetu ujambazi upo, kwahiyo
tukisema tuutokomeze itaeleweka kuwa tunawaonea wanaofanya ujambazi?
Na
inapotokea mzazi ana watoto majambazi, anawatetea kwa kutotaka wakamatwe na
kuchukuliwa hatua wanazozisitahili, pengine kutokana na mzazi kujinufaisha na
ujambazi huo, akikamatwa mzazi mwenyewe ili akaonyeshe waliko watoto wake
majambazi atakuwa anaonewa kweli?
Je,
wanaoutetea ujambazi huku wakijenga majumba na kuyazungushia uzio (fence) sawa
na za magereza, kwa maana ya kujifunga wenyewe kwa kuhofia hujuma za majambazi
tuwaeleweje? Kama unawatetea majambazi ya nini kuwahofia?
Hamas ni
kikundi sawa na Boko Haramu, Al – Shabaab, Al – Qaeda nakadhalika. Hamas wanahifadhiwa
na Palestina, nchi hiyo inaona furaha kikundi hicho kinapoishambulia Israwel
bila kujali kinasababisha maafa kiasi gani katika nchi hiyo. Je, Israel
isijilinde, isijibu mapigo? Na mapigo itayajibu vipi wakati Hamas wako ndani ya
Palestina wakiwatumia watu kama ngao zao?
Nikumbushe
kidogo Vita ya Kagera, 1978 – 79. Maaskari shupavu wa JWTZ walitaka kuiteka
miji ya Uganda bila kuihangamiza, lakini askari wa Amin wakawa wanapandisha
mizinga kwenye maghorofa na kuanza kuwashambulia askari wetu kwa chini! Ndipo
ikabidi JWTZ waanze kuyaporomosha baadhi ya maghorofa kuelekea kupata ushindi.
Sasa
wanaoilaumu Israel wanataka ifanye nini? Wanataka ikae tu ikubali kushambuliwa
na magaidi bila kujitetea kwa vile magaidi hao yamejificha kwenye watu na kuwageuza
ngao?
Kumbuka
ofisi za ubalozi wa Marekani, Dar es salaam na Nairobi, mwishoni mwa miaka ya
1990, zilishambuliwa na magaidi ambao
hawana uhusiano wa mbali na Hamas. Watanzania na Wakenya ndio waliokufa kwa
wingi, leo hii baadhi ya Watanzania wanataka magaidi wasisumbuliwe ili waendeleze
biashara yao ya ugaidi kwa sitarehe!
Mimi sitaki
Wapalestina wasio na hatia wauawe kama ambavyo sitaki Waisrael wasio na hatia
wauawe kwa kushambuliwa bila sababu yoyote. Kwahiyo la kufanya ni kutafuta
kiini cha mashambulizi ya Wapalestina, hasa kikundi cha Hamas, dhidi ya Israel
ni nini. Maana mashambulizi ya Waisrael dhidi ya Wapalestina yanaeleweka sababu
zake, ni kujibu mapigo.
Kinachopaswa
kupingwa na kulaaniwa kwa nguvu zote ni ugaidi pamoja na mataifa yanayoufuga
ugaidi. Tusijifanye tunaihurumia Palestina wakati inao mradi wa kufuga ugaidi
unaotusumbua hata sisi tusiohusika na mizozo yao.
Ni lazima
tuishauri nchi hiyo iachane na mradi huo ili amani ipatikane katika eneo hilo
kusudi roho za watu wasio na hatia zipate kulindwa.
Israel
haiwezi kuwa na nguvu ambazo haitakiwi kuzitumia kujilinda dhidi ya ugaidi. Utakuwa
ni uchizi kuwa na nguvu ambazo huwezi kuzitumia kujihakikishia usalama.
Hapo ndipo
nayaona madai mengine kama kituko, kwamba Hamas inaishambulia Israel kusudi
nchi hiyo inayoshambuliwa ikubali kukaa kwenye meza ya mazungumzo, kichekesho
kweli. Yaani Israel ikubali kukaa meza moja na Hamas kuzungumza kwamba yenyewe
ni taifa ambalo halipo katika ramani ya dunia!
Kitu kingine
ni kuwa madai ya kwamba Hamas ni kikundi kinachotumiwa na Palestina kutetea
maslahi ya Wapalestina hayawezi kuingia akilini hata kidogo. Sababu hata kama
Israel ikiamua kukubaliana na Palestina kwa kila kitu, mpaka kufikia taifa hilo
kujifuta kabisa, haiwezekani huo ukawa ndio mwisho wa Hamas. Lazima itatafutwa
sababu nyingine ya kikundi hicho kuendeleza ugaidi na mauaji ya watu wasio na
hatia.
Hebu
tuitazame Nigeria inavyosumbuliwa na Boko Haramu, Al – Shabaab ilivyoisambaratisha
Somalia na kisha kuigeukia Kenya, ina maana nako huko kuna Israel?
Kwahiyo
Watanzania wanaodai kwamba Tanzania ivunje uhusiano wa kibalozi na taifa hilo
teule, kwa mujibu wa vitabu vitakatifu, inawabidi watafakari kwanza kabla ya
kuendeleza madai yao hayo.
0784 989 512