“TWEYAMBE” NA MATUMAINI MAPYA KWA ZAO LA KAHAWA
Na Prudence Karugendo
BAADA ya kuteseka, kuhujumiwa, kufisidiwa, kutapeliwa nakadhalika,
kwa muda mrefu, wakulima wa kahawa wa Kamachumu, Muleba, mkoani Kagera,
wameamua kuanzisha Umoja wa Wakulima wa Kahawa ambao wameupa jina la
Tweyambe, au kwa kimombo “Tweyambe Coffee Growers Association”.
“Tweyambe” ni neno la Kihaya lenye maana ya kujihimu kwa pamoja, kuweka nguvu pamoja katika
kujihangaikia na kujiondoa kwenye ufukara.
Umoja huo umetokana na wakulima hao wa kahawa kufanyiwa mambo
machafu sana kwa muda mrefu na uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha KCU
(1990) Ltd. ambacho ndicho kinachoshughulikia zao la kahawa katika wilaya za
Muleba, Misenye, Bukoba Mjini na Vijijini, na wao kubaki wakikitegemea
kuanzia kwenye vyama vyao cha msingi.
Wakulima hao wanasema kwamba mfumo wa ushirika, tangu unaanzishwa,
ulikuwa mzuri na wenye manufaa kwa
wakulima hasa wa mazao ya biashara, lakini eti baada ya mfumo huo kuingiliwa na
wajanja, au waliokuwa wakiuendesha ushirika kujanjaluka na kuyageuzia kwao
manufaa yote ya ushirika, huku wakiwaacha wakulima wanafanya kazi ya
kuwazalishia wao tu bila wakulima wenyewe kupata chochote, ushirika ukabaki
kwenye mazoea tu bila kuwanufaisha wakulima kwa namna yoyote ile.
Wakulima wa Kamachumu wanatoa mfano kwamba walikuwa wakilitegemea
zao la kahawa liwawezeshe kukabiliana na
matatizo mbalimbali ya kiuchumi, kama vile kusomesha watoto, kuwa na makazi
bora, malazi bora, kupata huduma bora za kiafya nakadhalika. Lakini eti kwa
sasa mambo yamegeuka na kuwa ya ovyo, hawawezi kulitegemea tena zao hilo
liwaondolee matatizo ya kiuchumi. Hawawezi kuwapeleka watoto shule kwa
kutegemea kahawa, hawezi kuwa na mawazo ya kujenga nyumba bora kwa kutegemea
kahawa na mambo mengine mengi ambayo yamekwama kutokana na uchumi wao kuwa
mbovu.
Eti wamefikia kiasi cha kuliona zao hilo la biashara kama mateso
kwao, mateso ni pale wanapolazimika kuishughulikia kahawa bila kuyaona manufaa yake.
Lakini eti pamoja na mambo kuwa hivyo hawawezi kusema kwamba sasa
zao hilo limeisha thamani yake, eti thamani ya kahawa bado ni ileile ya tangu
zamani. Tofauti wanayoiona ni ya namna viongozi wa ushirika wa sasa wanavyonona
kuliko wale wa zamani, eti hiyo inawapa mawazo kuwa thamani ya kahawa kwa sasa
inaishia kwa viongozi wa ushirika tu badala ya kumfikia mkulima.
Sababu eti kila anayechaguliwa kwenye uongozi au kuajiriwa kwenye
ushirika akiwa mlalahoi, baada ya nusu mwaka anageuka na kuwa bwanyenye
akiwacheka na kuwadharau wakulima wenzake ambao ndio waajiri wake! Eti bila
kahawa kuwa na thamani, kama inavyodaiwa
kwa sasa, hali isingekuwa hivyo na vi
wachache wangeutamani uongozi katika ushirika.
Kwahiyo wakulima wa kahawa wa Kamachumu kupitia kwenye chama chao
cha msingi wakajaribu kulionyesha tatizo hilo la thamani ya kahawa yao
kuunufaisha tu uongozi wa ushirika, lakini uongozi wa chama kikuu ukatumia
nguvu kubwa, nguvu inayotokana pesa ya wakulima wanaushirika, kuwanyamazisha
wanaushirika hao wa Kamachumu.
Archard Felician Muhandiki ni mwakilishi wa Chama cha Msingi cha
Kamachumu, kutokana na mtu huyo kuujali sana uwakilisha wakulima bila kutaka
kuwasaliti kwa kujiunga upande wa uongozi na kuwahujumu, akaonekana ni
mtu hatari kwa ushirika anayepaswa kupigwa vita kwa kila namna!
Kwa maoni anasema, eti jinsi inavyochukuliwa na ushirika kwa ujumla,
kwa upande wa Kagera, ushirika maana yake ni pale kiongozi anapojinufaisha na
jasho la wakulima anapopata fursa ya kufanya hivyo. Eti mtu yeyote anayesita kuwahujumu
wakulima wakati yuko kwenye nafasi ya uongozi katika ushirika, safu nzima ya
uongozi wa ushirika inamchukulia kuwa si mwenzao na ikibidi inamzulia kashfa
kuwa anauhatarisha ushirika!
Eti kuna wakati imesemwa kwamba yeye, Muhandiki, haupendi
ushirika, kisa hataki uongozi ufanye ufisadi kwa pesa za wakulima! Eti
anayeonekana anaupenda ushirika ni yule aliye tayari kushirikiana na viongozi
wenzake wa ushirika kuiba pesa za wakulima, huyo ndiye mpenzi wa ushirika kwa
mtazamo wa viongozi wa ushirika waliojiweka wazi kwa ufisadi wa pesa za
wakulima.
