UNDUGU NA UHESHIMIWA
Kuuacha undugu ni dalili za
kuyakaribisha maangamizi
NA PRUDENCE KARUGENDO
YALIANZA kama masihara, mwanzoni mwa kipindi cha kwanza
cha awamu ya pili ya uongozi wa nchi yetu, wawakilishi wetu, wabunge, kwa
kusukumwa na kitu ninachoweza kukiita ibilisi wa umimi, wakaona kwamba haifai
wao kuendelea kuitwa ndugu. Kwa kutumia kinga waliyowekewa na Katiba ya nchi
wakaamua wao waitwe waheshimiwa! Kwahiyo wakawa wamejitenga na wananchi
wanaowawakilisha, wananchi wakabaki ni ndugu wao wakajipachika uheshimiwa!
Ikumbukwe neno
ndugu lilibuniwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwaka 1975, katika harakati
zake za kuilinda na kuidumisha tunu ya nchi ya umoja na mshikamano wa wananchi.
Sababu tunapoongelea tunu za nchi ni lazima tuelewe kwamba undugu ndiyo tunu ya
kwanza ambayo kila nchi inapaswa ijivunie. Bila undugu tunu zote zilizobaki ni
kazi bure.
Hata kama
nchi imejaaliwa kila aina ya utajiri lakini bila undugu wa kupendana,
kuthaminiana na kuchukuliana kwamba kila mmoja ni sehemu ya mwingine, utajiri
ilionao nchi ni lazima ugeuke balaa
linaloisukuma nchi husika kuelekea kwenye maangamizi huku ikionekana ina
umasikini unaonuka. Hakuna umasikini unaokaribiana na wa watu kutafunana wao
kwa wao, kwa maana ya kuuana, kutokana
na kukosa hisia za kiundugu.
Katika hilo
mifano ni mingi, nje ya bara letu la Afrika kuna nchi zilizojaaliwa utajiri wa
asili ikiwa ni pamoja na akili za kuutambua na kuutumia utajiri huo,
tuichukulie nchi mojawapo ya Urusi. Nchi hiyo iliwahi kuwa moja ya nchi mbili
tajiri na zenye nguvu sana duniani ikishindana na Marekani. Lakini Urusi
ilipokumbwa na ibilisi wa uhasama na kuusahau undugu ulioifanya ikafikia hapo
ilipokuwa, tunayaona yanayoitokea kwa sasa. Kila siku ni kutengana na kudundana
wao kwa wao huku ikimwaga damu na kuonyesha umasikini uliopitiliza!
Katika
Afrika kuna nchi kama Kongo DRC. Hiyo ni nchi iliyojaaliwa utajiri wa asili
kuliko hata nchi nyingi za Ulaya zinazojidai ni za dunia ya kwanza. Lakini
kukosekena kwa undugu katika nchi hiyo kumeifanya ionekane ni masikini kupita
kiasi. Kwa sasa nchi hiyo imegeuzwa uwanja wa vita isiyoeleweka maana yake ni
nini!
Kwa hapa
kwetu Tanzania undugu alioubuni Nyerere ulilenga katika kuwaweka wananchi
pamoja na kuwafanya waonane wao ni kitu kimoja, wachukuliane ni watu wa familia
moja, ili akipata mmoja wajione wamepata wote, akikosa mmoja wajione wamekosa
wote. Undugu uliowaondolea wananchi mikogo ya mmoja kumkoga mwingine kwa vile
mmoja kapata na mwingine kakosa.
Katika hali
hiyo haikuwa rahisi watu kuoneana husuda kitu ambacho kingeweza kusababisha
pengo kati ya aliyenacho na asiyekuwanacho, pengo ambalo ni kiini cha kijicho
na mwanzo wa chuki miongoni mwa wananchi. Kawaida chuki ndiyo huzaa uhasama na
hatimaye ugomvi, vita, wananchi kuanza kupukutishana roho zao wao kwa wao.
Kinyume cha neno
ndugu ni ubwana na utwana, bwana hakubali kuwa ndugu na mtwana, na mtwana
hakubali kuendelea na hali hiyo ya unyonge muda wote, hali ya kuwa chini ilhali
akimuona mwenzake yuko juu akimkandamiza. Kwa vyovyote vile atafanya kila njia
kujinasua huko chini alikokandamizwa.
Na hatua
hiyo haifanyiki kwa maelewano, sababu aliye juu akiufaidi ubwana anatamani
abaki hukohuko wakati aliye chini akitamani naye kuja juu, hapo ni lazima chuki
iwepo na matokeo yake ni mapambano na kumwaga damu. Mmoja akitafuta haki yake
ya uhai na utu na mwingine akitaka kuipoteza kabisa haki hiyo ya mwenzake.
Baada ya
Nyerere kuziangalia tofauti hizo na kuamua kubuni neno ndugu akiwa ameshawishiwa
na falsafa ya kiongozi mmoja wa kidini, Askofu Marehemu Christopher Mwoleka wa
Jimbo Katoliki la Rulenge, ya “Ili wawe na umoja”, uheshimiwa ulibaki tu kwa
watoa haki waliopewa dhamana ya kuzitafsri sheria za nchi, mahakimu na majaji.
