ADHA YA MICHANGO NA UGUMU WA MAISHA WA KUJITAKIA
Na Prudence Karugendo
NIPO kazini, mfanyakazi
mwenzangu ananiletea kadi ya kuomba mchango wa harusi ya mdogo wake. Papo hapo
nakumbuka kwamba siku hiyo ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha michango kwa ajili
ya sherehe ya kumuaga binti ya jirani yangu (send-off) anayeolewa juma lijalo.
Kwenye mkoba wangu kuna kadi nyingine tano zote zikidai michango kwa ajili ya
sherehe mbalimbali. Naona kuna ya kipa
imara, komunio, “birthday”, ubatizo, na nyingine ni kwa ajili ya “graduation”. Zote hizi zinatoka kwa ndugu, jamaa na
marafiki, ambao kila mmoja, kutokana na
ukaribu tulio nao, ana imani ya kupata mchango wangu usiopungua shilingi elfu
50!
Baada ya kufika nyumbani
nikitokea kazini nakuta mama (mke wangu) ameshika kadi inayomuarifu juu ya
shughuli ya kumfunda binti ya shoga yake (kitchen party). Unatakiwa vilevile
mchango usiopungua shilingi elfu 50 pamoja na doti moja ya khanga kwa ajili ya
sare! Haraka haraka kadi hiyo ananipatia mimi huku akiwa amenikazia macho
yanayoonyesha jinsi shughuli hiyo ilivyo muhimu kwake! Kwa hiyo kadi hiyo nayo
inaongezwa kwenye idadi ya kadi za michango nilizotoka nazo kazini!
Kabla sijakaa sawa rafiki
yangu ananipigia simu kunijulisha uzinduzi wa nyumba yake, anatumia lugha ya
masihara kama tulivyozoeshana, kwamba “nimpige tafu” japo kwa vikosi vitano vya Wanamsimbazi. Maana yake ni kwamba
ananialika kwenye tafrija ya uzinduzi wa nyumba yake pamoja na kuniomba mchango
wa elfu 50. Wekundu wa Msimbazi ni neno linalotumika kumaanisha noti ya shilingi elfu
kumi.
Kesho yake niko kazini napata
barua tatu kwa mpigo, zote kumbe ni kadi za kuomba michango! Kadi ya kwanza ni
ya kanisa. Kanisa la Parokia ya kijijini kwetu linatimiza miaka hamsini toka
lijengwe, kwahiyo wanaparokia popote walipo ulimwenguni wanaombwa kutoa
michango yao kwa ajili ya kulifanyia sherehe ya jubilii ya dhahabu kanisa hilo!
Barua nyingine(kadi) inatoka
kwa mjomba wake mama. Yeye anaomba mchango kwa ajili ya sherehe ya kumkaribisha
nyumbani kwake rafiki yake wa kuchanjia, sherehe inayoitwa kwa Kihaya “okutaya
omukago”. Anaomba tusimtupe mkono sababu anadumisha mila. Barua(kadi) ya tatu,
ambayo ndiyo kiboko ya zote, inatoka kwa Baba mkubwa. Anasema anatimiza miaka
tisini ya kuzaliwa, kwahiyo anataka kila mtoto amchangie elfu themanini na
zawadi juu, anatishia kumwaga radhi kwa yeyote atakaye kaidi maelekezo yake!
Haya ndiyo maisha ya kawaida
ya siku hizi. Michango michango kila kukicha. Michango ambayo inaendeshwa kwa
mtindo wa mashindano bila ya wachangishaji kuzingatia ugumu wa kipato
unaoikabili jamii yetu wala kufikiria jinsi ambavyo michango hiyo inavyoweza
kutumiwa katika mambo ya maendeleo zaidi ya kuonyeshana ufahari wa muda.
Jambo la kushangaza ni kwamba
jamii yetu imeukubali mtindo huu wa maisha, ambapo sasa kiwango cha chini cha kuchangia
kimepandishwa mpaka sh. 100,000 bila kujali kipato kimepanda kwa kiasi gani!
