MOYO WA MBOWE UNAPASWA UPONGEZWE NA KUIGWA
NA PRUDENCE KARUGENDO
UCHAGUZI
unaoendelea ndani ya Chadema ni mfano wa kuigwa katika medani ya kisiasa. Ni wa
kuigwa katika mambo kadhaa kama nitakavyoeleza hapa chini.
Kituko ni
kwamba wakati uchaguzi huo ndani ya Chadema ukiendelea yameanza kujitokeza
malalamiko na manung’uniko toka kwa watu walio nje ya chama hicho, ambao sio
wanachama, ya kwamba baadhi ya viongozi, hususan wa ngazi ya kitaifa, wamekaa
sana katika nafasi zao walizonazo ndani ya chama!
Wakati
nikiwa nimeduwazwa na malalamiko hayo, nikijiuliza watu hao wanawashwaje na
pilipili wasiyoila, rafiki yangu aliye kada wa chama tawala, CCM, akaniambaia
kwamba atashangaa sana ikiwa Chadema itamchagua tena Freeman Mbowe kuendelea
kuwa mwenyekiti wake! Madai yake ni kwamba Mbowe kakaa sana kwenye nafasi hiyo.
Kwa vile
madai ya aina hiyo yanatolewa na watu wenye akili timamu, hata kama wako nje ya
chama, nimeona kuna hatari maneno yao hayo yakawaingia na kuwapotosha hata
walio ndani ya chama wakidhani yana ukweli wa aina fulani, na hivyo kuwayumbisha kimtazamo. Ndiyo maana
leo nikaona suala hilo linafaa kuwa mjadala katika makala haya.
Nilimwambia
rafiki yangu huyo, ambaye sina hakika kama anaelewa chama chake CCM
kilikoanzia, kwamba Chadema ni chama ambacho bado kinajengwa tofauti na CCM
ambacho waliomo ni kama wapangaji tu wanaofurahia muundo wa nyumba wakati
wajenzi wake wachache waliobaki wakisimangwa.
Katika CCM
mara nyingi tumeshuhudia kebehi za aina mbalimbali kwa wale ambao tunaweza
kuwaita wajenzi wa chama hicho, maneno kama wazee hawafai, huu ni wakati wa
vijana, hawana lolote hao wanasubiri kufa tu nakadhalika, yanadhihirisha kwamba
wapangaji hawana shida tena na wajenzi.
Ni muhimu
kuelewa kwamba chama cha siasa kinajengwa na watu wenye moyo uliojaa dhamira ya
kweli, watu walio tayari kuterekeza mali na hata vipato pamoja na kila kitu
kilicho kwenye miliki zao kwa faida ya chama. Hao hawafanani kabisa na watu
wanaotafuta kupanga ndani ya chama kilichojengwa tayari.
Mfano mzuri
wa hapa nchini ni wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Aliongoza ujenzi wa TANU
na baadaye CCM. Wakati wa kuanzishwa kwa TANU Mwalimu aliamua kuacha kazi yake
nzuri na ya heshima sana enzi hizo, aliyoisomea kwa karibu miaka 7, Kampala na Edinburgh,
kwa ajili ya ujenzi wa chama hicho.
Baada ya
hapo Nyerere alikaa kwenye usukani kwa karibu miaka 37 bila manung’uniko yoyote
toka kwa yeyote. Aliporidhika kwamba chama chake kipo kwenye mwendo salama,
kutokana na kuizoea safari, ndipo akamuachia usukani mtu mwingine.
Sasa ni
chama gani kingine katika Tanzania ambacho kimeongozwa na mtu mmoja kwa muda
kama huo? Wanaosema kwamba Mbowe kakaa sana kwenye ukuu wa chama wanalijua hilo?
Pamoja na
uchanga wake, Chadema kinaye mwenyekiti wa tatu tangia kianzishwe, karibu sawa
na CCM chenye mwenyekiti wa nne tangia kianzishwe zaidi ya miaka 60 iliyopita.
Chadema kwa miaka 22 kinao wenyeviti 3, CCM kwa miaka 60 kinao wenyeviti 4!
