MSIMAMO WA SITTA NI WA KWAKE AU KAAGIZWA?
Na Prudence Karugendo
NILIDHANI Mheshimiwa Samuel Sitta alipoapa kuwa
mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alifanya hivyo kuleta imani yake kwa
wananchi kuwa ataiongoza shughuli
aliyokabidhiwa akiwa ameilinda, kwa uwezo wake kitaaluma, akiwa amefuata
utaratibu na sheria za sheghuli hiyo zinavyoelekeza, mpaka shughuli yenyewe
itakapokamilika.
Lakini sasa
yanayofanyika chini ya uongozi wake wakati shughuli hiyo ikiendelea yananifanya
nijiulize kwa nini Sitta alikubali kula kiapo! Maana ameamua kukibadili kabisa alichokabidhiwa na kuleta kingine, cha kwake,
tofauti na kiapo chake kinavyomuelekeza, kana kwamba alikabidhiwa shughuli hiyo
iwe mali yake binafsi!
Shuguli hiyo
ninayoisema ni ya kuongoza Bunge Maalumu la Katiba. Bunge hilo limeundwa kwa ajili
ya kuandika Katiba ya nchi, baada ya
kuyapitia na kuyajadili maoni ya wananchi yanayotaka Katiba yao iwe na
mwonekano wa namna gani, yaliyomo kwenye
rasimu iliyokabidhiwa kwa Bunge hilo linaloongozwa na Sitta.
Hicho ndicho
kitu ambacho Sitta na wajumbe wa Bunge hilo waliapa kukifanya wakiwa
wameyaheshimu matakwa ya wananchi.
Lakini sasa,
badala yake, Sitta anaonekana kuliongoza Bunge hilo kufanya kitu kilicho nje
kabisa ya kiapo chake! Mbali ya kuridhia kuondolewa vifungu kadhaa vya maoni ya
wananchi kwenye rasimu, jambo linaloonekana ni kutowaheshimu wananchi ambao
ndio wenye Katiba, Sitta kadiriki kufanya kazi nyingine kabisa nje ya kiapo
chake!
Kaanza
kukusanya upya maoni toka kwa makundi mbalimbali ya wananchi, kazi
iliyokwishafanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya kiapo, yeye anaamua
kuirahisisha na kuifanya nje ya kiapo. Sitta kaapishwa kuijadili rasimu na
ikiwezekana kuiboresha, si kukusanya upya maoni ya wananchi maana hiyo si kazi
yake.
Katika
kuhalalisha kinachojionyesha kama uchakachuaji wa maoni ya wananchi, rasimu,
Sitta katamka kuwa rasimu sio msaafu. Nadhani kwa hapo maana yake ni kwamba
alikuwa nayo haki ya kuyachakachua maoni ya wananchi kadiri atakavyo kwa vile
maoni hayo sio jambo lililokuwa na kinga ya Kimungu.
Aidha, Sitta
aliongeza akisema kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu sio mazuzu, kauli
inayoonekana imejaa utata mwingi. Sababu kama kataja mazuzu ina maana yeye
kwenye fikra zake kaishawaona hao mazuzu, ingebidi atueleze ni kina nani? Au
tuseme mfumo mzima uliobariki wazo la upatikanaji wa Katiba Mpya, baadaye
ikaundwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na wananchi waliotoa maoni, ndio
umejaa mazuzu?
Sababu
kitendo cha wewe kujiona sio zuzu na hivyo kuamua kuifumua kazi nzima
uliyokabidhiwa kwa kiapo ili ukaiboreshe bila kupunguza kilichomo, kinaonyesha
waliokukabidhi kazi hiyo ndio mazuzu!
Hiyo
imejidhihirisha kufuatia msisitizo wake wa kuwa rasimu aliyokabidhiwa
ilionekana kujaa mapungufu, kwahiyo, kwa tafsiri yangu, wasiokuwa mazuzu
wakaamua kuifumuoa na kuiunda upya badala ya kuiboresha kama walivyoapishwa
kufanya!
Lakini kama
mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya unasimamiwa na sheria maamuzi hayo ya
Sitta ya kukiuka maoni ya wananchi yanatokana na kifungu kipi cha sheria?
Sababu sasa kinachofanyika sio kuboresha kilichopo kama sheria inavyosema,
maana kilichopo ni rasimu iliyotengenezwa kutokana na maoni ya wananchi
yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Sitta akaapa kuizingatia katika
kuandika Katiba mpya.
Lakini
badala yake anakusanya upya maoni ya wananchi, bilashaka kwa namna inavyompendeza
yeye binafsi na sio kama anavyoona inafaa. Neno kufaa linatumika kwa ajili ya
umma. Ni kwa vipi atatushawishi tukubali kuwa anaboresha kulingana na kiapo
chake?
Bunge
Maalumu la Katiba linakusanya maoni ya wananchi! Kama ulikuwepo uwezekano wa Bunge
hilo kukusanya maoni na kuyafanyia kazi ili ipatikane Katiba Mpya kwa nini rais
hakushauriwa kutojihangaisha kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kusudi lenyewe
liweze kuyakamilisha yote kwa pamoja?
Na kwa jinsi
mambo yanavyoenda, kufanyika bila dalili zozote zinazoonyesha kuwa kuna kiapo
kinachowazuia watu wasitoke nje ya mipaka fulani wanapotekeleza shughuli
waliyopewa, kulikuwepo na sababu gani ya kuwaapisha watu katika shughuli kama
hii?