Ingetokea mtu akaitisha mchango
kwa ajili ya kumpeleka mtoto wake kidato cha kwanza lazima maneno ya kejeli yangejitokeza….mtu
huyu kama hana hela ya kumpeleka mtoto wake shule si bora amuache akauze
madafu, kila mtu anayo majukumu yake, basi ilmradi maneno ya kukatisha tamaa
ili pasitokee watu, katika jamii tuliyomo,
wenye mawazo ya kuwashirikisha wenzao
kufanya mambo yenye faida endelevu.
Wanajamii hawako tayari
kumchangia mtoto wa mwenzao ili aende shule kwa sababu wanaamini faida ya
kufanya hivyo wanaijua wazazi wa mtoto husika peke yao. Lakini mtoto huyo huyo
angekuwa anaoa na watu wale wale wakapelekewa kadi za kuombea michango ya
harusi wako tayari kuchanga kwa moyo mkunjufu! Hiyo ni pamoja na kuelewa mtindo
wa ndoa za ziku hizi ambazo nyingi hazidumu kwa zaidi ya mwezi mmoja!
Ni wazi kwamba watu
hawachangii ili kumwezesha kijana wa jamaa yao apate jiko, sababu kwa kijana
huyo kupata jiko ni sawa na ambavyo angepata elimu, vyote viwili havionyeshi
kurudisha faida ya moja kwa moja kwa wachangiaji, ila kinachoangaliwa ni namna
mchangiaji atakavyo nufaika na mchango anaoutoa. Mtu anayechangia harusi
anategemea kualikwa siku yasiku, na hii maana yake ni kula kunywa na
kuserebuka.
Wakati anayejitosa kuchangia
elimu ni kama anaona ametupa pesa yake kwa vile hajui ni lini itatokea naye aalikwe kuserebukia
mafanikio ya elimu aliyoichangia.
Kukosekana kwa fikira za
kubuni, kupanga na kufanya mambo yenye manufaa endelevu ni tatizo kubwa
linalochangia ukomavu wa ufukara katika jamii yetu. Pamoja na hilo, kitendo cha
watu, kwenye jamii yetu, kupendelea kuonyeshana ufahari hata kwa wale wasio na
uwezo endelevu wa kuhimili ufahari huo ni tatizo lingine. Na ni tatizo hili
linalosababisha mfumuko wa michango ninayoiongelea hapa. Michango ambayo, kwa
vile faida yake ni vigumu kuonekana, sioni sababu ya watu kuendelea
kuchangiana.
Moja ya makabila yaliyokuwa
na dira ya maendeleo toka zama za wahenga hapa nchini ni kabila la Wahaya.
Wahaya walifanikiwa kupata maendeleo kutokana na, pamoja na mambo mengine, kuwa na malengo
mazuri katika kukabiliana na kila kilichoonekana kuwa kikwazo katika njia yao
ya kutafuta maendeleo. Walifanikiwa kufanya mambo kadhaa yaliyoonekana kuwa
msingi thabiti wa maendeleo yakiongozwa na elimu kiasi cha makabila mengine
kuwabatiza jina la utani la “Nshomile”. Maana ya nshomile ni nimeelimika.
Siri moja ya mafanikio ya
Wahaya kimaendeleo ilikuwa ni kushirikishana kwa lengo la kutafuta maendeleo
hayo. Mfano, kijana alipokuwa anakaribia kuoa alikuwa anawaomba mchango vijana
wenzake. Mchango wenyewe ulikuwa ni kumsaidia kijana mwenzao kutafuta miti,
fito na nyasi kwa ajili ya kujengea na kuezekea ili siku ya kuoa awe amepata kibanda chake. Hili ni jambo lililo
katika mtizamo wa maendeleo. Wazazi wa kijana kwa upande wao, siku ya kuoa
kijana wao ilipokuwa inakaribia, walikuwa wakipita kwa wazee wenzao wakiomba
ndizi kwa ajili ya chakula cha sherehe ya harusi na ndizi kali kwa ajili ya
kutengenezea pombe(olubisi) ya harusi. Michango hiyo inajulikana kwa Kihaya
kama “omutwelo gw’ekitoke n’enkundi”, basi kijana anaoa mambo yanaendelea.
