UFISADI WAUMALIZA USHIRIKA NCHINI
Na Prudence Karugendo
WAKATI ushirika nchini unachungulia kaburi
wanaushirika wanayo mengi ya kusema kuhusu janga hilo, janga la kutokomea kwa
ushirika na kuuacha ubaki kwenye historia tu. Wadau wengi wa ushirika wanasema
kwamba janga hilo linaloukabili ushirika halitokani hata kidodo na nguvu za
asili zilizo nje ya uwezo wa binadamu wa kulidhibiti, kwamba janga hilo
linatokana na nguvu za binadamu wenyewe tena waliopewa jukumu la kuutumikia
ushirika, kuulinda na kuuimarisha.
Wanaushirika
wengi wanasema kwamba tatizo linalijitokeza ni la viongozi wa ushirika
kuuchukulia ushirika kama shamba la bibi ambamo wanaweza kuchuma bila kupalilia,
wanaangalia matunda ya shamba tu na sio usitawi wa shambalenyewe.
Eti
kinachofanywa na viongozi wa ushirika ni tofauti na inavyofikiriwa kwamba
viongozi hao wameugeuza ushirika kuwa mali yao binafsi, sababu eti mwenye mali
binafsi ni lazima aionee uchungu mali yake hiyo na hivyo kuichukulia kwa uangalifu
wa hali ya juu, kwamba hiyo ni tofauti na hali halisi ilivyo kwa sasa ambapo
viongozi wa ushirika ni kama wanaukomoa ushirika kwa kufanya mambo bila kuujali
mustakabali wake.
Wanasema
kwamba kitendo cha uongozi wa ushirika, uwe wa kuchaguliwa au wa kuajiriwa,
kufuja mali za ushirika kana kwamba ni kukomoana kinadhihirisha ufisadi
uliooza. Eti kisichoeleweka ni kwa nini mamlaka ya juu yanayopaswa kuusimamia
ushirika na kuuongoza yanayaona hayo yote bila kuchukua hatua yoyote?
Wanasema
kwamba waziri mwenye dhamana ya ushirika yupo, anazisikia kelele zinazopigwa na
wanaushirika lakini kaamua kukaa kimya bila kuzifanyia lolote kelele hizo,
Mrajis wa Vyama vya Ushirika yupo, naye eti anazisikia kila wakati kelele
zinazopigwa na wanaushirika lakini kaamua kuzipuuza. Hiyo ni mbali na wale
walio karibu zaidi na wanaushirika kwa maana ya warajis wasaidizi pamoja na
maafisa ushirika.
Kimya hicho
cha wenye jukumu la kuulinda na kuulea ushirika nchini ni kama kinaonyesha
kwamba viongozi wa ushirika wanazo baraka zote za kuuhujumu na kuufisidi
ushirika kwa namna wanavyoweza hata kama ni kuunyongelea mbali, wanadai wadau
hao wa ushirika.
Chama
kimojawapo cha ushirika kinachochungulia kaburi ni KCU (1990) Ltd. cha mkoani
Kagera. Chama hicho chenye historia ndefu katika nyanja ya ushirika, kwa sasa kiko taabani. Wanaushirika wa KCU
(1990) Ltd. wanasema anayeona kwamba chama hicho kinataabika kwa sababu ya kitu
kingine mbali na ufisadi ni bora ajitokeze na kukisema kitu hicho. Eti wao
kamwe hawawezi kwenda kwa mganga wa kienyeji kutafuta sababu za ushirika wao kuwa
taabani wakati kila kitu kinajionyesha wazi.
Sababu eti
mengi yamesemwa na kuuandikwa juu ya ubadhirifu unaofanyika katika chama hicho,
ila la kushangaza ni kwamba hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na mamlaka ya
juu dhidi ya ubadhirifu huo unaoelekea kuitokomeza KCU (1990) Ltd..