Wengine wote tukaanza kujitambulisha kama ndugu. Dunia nzima ilituheshimu kwa
uamuzi huo
Kimantiki,
watafsiri hao wa sheria waliachwa waendelee kuwa waheshimiwa ili wapate fursa
ya kuitekeleza kazi yao kwa ufasaha bila ya upendeleo wala kuoneana. Sababu
katika undugu ingewawia vigumu kuitafsiri sheria jinsi ilivyo. Fikiria hakimu
au jaji jinsi ambavyo angeweza kumwambia ndugu yake kuwa kakosea kwa mujibu wa
sheria hivyo anatakiwa kutumikia kifungo kwa muda fulani. Kutokana na hilo hao
wakaachwa waendelee kuwa waheshimiwa kusudi uamuzi wao uendelee kuheshimika
bila kuonekana umeegemea upande wowote kutokana na kushawishiwa na neno ndugu.
Lakini
kiajabu wawakilishi wetu, kiulevi tu, ulevi wa madaraka ya nafasi tulizowapa,
kama alivywahi kusema Mwalimu, wakaamua nao waitwe waheshimiwa! Niliwahi
kuhoji, kama wao wabunge au wawakilishi wanataka wawe waheshimiwa, je, sisi
wananchi tuliowatuma tuwe kina nani?
Sababu kazi
wanayoifanya wabunge tulipaswa tuifanye sisi wenyewe, lakini kutokana na
uwezekano huo kuwa finyu sana ndipo ikaonekana tuwachague baadhi yetu
wakatuwakilishe baada ya kuitenga nchi katika maeneo ya uwakilishi ambayo
katika lugha nyingine yanaitwa majimbo. Sasa uheshimiwa wao uliowabagua
wananchi unatoka wapi?
Ajabu ni
kwamba baada ya wawakilishi wetu hao kukataa kuendelea kuitwa ndugu, watumishi
wengine wa umma nao wakadandia hapohapo, nao wakaanza kujiita waheshimiwa!
Madiwani nao wakajiita waheshimiwa, watendaji wa tarafa, wakuu wa wilaya, wakuu
wa mikoa nakadhalika, wote wakataka waitwe waheshimiwa! Neno ndugu lililokuwa
linatuweka karibu na kutufanya wamoja likafa kifo cha kulazimishwa! Ni baada ya
wananchi nao kuacha kulitumia baada ya kuona limepoteza maana, wakaanza tena
kuitana mabwana!
Baada ya
undugu kuuawa nini kingine tukitarajie cha kutufanya tuendelee kuwa wamoja?
Madhara ya kifo hicho cha undugu tumeanza kuyaona. Zamani tulipokuwa
tunatofautiana kwa hoja tulitafuta muafaka kwa wepesi tukiamini kuwa sote ni
ndugu. “Ndugu hapa umekosea, hatunabudi kufanya hivi na hivi”. Heshima iliwekwa
mbele, pamoja na kuitana ndugu tulijali sana tofauti za kiumri na wadhifa
alionao mtu katika jamii yetu.
Lakini
kufuatia kifo cha neno ndugu, sasa kijana akitofautiana na mzima, hata mtu huyo
awe ni mzee na mwenye wadhifa wa aina gani, kijana anaamua kumuwasha mzee vibao
hata iwe kwenye kadamnasi! Rejea ya Makonda na Mzee Warioba. Huko ndiko tuliko
kwa sasa, maadili yamepotea au kufa kabisa yakiwa yamesindikizana na neno ndugu,
ni katika maangamizi.
Hatuna tena
umoja, heshima wala adabu. Ni heri ya wanyamapori, sababu kimaumbile wanyama
wanayo maadili yao ambayo hawawezi kuyakaidi hata mara moja.
Umimi umeyabadili maadili katika jamii yetu.
Mabadiliko haya tunayoyaona, binafsi, siamini hata kidogo kama yamelenga katika
kuinufaisha jamii yetu, ninachokiona ni kwamba yamelenga kuzinufaisha nafsi
fulanifulani bila kujali jamii imekaaje katika upana wake. Ni kila mmoja
kupigania nafsi yake na ikibidi kukipora kilicho cha jamii!
Mfano,
haiwezekani kwamba mtu kuwa na akaunti ya “vijisenti” Ughaibuni ni kwa faida ya
Watanzania wote, hiyo ni kwa faida yake binafsi na familia yake. Na si ajabu
vijisenti hivyo vinavyofichwa Ughaibuni vikawa vimepatikana kiharamu kwa
gharama ya roho za Watanzania wote, na hiyo ikawa ndiyo sababu ya vijisenti
hivyo kufichwa nje ya nchi.
Fikiria
Watanzania wanakufa kwa kukosa vitu kama mahospitali na madawa ambavyo
vingeyanusuru maisha yao kutokana na magonjwa yanayotibika, kisa hakuna pesa ya
kufanya vitu hivyo vipatikane, pesa imekwapuliwa na kufichwa ughaibuni ikidaiwa
ni vijisenti!
Sasa Katiba
ya nchi inatengenezwa katika muundo wa
kuubariki ujambazi huo uliokusudia kuyateketeza maisha ya wananchi, wakati
huohuo wahusika wanajiuliza kwa nini wasifanye hivyo wakati wao ni waheshimiwa
na wananchi ni walalahoi, kwani wana undugu nao wakati neno ndugu lilishapotea?
Ila tukae
tukielewa kwamba kwa kulipoteza neno ndugu katika kujitambulisha tumepoteza
tunu nambari moja ya nchi yetu, tunu zilizobaki zote zitakuwa ni kazi bure
kuzizingatia, kilichobaki ni maangamizi tu.
0784 989 512