Siku hizi mambo yamebadilika.
Wahaya nao, kama jamii nyingine, wameathiriwa na hali hii ya sasa, inayojieleza
kuwa ndiyo maendeleo ya wakati tulio nao. Hali ya kufanya mambo bila malengo ya
baadaye, ilmradi kufurahisha watu na kutafuta sifa ya wakati huo tu! Kwa maana
hiyo hutamsikia mtu, hata huku mjini, anakwambia kwamba anaomba ndizi kali kijana
wake anaoa, ilhali akijua kwamba mashamba ya ndizi kali tumeyaacha Bukoba!
Kumbe maana yake anaomba mchango wa hela kiujanja ili atimize malengo yake ya
kutangaza ufahari!
Hata wale walio kijijini
wanaposema ndizi na ndizi kali siku hizi wanakuwa wanamaanisha mchango wa pesa.
Mtu atakushangaa akija kwako kuomba ndizi na ndizi kali kwa ajili ya sherehe halafu wewe humuongoze kwenda shambani
kumuonyesha mikungu ya ndizi na ndizi kali yenye thamani isiyozidi sh. 20, 000,
wakati kichwani mwake alikuwa amepiga
mahesabu ya kupata mchango wa sh. 100,000!
Hii inadhihirisha kwamba kinachotiliwa
maanani siku hizi ni kiwango cha ufahari wa harusi bila kujali hao wanaooana
wataishi maisha ya kiwango gani, hata kama ni kuoana leo na kesho yake
wakaachana hiyo wazazi haiwahusu. Wao wanachojali ni kulinda heshima yao kwa
kumfanyia mtoto wao harusi ya kifahari. Na kibaya zaidi hawategemei ufahari huo
utoke mifukoni mwao, bali mifukoni mwa wenzao!
Kipindi fulani jirani zetu
Kenya walikuwa wanaonekana wako mbele yetu kimaendeleo. Kielimu walikuwa mbele
yetu, kiafya walikuwa mbele yetu, miundombinu yao ilikuwa imeboreshwa kuliko
yetu. Hakuna miujiza yoyote tunayoweza kudai kwamba walikuwa nayo hawa jirani
zetu iliyokuwa ikiwafanya wawe mbele yetu kwa karibu kila kitu.
Kitu pekee walichokuwa nacho
ni ule moyo wa kutaka maendeleo. Kwa kuzingatia hali ya ufukara waliyokuwa
nayo, ufukara ambao kiwango chake hakikupishana na kiwango cha ufukara wetu,
waliamua kuikumbatia sawa sawa kaulimbiu iliyoanzishwa na Babawa Taifa lao, Mzee Jommo Kenyatta, “harambee twende pamoja.”
Ni kaulimbiu iliyokuwa ikiwatia hamasa ya kuunganisha nguvu zao ili kuyakabili
mambo yaliyokuwa yanaonyesha kwamba vinginevyo yangewazidi nguvu katika
harakati zao za kusaka maendeleo.
Kwa mtindo wa harambee
waliweza kujenga mashule, mahospitali, barabara n.k. Pia waliweza kusomesha watoto
wao kwa mtindo uleule wa harambee mpaka kufikia vyuo vikuu na wakati mwingine
kuwapeleka baadhi ya vijana wao kusomea
ng’ambo. Wenzetu kule ni kawaida yao kuitisha mikutano ya harambee, na mtu
akishapewa habari ya mkutano wa harambee moja kwa moja anakuwa ameishaelewa
kuwa anaenda kushirikishwa katika jambo la maendeleo.
