MAGAZETINI LEO ALHAMISI NOV 27,2014
Saa za waliochota Sh bil 321 IPTL zahesabika
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kila aliyehusika katika kashfa ya
uchotwaji wa Sh bilioni 321 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), abebe msalaba wake bila kujali
cheo chake na kwamba muda wa kulindana umekwisha.Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye walipokuwa wakihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais asiyekuwa na wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya, alisema ni vema watu wanaotajwa katika kashfa hiyo wakae pembeni ili kutoitia doa serikali na chama tawala. Profesa Mwandosya alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambao pia ni wanachama wa CCM.
“Kwa sasa hivi vikao vya chama na serikali vinaendelea, ni lazima ripoti iwasilishwe bungeni, mambo yawe hadharani ili mbivu na mbichi zijulikane.
“Kwa maoni yangu, naamini kabisa kuwa ni vema wale wote wanaotajwa kwenye hili suala la IPTL, wakakaa kando ili kuepuka kukipaka chama na serikali matope,” alisema Profesa Mwandosya.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema wajiuzulu kutokana na kutajwa katika kashfa hiyo.
Katika mkutano huo, Nape alisema watakaobanika kuhusika katika kashfa hiyo, wanapaswa kuwajibishwa bila kujali nafasi zao.
“Katika hili naomba niseme kila ambaye atabainika kuhusika achukuliwe hatua, kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe. Hatutakubali kuona watu waliohusika katika sakata hilo wanaachwa, lazima wachukuliwe hatua.
“CCM tunaheshimu miiko ya uongozi na maadili, hivyo hili la Escrow lazima waliohusika wachukuliwe hatua,”alisisitiza Nape.
Kwa upande wake Kinana alisema muda wa viongozi ndani ya chama hicho kulindana umekwisha na uvumilivu sasa basi.
Kinana ambaye hakuzungumzia kabisa sakata la Escrow, alitumia nafasi hiyo kuwaambia wananchi. “Si sawa mwizi kumlinda mwizi, haiwezekani mtu anaharibu halafu anaachwa.
“Muda wa kulindana haupo tena ndani ya CCM. Uvumilivu umefika mwisho. Muda wa kubebana na kuvumuliana sasa umekwisha,”alisisitiza Kinana.
Alisema CCM haiko tayari kuendelea kulindana na kubebana wakati mambo yanaharibika huku akisisitiza kazi ya chama hicho ni kuisimamia Serikali.
CUF
Nacho Chama cha Wananchi (CUF), kimemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo na wengine wanaotajwa katika kashfa hiyo kujiuzulu wenyewe vinginevyo rais atengue uteuzi wao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba alisema viongozi wengine wanaopaswa kuwajibika ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG),Jaji Frederick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi.
Alisema licha ya hatua hiyo, pia akaunti zote za benki zinazotajwa kupitisha fedha za Escrow ni vyema zikafungwa na fedha zirudishwe serikalini.
Profesa Lipumba pia alitaka mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Lugemalila iliyokuwa na asilimia 30 za hisa IPT na mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi, aliyenunua kampuni hiyo ya kufua umeme, wafikishwe mahakamani.
Alisema chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya kuona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).
“Tanesco walipaswa kurejeshewa sh bilioni 321 zilizolipwa kwa ITPL kati ya mwaka 2002 na 2012, kwa hiyo fedha zote za akaunti ya escrow jumla ya Sh bilioni 306 ni mali ya tanesco na bado wanaidai IPTL bilioni 15.
“Kutokana na hali hiyo, watuhumiwa hao wanapaswa kufikishwa mahakamani kutokana na kufanya ufisadi mkubwa wa namna hiyo wakati wananchi wanaishi katika mazingira magumu,”alisema Profesa Lipumba.
Alisema katika ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa kampuni ya PAP haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za kampuni ya Merchmar ya nchini Malaysia katika IPTL kwa sababu zilikua zimezuiwa na mahakama.
“PAP hawana hati halisi za hisa hizo, pia ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walinunua hisa kwa sh milioni 6 badala ya dola milioni 20, hali iliyoikosesha serikali mapato ya Sh bilioni 8.7.
“Kosa hilo pia linawahusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kanda ya Ilala ambao walihusika katika kupokea kodi ya mauzo hayo,”alisema.
Prof. Muhongo
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema hajiuzulu ng’o.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam juzi, Profesa Muhongo alisema uamuzi wa kujiuzulu unaweza kusababisha rasilimali za wananchi kuibwa zaidi.
“Siwezi kujiuzulu kwa ajili ya kauli za watu…nafanya kazi kwa maslahi ya wananchi, kama kuna watu wanadhani nitajiuzulu ili nitengeneze mianya ya kula rushwa, wamejidanganya… sijiuzulu ng’o,”alisema.
Alisema hafanyi kazi kwa ajili ya kusikiliza maneno ya watu, bali kutetea rasilimali za wananchi, hivyo hawezi kuhusishwa na mambo yasiyomuhusu.
“Hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha wazi sijala hata shilingi kumi, na siwezi kufanya hivyo kwa sababu nawatumikia wananchi kwa nia na moyo mmoja. Wanaotaka ning’oke wana mambo yao binafsi, narudia tena kusema sing’oki.
“Sijatenda kosa baya lolote, wezi, walarushwa na wababaishaji wananiogopa na kunihofia,” alisema.
Alisema mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikimtuhumu bila ya kuwa na ushahidi.
“Sitaki kutetewa, bali wanapaswa kuandika habari zenye ukweli ambazo zimefanyiwa utafiti kabla ya kutoa hukumu,” alisema.
Pinda ausia serikali
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema ili kuweza kuridhisha nyoyo za Watanzania katika kashfa ya IPTL, ni lazima Serikali ijipange ili kuweza kutoa majibu yatakayoridhisha kuhusiana na suala la IPTL.
Amesema kwa kipindi cha sasa Taifa linapita katika wakati mbaya na mgumu wa lala salama kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Dodoma alipokuwa akitoa hotuba ya kumweka wakfu Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kati wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani, ambapo alisema hivi sasa kumekuwa na kampeni za kuchafuana mbele ya jamii.
“Baba Askofu kipindi hiki ni kibaya tunasema lala salama, kubwa ni Serikali kutoa maelezo yatakayotuaminisha kwa wananchi. Ila uadilifu mkubwa unahitajika serikalini kwa sababu kuna mapesa.
“…Kipindi hiki ni cha lala salama kwa hiyo watu wengine wamekuwa wakichafua wengine kwa ajili ya kutaka kupata madaraka ya nchi,” alisema Pinda.
Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Shabani Matutu na Ramadhan Hassan, Dodoma