KATI YA KOMBA NA MBOWE NANI ALIPASWA KUHOJIWA NA POLISI?
NA PRUDENCE KARUGENDO
UKIUKAJI wa haki za binadamu tuliokuwa tukiusikia kwa
wenzetu, hususan nchini Afrika Kusini
enzi za makaburu, kuikandamiza haki ya walio wengi kwa manufaa ya wachache,
sasa tunaushuhudia wenyewe hapa nchini kwetu!
Vitendo vya kutumia mabavu ya dola kupita
kiasi, kuwasakama na kuwakandamiza walio msitari wa mbele kutetea haki ya umma,
kuwasambaratisha wananchi wanaowaunga mkono watetezi wao bila kujali kwamba
wananchi hao hawana silaha yoyote ya kujihami,
au kama ni watoto, wazee, walemavu nakadhalika, ndiyo yanayojionyesha
hapa kwetu kwa sasa!
Ikumbukwe
enzi hizo za makaburu Tanzania ilikuwa msitari wa mbele kuyapinga na kuyalaani
matendo hayo ya kinyama yaliyokuwa yanafanywa na makaburu dhidi ya wananchi wa
Afrika Kusini. Sijui kwa sasa ambapo ukatili huo dhidi ya wananchi wapenda haki
umehamia Tanzania nani atakuwa msitari
wa mbele kuupinga na kuulaani, pengine Afrika Kusini yenyewe!
Inapofikia
mahali mwenye kuahidi uovu wa hatari akaonekana shujaa, lakini mwenye kuuliza
kwa nini uovu uahidiwe akaonekana mhalifu na kuitwa akahojiwe na Polisi,
tunawezaje kuitofautisha nchi yetu na Afrika Kusini enzi za makaburu?
Isipokuwa
kuna tofauti kidogo inavyoonyesha unafuu kwa vyombo vya dola vya makaburu.
Pamoja na vyombo vya dola vya Tanzania kujitahidi kuiga staili ya ukandamizaji
wa makaburu lakini kuna mahali vinaonekana kuzidisha ukatili ambao makaburu
hawakuwahi kuufanya.
Mfano, kuua na kujeruhi wanahabari ni matukio ya
kinyama ambayo hayakuwahi kufanywa na makaburu. Na kibaya zaidi hapa kwetu
wanaosimamia unyama huo wanapandishwa vyeo kama motisha wa kazi hiyo ya kinyama
wanayokuwa wameisimamia! Mfano mmojawapo ni wa aliyekuwa RPC wa Iringa, Michael
Kamuhanda, aliyepandishwa cheo toka SACP
na kuwa DCP baada ya kusimamia na kufanikisha mauaji ya mwanahabari, Daudi
Mwangosi, kule Nyololo, Iringa.
Hebu
tuangalie yanayojaribu kufanana. Chama cha ANC, Afrika Kusini, kilichokuwa
kikiungwa mkono na wananchi wazalendo walio wengi, kiliwatia makaburu tumbo
joto na kuwafanya waanze kukitabiria kila lililokuwa baya. Lakini haikusaidia
kitu sababu utabiri haukutimia mpaka makaburu walipolazimika kukipiga marufuku
nchini mle.
Hapa kwetu
kila chama cha upinzani kinachochomoza na kukikaba vizuri chama tawala
kinasakamwa kwa aina mbalimbali na chama tawala na kuhakikisha nguvu za chama
hicho pinzani zinapotea. Hiyo yote imekuwa tofauti kwa Chadema.
Pamoja na
makada mbalimbali wa CCM kutabiri kwamba mwisho wa Chadema ni 2014, sasa ni
mwezi wa 9 na Chadema ndio kwanza inaonyesha kuimarika kuliko muda wote
uliopita, hasa baada kumalizika mkutano wake mkuu wa majuzi ambao mafanikio
yake hayajawahi kuonyeshwa na mkutano wa chama chochote kingine cha upinzani
toka mfumo wa vyama vingi urudishwe nchini.
Hata makamu
wa mwenyekiti wa CCM, Philph Mangula,
amekiri kuwa kuna mambo amejifunza kwenye mkutano huo wa Chadema wakati akitoa
salaamu kwa wajumbe wa mkutano huo.
