Bukobawadau

MISS TANZANIA NA UDANGANYIFU

Sitti angevuliwa taji kunusuru jina la nchi
Na Prudence Karugendo
TANZANIA  ni jina kubwa, ingawa sisi Watanzania kwa sasa tunafanya jitihada kubwa za makusudi, na pengine kwa kutokujua, kuhakikisha tunalishusha hadhi jina la nchi yetu. Yapo mengi yanayofanyika kwa bahati mbaya na kwa makusudi, hasa yakiwa yamelenga kwenye maslahi binafsi, bila kujali kuwa mambo hayo yanalichafua jina la nchi yetu na kulishushia hadhi yake.
Kwa sababu hiyo Watanzania tunaoithamini nchi yetu tungepinga kwa nguvu zetu zote kitendo cha kulishusha hadhi jina la nchi yetu kupitia kwenye mambo yasiyo na faida yoyote kwa nchi yetu, hususan matendo yaliyolenga kwenye maslahi binafsi ya watu wasio na uchungu wa kuliona jina la nchi yetu likidhalilika.
Mfano ipo kampuni ya Lino International Agency inayojihusisha na mambo ya urembo nchini. Kampuni hiyo ndiyo inayoshughulika na kumpata mlimbwende wa kike hapa nchini kwetu. Kibaya ni kwamba mrembo akishapatikana haishii hapahapa nchini, anaenda kwenye mashindano ya kumtafuta mrembo wa dunia akiwa anawaiwakilisha Tanzania.
Hayo ni mashindano ya kimataifa, ikishafikia hatua hiyo jukumu la kumbeba mrembo anayeiwakilisha nchi linageuka kuwa la kitaifa, Lino International Agency inabaki ni wakala tu.
Hata kama taifa halichangii kitu,  kitendo cha nchi kukubali jina lake litumike kwenye mashindano hayo ya kimataifa ya urembo tayari ni mchango mkubwa uliovuka kiwango cha kampuni inayoendesha masindano hayo kitaifa, Lino International Agency.
Kwahiyo chochote kinachotokea kwa mrembo anayeiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo ya kimataifa kinapaswa kihesabike kimeitokea Tanzania na siyo Lino International Agency wala mkurugenzi wake, Hashimu Lundenga. Kwahiyo kama ni kibaya linalofadhaika ni taifa na wananchi wake wote.
Kwa maana hiyo hatuwezi kukubali kumuona mrembo anayefanya mambo ya aibu ili apate urembo wa taifa sisi tukae kimya bila kusema lolote kana kwamba ni jambo lisilotugusa kabisa. Ikumbukwe kwamba baada ya hapo aibu atakayokwenda kuisomba huku anakokwenda kuiwakilisha nchi anaibwaga vichwani mwa Watanzania wote na kuilazimisha aibu hiyo kuwa jukumu la Watanzania kuibeba wanapenda wasipende.
Laiti aibu hiyo ingekuwa inaishia kichwani mwa Lundenga na kampuni yake nisingejihangaisha kama ninavyofanya kwa sasa. Tatizo ni kwamba aibu hiyo inanigusa,  nalazimika kuibeba.
Kuibuka kwa kashfa ya udanganyifu inayomkabili Redd’s Miss Tanzania 2014, Sitti Abbasi Mtemvu, ni jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa. Kashfa ya binti huyo kudanganya umri wake ili aupate urembo wa nchi.
Katika hali ya ungwana na umakini mrembo huyo angejivua mwenyewe taji hilo baada ya kugundua kuwa ujanja wake umejulikana kuliko kusubiri kupigiwa kelele na umma kama ilivyo sasa. Aina yoyote ya kujitetea katika jambo la wazi namna hii ni lazima izidishe ugumu wa mambo wa kutaka kuifanya Tanzania izidi kuonekana ni nchi ya uchakachuaji.
Hati ya kusafiria ya Sitti Mtemvu iliyotolewa Februari 15, 2007, inaonyesha alizaliwa Mei 31, 1989. Baada ya hapo akapata leseni ya udereva iliyotolewa Texas nchini Marekani tarehe Machi 26, 2013, ikionyesha kazaliwa tarehe kama iliyopo kwenye hati yake ya kusafiria. Lakini katika kumkingia kifua Lundenga anasema Sitti alizaliwa Mei 31, 1991! Hata kama tarehe hiyo ina ukweli tayari leseni ya udereva pamoja na hati ya kusafiria vinaonyesha kuwa kuna udanganyifu uliotokea, iwe katika kupata hati ya kusafiria, leseni ya udereva au urembo wa Tanzania. Sababu vinatofautiana kwa mtaja mtu yuleyule.
