Bukobawadau

UKAWA WAUNGWA MKONO MGOMBEA MMOJA

Baada ya vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukubaliana kumsimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu mwakani, baadhi ya wasomi na viongozi wa asasi za kiraia wameunga mkono hatua hiyo.

Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu, alisema lengo la kuundwa kwa Ukawa lilikuwa ni kuunganisha nguvu kusaidia mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ambayo alidai kupinduliwa.

Prof. Baregu, alisema maazimio ya Ukawa yatasaidia kuunganisa makundi mengine yaliyokuwa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ambayo yalikuwa na nia moja na umoja huo, hivyo kutia nguvu baadaye.

“Lengo ni zuri, wanahitaji kujipanga upya. Ni uamuzi ambao utaimarisha vyama vya siasa hapo baadaye. Itasaidia katika vuguvugu hilo la katiba mpya kwa kuunganisha asasi za kiraia na wale ambao hawakuridhika na mchakato wa katiba mpya. Itasaidia kuwaunganisha Ukawa na Watanzania kwa ujumla,” alisema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, alisema: “Mimi ninaafiki, wanaweza wakaleta ushindi mkubwa sana, kwani ninavyoamini umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Kwa mujibu wa Kibamba, Ukawa wakifanikisha kutekeleza malengo hayo, wapigakura katika chaguzi zijazo watakuwa na hamasa kubwa na kutafanya vyama vingine vya siasa ambavyo havikuungana na Ukawa kuweza kufutika kwa kutolea mfano kwa Marekani.

Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tangayika (TLS), Francis Stolla, aliunga mkono hoja hiyo, kwa kusema: “Sasa hakutakuwa na kugawana kura. Wakitekeleza kweli, litaweza kuleta mafanikio makubwa kwa chaguzi zijazo.”

CHANZO: NIPASHE
Next Post Previous Post
Bukobawadau