Kutokana na
mkutano huo kudhihirisha utabiri feki wa makada wa CCM, ni wazi kuwa CCM
hawakuufurahia au kuyafurahia mafanikio hayo ya Chadema. Hivyo zikaanza
kufanyika mbinu nyingine za kukisakama chama hicho katika jitihada za kutaka
kukidhoofisha, mbinu zinazosukumwa na woga wa mabadiliko walio nao makada wa
chama tawala.
Mara nyingi
woga wa mabadiliko ya kisiasa katika
nchi nyingi unaletwa hasa na mambo mawili. Moja ni ubinafsi na pili ni uovu
dhidi ya umma. Haijawahi kutokea woga wa aina hiyo ukatokana na uzalendo kwa
nchi.
Yeyote aliye
mzalendo atakuwa anafanya mema kwa nchi yake na kwa wananchi wenzake. Mzalendo
wa aina hiyo hawezi kuyahofia mabadiliko
ya kisiasa nchini mwake hata kidogo. Sababu hana deni lolote kwa nchi yake wala
kwa wananchi wenzake.
Mfano mzuri
kwa hilo uko katika nchi zilizoendelea kama Marekani, Wingereza na nchi
nyingine nyingi za Magharibi. Hata katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Mbali
zikiongozwa na nchi za India na Japan. Katika nchi hizo vyama vya siasa vyenye
itikadi tofauti vinabadilishana uongozi wa nchi bila woga wowote, ni kwa sababu
vinajiamini kuwa havina madeni ya uovu vinaoufanya vikiwa madarakani.
Katika
siasa, hasa za bara la Afrika, kuna aina mbili ya wanasiasa. Wapo wanaofanya
siasa kiuzalendo na wengine wakifanya siasa kama shughuli yao binafsi,
wabinafsi. Aina hiyo ya pili ndiyo inayozalisha mafisadi, na ndiyo yenye
kuhofia mabadiliko. Wanasiasa wote wa aina hizo mbili tunawatambua kwa matendo
yao.
Mfano, mwaka
2005, aliposhinda Kikwete na kutangazwa rais wa Tanzania kwa kipindi cha miaka
5 ya mwanzo aliyekwenda wa kwanza kumpongeza kwa kumkumbatia alikuwa ni
mpinzani wake katika uchaguzi huo, Freeman Mbowe. Kilichoonekana ni kwamba
Mbowe hakuwa na kinyongo cha kuukosa urais sababu alichokuwa anawania
kilitokana na msukumo wa uzalendo na sio ubinafsi. Sababu wapo walioonyesha
moyo wa ubinafsi kwa kutoenda kwenye sherehe za kumtangaza rais mwaka huo.
Rais Kikwete
naye kwa moyo wake wa uzalendo, wakati
anamalizia muda wake wa uongozi wa nchi, akakubaliana na upinzani kuiachia nchi
Katiba Mpya. Ni uamuzi wa kiuzalendo. Lakini baadhi ya watu waliomzunguka
wakiutanguliza ubinafsi katika chama chake, CCM, wakamlaumu kwa uamuzi wake huo,
wengine wakidai kwamba suala hilo
halikuwa kwenye Ilani ya chama chao!
Mpaka
wengine wamefikia hatua ya kumtukana rais kiaina wakijidai wanamtukana Jaji
Warioba ilhali wakielewa kwamba Warioba alikuwa akifanya kazi aliyopewa na Rais
Kikwete kuifanya kwa niaba yake kama msaidizi tena chini ya kiapo.
Ndiyo maana
watu hao wabinafsi na watovu wa uzalendo wamediriki kuuchakachua uzalendo wa Kikwete
kwa nchi yake kwa kuyabadilisha maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka
kusudi ibaki vilevile kama ilivyokuwa
mwanzo, tena bila kuzingatia wala kujali gharama kubwa iliyokwisha kutumika mpaka
kufikia hapo.
Watu hao
hawawezi kuijali gharama sababu hawana uzalendo unaowatuma kufanya hivyo.
Kilichopo ni ubinafsi tu basi.
Baada ya
mambo kuwa hivyo ndipo likajitokeza kundi la wazalendo na kujiita Umoja wa
Katiba ya Wananchi, UKAWA. Kundi hilo linapinga juhudi zote zinazofanywa na
walioukosa uzalendo na kuutanguliza ubinafsi.
