VSO NA PCF WATOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 80 KUBORESHA MAZINGIRA YA UFUNDISHAJI NA KUJIFUNZIA ILI KUINUA KIWANGO CHA ELIMU KAGERA
Mkuuwa Mkoa wa Kagera ameyapongeza mashirika binafsi ya Vulutary
Service Overses (VSO), na Pestallozi
Chirdren Faundation (PCF) kwa kunuia kuinua kiwango cha ubora wa elimu
katika Halmashaauri ya Wilaya ya Bukoba kwa kutoa zaidi ya shilingi 80 milioni kuboresha
mazingira ya ufundishaji na kujifunzia.
Pongezi
hizo zilitolewa na Kanali Mstaafu Fabian Massawe tarehe 21/10/2014 wakati wa
hafla fupi ya kutembelea, kukagua na kupokea rasmi kazi zilizotekelezwa na
mashirika ya VSO na PSF katika shule za Msingi Nyakato na Kalwoshe Kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.
Mashirika
ya VSO na PCF kwa kushirikiana walibuni mkakati wa pamoja wa kuboresha
mazingira ya ufundishaji na kujifunzia ambao ulianza mwaka 2011 na lengo kubwa
likiwa ni kuweka mazingira bora ya mtoto kujifunzia, kuweka mbinu shirikishi
katika ufundishaji kati ya mwalimu na wanafunzi aidha kuandaa zana za
kufundishia zenye gharama nafuu.
Aidha
mwaka 2013 VSO na PCF kwa pamoja
waliamua kukarabati Shule za Msingi Nyakato na Kalwoshe zilizokuwa katika hali
mbaya kutokana na shule hizo kuwa kongwe na miundombinu yake ilikuwa tayari
imeharibika vibaya sana hadi kupelekea walimu na wanafunzi kunyeshewa mvua
wakiwa madarasani na ofisini.
VSO
na PCF wameweza kukarabati vyumba vya madarasa 5 na
ofisi 2 na kubadilisha bati, kujenga vyoo 2 vyenye matundu 8, kujenga
matenki 2 ya maji kwa ajili ya wanafunzi kusafisha mikono yao mara watokapo
chooni, aidha yalitolewa madawati 144 meza 6 na kabati 1 ya mwalimu katika
shule ya Msingi Nyakato.
Shule
ya Msingi Kalwoshe VSO na PSF waliweza kukarabati madarasa 3, kujenga makta
mpya 1 na vifaa vyake vyote, pia walijenga vyoo 2 vyenye matundu 8, pamoja na
matenki mawili ya maji kwaajili ya wanafunzi kusafisha mikono, na kutoa madawati 44 kwa watoto wa awali pamoja na
viti vya walimu.
Aidha
VSO na PCF imetoa mafunzo ya elimu ya mbinu za ufundishaji kwa njia shirikishi
na kuandaa zana za kufundishia za gharama nafuu ambazo zinapatikana kwenye
mazingira husika kwa walimu 48 ambao watatumika kama wakufunzi kueneza elimu
hiyo katika mkoa mzima.
Bi
Beatrice Nalingingwa ni Mkurugenzi wa shirika la PCF lenye makao makuu yake
nchini Switzeland alisema lengo la shirika lake ni kulinda haki ya mtoto, kutoa
elimu bora, ushirikishwaji wa watoto,
na ndiyo maana waliamua kushirikiana na VSO kuboresha utoaji wa elimu mkoani
Kagera.
Walimu
wakuu wa Shule za Msingi Kalwoshe na Nyakato waliwashukuru VSO na PCF kwa kile
walichokifanya na kuwaboreshea mangira ya kufundishia na kujifunzia wanafunzi
na kuondoa kero za kunyeshewa mvua darasani na ofisini wakati wakitekeleza
majukumu yao.
Kanali
Massawe akihitimisha hafla fupi hiyo alitoa wito kwa mashirika mengine nchini
kama hayo kutoa misaada ya elimu ili kuupandisha mkoa wa Kagera kielimu. Aidha alitoa wito kwa walimu kutumia maktaba
zilizojengwa kujiendeleza kielimu pamoja na kuweka mkazo kwa nidhamu ya
wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuzingatia usafi na unadhifu wa wanafunzi wao.