Kwahiyo Bwana Muhandiki naye hafichi chochote, anasema kama
ushirika maana yake ni kuwaibia wakulima basi yeye haupendi ushirika wa aina
hiyo. Na eti yuko tayari kulieleza hilo kwa kila mkulima kama ambavyo amekuwa
akijitolea kutoka Dar es salaam, kwa usafiri wa ndege kwenda na kurudi Bukoba,
kuhudhuria mikutano ya Chama Kikuu cha KCU (1990) Ltd..
Anasema malipo ya juu kwa kila mjumbe kuhudhuria vikao vya KCU
(1990) Ltd. kwa mara moja ni shilingi laki tano, wakati yeye anatumia
mpaka shilingi milioni mbili zake mwenyewe kuhudhuria vikao hivyo. Lakini
anasema hizo laki tano wanazopewa wajumbe wanaokwenda kwenye mkutano wa chama
kikuu zinawatosha kuwasaliti wakulima wenzao wanaowawakilisha, eti kulingana na
maisha ya kijijini yalivyo kwa sasa kwa wajumbe wengi hizo ni pesa nyingi mno!
Ukweli huo ndio uliowafanya wanaushirika wa Chama cha Msingi
Kamachumu kufanya uamuzi wa kuuondoa madarakani uongozi wa chama hicho lakini
uongozi huo ukakingiwa kifua na uongozi wa Chama Kikuu, kiasi cha KCU (1990) Ltd. kutumia pesa za
wakulima kuweka wakili wa kuutetea mahakamani uongozi wa chama hicho cha msingi!
Swali walilonalo wanaushirika wa Kamachumu ni la kwa nini wao waushitaki uongozi wa chama chao cha msingi,
kutokana na uovu unaoufanya dhidi ya wanachama, lakini ujitokeze uongozi wa chama kikuu
kuyajibu mashitaka hayo kwa kumweka wakili wakati hauhusiki na mashitaka hayo?
Baada ya kuona hivyo wanaushirika hao wakaamua kuachana na aina
hiyo ya ushirika wa kuhujumiana na kuamua kuanzisha kitu kingine kabisa nje ya
ushirika uliozoeleka, ilmradi kutafuta njia za kujinufaisha na zao lao la
kahawa.
Chama kilichotangulia kufanya kitu cha aina hiyo, kuukataa ufisadi unaofanywa na uongozi wa
chama kikuu, ni Chma cha Msingi Magata, nacho cha wilayani Muleba, ambacho kwa
sasa kinajitegemea baada ya kuitua chini KCU (1990) Ltd. iliyogeuka mzigo mzito
usiobebeka.
Umoja unaopangwa kusajiliwa ni Tweyambe. Ni aina ya ushirika ambao
wanasema wataulinda kwa makini ili usiingiliwe na virusi vya ufisadi. Wataweka
ukomo wa uongozi ili kumwezesha kila mwenye uwezo wa kuongoza apate nafasi hiyo
bila kulazimika kutoa rushwa.
Pia wanasema kwamba muundo wa uongozi wanaoutaka kwenye umoja wao
sio kama ule wa chama kikuu cha ushirika, ambapo uongozi wa chama kikuu unatumia
mapato yote ya chama na hata pesa ya kukopa kujinufaisha wenyewe, wakati
wakulima hawapati kitu. Wao wanataka kama kuna ziada itakayopatikana iwafikie
wanaumoja wote.
Tweyambe wanapanga kuhakikisha kahawa yao inakuwa safi kiasi cha
kuiwezesha kupata soko kirahisi na kuwarudishia faida kwa muda mfupi. Eti
hawatahitaji kuwa na mlolongo wa viongozi watakaolazimika kula mapato yote
yanayotokana na jasho lao kama ilivyo kwa chama kikuu cha ushirika.
Kitu kingine ni kwamba, hata kama waliotoa wazo hilo la kuwa na
umoja wa Tweyambe ni watu wa Kamachumu, sio lazima kwamba umoja huo unapaswa
uwe wa kwao peke yao. Eti wanawakaribisha wadau wote wa zao la kahawa katika
mkoa wa Kagera kwenye umoja huo ili waunganishe nguvu zao pamoja dhidi ya
ufisadi unaolikabili zao lao la kahawa mkoani humo.
Tweyambe wanasema kwamba ufisadi katika ushirika umetamalaki kote
ambako ushirika umeweka mizizi. Eti kibaya zaidi ni Sheria ya Vyama vya
Ushirika ambayo inaonekana kuulinda huo
kwa kutotaka wanaohujumu ushirika washitakiwe mahakamani. Eti haiwezekani mtu
afanye wizi halafu umpelekee kesi ya wizi huo akaishughulikie yeye na
kujiadhibu mwenyewe.
Eti kwa kufanya hivyo sheria hiyo ni kama inaulea ufisadi ndani ya
ushirika, kitu kinachoufanya ushirika usieleweke vizuri nini malengo yake.
Kwamba kama malengo ya ushirika ni kuwainua na kuwaendeleza wakulima basi
sheria ingekuwa wazi kwamba wanaokwenda kinyume na malengo hayo ya ushirika
washitakiwe mara moja na ikibidi wafungwe au pamoja na kufilisiwa mali zao ili
kujaribu kufidia jasho la wakulima.
0784 989 512