UTAPELI WA KANISA LA KIMAREKANI
Na Prudence Karugendo
KUNA usemi wa kwamba wageni walikuja barani kwetu, Afrika,
kwa kutumia ushawishi wa neno la Mungu na kuwaambia wenyeji “fumbeni
macho tusali”, wenyeji walipofumbua macho kila kitu kilikuwa kimeporwa,
ardhi, maliasili na kila kilichokuwa kwenye uwezekano wa kusombwa na wageni
hao!
Hiyo ni dhana iliyo na kila ukweli wa kimuonekano, sidhani kama
kuna yeyote anayepingana nayo, lakini inaongelea wakati huo. Kwa wakati huu wa
dunia ya kiustaarabu, kuheshimiana na kutendeana haki, sidhani kama kuna nafasi
tena ya kuukumbatia usemi huo.
Ila kuna jambo moja la kusikitisha na kustaajabisha lililofanywa
na Kanisa moja la Kimarekani, SDA, na kuonekana ni la kiutapeli kupitiliza
kiasi kwamba nimelazimika kutengeneza makala haya kwa lengo la kuuliza ubalozi
wa Marekani hapa nchi kama unakubaliana na kitu hicho, vinginevyo ubalozi huo
utasaidie kutupatia ufafanuzi kuhusu jambo hilo lililofanywa na Kanisa hilo la
nchini kwake.
Bwana mmoja, Mtanzania, jina limehifadhiwa kwa sasa,
aliajiriwa na Baraza Kuu la Kanisa la SDA Tanzania, tangu mwaka 1986 mpaka
1999, alipohamishiwa kwenye kitengo cha kanisa hilo kilichoitwa International
Health Foods of the SDA church (T) Ltd., ambacho kilitengenezwa kama Mfuko wa
Hifadhi wa kanisa hilo.
Kati ya mwaka 2002 / 3 kulitokea kutoelewana kati yake na uongozi
wa kitengo hicho kulikoishia kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, ambako mwaka 2008
mahakama hiyo ilitoa hukumu iliyompa haki Mtanzania huyo.
Matokeo yake kitengo cha International Health Foods of the SDA church
kiliamuriwa na Mahakama kumlipa malipo
yake yote ya nyuma tangu mgogoro huo ulipoanzia mpaka ambapo kampuni
ingewasilisha malipo hayo.
Katika kuhakikisha kwamba kitengo hicho kingetimiza amri ya
mahakama bila matatizo yoyote Mtanzania huyo aliomba na kupewa amri ya mahakama
ya kuzuia mali za International Health Foods of the SDA Church, kwamba iwapo
kitengo hicho kingeshindwa kumlipa mafao yake kama ilivyoamriwa na Mahakama
basi mali hiyo iuzwe ili kufidia mafao yake hayo.
Licha ya amri hiyo ya mahakama, kitengo hicho cha Kanisa la
SDA, kiliuza kinyemela mali yake mwaka 2008 na kuihamishia pesa iliyotokana na
mauzo hayo kwenye akaunti ya Baraza Kuu la SDA mjini Pittsburg Marekani. Na
katika kufanya hivyo sio tu kwamba kitengo hicho kilikiuka sehemu ya hati ya
makubaliano ya kuanzishwa kwake inayoeleza wazi kwamba iwapo kitavunjwa mali
zake zote zitakabidhiwa kwa Kanisa la SDA Tanzania, bali pia kilikana uhusika
wa pesa iliyotokana na uuzaji wa mali zake kulipia deni la Mtanzania huyo! Kwa
sasa kitengo hicho kimefutwa.
Mwananchi huyo, huku akionyesha nyaraka mbalimbali zinazohusiana
na suala hilo, anasema kwamba amejaribu kulifuatilia suala lake
tangu mwaka 2008 mpaka mwaka 2013, akieleza hatma yake huku
akilitaka Baraza Kuu la SDA kumtendea haki kulingana na maadili ya kanisa.
Lakini cha kustajaabisha hakupokea jibu lolote toka kwa wahusika!
Ndugu yetu huyo anasema kwa vile pesa iliyopatikana kutokana
na mauzo yaliyofanyika kinyume cha sheria, kwa vile mali hiyo ilikuwa
imezuiwa kwa amri ya mahakama ya Tanzaia kama dhamana kwa malipo yake halali,
iko kwenye akaunti ya Baraza Kuu la Kanisa la SDA nchini Marekani, ndiyo maana
anataka Baraza hilo ambalo, aliyekuwa mwajiri wa wake ni kitengo chake,
lifanye mpango wa kumlipa madai yake hayo.
Katika kuhangaika huku na huko, ndipo , kupitia akafanikiwa kupata
mawasiliano na Mwanasheria Mkuu wa Baraza Kuu la Kanisa la SDA, nchini
Marekani. Baada ya kumweleza kisa chote mwanasheria huyo akajibu kwamba kitengo
alichokuwa ameajiriwa Mtanzania huyo kilianzishwa kama kampuni ya
Kitanzania inayojitegemea, na yenye ukomo wa madeni, “Limited liability
company”.
Akaongeza kwamba kampuni hiyo ndiyo iliyokuwa mwajiri wa mtu huyo,
na kwamba ndiyo iliyomwachisha kazi kabla ya kusimamisha shughuli zake na
baadaye, kwa muda mfupi, kufutwa kabisa hata kabla ya Mtanzania huyo
kukata rufaa. Mwanasheria huyo akasisitiza kwamba madai ya mwajiriwa huyo
ni dhidi ya kampuni hiyo ambayo haipo tena, na sio dhidi ya Kanisa
la SDA la Marekani.
Jambo hilo ndilo linadhihirisha utapeli unaofanyika. Sababu tangu
mwanzo kampuni hiyo ilianzishwa na kujulikana kama kitengo cha kanisa la SDA,
na baada ya kuuzwa kwa mali yake na kampuni kufutwa pesa iliyopatikana
ilihamishiwa kwenye akaunti ya Baraza Kuu la Kanisa la SDA nchini
Marekani. Kwa nini kanisa liikane kampuni wakati linapokea pesa
iliyotokana na mauzo haramu ya mali ya kampuni hiyo likiiona pesa hiyo ni
halali yake? Na kama linaona madai ya kuikana kampuni hiyo ni ya kweli halioni
kwamba kuichukua pesa iliyotokana na kitu linachokikana kuwa ni utapeli?
Katika kumjibu Mwanasheria Mkuu wa Kanisa la SDA, Mtanzania huyo
alisema kwamba kampuni ya IHFA ndiyo iliyokata rufaa katika
Mahakama ya Tanzania dhidi ya uwamuzi wa awali uliompa haki zake, na wala sio
yeye aliyefanya hivyo kama mwanasheria huyo wa SDA anavyodai.
Mtanzania huyo akaongeza kwamba, hatahivyo, Mahakama
ambako IHFA ilipeleka rufaa kusudi asipewe haki yake, ilitoa
hukumu iliyokuwa inathibitisha usahihi wa hukumu ya mahakama ya awali, kwamba
alipwe haki zake zote.
Lakini wakati anahangaika na masuala ya kimahakama,
IHFA Ltd. iliendelea na mipango ya kuuza mali yake ilizokuwa
zimeshikiliwa kwa amri ya mahakama na kufanikiwa kuiuza kinyemela mwezi
Julai, 2008.
Kitu kingine ni kwamba baadhi ya wadhamini wa IHFA Ltd. walikuwa
ni maafisa waandamizi wa Kanisa la SDA toka makao makuu, Marekani, kama
inavyoonyeshwa kwenye hati iliyoanzisha kampuni hiyo ya kanisa.
Baada ya Mtanzania huyo kutoa maelezo hayo kwa mwanasheria wa
Baraza Kuu la Kaniza la SDA hakuna jibu lililopatikana toka kwanasheria huyo wa
kanisa zaidi ya kufanya kitu ambacho vijana wa kisasa wanakiita kuingia mitini!
Mwanasheria huyo wa kanisa hakuendeleza zaidi mawasiliano.
Hiyo inadhihirisha kwamba kilichofanywa na kanisa hilo la SDA
kilidhamiriwa na kukusudiwa. Hivyo picha inayojitokeza ni ya kwamba baadhi ya
makanisa yanakuja hapa nchini kwa lengo la kuchuma tofauti na
inavyodhaniwa kwamba yanaleta neno la Mungu. Sababu hakuna namna ambavyo Mungu
anaweza kuelekeza kwamba nenda ukamuibie mwenzako.
Tutaona kwamba mtindo huo, kama ulioonyeshwa na Kanisa la SDA,
hauna tofauti hata kidogo na dhana niliyoielezea mwanzo ya “walikuja wakasema
fumba macho tusali, wenyeji walipofumbua macho kila kitu kilikuwa kimeporwa”!
Katika hali ya kawaida, hata kwa asiye na imani ya Kimungu,
kumpora aliye fukara, masikini, ni jambo linalomwia gumu kulifanya, hata jambazi
mzoefu anaona utata wa kufanya hivyo.
Kwahiyo kanisa hilo la SDA, kanisa la Kimarekani, taifa kubwa na
tajiri kupindukia, linapofanya jambo la namna hiyo, utapeli katika nchi changa
na masikini, linataka lionekaneje? Linaijengea picha gani nchi yake lilimoweka
makao yake makuu?
Na je, Marekani kama nchi inayojiheshimu na kuheshimika
inalitazama vipi jambo hilo linaloichafua kwa kuipaka matope? Ni kweli
italiachia kanisa hilo liendelee na mtindo huo wa kukwapua penye kidogo na
kuzidi kujaza penye kingi, palipojaa tayari?
0784 989 512