Lakini hata
hivyo, mafanikio aliyokipatia Nyerere chama hicho mpaka alipong’atuka ndiyo
yanayokifanya CCM kitambe kwa sasa, pamoja na mengine mengi kuachwa au
kubomolewa na wanaopanga katika chama hicho kwa wakati huu. Ndipo tuelewe
kwamba mpangaji na mjenzi wana thamani tofauti katika jengo lolote liwalo.
Hebu
tuigeukie Chadema. Mafanikio ya Mbowe katika chama hicho yanalinganishwa au
kufananishwa na yapi yaliyowahi kutokea
tangu kianzishwe? Na kama hayapo, hivyo anayesema kwamba mwenyekiti huyo
amekaa sana kwenye nafasi hiyo tunawezaje kusema kwamba anakitakia mema chama
hicho wakati chenyewe bado kinayaona hayo mafanikio kama mwanzo wa safari yake?
Hiyo maana
yake ni kwamba anayemchoka Mbowe kwa sasa ni kama ameyachoka mafanikio ambayo
chama anachokiongoza kinaendelea kuyapata. Inawezekanaje mtu wa aina hiyo
tukamuona mwema kwa chama hicho?
Ikumbukwe
kwamba Mbowe kaamua kuachia shughuli zake zote na kujikita katika kukijenga
chama, tangu mwanzo sijaona dalili zozote kwamba alitaka chama ndicho kimjenge
yeye badala yake. Ni watu wachache wenye maamuzi magumu ya kiasi hicho.
Namkumbuka
Mzee Mandela alipoamua kuachana na mkewe wa kwanza, Evelyn, kwa ajili ya ANC.
Sio wengi wenye ujasiri huo.
Hivyo
anayedai kuwa mwenyekiti huyo, Mbowe “Sauti ya Radi”, amekaa sana kwenye
uongozi wa Chadema halijui alisemalo kwa vile ni wazi anakuwa ametumwa na
maasimu kufanya hivyo.
Hata hivyo
wanaokuwa wamemtuma mtu wa aina hiyo wanakijua walichokilenga, sababu wao
wanayaelewa mafanikio ya mwenyekiti huyo aliyokipatia chama chake. Ni kwamba
hawayataki kwa vile yanawatia kiwewe. Inasemwa kwamba adui muombee njaa.
Mwenyekiti
huyo wa Chadema anapaswa atofautishwe na wale wanaoingia kwenye chama wakiwa
hawana chochote, hawana umaarufu wala mali, wakitegemea kuvipata ndani ya
chama. Wengine baada ya kuvipata wanavitumia kama mtaji wa kukisaliti chama.
Ndipo wanayafikiria mapinduzi kwa kutumiwa na maasimu wa chama ili
kukiyumbisha.
La
kuzingatia ni kwamba Mbowe hakuingia Chadema ili kutafuta umaarufu wala mali.
Mimi binafsi nilimjua Mbowe, achilia mbali baba yake mzazi aliyekuwa mmoja wa
wafadhili wa harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu, wakati hajawa na mpango
wa siasa, umaarufu alikuwa nao tayari. Kwahiyo hatuwezi kusema siasa ndiyo
imembeba na kufanya ajulikane ikiwa imempa umaarufu alio nao kwa sasa.
Kwa upande
mwingine ipo mifano mingi ya watu wanaohangaika huku na huko wakitafuta
umaarufu na pengine mali. Mfano tumewaona vijana waliokuwa wameivamia Chadema,
na bila kujua chama hicho kikawapatia umaarufu wa uhakika. Baada ya lengo lao
kutimia vijana hao wakautumia umaarufu huo kuanzisha vurugu ndani yake, lakini
wakaenguliwa. Kwa vile mtaji wa umaarufu tayari walikuwa nao wakautumia
kuanzisha chama kingine cha siasa, ni haki yao.
Ila kwa
vyovyote vile chama hicho kipya kitabaki kuwa zao la Chadema kama ilivyo CCM
kwa vyama vya TANU na ASP. Hakiwezi kufanya lolote zuri pasipo kupongezwa
Chadema kwanza, hata kama kuanzishwa kwake zilikuwa ni njama za kuidhoofisha
Chadema.