Kwahiyo
Ukawa kwa kuliona kundi la wabinafsi limeng’ang’ania kuendelea na mchakato
ambao hata aliyeuanzisha, Rais Kikwete, kaishakata tamaa kuwa hauwezi kuzalisha
kile alichokikusudia kwa wakati huu, likaamua kuususa mchakato huo.
Ndipo
Chadema, kupitia kwenye mkutano wake mkuu, likatolewa tamko la kuwataka
wananchi kuupinga ubadhirifu wa kutumbua bure pesa za walipakodi unaofanywa na
wabinafsi hao pasipo lolote linalotegemewa kupatikana.
Kinachodhihirisha
ubinafsi huo ni kwamba hata baadhi ya wale waliogoma kushuhudia Kikwete
anatangazwa kuwa rais kwa mara ya kwanza, kutokana na hasira za wao kuukosa
urais, leo hii nao wamo wakijifanya kukiendeleza kitu alichokianzisha Kikwete
lakini akiwa hana imani tena kama kinaweza kufanikiwa! Kama huo sio ubinafsi ni
kitu gani?
Tamko la
kuupinga ubinafsi na ubadhirifu huo lililotolewa na mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe, linaonekana lilivyovaliwa njuga na mamlaka za juu za nchi
likidaiwa ni la uchochezi. Mwenyekiti huyo ameitwa na kuhojiwa Polisi juu ya
tamko hilo.
Nashindwa
kupata uwiano kati ya tamko hilo la kuupinga ubadhirifu dhidi ya pesa ya
walipakodi na tamko lililotolewa Bungeni na kada wa CCM, John Komba, la kutaka
kuanzisha vita ya msituni iwapo matakwa yake hayatafanikiwa! Lakini Polisi
haikuchukua hatua yoyote dhidi ya kauli hiyo ya kigaidi!
Badala yake
Polisi inahangaika na kauli ya Mbowe ya kuwataka wananchi waandamane ili
kutetea pesa yao inayoteketezwa na wabinafsi wasiowajali wananchi wenzao!
Kumbuka
wagonjwa wengine wanakata roho kwa kukosa madawa, kisa hakuna pesa, wanafunzi
wa elimu ya juu wanakosa kuendelea na masomo yao kisa hakuna pesa ya mkopo,
walimu wanakosa vitendea kazi kwa kisingizio hichohicho. Wafanyakazi wa kima
chini bado kipato chao kwa mwezi hakilingani na pesa inayofujwa kwa siku na mtu
mmoja kule Dodoma nakadhalika.
Hata kama
Katiba ingepatikana kweli, ina maana kuishughulikia kunawafanya wahusika wawe
viumbe tofauti na Watanzania waliobaki kiasi cha kuwaachia wakatumbue pesa yote
hiyo bila kuyajali niliyoyataja hapo juu?
Ni Mtanzania
gani asiyeuona ubadhirifu huo? Hasa inaposemwa kwamba Katiba Mpya haiwezi
kupatikana kwa kipindi hiki, lakini baadhi ya wananchi waliokosa uzalendo wakang’ang’ania
kuendelea na zoezi hilo la kuikamua nchi yao bila huruma yoyote?
Kwahiyo
tamko la maandamano ya amani kuupinga ufujaji huo linaonekana linahatarisha
amani na usalama wa nchi. Lakini lililotolewa na mbinafsi Komba, la kwenda
msituni kuanzisha vita, kwa wahusika hilo halitishii chochote kwa usalama wa
nchi!
Kwenda
msituni ni kuua utulivu na usalama wa nchi, ni kuua wananchi, kuua uchumi wa
nchi na kuiua nchi yenyewe kwa ujumla. Lakini aliyetoa tishio hilo mpaka sasa
anaonekana ni jasiri na shujaa!
Wakati kauli
ya Komba inaonekana ni hatari kwa nchi na wananchi, kauli ya Mbowe ni hatari
kwa ubadhirifu na ufisadi unaoendelea kuiteketeza nchi yetu.
Kitu kingine
ni kwamba kauli ya Mbowe inalenga kulilinda kusudio la Rais Kikwete la
kujiandikia historia pekee ya kuiachia nchi Katiba mpya na iliyo bora, kusudio
ambalo baadhi ya wabinafsi hawalipendi na kuamua kulitengua.
Sasa kati ya
Mbowe na Komba nani mbaya na nani adui kwa nchi yetu? Nani alipaswa ahojiwe na
Polisi kama kweli hekima inatamalaki?
0784 989 512