UKAWA WAFICHUA NJAMA ZA KUIZIMA IPTL BUNGENI
Dodoma. Wakati kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) ikianza kupitia ripoti ya IPTL kuhusu uchunguzi wa
ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow, wabunge wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), umedai kwamba kuna mikakati imeandaliwa kuzima ripoti
hiyo kusomwa na kujadiliwa bungeni.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema
jana kwamba moja ya mikakati hiyo ni madai ya kuwapo barua ya Mahakama
kuzuia mjadala huo akisema mkakati huo unatokana na ukubwa wa kashfa na
jinsi inavyowahusisha viongozi waandamizi serikalini.
Mbatia aliyeambatana na kundi kubwa la wabunge
kutoka Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, alisema: “Iko mikakati na mbinu za
kila aina kulihujumu Bunge lisisimamie fedha za walipakodi, ndiyo maana
kuna danadana na tuna taarifa za kuwapo barua kutoka mahakamani kuzuia
jambo hilo lisijadiliwe bungeni kwa madai eti kuna kesi.
“Mahakama haiwezi kuingilia shughuli za Bunge,
inatia wasiwasi kwa kuwa Ofisi ya Bunge nayo imekuwa na danadana kila
siku kwa kubadilisha badilisha ratiba wakati sisi tunataka hawa
waliohusika kwenye kashfa hii wachukuliwe hatua.”
Pia, alisema kuna taarifa kwamba Serikali inadai haina fedha, ikitaka kufupisha Bunge na suala hilo lisijadiliwe sasa hivi.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Mnyaa
alisema: “Serikali inategesha tegesha tu mambo bungeni na ndiyo maana
leo (jana) wameahirisha Bunge hadi kesho (leo) bila sababu za msingi,
wanafinya muda wa sisi kujadili sakata hili,” alisema Mnyaa.
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu
alisema escrow ni kama ilivyokuwa kashfa ya Richmond ambayo iliwang’oa
wahusika wakuu bungeni, hivyo haiwezekani isijadiliwe bungeni kwa madai
kwamba Mahakama imezuia...
“Hakuna utaratibu kama huo wa Mahakama kuelekeza Bunge kitu gani kifanyike na gani kisifanyike pia hata Katiba hairuhusu hilo.”
Lissu alishangazwa na Naibu Spika, Job Ndugai
kuahirisha Bunge jana hadi leo kwa madai kuwa yeye (Lissu) alikuwa
hajakamilisha taarifa ya upinzani kwenye muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014 akidai kuwa huo ni
upotezaji wa muda.
“Nilimwomba Naibu Spika kuwa aahirishe muswada huo
hadi kesho kwa kuwa ulikuwa umepangwa tarehe 25 lakini ghafla
ukabadilishwa na mimi sikuwapo kwa muda wote huo. Sikuomba aahirishe
Bunge nilimwomba aahirishe muswada tu,” alisema Lissu.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema naye
amesikia kuwapo barua ya Mahakama kuzuia mjadala huo na kusema kama ni
kweli, halitakuwa sahihi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika
Operesheni Delete CCM mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa alisema si Waziri Mkuu wala Jaji Mkuu anayeweza kuuzima
mjadala wa escrow bungeni.
Alisema kashfa hiyo ambayo chama chake kina nyaraka zake na
ripoti za uchunguzi wa escrow na Takukuru, lilianzia bungeni na lazima
lijadiliwe na kumalizikia bungeni.
Ndugai ajibu hoja
Akizungumzia madai hayo, Ndugai alisema hajui kama
kuna barua kutoka mahakamani kuzuia mjadala wa escrow bungeni na suala
hilo litawasilishwa na PAC bungeni Novemba 27 kama ilivyopangwa.
“Waiamini kamati, kwanza hawa wa upinzani ni yao
(kamati) haiongozwi na CCM, mimi naamini kamati itafanya kazi nzuri.
Sidhani kama kanuni zinaruhusu kugawa ripoti hiyo kwa kuwa ni siri,
kanuni hairuhusu.”
Rejea
Ripoti ya Tegeta Escrow inatokana na uchunguzi
maalumu wa Sh306 milioni zilizochotwa katika akaunti ya escrow ndani ya
Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Fedha hizo zilitokana na gharama za uwekezaji
zilizokuwa zinalipwa na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL baada ya kutokea
mgogoro wa kibiashara baina ya wabia hao.
Tanesco ililalamika kuwa ilikuwa inailipa zaidi
IPTL kinyume na gharama halisi za uwekezaji, hivyo kuamuliwa na Mahakama
kuwa fedha hizo ziwekwe katika escrow hadi upatikane ufumbuzi wa
mgogoro huo lakini zikachukuliwa kabla kesi kuamuliwa.
MWANANCHI
MWANANCHI