Vilevile
tulimshuhudia mwanasiasa mmoja, mkongwe, aliyeanzia chama tawala kama mpangaji
lakini, sababu chama chake kilipomwelekeza afuate utaratibu fulani kikiamini ni
mzalendo ndani yake, yeye akaamua kuuvua kabisa uanachama na kujaribu
“ubangaizaji” katika upinzani. Lakini kutokana na kukosa uzalendo mtu huyo
akalazimika kuvizunguka karibu vyama vyote vya upinzani akitafuta pa kujibanza
kupata maslahi binafsi.
Ndipo
baadaye, baada ya kuhakikisha ametaabika vya kutosha, chama tawala kikamshika
mkono na kumrudisha kwake. Sasa mtu huyo anaapa kuubomoa upinzani bila kujali
hifadhi uliyompatia kutokana na tabia yake ya kukosa uzalendo.
Nani anaweza
kusema mtu huyo ana nia thabiti ya ujenzi na uimarishaji wa mahali alipo kwa
sasa hata kama yeye anafanya kila hila ili umma uamini hivyo? Sababu
anayoyasema kwa upinzani kwa sasa ndiyo yaleyale, au zaidi, aliyoyasema kwa CCM
pale alipohamia kwenye upinzani akiiona CCM haifai.
Lazima yeye
atabaki ni mpangaji tu mwenye kuhamia kwingine kila anapoona nyumba aliyomo
imeanza kuyumba. Hana dalili zozote za ujenzi wala ukarabati wa mahali alipo.
Kwa upande
wa Chadema wapo watu, hasa vijana, wenye dhamira ya kweli ya ujenzi na
uimarishaji wa chama hicho. Uzalendo wao ndani ya chama hicho siutilii shaka
hata kidogo kulingana na unavyojionyesha, hauna madoa.
Kwa hapa
nitoe mfano wa kijana mmoja, Kamanda Baraka Leonard Mfilinge, mwenyeji wa
Ilula, Iringa. Kijana huyo ana moyo wa aina yake kiitikadi na katika ujenzi wa
Chadema. Ni mzalendo wa kweli kiitikadi.
Tulipofahamiana
ndipo alipokuwa amemaliza kidato cha 6. Mapenzi yake kwa Chadema yamemfanya
aachane na elimu ya Chuo Kikuu kwanza, alikatisha masomo chuoni na kurudi
kufanya kazi za kujitolea akipita maeneo mbalimbali, hasa ya vijijini kule kwao
Iringa, akiinadi Chadema kwa vijana na wazee. Hiyo ni kazi aliyoanza kuifanya
akiwa hajulikani kwa ngazi yoyote kichama.
Mara nyingi
amefanya hivyo akitembea kwa miguu na mara nyingine akishinda njaa kutokana na
kutokuwa na kipato chochote.
Kusema
ukweli anayoyafanya Baraka Mfilinge kwa Chadema nashindwa kuyatofautisha na
aliyoyafanya Mwalimu Nyerere kwa TANU baada ya kuacha kazi ya uwalimu St.
Francis College (Pugu).
Harakati za
Baraka kuitumikia Chadema zimemfikisha mpaka ngazi ya kitaifa ambako ameshiriki
katika chaguzi mbalimbali kama uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Sombetini –
Arusha, Kiborolonyi – Moshi, Kiomoni – Tanga, Bagamoyo, Ng’ang’ange, Ukumbi,
Ibumu, Kalenga na Chalinze.
Kwa sasa
Baraka kachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA),
mkoa wa Iringa. Na sasa kagombea nafasi ya Uratibu na Uhamasishaji wa Vijana
kitaifa.
Kama kweli
tumedhamiria upinzani wa kweli katika siasa za Tanzania ningewaomba wana
Chadema wawafikirie watu wa aina ya Baraka Leonard Mfilinge katika ujenzi na
uimarishaji wa chama hicho.
Nimalizie kwa
kusema kwamba isitokee hata mara moja chama cha siasa kikakubali kusikiliza
ushauri na ushawishi toka nje ya chama kinapofanya mambo yake ya ndani, kama
uchaguzi. Hata Msajili wa Vyama vya Siasa nchini hapaswi kufanya hivyo. Yeye
anachotakiwa kukifanya ni kuangalia kama taratibu na kanuni vimefuatwa
kulingana na katiba ya chama iliyopelekwa kwake. Vinginevyo atakuwa anatumiwa
kukiua alichowekwa kukisimamia na kukilinda.
0784 989 512