Tofauti na kwa wenzetu, huku
kwetu mtu akiitiwa kikao kitu cha kwanza atakachokifikiria ni sherehe! Na kwa
vile sio kawaida watu kulipa michango katika kikao cha kwanza, mara nyingi kikao cha kwanza kinapata watu wengi. Sababu
ya watu kuwa wengi katika kikao cha kwanza ni kwamba watu wanakuwa wanaelewa mtayarishaji wa kikao hicho, haikosekani atakuwa ameandaa vitu vya kuwatia
hamasa wanakikao, ili waweze kutoa ahadi
za michango iliyonona. Kwa hiyo atakuwa ameandaa vivywaji pamoja na vitafunwa.
Wanakikao wakishafika na
kuelezwa matilaba ya kikao pamoja na kuhudumiwa kwa vinywaji na vyote
vilivyoandaliwa, huwa hakuna anayeona tatizo la kutoa ahadi anayoona mdomo wake
unaweza kuitamka. Kutamka ahadi siyo tatizo, mbinde ipo katika kulipa ahadi
hiyo. Kawaida baada ya kikao, siku hizi, kuna kitu kinachoitwa “kichefuchefu”
yaani kuchangia vinywaji kwa ajili ya kikao kinachofuatia. Hapo ndipo watu huanza
kuteleza kwa kujifanya wengine wanaenda chooni kumbe ndiyo moja kwa moja wakiuwahi
mzunguko wa bakuli la kichefuchefu kabla haujawafikia! Wale wanaokosa nafasi ya
kuteleza bahati mbaya wakabambwa na bakuli la kichefuchefu, huku wakijua kwamba
wameishatoa ahadi zinazolingana na uwezo wao wa kutamka, siyo uwezo wa kulipa,
hutawasikia wakisema, tena kwa kujiamini, kuwa kwa leo hela sina ila naahidi
sanduku moja la bia kwa kikao kijacho, mwingine ataahidi sanduku mbili za soda,
kumbe watu hao tayari wamejifukuza, ndio
hawaonekani tena katika vikao hivyo!
Kama nilivyosema hapo juu
vikao na michango ya aina hii ni kwa ajili ya kufanikisha umaarufu wa kuonyesha
ufahari wa muda tu.
Haitokei vikao hivi vikawa
kwa ajili ya kupanga kitu cha maendeleo endelevu. Mathalani, katika baadhi ya sehemu hapa nchini, utakuta mtu anao vijana kama wanne wote wakiwa
hawana la kufanya, wawili wakitishiwa na janga la uvutaji wa bangi na
kutumbukia kwenye magenge ya vibaka wakati wawili waliobaki wananyemelewa na umalaya
wa reja reja (uchangudoa). Ukimuuliza kwanini vijana hao hakuwatafutia angalau vyuo
vya ufundi ambavyo vingeweza kumgharimu kama shilingi milioni mbili kwa wote wanne,
jibu unakuta liko tayari. Pesa sina, ninayo akiba yangu shilingi laki tatu
ambayo nataka nijazie kutoka kwa watakaonichangia ili zifikie japo milioni
tano, mwisho wa mwezi nataka niwacheze ngoma mabinti zangu wawili. Halafu atasisitiza
kwa kutamba, unajua si mchezo kuwatoa wali wawili kwa pamoja, nataka wanitambue
mtaa huu mimi ni nani!
Wakati mwingine mtu anatishiwa
na mauti kwa kukosa shilingi laki moja tu za kulipa hospitali ili akapasuliwe
busha! Lakini mtu huyo huyo mwezi uliopita alichangiwa hadi shilingi milioni 7
wakati anamtoa mwali!
Kama hatukujitahidi
kubadilisha mtindo huu wa maisha ieleweke kwamba tunajimaliza sisi wenyewe.
Tuchangie kwa kipimo, kwa maana ya kujali tunachokichangia tukiwa
tumelinganisha na kipato tunachokipata, vinginevyo ugumu wa maisha unaojitokeza
tunaulazimisha sisi wenyewe.
0784 989 512