WANAUSHIRIKA KAMACHUMU WAFANYIWA VITENDO VYA KIHUNI
Na Prudence Karugendo
CHAMA cha Msingi Kamachumu ambacho ni kati ya vyama
vya msingi vinavyounda Chama Kikuu cha Ushirika cha KCU (1990) Ltd., mkoani
Kagera, kimefanyiwa uhuni mbaya sana ambao umemuacha kila mwanaushirika wa
sehemu hiyo akijiuliza kama huo ni ushirika au kikundi cha watumwa
waliokusanywa na kupewa maagizo ya nini cha kufanya na mamlaka iliyo juu yao
bila wao kuhoji lolote!
Tofauti na
hali halisi ilivyo, kwamba ushirika ni chombo cha hiari ambacho wananchi
wanaamua wenyewe kukianzisha bila kushurutishwa ili kupata nguvu ya pamoja
katika kukifanikisha walichokilenga, wananchi wa Kamachumu wamejikuta wanageuka
wafungwa ndani ya ushirika wao wakiamriwa kumsikiliza mtu mmoja tu
aliyejipachika ubwana jela na kuwataka wanaushirika hao wafanye namna
anavyotaka yeye na si vinginevyo.
Kisa
chenyewe, kama wanavyosimulia wanaushirika wa Kamachumu, kiko hivi; Kutokana na
Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera, KCU (1990) Ltd., kufanya mambo mengi
yaliyo na picha ya ufisadi huku wakulima wa kahawa, ambao ndio wadau pekee wa
chama hicho, wakitaabika kwa ukata pasipo kuyaona manufaa yoyote ya zao la
kahawa wala kuiona faida ya kuwa na ushirika, ndipo chama hicho cha msingi
Kamachumu kwa kumtumia mwakilishi wake mmoja,
kikaanza kupaza sauti kuhoji mambo mbalimbali ambayo uongozi wa KCU (1990) Ltd. hautaki yaulizwe wala
kujadiliwa.
Baada ya
hapo uongozi wa KCU (1990) Ltd. ukaanza kuwaangaza wale unaodai wanaleta
kidomodomo ili washughulikiwe. Ndipo ikabainika kwamba mwakilishi mmoja wa
Kamachumu, Archard F. Muhandiki, ndiye mwenye kuleta hoja zisizotakiwa na
uongozi wa chama kikuu na hivyo kuamua afukuzwe kwenye mikutano ya chama hicho
kikuu.
Kilichofuatia
ni wanaushirika wa Kamachumu kuhoji uhalali na usahihi wa mwakilishi wao kuvuliwa
kinyemela jukumu lake la uwakilishi alilopewa na wanaushirika wenzake katika
chama chake cha msingi.
Wanaushirika
hao wakasema kwamba kuzuiwa kwa mwakilishi wao kuhudhuria mikutano ya chama
kikuu ni sawa na chama chao cha msingi
kutengwa na chama hicho kikuu au kuondolewa kabisa kwenye ushirika huo
wa KCU (1990) Ltd.. Maana wanasema kwamba chama chao cha msingi hakiwezi
kushiriki bila kushirikishwa kwa maana ya kuwakilishwa.
Kufuatia
mtafaruku huo kati ya Chama Cha Msingi Kamachumu na KCU (1990) Ltd.,
wanaushirika wa chama hicho wakalazimisha uitishwe mkutano wa dharura ili,
pamoja na mambo mengine, wakaliongelee hilo la mwakilishi wao kufanyiwa hujuma
na KCU (1990) Ltd. akiwa anatimiza majukumu yake kwa mujibu wa taratibu za ushirika.
Kutokana na
tuhuma ambazo wanaushirika wa Kamachumu walizielekeza kwa mwenyekiti wao, Super
Karugaba, zinazodai kwamba anashirikiana na uongozi wa chama kikuu kukihujumu
chama chao, wanaushirika hao wakapiga kura ya kutokuwa na imani na mwenyekiti huyo.
Karugaba akaondolewa marakani pamoja na makamu wake kwa nguvu za wanaushirika.
Kwahiyo Kamachumu wakabaki hawana uongozi.
Wanaushirika
hao walihakikisha hayo yote yanawasilishwa kwa Afisa Ushirika wa wilaya ya
Muleba kama utaratibu unavyoagiza. Pia wakamtaka afisa huyo kupanga tarehe ya
kuitisha uchaguzi wa kuupata uongozi mpya wa chama hicho cha msingi. Lakini
wanasema bahati mbaya au kwa makusudi Afisa Ushirika huyo aliamua kukaa kimya
bila kuwajibu lolote!
Kamachumu ni
eneo linalozalisha kahawa kwa wingi katika mkoa wa Kagera; kwahiyo ndilo
tegemeo kuu la kahawa la KCU (1990) Ltd., na ndiyo maana chama hicho kinawekeza
sana nguvu zake katika eneo hilo huku kikiwa hakitaki pawepo na uongozi imara
na uwakilishi unaojisimamia.
KCU (1990)
Ltd. iliendelea kumtambua Super Karugaba kama mwenyekiti wa Kamachumu pamoja na
ukweli kwamba mwenyekiti huyo alikuwa hatambuliwi tena na wanaushirika wa chama
hicho kwa vile walishamuondoa kwenye uongozi.