Kwahiyo hata kama yeye anaona ugumu wa kujivua taji hilo, basi kamati inayoandaa mashindano hayo ya ulimbwende chini ya mwenyekiti wake, Lundenga, ingemsaidia kufanya hivyo kuliko kumkingia kifua kwa njia za aibu. Hiyo ni katika kuinusuru heshima ya nchi, ya kwake mwenyewe na ya kina Lundenga.
Hatua hiyo itamuondolea Sitti utata wa kuonekana aliidanganya serikali ya Marekani kuhusu umri wake ili ikampatie leseni ya kuendeshea gari, kitu kinachoweza kumfanya apigwe marufuku kukanyaga tena nchini mle.
Lundenga naye, badala ya kueleza mambo yenye ushawishi katika kashfa hiyo anazidi kumdidimiza Sitti akidhani ndiyo kumkingia kifua! Anasisitiza kwamba alizaliwa 1991 bila kuelewa kwamba kwa kufanya hivyo anamchongea mrembo huyo kwa Idara ya uhamiaji ya hapa nchini na seriakli ya Marekani ambako Sitti alidanganya kuwa alizaliwa mwaka 1989.
Katika hatua nyingine mrembo huyo alipobanwa na wanahabari aeleze kwa nini cheti cha kuzaliwa kitolewe zaidi ya miaka 23 tangu tarehe anayodai ndiyo ya kuzaliwa kwake, akadai cha kwanza kilipotea, alipoulizwa aliripoti kituo gani cha Polisi kuhusu upotevu huo akajibu kwamba hakujiandaa kujibu swali hilo!
Penye ukweli uongo hujitenga, mtu anayesema ukweli hapaswi kujiandaa ili aseme ukweli. Anayesema uongo ndiye hujiandaa aseme nini na aache nini, kuusema ukweli hakuhitaji maandalizi yoyote.
Hata kwa Lundenga ni hivyohivyo, angeelewa anasema ukweli hasingehitaji kujiandaa alipoulizwa kwa mara ya kwanza kuhusu kashfa hiyo ya Sitti. Angejibu bila kusubiri kwa vile hakuna alichopaswa kukiazima, lakini katika uongo lazima yapo maneno ya kuazimwa na mengine ya kuchongwa. Ndiyo maana Lundenga alihitaji muda kujibu kashfa hiyo.
Sitti Abbasi Mtemvu ni binti mzuri na mwelewa wa mambo anayeweza kuiwakilisha vizuri nchi yetu hata kutwaa taji la dunia. Kimbembe ni suala hilo la udanganyifu na uchakachuaji ambalo halikubaliki kimataifa. Sababu ikishajulikana tu kuwa alichakachua, hata kama kaishavishwa taji la dunia itabidi avuliwe.
Na si ajabu huo ukawa mwisho wa Lundenga kuyaona mashindano hayo. Sababu taji la mrembo wa dunia linahitaji binti, pamoja na mambo mengine, awe mwadilifu kamili. Kamwe mdanganyifu hajawahi kuwa mwadilifu, mdanganyifu atawawakilisha vipi waadilifu?
Mheshimiwa Abbasi Mtemvu, baba yake mrembo wetu, anaingiza siasa katika mambo haya ya urembo kwamba wanaosema binti yake kadanganya umri wake wamekitazama kiti chake cha ubunge! Hiyo ni aibu nyingine.
Dunia inaweza kujiuliza kwamba udanganyifu wa kisiasa nchini Tanzania sasa unaanzia hata kwenye urembo? Bora yeye angenyamaza kimya na kuliacha suala hilo kwa binti yake na kamati inayoshughuli mambo hayo ya urembo.
Hiyo ni kwamba ushahidi uliopo unaigusa hata nchi ambayo udanganyifu ni kashfa kubwa sana na haramu, Marekani, nchi ambayo udanganyifu uliwahi kumtoa rais Ikulu. Kumbuka kashfa ya Watergate.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau