Bukobawadau

ASHUKIWA MAUAJI YA BABA MZAZI - MULEBA

Kamanda wa polisi mkoani  Kagera Henry Mwaibambe
 JESHI la Polisi mkoani Kagera linamshikilia Issa Sadick (49), Mkazi wa Itongo tarafa ya Nshamba Wilaya ya Muleba kwa tuhuma za mauaji ya baba yake mzazi na mama yake wa kambo.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Henry Mwaibambe, amethibitisha kutokea kwa tukio   hilo lililotokea juzi majira ya saa 2:45 usiku Kijiji cha Itongo wilayani humo.
Mwaibambe, alisema Sadick Hamis (84), aliuwawa kwa kucharangwa mapanga na kisha kutenganishwa kichwa na kiwiliwili wakati mkewe Zamda Sadick (44), pamoja na mtoto  wao Juma Sadick (15), walifariki wakiwa katika hospitali teule ya Rubya baada ya nao kucharangwa mapanga.
Alisema familia ya mzee Hamis ilivamiwa na watu wasiojulikana wakaanza kuwakata  mapanga na kumuacha mtoto wao wa kike, Aza Sadick (19), mwanafunzi wa shule ya Sekondari Rukondo kidato cha tatu, bila kumzuru sehemu yoyote ile na badala yake walichukuwa simu yake ya mkononi.
Alisema familia hiyo ilikuwa na ugomvi wa muda mrefu, kwa madai kwamba Baba wa familia hiyo alikuwa akitoa huduma kwa upendeleo kwa mke wake wa nne, Zamda.
“Inawezekana kwa sababu Hamis alikuwa na wake wanne, yawezekana wake zake wengine watatu na watoto wao walihisi kuna dalili ya mke mdogo kupewa nafasi kubwa ya kurithishwa mali pamoja na mwanae Juma aliyefia katika hospatali teule ya Rubya,” alisema Kamanda Mwaibambe.
Alisema katika mgogoro huo, mtuhumiwa ndiye aliyekuwa kinara na ndio maana jeshi la polisi linamshikilia kwa mahojiano zaidi.
Na Ashura Jumapili
Next Post Previous Post
Bukobawadau