Swali
linaloonekana kuwasumbua sana wanaushirika hao ni la kwamba uongozi wa chama
cha msingi unapaswa utambuliwe na nani kwanza? Wanaushirika wanaouchagua au
chama kikuu kinachoundwa na vyama vya msingi? Wanauliza kama chama kikuu ndicho
kinavimiliki vyama vya msingi au vyenyewe kwa umoja wake ndivyo vinakimiliki
chama kikuu?
Sababu eti
bila chama kikuu vyama vya msingi vinaweza vikaendelea kuwepo, lakini bila
vyama vya msingi vya ushirika hapawezi pakawepo chama kikuu cha ushirika!
Kwahiyo
kutokana na chama kikuu, KCU (1990) Ltd. kutopenda kumpoteza Karugaba,
mwenyekiti aliyeondolewa madarakani Kamachumu, kwa faida inayojulikana kwa KCU
peke yake, chama hicho kikuu kikamkingia kifua kwa njia za kustaajabisha. Kwa
kutumia mabavu, njama na vitisho dhidi ya wanaushirika wa chama cha msingi
Kamachumu.
Ulipofika
wakati wa uchaguzi uliofanyika ndani ya ushirika kwa mwaka huu, uliofanyika kwa kuanzia na vyama vya msingi tarehe 5
Septemba, fomu za wagombea zikatolewa kinyemela bila matangazo yoyote kusudi
wanaushirika wanaohofiwa na uongozi wa chama kikuu wasiweze kuziona na kupata
nafasi ya kugombea.
Baada ya
hapo kilichofanyika katika uchaguzi wa Chama Cha Msingi Kamachumu ndicho
kimegeuka simulizi, sababu kimewaacha wananchi wakijiuliza wao ni wanaushirika
au ni wafungwa?
Uchaguzi huo
ulipaswa kusimamiwa na Afisa Ushirika wa wilaya ya Muleba kutokana na eneo la
Kamachumu kuwa katika wilaya hiyo. Lakini sivyo ilivyokuwa.
Kwa hisia za
kwamba Afisa Ushirika wa Muleba alikuwa na deni kwa wanaushirika hao wa
Kamachumu la kutowajibu barua yao iliyomtaka aitishe uchaguzi kuziba pengo
lililoachwa na uongozi uliondolewa madarakani, ikafanyika mipango yeye asiende
kule na badala yake akaombwa Afisa Ushirika wa wilaya ya mbali, Misenyi, iliyo mpakani mwa Tanzania na Uganda,
Amphrey Kachelele, ndiye akasafiri
kwenda kusimamia uchaguzi huo.
Afisa
Ushirika huyo, bilashaka baada ya kuelezwa kinachoendelea Kamachumu, akajiandaa
kivita. Eti hakuthamini hata kidogo kama aliokutana nao ni watu wazima wenye
heshima zao na waliokuwa wanafanya kitu kilicho chao na kwa manufaa yao!
Wanaushirika
hao wa Kamachumu wanasema msimamizi huyo wa kuazimwa alipofika kwenye mkutano
wao wa uchaguzi akaanza kumwaga vitisho na majigambo, akisema kwamba yeye ni
msomi wa hali ya juu na kwamba mkutano ule ni wa kwake. Eti akaongeza kwa
kujigamba kwamba hata kama angekuwepo Rais Kikwete ingembidi rais akae kule!
Eti akasema kwahiyo hataki mtu yeyote kufanya “vyoko” hata kama angekuwa rais!
Na kwa vile
fomu za kuombea nafasi za kugombea zilifichwa kiasi kwamba wanaushirika walio
wengi hawakuziona, wajumbe, wanaushirika wa Kamachumu, hawakujua ni nani
aliyekuwa anagombea uenyekiti wa chama chao cha msingi, kabla ya kuelezwa na
msimamizi kuwa anayegombea uenyekiti ni mtu mmoja tu, Super Karugaba,
mwenyekiti aliyeondolewa madarakani na wanaushirika kutokana na kukihujumu
chama chao.
Kwahiyo
msimamizi, kama alivyoelekezwa na waliompeleka kule, akaamuru kura zipigwe za
ndiyo au hapana! Hiyo yote ni katika kumlinda Karugaba asiondoke kwenye
uenyekiti ambao ameukalia kwa zaidi ya miaka 30 kinyume na kanuni za vyama vya
ushirika.
Pia inasemwa
kwamba msimamizi huyo toka Misenyi alishasema kwamba mkutano huo, aliouita wa
kwake, ni lazima ungefanyika hata kama wanaushirika wote wa Kamachumu
wangeususa akabaki yeye peke yake!
Hilo ndilo
jambo lililowashtua wanaushirika hao wa Kamachumu na kumuona msimamizi huyo
kuwa kaenda kwao kishari na wala sio kusimamia uchaguzi.
Kibaya zaidi
ni kwamba msimamizi huyo alidiriki kuchukua karatasi ya kupigia kura toka kwa
mmoja wa wapiga kura na kuichanachana mbele ya wajumbe wote wa mkutano huo
akidai kwamba mjumbe huyo kaichelewesha
kura hiyo!
Swali kuu
walilobaki nalo wanaushirika hao wa Kamachumu ni la kwamba kweli huo ndio
ushirika au ni ufungwa? Swali hilo wanalielekeza kwa Rais Jakaya Kikwete ili
aweze kuwafikiria akiwa ameufikiria ushirika kwa ujumla. Sababu wanasema kwamba
maji yamewafika shingoni na hawana pengine pa kukimbilia.
0784 989 512