KIKAO CHA KAZI RC NA WATENDAJI MULEBA LEO
MAANA HALISI YA MAABARA TATU ZILIZOKAMILIKA KILA SHULE MKOANI KAGERA YAONGEZA UCHAKARIKAJI WA WATENDAJI
KUZIKAMILISHA KABLA YA DESEMBA 5, 2014
Mkuu wa Mkoa wa Kagera abadili upepo
wa maana halisi ya maabara tatu zilizokamilika
mkoani hapa kuwa ni zile zenye miundombinu yote inayotakiwa kuwemo katika kila
chumba kwenye vyumba vitatu kama mifumo ya gesi na maji pia samani isipokuwa vifaa tu ambapo alibadili mtazamo wa
watendaji walio wengi kuwa maabara iliyokamilika ni maboma ya vyumba vitatu tu.
Upepo wa maana halisi ya maabara
iliyokamilika ulibadilika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella kuitisha kikaokazi cha watendaji wakuu wa
serikali katika mkoa wa Kagera ili kujadili na kutoa taarifa ya ujenzi wa
maabara na kuweka mikakati jinsi ya
kukamilisha maabara hizo ifikapo Desemba 5, 2014.
Katika kikao hicho kilichofanyika
Wilayani Muleba tarehe 17/11/2014 Mkuu wa Mkoa aliwaonya watendaji hao wakuu
waserikali katika ngazi za Halmashauri za wilaya kuhakikisha maabara
zinakamilishwa na miundombinu yake na siyo kujenga maboma tu alafu kujiridhisha
kuwa tayari maabara zimekamilika.
Mhe. Mongella aliagiza kuwa rikizo zote na safari za Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Idara
kusitishwa mara moja ili kuhakikisha ujenzi wa maabara unakamilika ambapo
alitoa tarehe ya mwisho ya kumkabidhiwa maabara zote kuwa ni tarehe 5/12/2014 mkoa mzima na hatopenda mzaha wala
maelezo bali kukabidhiwa maabara tu.
Akifafanunua ufanisi wa ujenzi wa
maabara Mkuu wa mkoa John Mongella alisema kuwa ujenzi hautegemei mtu mmoja
mfano Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri bali inatakiwa kushirikiana kwa pamoja kama mfumo wa utawala ulivyo kuanzia ngazi za
juu mpaka chini kila mmoja anahusika moja kwa moja katika suala hilo la
maendeleo.
Hadi sasa Mkoa wa Kagera unahitaji
jumla ya maabara 570 zilizokamilika ili kutumiwa na wanafunzi wa elimu ya
sekondari hasa katika shule za kata
ambazo hapo awali hazikuwa na maabara hata moja lakini ujenzi umefikia asilimia
31.8 ambapo bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kufikia asilimia 100.
Maagizo: Katika
kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa maagizo makuu manne kwa watendaji ili
wayafanyie kazi mara moja bila mzaa katika kusukuma maendeleo ya wananchi mbele
.
Kwanza, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya
wakishirikiana na Madiwani kuhakikisha wanabadili vipaumbele vya maendeleo na
kupeleka fedha zote katika kukamilisha ujenzi wa maabara, aidha makusanyo yote ya vyanzo vya ndani yaelekezwe
katika kukamilisha vyumba vya maabara kila wilaya.
Pili,
Kuimarisha na kuthibiti ukusanyaji wa mapato ya ndani ambayo ndiyo uti wa
mgongo katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi na uendeshaji wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Halmashauri za Wilaya
zinatakiwa kusimamia ipasavyo mapato ya ndani ili kuacha utegemezi
unaosababisha miradi mingi ya maendeleo kukwama.
Tatu,
Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali katika Halmashauri za
Wilaya, Mkuu wa mkoa aligiza kila Halmashauri kuhakikisha inapata hati safi na
hatovumilia mtendaji yeyote atakayesababisha hoja bali atakula naye sahani
moja.
Nne, Ulinzi na Usalaama, Halmashauri za wilaya
ziliagizwa kutenga bajeti ya kununualia sare za mgambo (Jeshi la Akiba) wakati
wanapohitimu mafunzo yao. Aidha mkuu wa mkoa alisema atahakikisha mfumo wa
utawala unafanya kazi katika kupambana na wahamiaji haramu, wavamizi wa mapori
ya hifadhi na uharibifu wa misitu.
Kikao kazi hicho cha Mkuu wa mkoa na watendaji wa
serikali kilihudhuriwa na Wakuu wa
Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na Manispaa, Wenyeviti wa
Halmashauri,Wahandisi, Maafisa Elimu wa Wilaya, Maafisa Mipango wa
Halmashauri pia na Watendaji waandamizi
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakiongozwa na Katibu Tawala mkoa Bw. Nassor
Mnambila
Na: Sylvester Raphael