Kama madai
ya Sitta ni ya kweli, naye kala kiapo, kwa nini baada ya kuona rasimu imejaa
mapungu mengi asishauri Bunge livunjwe ili mchakato ukaanze upya? Au kama hilo lisingewezekana
kutokana na kufungwa na sheria iliyoliunda Bunge hilo, kwa nini yeye asijiuzulu
katika kuonyesha msisitizo. Sababu hakuna sheria inayomzuia mtu kufanya hivyo
tena ikiwa ni kwa manufaa ya umma, kuliko kujifanyia mambo yaliyo nje ya sheria
kwa madai ya kuunufaisha umma.
Katika
mazingira ya aina hii tunawezaje kuitarajia Katiba Mpya itakayomlazimisha mtu
aape kuilinda? Sababu kinapopatikana kwa kukiuka kiapo kinawezaje kikamhitaji
mtu ale kiapo ili kukilinda?
Tukiufuatilia
msimamo wa Sitta ulivyo, kwamba mambo ya kisheria sio msaafu, tunaweza
tukajiuliza kwa nini tuhangaike kuandika Katiba? Sababu sidhani kama tunaweza
kuipata Katiba iliyo na kinga ya Kimungu, kwa maana ya msaafu. Tutaishia kupata
Katiba ambayo kila mmoja wetu anaidharau kwa msimamo huohuo, kama wa Sitta, wa kwamba taratibu zilizoundwa na mwanadamu
sio maelekezo ya Mungu, nani atakayeiheshimu Katiba Mpya?
Lakini
inawezekanaje watu wenye akili timamu tushindwe kujiwekea taratibu na kanuni za
kuendesha maisha yetu na kuziheshimu eti kwa vile sio maelekezo ya Mwenyezi
Mungu? Sisi tutakuwa ni viumbe wa aina gani?
Kwa
mpangilio huo tunawezaje kuwa na sheria? Sababu kwa hoja hiyo ya Sitta, ambaye
ni mwanasheria kitaaluma, sheria zote tunazozitumia zinatokana na utaratibu
tuliojiwekea na kujitengenezea sisi wenyewe, sio maagizo ya Mungu kusema kwamba
tumeyatoa kwenye misaafu.
Hivyo Sitta,
akiwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la kuandika Katiba Mpya ya nchi yetu,
anapojiona ana haki ya kuuchakachua utaratibu wote uliotokana na mapendekezo ya
wananchi kwa vile eti utaratibu huo sio msaafu, anataka kutuonyesha nini?
Kwamba Katiba itakayopatikana haitakuwa na ulazima wa kuheshimiwa kwa vile sio
msaafu? Au kwa vile yeye kawa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba tayari
anajiona kageuka na kuwa na nguvu za Kimungu kiasi kwamba atakachokipitisha
yeye tayari kitakuwa na baraka za Mungu kikiwa kama msaafu!
Hatahivyo
yeye Sitta anadai kwamba yanayosemwa kuwa anakwenda kinyume cha utaratibu wa
sheria iliyoanzisha mchakato wa Katiba Mpya yanasukumwa na chuki dhidi yake,
sijui chuki gani! Kwa nini wananchi wamchukie kama angekuwa anafanya mambo
kulingana na matakwa ya walio wengi? Na kwa nini wasimseme kama wanaona
anayoyafanya yamelenga kukinufaisha kikundi cha wachache akiwa amewaweka walio
wengi pembeni?
Niseme
kwamba mawazo ya aina hiyo hayajaanzia kwa Sitta, tukiiangalia historia ya nchi
mbalimbali duniani tutaona kwamba walikuwepo waliokuwa na mawazo kama hayo ya
Sitta. Inabidi historia hiyo tuizingatie kusudi ituwezeshe kutorudia makosa.
Mfano mzuri
ni wa nchi ya Afrika Kusin. Katika nchi hiyo iliandikwa Katiba mwaka 1902
ambayo haikuwahusisha wananchi walio wengi, ikaonekana ni Katiba ya upande
mmoja wa watawala weupe. Pamoja na Katiba hiyo kudumu kwa karibu miaka 100,
haikuzuia kuandikwa Katiba nyingine ya mpito mwaka 1993 iliyoweka mazingira ya
usawa kwa watu wote wa nchi hiyo.
La
kuzingatia ni kwamba kwa kipindi chote cha Katiba ya kwanza wananchi wa Afrika
Kusini walilazimika kuishi bila amani wakati ilikuwa ni lazima Katiba inayowahusisha
wananchi wote ipatikane. Si bora wangelipa kodi Januari wakaishi kwa amani
kuliko kuishi kwa kujificha maporini lakini wakaja kukamatwa Disemba na kuilipa
kodi pamoja na viboko juu! Huo ni usemi uliokuwa na hekima ya aina yake, “heri
kulipa kodi Januari kuliko kulipa Disemba”.
Kama kweli
mfano huo tunauelewa, kwamba kwa hali yoyote lazima ipatikane Katiba
inayotokana na matakwa ya wananchi, hata kama itachelewa, kwa nini tukubali
kufanya mambo ya kupoteza muda?
Kwa
kulitilia hilo maanani, hatunabudi kujiuliza kwamba msimamo huo alionao
mwanyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, ni wa kwake mwenyewe kadri mawazo
yake yanavyomtuma au naye anapata shinikizo toka kwingine kuyafanya hayo?
0784 989 512