Inasemwa
kwamba kutochukuliwa hatua dhidi ya ubadhirifu ndani ya KCU (1990) Ltd. ni
sababu moja kubwa inayozidi kuwapa jeuri na kiburi viongozi wa ushirika huo na
kuwafanya waongeze nguvu za ufisadi kwa vile wanaelewa hakuna kitakachofanyika.
Maana eti wameiziba mianya yote ambayo ingeweza kuwawajibisha na kuwaacha
wakulima, wanaushirika, ambao hawana la kufanya kulingana na ubovu wa sheria za
ushirika ulivyo.
Mmoja wa
wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. anayekerwa sana na ufisadi ndani ya ushirika
huo, Archard Felician Muhandiki, anashangazwa sana na hatua ya serikali
kuwafumbia macho na kutowachukulia hatua yoyote viongozi na watumishi wa
ushirika huo ambao wamejivisha ufisadi husiohojika.
Anasema
kwamba pamoja na viongozi wa ushirika huo kukiri tuhuma za ufisadi dhidi yao
haoni lolote linaloelekea kukabiliana na kashfa hiyo.
Muhandiki
anasema kwamba hakuna kitu kilichomuuma kama kile cha yeye kupeleka malalamiko
yake moja kwa moja kwa waziri anayehusika na ushirika lakini waziri huyo
akayarudisha malalamiko hayo kwa uongozi wa KCU (1990) Ltd. akiushauri ukamuite
Muhandiki na kumfukuza kwenye ushirika kama ingebidi. Muhandiki anasema hayo
yalielezwa na mwenyekiti wa KCU (1990) Ltd. kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho
na yamerekodiwa.
Muhandiki
anasema kwamba yaliyokwisha semwa na kuandikwa juu ya ufisadi unaofanywa na
uongozi wa KCU (1990) Ltd. ni mengi sana, eti kama tuhuma zote hizo zingelikuwa
ni za uongo ni kitu gani kinauzuia uongozi huo kwenda mahakamani ili
kujisafisha?
Anasema, eti
badala yake KCU inahangaika usiku na mchana, ikizitumia pesa za chama hicho,
kuhakikisha tuhuma hizo zinafukiwa, jambo linalodhihirisha pasipo na shaka kuwa
tuhuma hizo ni za kweli. Anasema kwamba inawezekana hiyo ikawa ndiyo sababu ya
KCU kuukingia kifua uongozi wa Chama cha
Msingi Kamachumu kwa kutumia vibaya pesa ya wanaushirika kuuwekea mawakili wa
kuutetea mahakamani dhidi ya wanachama waliofungua kesi ya kuuwajibisha.
Anaeleza
kwamba ufisadi unafanyika na kuhujumu ushirika halafu inatumika gharama
nyingine kubwa ya ushirika huohuo kuifunika hujuma husika. Anauliza katika aina
hiyo ya ufisadi kinaofanyiwa chama hicho kikuu kitawezaje kupona?
Wanaushirika
wengine wa KCU (1990) Ltd. wanasema kwamba chama hicho kwa sasa kimebaki jina
tu bila ya uhai wowote wa kujiendesha. Eti wafanyakazi wengi wa chama hicho
wamepunguzwa kutokana na ukosefu wa pesa za kuwalipa mishahara, na haijulikani pesa ya kununulia kahawa toka
kwa wakulima kwa musimu huu itapatikana wapi. Inasemekana hata pesa ya kitengo cha
mauzo ya nje, kinachoitwa Moshi Export, imekombwa yote na kukiacha kitengo
hicho kikiidai KCU (1990) Ltd..
Kutokana na
hali hiyo ya kutatanisha na kutia majonzi kuhusu mwenendo wa ushirika huo,
ndiyo maana kwa sasa wakulima wa kahawa ambao ni wanachama wa ushirika huo
wanausubiri kwa hamu umoja wa wakulima wa kahawa ulioanzishwa na wanachama wa
Kamachumu na kuupa jina la Tweyambe Coffee Growers. Wanasema umoja huo utakuwa
mkombozi wao baada ya ushirika kukatishiwa njiani safari yake.
0784 989 512