MH.MASSAWE NA MIKAKATI MIPYA YA UJENZI WAMAABARA KWA MADIWANI NA WATENDAJI
Mkuu wa mkoa wa Kagera aibua mikakati
mipya ya ujenzi wa maabara tatu kila
shule ya Kata (shule za serikali) ili ujenzi ukamilike kwa wakati katika kutekeleza agizo
la Rais Kikwete la Januari 2013
linalowataka wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya kuhakikisha maabara zote
zinakamilika ifikapo Novemba 30, 2014.
Kanali Mstaafu Fabian Massawe
ameamua kuhudhuria vikao vya mabaraza ya
Madiwani kila Halmashauri kuzungumza na Madiwani ili kupokea taarifa zao na
mikakati ya ujenzi wa maabara tatu kila shule imefikia wapi katika utekelezaji aidha
kuwapa mbinu mpya kuhakikisha maabara hizo zinakamilika kwa wakati .
Katika vikao hivyo vinavyoendelea
mkoani Kagera katika Halmashauri zote Mkuu wa mkoa amekuwa akipokea taarifa ya kila
kata kutoka kwa Diwani husika kuhusu hatau iliyofikiwa katika kukamilisha
ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara za fizikia, kemia na Baiologia katika shule
husika.
Mikakati mipya aliyowapa madiwani
katika mabaraza yao Mkuu wa Mkoa wa Kagera ni kutumia ushawishi mkubwa badala ya kutumia nguvu kwa wananchi
kukusanya michango ili kukamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kila shule.
Kuhamasisha wananchi kuchangia
vifaa vya asili kama mchanga, mawe, kokoto na matofali badala ya kuwabana kuwa
watoe michango ya fedha tu ili mwananchi kila mwenye uwezo wa kupata vifaa
hivyo avitoe au asiyeweza atoe kiasi cha fedha kulingana na gharama za vifaa kwa kila mwananchi.
Mkakati mwingine alioutoa kwa
madiwani Kanali Massawe ni kuitisha harambee ya wananchi wote na wazawa wenye
uwezo walioko nje ya mkoa ili kuchangia
ujenzi wa maabara ukamilike kwa wakati na ifikapo Novemba 30, 2013
akatoe taarifa kwa Rais Kikwete.
Mkakati mwingine ni Madiwani kukubali kubadilisha vipaumbele
vyao ambavyo vilikuwa vimetengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2014/15 ili
fedha hizo za miradi ya maendeleo ziende katika ujenzi wa maabara kwani maabara
pia ni kipaumbele kwa maendeleo ya wananchi.
“Nawashauri sasa Waheshiiwa
Madiwani mkishirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na menejimenti yake
kuangalia uwezekano wa kufanya mabadiliko ya vipaumbele (re- allocation) ili
kuchangia ujenzi wa maabara. Lakini mchakato huo unatakiwa kupitia katika
baraza la madiwani ili ukubaliwe na madiwani.” Alisistiza Kanali Massawe.
Aidha, Kanali Massawe katika
ziara hiyo aliambatana na Katibu Tawala Msaidizi Serikali za mitaa Bw. David
Lyamboko ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi
jinsi ya kubadili vipaumbele vya miradi iliyopangiwa fedha katika bajeti ya
mwaka wa fedha 2014/15 ili fedha hizo ziweze kwenda katika ujenzi wa vyumba
vitatu vya maabara kila shule katika halmashauri husika.
Bw. Lyamboko aliyashauri mabaraza
ya Madiwani kuwa mara baada ya kuangalia miradi iliyopangiwa bujeti ambayo
itabadilishwa vipaumbele vyake kwenda kwenye ujenzi wa maabara inatakiwa mchakato uanziae kwenye ngazi ya
vijiji kwa kuandikwa mihtasari na kwenda mpaka ngazi ya halmashauri kwa kufuata
taratibu na sheria zilizopo.
Madiwani wakiwasilisha taarifa
zao walisema wanakabiliwa na changamoto kubwa katika ujenzi wa maabara hasa
baadhi ya wanansiasa kuwagomesha wananchi kuchangia, wananchi kuwadhuru kwa
kuwapiga watendji wakikusanya michango ya ujenz,i na wananchi kuchangia kwa
kasi ndogo sana.
Akijibu changamoto hizo Kanali
Massawe aliwaagiza watendaji wa kata kuchukua hatua mara moja kwa mwananchi
yeyote anayegoma kuchangia ujenzi wa maabara katika kijiji chake. Aidha
aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia siku hadi siku kujua kinachoendea katika
maeneo ya ili ifikapo Novemba 30, 2014 maabara hizo ziwe zimekamilika.
Kuanzia tarehe 3/11/2014 Kanali
Massawe anaanza kutembelea Halmashauri zote za Wilaya kukagua ujenzi wa maabara
tatu kila shule. Hadi kufikia Septemba 2014 kati ya maabara 570 zianazotakiwa
kujengwa mkoani Kagera ni 136 zilikuwa zimekamilika asilimia 23.8